2010–2019
Ili Nuru Yetu na Ipate Kuwa Bendera kwa Mataifa
Aprili 2017


Ili Nuru Yetu na Ipate Kuwa Bendera kwa Mataifa

Injili ya Mwokozi na Kanisa Lake la urejesho hutupa fursa nyingi kwa nuru yetu kuwa sehemu ya bendera kuu kwa mataifa.

Miaka mingi iliyopita, nikihudumu kama mwalimu wa seminari, nilisikia mmoja wa wafanyakazi wenzangu akiwauliza wanafunzi wake kutafakari juu ya swali lifuatalo: Kama ungeliishi katika siku za Mwokozi, kwa nini unafikiri kwamba ungemfuata kama mmoja wa wafuasi Wake? Walifika hitimisho kwamba wale wanaomfuata Mwokozi siku ya leo na kujitajidi kuwa wafuasi Wake pengine pia wangeweza kufanya hivyo wakati huo wa kale.

Tangu wakati huo, nimewaza juu ya swali hilo na hitimisho lao. Mara nyingi nashangaa jinsi ambavyo ningejisikia kumsikia Mwokozi Mwenyewe aliposema yafuatayo katika Mahubiri ya Mlimani:

“Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima.

“Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani.

“Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.”(Mathayo 5:14–16).

Je, unaweza kufikiria jinsi ambavyo ungejisikia kama ungeisikia sauti ya Mwokozi? Hakika, hatupaswi kufikiria. Imekuwa ni tukio la mara kwa mara kwetu sisi kusikia sauti ya Bwana kwa sababu tunaposikia sauti ya watumishi Wake, ni sawa sawa na Yake.

Katika mwaka 1838, sawa na ujumbe uliotolewa katika Hotuba ya Mlimani, Bwana alitangaza yafuatayo kupitia kwa Nabii Joseph Smith:

“Kwani hivyo ndivyo kanisa langu litakavyoitwa katika siku za mwisho, hata Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

“Amini ninawaambia ninyi nyote: Inukeni na mn’gare, ili nuru yenu ipate kuwa bendera kwa ajili ya mataifa” (M&M 115:4–5).

Siku zetu ni siku za kipekee kiasi kwamba zilionyeshwa hata katika maono ya nabii Isaya; yeye pia aliona na kutabiri siku hii ya Urejesho wa Kanisa la Yesu Kristo na madhumuni yake, akisema, “Naye atawatwekea mataifa bendera, atawakutanisha watu wa Israeli waliotupwa, atawakusanya watu wa Yuda waliotawanyika, kutoka ncha nne za dunia” (Isaya 11:12).

Katika muktadha wa kimaandiko, bendera, au alama, ni bendera ambayo itawafanya watu wakusanyike katika umoja wa kusudi. Katika nyakati za kale, bendera iliashiria mahali pa kukusanyika kwa wanajeshi katika vita. Tukizungumza kiishara, Kitabu cha Mormoni na Kanisa Lililorejeshwa la Yesu Kristo ni bendera kwa mataifa yote. Ona Guide to the Scriptures, “Ensign,” scriptures.lds.org.

Bila shaka, mojawapo ya bendera kubwa ya siku hizi za mwisho ni huu mkutano mkubwa wa ajabu, ambapo kazi kubwa na mpango wa Baba yetu wa Mbinguni wa “kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu” (Musa 1:39) inaendelea kutangazwa.

Kuendelea kufanya mkutano mkuu ni mojawapo ya shuhuda kubwa juu ya ukweli kwamba sisi kama Watakatifu wa Siku za Mwisho “tunaamini yale yote Mungu ameyafunua, na ambayo sasa anayafunua, na tunaamini kwamba bado Yeye atayafunua mambo mengi makuu na muhimu yahusuyo Ufalme wa Mungu” (Makala ya Imani 1:9).

Hivyo basi, ni nini Bwana amekifunua kupitia kwa Rais Thomas S. Monson ambacho tunahitaji kuendelea kufanya ili nuru yetu iweze kuwa bendera kwa mataifa? Je, ni baadhi ya mambo gani muhimu yanayopaswa kufanywa wakati huu angavu wa kujenga Sayuni na wa kuwakusanya Israeli?

Bwana daima amefunua mapenzi Yake kwetu “mstari juu ya mstari, amri juu ya amri, hapa kidogo na pale kidogo” (2 Nefi 28:30). Kwa hiyo, hatupaswi kushangaa kwa kile kinachoweza kuonekana kama mambo madogo kwa sababu ya asili yake rahisi na inayojirudia, kwa kuwa Bwana tayari ametushauri, Akituambia kwamba “heri wale wanaosikiza kanuni zangu, na kutii mashauri yangu, kwani watasoma hekima; kwani kwa yule atakayepokea nitampatia zaidi”.(2 Nefi 28:30).

Nashuhudia kuwa kupitia kwa “mstari juu ya mstari, amri juu ya amri, hapa kidogo na pale kidogo” na kwa kusikiliza mashauri ya viongozi wetu, tutakuwa na mafuta kwa ajili ya taa zetu yatakayotuwezesha kutoa nuru kwa wengine kama vile Bwana alivyotuagiza sisi.

Wakati kuna mambo mengi tunayoweza kufanya, ili kuwa nuru na mfano kwa  wengine, mimi ningependa kuzingatia mambo matatu: kuishika siku ya Sabato; kuharakisha kazi ya wokovu pande zote za pazia; na kufundisha kwa njia ya Mwokozi.

Nuru ambayo tunazungumzia inatokana na bidii tunayofanya katika kuishika siku ya Sabato, Kanisani na pia nyumbani; ni nuru inayokua tunapojiweka bila mawaa kutokana na ulimwengu; ni nuru inayotokana na kutoa sakramenti zetu siku Yake takatifu na kwa kufanya ibada zetu kwa Yule aliye juu sana, yote ambavyo yanatuwezesha daima kuwa na Roho Wake pamoja nasi. Ni ile nuru ambayo inakua na inakuja kuonekana wakati tunaporudi nyumbani tukiwa na hisia za msamaha ambazo Rais Henry B. Eyring alizungumza kuzihusu katika mkutano mkuu wa Oktoba iliyopita ambapo alisema: “Kati ya baraka zote tunazoweza kuhesabu, kuu zaidi kati yazo ni hisia za msamaha ambao huja tunapopokea sakramenti. Tutasikia upendo mkubwa na shukrani kwa ajili ya Mwokozi, ambaye dhabihu Yake kuu iliwezesha kusafishwa Kwetu kutokana na dhambi” (“Gratitude on the Sabbath Day, Liahona, Nov. 2016, 100).

Tunapoishika kitakatifu siku ya Sabato na kushiriki sakramenti, hatusafishwi tu, lakini pia nuru yetu pia inaang’aza zaidi.

Nuru yetu pia inakua tunapotenga na kuweka wakfu wakati wa kutafuta majina ya mababu zetu, kupeleka majina yao hekaluni, na kuwafundisha familia zetu na wengine kufanya hivyo.

Kazi hii takatifu ya hekalu na historia ya familia ambayo tunashiriki na Watakatifu pande zote mbili za pazia inasonga mbele zaidi kuliko hapo awali kadri mahekalu ya Bwana yanavyojengwa. Sasa vile mahekalu yana ratiba maalum kwa ajili ya makundi ya familia zinazokuja na kadi za majina ya familia zao, mke wangu na mimi tumekuwa na uzoefu wa kupendeza kwa kuwa tumehudumu hekaluni pamoja na watoto wetu na wajukuu wetu.

Tunapopata na kupeleka majina hekaluni na kuwafundisha wengine jinsi wapasavyo, tunang’ara kama bendera.

Kujifunza kufundisha jinsi Mwokozi alivyofundisha ni njia nyingine ambayo tunaweza kuinuka na kuangaza. Nafurahi pamoja na kila mtu ambaye anajifunza jinsi ya kufundisha kwa njia ya Mwokozi. Niruhusu nisome kutoka kwa jalada la mwongozo mpya wa mafundisho: “Lengo la kila mwalimu wa injili—kila mzazi, kila mwalimu aliyeitwa rasmi, kila mwalimu wa mafundisho ya nyumbani na mwalimu wa utembeleaji, na kila mfuasi wa Kristo—ni kufundisha mafundisho safi ya injili kwa njia ya Roho, … ili kuwasaidia watoto wa Mungu kujenga imani yao kwa Mwokozi na kuwa zaidi kama Yeye” (Kufundisha katika Njia ya Mwokozi [2016]).

Sasa hivi, maelfu ya walimu wetu waaminifu wanashikilia juu nuru wanapojifunza jinsi ya kufundisha katika njia ya Mwokozi. Katika muktadha huu, mkutano mpya wa baraza la waalimu ni njia ya kuinuka na kuangara wakati wanafunzi wanapokutana kwa mzunguko wa bendera ya mafundisho ya Kristo, kwani “msingi wa mafundisho jinsi Mwokozi alivyofundisha ni kuishi jinsi Mwokozi alivyoishi” (Kufundisha katika Njia ya Mwokozi, 4).

Tunavyofundisha na kujifunza katika njia Yake na kuwa zaidi kama Yeye, nuru yetu inang’ara zaidi na haiwezi kufichwa na inakuwa bendera kwa wale ambao wanatamani nuru ya Mwokozi.

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, hatupaswi na haifai kuficha nuru yetu. Mwokozi wetu alituamuru kuacha nuru yetu ing’are kama mji ulio juu ya mlima au kama nuru itokayo kwenye mshumaa uwakao. Tunapofanya hivyo, tunamtukuza Baba yetu aliye Mbinguni. Injili ya Mwokozi na Kanisa Lake la urejesho hutupa fursa nyingi kwa nuru yetu kuwa sehemu ya bendera kuu kwa mataifa.

Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ni nuru ambayo tunapaswa kuiakisi, katika jina la Yesu Kristo, amina.