2010–2019
Rudi na Upokee
Aprili 2017


Rudi na Upokee

Kurudi katika uwepo wa Mungu na kupokea baraka za milele ambazo huja kupitia kufanya na kushika maagano ni malengo ya muhimu tunayoweza kuweka.

Kaka zangu na dada zangu; sasa ni kazi yangu kuongea nanyi, na kazi yenu ni kusikiliza. Lengo langu ni kumaliza kazi yangu kabla hamjamaliza ya kwenu. Nitajitahidi kufanya vyema.

Kwa miaka kadhaa, Nimechunguza kwamba wale wanaokamilisha mengi katika dunia hii ni wale wenye maono juu ya maisha yao, wenye malengo ya kuwafanya walenge maono yao na mipango yenye mbinu za jinsi ya kuyafikia. Kujua ni wapi unaelekea na jinsi unavyotarajia kufika pale yaweza kuleta maana, dhumuni, na mafanikio katika maisha.

Baadhi wanapata tatizo kutofautisha kati ya lengo na mpango mpaka watakapojifunza kuwa lengo ni kusudio au hatima, wakati mpango ni njia ambayo itakufikisha hapo. Kwa mfano, tunaweza kuwa na lengo kuendesha gari kuelekea eneo fulani lisilojulikana sana, na kama baadhi yenu ninyi wakina dada mnavyofahamu, sisi wanaume mara nyingi tunadhani tunajua namna ya kufika hapo—mara nyingi husababisha msemo wetu, “najua—lazima iwe karibu tu na kona ijayo.” Mke wangu lazima anatabasamu. Lengo lilikuwa wazi, lakini hakukuwa na mpango mzuri uliowekwa kufikia hatima.

Kuweka malengo ni muhimu hasa ukianza na hatima katika akili.” Na kupanga ni kutengeneza njia ya kufikia hatima. Funguo ya furaha ipo katika uelewa wa makusudio yapi ni ya muhimu kwa kweli—na kisha kutumia muda wetu, juhudi, na kipaumbele katika vitu vyenye njia sahihi ya kutufikisha hapo.

Mungu, Baba yetu wa Mbunguni, ametupa mfano mkamilifu wa kuweka malengo na kufanya mipango. Lengo Lake ni “kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu,”1 na njia Zake kufikia hili ni mpango wa wokovu.

Mpango wa Baba yetu mpendwa wa Mbinguni ni pamoja na kutupatia mahala pa kukua, kujinyoosha, kujifunza, kwa njia ambayo tunaweza kuwa hasa kama Yeye. Kuzivika roho zetu za milele katika miili, kuishi kutokana na mafundisho na amri za Mwanawe , Bwana Yesu Kristo, na kutengeneza familia za milele kunaturuhusu, kupitia Upatanisho wa Mwokozi, kukamilisha lengo la Mungu la kutokufa na uzima wa milele kwa watoto Wake pamoja Naye katika ufalme wa selestia.

Kuweka lengo kwa busara ni pamoja na uelewa kwamba malengo ya muda mfupi ni ya ufanisi tu endapo yatatupeleka kwenye malengo ya muda mrefu yenye kueleweka wazi. Nina amini kwamba kitu kimoja muhimu ili kupata furaha ni kujifunza jinsi ya kuweka malengo yetu na kuanzisha mipango yetu binafsi ndani ya mpango wa milele wa Baba yetu wa Mbinguni. Kama tutatazama katika njia hii ya milele, hatutashindwa kufaulu kurudi katika uwepo Wake.

Ni vizuri kuwa na malengo na mipango ya taaluma zetu, elimu yetu, hata kwa mchezo wetu wa gofu. Ni muhimu kuwa na malengo kwa ajili ya ndoa zetu, familia zetu, na mabaraza na miito ya Kanisa; hii hususani ni kweli kwa wamisionari. Lakini malengo yetu makubwa na makuu kabisa yanapaswa kuendana na mpango wa milele wa Baba yetu wa Mbinguni. Yesu alisema, “Tafuteni kwanza ufalme wa Mungu na haki yake, na hivi vitu vyote vitaongezwa kwenu.”2

Wataalam wa kuweka mipango wanatuambia kuwa jinsi mpango ulivyo rahisi na mnyoofu, ndivyo utakavyokuwa na nguvu zaidi. Pindi tunapoweza kufanya lengo kuwa taswira moja iliyo wazi au neno moja au mawili yenye nguvu na ishara, lengo hilo linaweza kuwa sehemu yetu na mwongozo wetu karibu kwa kila tutakachofikiria na kufanya. Naamini kwamba kuna maneno mawili ambayo, kwa mtazamo huu, yanaashiria malengo ya Mungu kwetu sisi na malengo yetu yaliyo muhimu zaidi kwetu sisi wenyewe. Maneno ni rudi na pokea.

Kurudi katika uwepo Wake na kupokea baraka za milele ambazo huja kupitia kufanya na kushika maagano ni malengo ya muhimu tunayoweza kuweka.

Tunarudi na kupokea kwa kuwa na “imani isiyotingishika katika [Bwana Yesu Kristo], kwa kutegemea kabisa” ustahili Wake, “msonge mbele mkiwa na imani imara katika Kristo, mkiwa na mng’aro mkamilifu wa tumaini, na upendo kwa Mungu na wanadamu wote … , mkisherekea neno la Kristo, na kuvumilia hadi mwisho.”3

Lusiferi hakukubaliana na mpango wa Baba yetu ambao ulituruhusu kurudi katika uwepo Wake na kupokea baraka Zake. Ukweli, yeye alipinga na kujaribu kubadilisha kabisa mpango wa Baba yetu, akitaka kujichukulia utukufu, heshima, na uwezo wa Mungu. Matokeo yake, alitupwa nje pamoja na wafuasi wake kutoka katika uwepo wa Mungu “Naye akawa Shetani, ndiyo, hata ibilisi, baba wa uongo wote, ili kudanganya na kuwapofusha watu, na kuwaongoza utumwani kadiri apendavyo, hata wengi kadiri wasivyosikia sauti [ya Bwana].”4

Kwa sababu ya uchaguzi wake kabla ya ulimwengu kuwepo, Shetani hawezi kurudi wala kupokea. Kitu pekee alichobaki nacho ni kupinga mpango wa Baba kwa kutumia kila kishawishi kinachowezekana na majaribu ili kutuangusha na kutufanya kuwa wenye huzuni kama yeye alivyo.5 Mpango wa Shetani kukamilisha lengo lake baya hutumika kwa kila mtu, kizazi, tamaduni, na jamii. Yeye hutumia sauti kubwa—sauti ambazo hulenga kumeza sauti ndogo na tulivu ya Roho Mtakatifu ambayo inaweza kutuonesha “vitu vyote tunavyopaswa kufanya ili turudi na kupokea.6

Sauti hizi ni mali ya wale wasiojali ukweli wa injili na wanaotumia intaneti, mitandao na machapisho ya kijamii, redio, televisheni, na filamu kuonesha uovu, vurugu, lugha chafu, uchafu na vitu hovyo hovyo katika njia ya ushawishi kiasi kwamba hutuondoa katika malengo yetu na mipango tuliyonayo ya milele.

Sauti hizi zinaweza pia kuwajumuisha watu wenye nia nzuri ambao wamepofushwa na falsafa za kidunia za watu ambao wanatafuta kuharibu imani na kupindisha mtazamo wa milele wa wale ambao wanajaribu tu kurudi katika uwepo wa Mungu na kupokea “vyote Baba [yetu] Alivyonavyo.”7

Nimegundua kwamba kukaa kwa umakini katika kurudi na kupokea baraka zilizoahidiwa, nahitaji kila mara kutafuta muda kujiuliza binafsi, “Ninaendeleaje?”

Ni kama kuwa na usahili binafsi, wa kipekee kwangu mimi mwenyewe. Na kama hilo linaonekana si la kawaida, tafakari kuhusu hilo: ni nani katika hii dunia anakufahamu kuliko unavyojijua mwenyewe? Unajua mawazo yako, matendo yako binafsi, matamanio yako na ndoto zako, malengo na mipango. Na unafahamu vyema kuliko mtu yeyote ni namna gani unavyoendelea katika barabara ya kurudi na kupokea.

Kama muongozo kwangu, wakati huu wa usahili binafsi, wa kipekee, napenda kusoma na kutafakari maneno ya kujichunguza yapatikanayo katika sura ya tano ya Alma, ambapo Alma anauliza: “Je mmezaliwa kiroho katika Mungu? Mmepokea mfano wake katika nyuso zenu? Mmeshuhudia mabadiliko haya makuu katika mioyo yenu?8 Maswali ya Alma ni ukumbusho wa nini malengo na mipango yetu inapaswa kuhusisha ili tuweze kurudi na kupokea.

Kumbuka mwaliko wa Mwokozi “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

“Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu.”9

Tunapoongezeka katika imani yetu katika uwezo wa Yesu Kristo wa kutupa raha katika nafsi zetu kwa kutusamehe dhambi, kukomboa mahusiano yasiyo kamili, kuponya vidonda vya kiroho vinavyozuia ukuaji, na kuimarisha na kutuwezesha kupata sifa za Kristo, tutashukuru kwa undani zaidi ukuu wa Upatanisho wa Bwana Yesu Kristo.10

Katika wiki zijazo, tafuta muda kurudia malengo na mipango ya maisha yako na hakikisha inalingana na mpango mkuu wa furaha wa Baba yetu wa Mbinguni kwa ajili ya furaha yetu. Kama unahitaji kutubu na kubadilika, basi zingatia kufanya hivyo sasa. Chukua muda kutafakari kwa maombi kuhusu marekebisho yanayohitajika kukusaidia “jicho lako kuwa kwenye utukufu wa Mungu.”11

Lazima tuyaweke mafundisho na injili ya Yesu Kristo kuwa kitovu cha malengo na mipango yetu. Pasipo Yeye, hakuna lengo la milele linalowezekana, na mipango yetu ya kupata malengo yetu ya milele hakika haitafanikiwa.

Picha
Hati ya “Kristo Aliye Hai”

Msaada mwingine wa ziada ni “Kristo Aliye Hai: Ushuhuda wa Mitume,”12 ambao ulitolewa kwa Kanisa Januari 1, 2000. Iweke nakala mahali unapoweza kuiona, na chukua muda kupitia kila sentensi iliyopo katika ushuhuda huu wenye mwongozo wa kiungu juu ya Kristo kupitia mashahidi Wake maalum walio weka saini.

Picha
“Kristo Aliye Hai” na tangazo la familia

Ningeliwaomba musome pamoja na “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu.” Tunazungumza mara nyingi kuhusu tangazo la familia, lakini kumbuka kulisoma kwa kuzingatia uwezo wa wokovu wa Kristo Aliye Hai. Pasipo Kristo Aliye Hai, matarajio yetu tunayoyapenda mno hayatatimilika. Kama vile tangazo la familia linavyosema: Mpango mtakatifu wa furaha unawezesha uhusiano wa familia kuendelezwa zaidi ya kaburi. Ibada na maagano matakatifu yaliyopo katika mahekalu matakatifu hutuwezesha kurudi katika uwepo wa Mungu na kwa familia kuungana milele.”13

Hii inaweza kutokea tu kwa sababu Kristo Aliye Hai ni Mwokozi Aliye lipia dhambi na Mkombozi wa Ulimwengu.

Katika mtazamo huu, unaweza pia kuamua kupekua maandiko ili kupanua uelewa wako wa kweli mahususi katika “Kristo Aliye Hai.”

Kusoma kwa maombi “Kristo Aliye Hai” ni kama kusoma ushuhuda wa Mathayo, Marko, Luka, Yohana, na manabii wa Kitabu cha Mormoni. Itaongezea imani yako katika Mwokozi na kukusaidia kumtazama Yeye unapofuatilia mipango yako ili kufikia malengo yako ya milele.

Mbali na makosa yetu, mapungufu, mizunguko, na dhambi, Upatanisho wa Yesu Kristo hutuwezesha kutubu, kujiandaa kurudi na kupokea baraka zisizo na kipimo alizoahidi Mungu—kuishi milele na Baba na Mwana katika daraja kuu la ufalme wa selestia.14

Sasa kama wote mnavyojua, hakuna atakaye kimbia kifo; kwa hiyo, lengo letu la muda mrefu na mpango unapaswa uwe kwamba tunaporudi kwa Baba yetu wa Mbinguni, tutapokea “vyote Alivyopanga” kwa kila mmoja wetu.15

Nashuhudia hakuna lengo kubwa katika maisha kuliko kuishi milele pamoja na Wazazi wetu wa Mbinguni na Mwokozi mpendwa, Bwana Yesu Kristo. Lakini ni zaidi ya lengo letu—pia ni lengo Lao. Wana upendo mkamilifu kwetu, wenye uwezo zaidi hata tunavyoweza kuelewa. Wao kiujumla, kabisa, milele wako pamoja nasi. Sisi ni kazi Yao. Utukufu wetu ni utukufu Wao. Zaidi ya kitu chochote, Wanatuhitaji turudi nyumbani— turudi na tupokee furaha ya milele katika uwepo Wao.

Kaka zangu na dada zangu, wiki moja ijayo, tutasherehekea Jumapili ya Matawi—tukikumbuka kuingia Kwake kwa ushindi katika Yerusalemu. Katika wiki mbili zijazo, tutasherehekea Jumapili ya Pasaka—tukikumbuka ushindi wa Mwokozi dhidi ya mauti.

Tunapoweka mtazamo wetu kwa Mwokozi wakati wa Jumapili hizi muhimu, hebu tumkumbuke Yeye na kuamsha sharti letu la maisha yote la kushika amri Zake. Hebu tuangalie ndani kabisa katika maisha yetu binafsi, tukiweka mipango yetu binafsi na kuelekeza mipango yetu kulingana na njia ya Mungu ambayo itatupeleka kwenye fursa yetu ya thamani ya kurudi na kupokea—ambayo ndiyo sala yangu katika jina la Yesu Kristo, amina.