2010–2019
Hamu ya Nyumbani
Oktoba 2017


Hamu ya Nyumbani

Geuza nafsi yako kuelekea nuruni.Anza safari yako mwenyewe kwenda nyumbani. Ukiwa unafanya hivyo, maisha yako yatakuwa mazuri, ya furaha, na yenye malengo.

Karibuni, tulipokutana na Rais Thomas S. Monson, alionyesha, kwa tahadhima kuu na uso wa furaha, jinsi anavyompenda Bwana na kuwa anajua kwamba Bwana anampenda. Kaka na dada zangu wapendwa, najua kwamba Rais Monson ana shukrani sana kwa ajili ya upendo wenu, maombi yenu, kujitolea kwenu kwa Bwana na injili Yake kuu.

Bobbie Mbwa wa Ajabu

Karibu karne iliyopita, familia kutoka Oregon walikuwa kwenye mapumziko Indiana—zaidi ya maili 2,000 (3,200 km)—wakati walipompoteza mbwa wao mpendwa, Bobbie. Familia yenye majonzi walimtafuta mbwa kila mahala bila mafanikio. Bobbie hakuweza kupatikana.

Kwa moyo uliovunjika, wakarudi nyumbani, kila maili iliwafanya wawe mbali zaidi na mnyama wao waliyempenda.

Miezi sita baadaye, familia ilishangazwa kumwona Bobbie kwenye ngazi ya mlango wao huko Oregon. “Akiwa mchovu, amekonda, miguu imechimbika hadi kwenye mifupa—[alionekana] alikuwa ametembea umbali wote … peke yake.”1 Hadithi ya Bobbie imeteka mawazo ya watu wengi Marekani, na akajulikana kama Bobbie Mbwa wa Ajabu.

Bobbie siyo mnyama pekee aliyewashangaza wanasayansi kwa hisia za ajabu za kuongoza na kurudi nyumbani. Baadhi makundi ya vipepeo monaki wanahama kwenda maili 3,000 (4,800 km) kila mwaka kwenye mazingira mazuri yanayofaa kwa kuishi. Kobe wenye ngozi kwa juu husafiri kuvuka Bahari ya Pasifiki kutoka Indonesia hadi pwani ya California. Nyangumi wenye kibyongo wanaogelea katika maji baridi ya Ncha ya Kaskazini na Kusini kuelekea ikweta na kurudi. Labda hata zaidi ya kushangaza, membe ya akitiki huruka kutoka Duara ya Akitiki hadi Antaktika na kurudi kila mwaka, maili 60,000 (97,000 km).

Wakati wanasayansi wanajifunza tabia hii ya kuvutia, wanauliza maswali kama vile “Ni kwa insi gani wanajua wapi pa kwenda?” na “Ni kwa jinsi gani kila kizazi kinajifunza tabia hii?”

Wakati ninaposoma jambo hili lenye nguvu kwa wanyama, siwezi kukosa kujizuia kushangaa, “Hivi inawezekana kwamba wanadamu wana tamaa inayofanana na hii—mfumo wa ulinzi wa ndani, kama ukipenda—ambayo huwavuta nyumbani mbinguni?”

Ninaamini kwamba kila mwanaume, mwanamke, na mtoto amehisi wito wa mbinguni wakati fulani katika maisha yake. Ndani yetu kuna hamu ya kufika nyuma ya pazia na kuwakumbatia Wazazi wa Mbinguni ambao mwanzo tuliwajua na kuwapenda.

Wengine wanaweza kuzima hamu hii na kuua nafsi zao kwa wito wake. Lakini wale ambao hawazimi mwanga huu ndani yao wanaweza kuanza safari ya ajabu—uhamiaji wa ajabu kuelekea mbinguni.

Wito wa Mungu Kwako

Ujumbe mzuri wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni kwamba Mungu ni Baba yetu, kwamba anatujali, na kwamba kuna njia ya kurudi Kwake.

Wito wa Mungu kwako

Mungu anajua kila wazo lako, huzuni yako, na matumaini yako makubwa. Mungu anajua mara zote ulizomfikiria Yeye. Mara zote ulizohisi furaha isiyo na kikomo. Mara zote ulizolia katika upweke. Mara zote ulizohisi huna msaada, umechanganyikiwa, au mwenye hasira.

Hata hivyo, bila kujali historia yako—kama umejikwaa, umeshindwa, ukahisi kuvunjika moyo, machungu, kusalitiwa, au kupigwa—jua kwamba haupo peke yako. Mungu bado anakuita.

Mwokozi ananyosha mkono Wake kwako. Na, kama alivyofanya kwa wale wavuvi waliosimama kando ya bahari ya Galilaya hapo kale, kwa upendo usio na mwisho Anaongea nawe: “Njoo unifuate.”2

Kama utamsikiliza Yeye, Ataongea nawe siku hii ya leo.

Unapotembea katika njia ya ufuasi—unapoelekea kwa Baba wa Mbinguni—kuna kitu ndani yako ambacho kitadhihirisha kwamba umesikia wito wa Mwokozi na kuuelekeza moyo wako nuruni. Kitakuambia kwamba upo katika njia sahihi, na kwamba unarudi nyumbani.

Toka mwanzo wa nyakati, manabii wa Mungu wamewahimiza watu wa siku zao “kutaifuata sauti ya Bwana, Mungu wako, … kwa kuyashika maagizo yake, na amri zake, … [na] ukimwelekea [Yeye], kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote.”3

Maandiko yanatufundisha sisi maelfu ya sababu kwa nini tunatakiwa kufanya hivi.

Leo, naomba nitoe sababu mbili za kwa nini tunatakiwa kumgeukia Bwana.

Kwanza, maisha yako yatakuwa mazuri.

Pili, Mungu atakutumia wewe kuyafanya maisha ya wengine kuwa mazuri.

Maisha Yako Yatakuwa Mazuri

Ninashuhudia kwamba tunapoanza au kuendelea na safari ya ajabu inayoongoza kwa Mungu, maisha yetu yatakuwa mazuri zaidi.

Hii haimanishi kwamba maisha yetu hayatakuwa na huzuni. Wote tunawajua wafuasi wema wa Kristo walioteseka na kukosa haki—Yesu Kristo Mwenyewe aliteseka zaidi ya yeyote. Kama vile Mungu hufanya “jua lake lichomoze kwa waovu na wema,” Yeye pia anaruhusu mateso kuwajaribu wenye haki na wasio na haki.4 Hakika, wakati mwingine inaonekana kwamba maisha yetu ni magumu zaidikwa sababu tunajaribu kushikilia imani yetu.

Hapana, kumfuata Mwokozi hakutaondoa majaribu yote. Badala yake, kutaondoa vizuizi kati yako na msaada ambao Baba yako wa Mbinguni anataka kukupa. Mungu, atakuwa pamoja nawe Ataongoza hatua zako. Atatembea kando yako na hata kukubeba wakati mahitaji yako ni makubwa.

Utapata matunda mazuri ya Roho: “upendo, furaha, amani, uvumilivu, upole, wema, [na] imani.”5

Matunda haya ya kiroho si matokeo ya maisha ya kimwili, mafanikio, au bahati. Yanakuja kwa kumfuata Mwokozi, na yanaweza kuwa watumishi wetu waaminifu hata katikati ya dhoruba kali.

Moto na ghasia za maisha ya kifo huweza kutishia na kuogopesha, lakini wale wanaoelekeza mioyo yao kwa Mungu watazungukwa na amani Yake. Furaha yao haitapuzwa. Hawatatelekezwa au kusahaulika.

“Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote;” maandiko yanafundisha, “wala usizitegemee akili zako mwenyewe. Katika njia zako zote mtambue Yeye, naye atayaongoza mapito yako.”6

Wale wanaotii wito wa ndani na kumtafuta Mungu, wale wanaoomba, wanoamini, na kutembea njia Mwokozi ameandaa—hata kama pia wanaanguka katika njia hiyo wakati mwingine—wanapata uhakikisho kwamba “vitu vyote vitafanyakazi pamoja kwa ajili ya wao.”7

Kwani Mungu“huwapa nguvu wachovu na kuwaongezea uwezo wadhaifu.”8

“Kwa maana mwenye haki huanguka mara saba akaondoka tena.”9

Na Bwana katika uzuri Wake anauliza:

Je, unatamani kupokea shangwe ya kudumu?

Je, unatamani kuhisi ndani ya moyo wako amani ambayo ipitayo akili zote?10

Basi igeuze nafsi yako kuelekea nuruni.

Anza safari yako mwenyewe kwenda nyumbani.

Ukiwa unafanya hivyo, maisha yako yatakuwa mazuri, ya furaha, na yenye malengo.

Mungu Atakutumia Wewe

Katika safari yako ya kurudi kwa Baba wa Mbinguni punde utagundua kwamba safari hii siyo tu kuzingatia maisha yako mwenyewe. Hapana, njia hii isiyoepukika inakuongoza wewe kuwa baraka katika maisha ya watoto wengine wa Mungu—ndugu zako na dada zako. Na kitu cha kushangaza kuhusu safari ni kwamba unapomtumikia Mungu, na unapowajali na kuwasaidia wenzako, utaona mafanikio makubwa katika maisha yako mwenyewe, kwa njia ambazo huwezi kuamini kamwe.

Huenda hujifikirii kama una thamani; huenda hufikirii kuwa wewe ni baraka katika maisha ya mwingine.Mara nyingi, tunapojitazama wenyewe, tunaona udhaifu na mapungufu yetu. Tunaweza kufikiri tunahitaji kuwa “zaidi” ya kitu fulani ili Mungu atutumie—kuwa na akili zaidi, tajiri zaidi, haiba kubwa, kipaji zaidi, kiroho zaidi.Baraka zitakuja siyo kwa wingi kwa sababu ya uwezo wako bali ni kwa sababu ya chaguzi zako. Na Mungu wa ulimwengu atafanya kazi ndani na kupitia wewe, akiinua juhudi zako za unyenyekevu kwa madhumuni Yake.

Kazi yake mara zote imeendelea juu ya kanuni hii muhimu: “Na kutokana na mambo madogo huja yale yaliyo makuu.”11

Akiwaandikia Watakatifu wa Korintho, Paulo aliona kwamba siyo wengi wao watakaofikiriwa kuwa wenye busara kwa vipimo vya duniani. Lakini hiyo haikujalisha, kwa sababu “Mungu amechagua vitu dhaifu vya dunia ili kuharibu vitu vyenye nguvu.”12

Historia ya kazi ya Mungu imejaa watu wanaojidhania wenyewe kuwa hawafai. Lakini wanatumikia kwa unyenyekevu, wakitegemea neema ya Mungu na ahadi Yake: “Na mkono wao utakuwa mkono wangu, na nitakuwa ngao yao … , watapigana kiume kwa ajili yangu; na … nitawalinda.”13

Majira ya kiangazi yaliyopita familia yetu ilipata nafasi ajabu ya kutembelea sehemu za mwanzo za historia ya Kanisa mashariki mwa Marekani.Kwa njia ya maalumu, tuliishi tena historia ya wakati huo. Watu niliosoma sana kuwahusu—watu kama Martin Harris, Oliver Cowdery, na Thomas B. Marsh—wakawa halisi zaidi kwangu tukiwa tunatembea mle walimotembea na kutafakari dhabihu walizozitoa ili kujenga ufalme wa Mungu.

Walikuwa na sifa nyingi nzuri ambazo ziliwawezesha kufanya michango muhimu kwenye Urejesho wa Kanisa la Yesu Kristo. Lakini pia walikuwa binadamu, wanyonge, na wadhaifu—kama wewe na mimi tu. Wengine walijikuta kinyume na Nabii Joseph Smith na wakaanguka na kutoka Kanisani. Baadaye, wengi wa watu walewale walibadili mioyo yao, wakajinyenyekeza, na kwa mara nyingine wakaomba na kupata ushiriki pamoja na watakatifu.

Tunaweza kuwa na tabia ya kuwahukumu ndugu hawa na waumini kama wao. Tunaweza kusema, “Nisingeweza kamwe kumwacha Nabii Joseph.”

Hali hiyo inaweza kuwa ni kweli, hatujui ilikuwa vipi kuishi katika nyakati zile, katika hali hizo. Hapana, hawakuwa wakamilifu, lakini inatia moyo kiasi gani kujua kwamba Mungu aliweza kuwatumia wao. Alijua uwezo na udhaifu wao, na aliwapa nafasi ya ajabu ya kuchangia mstari au melodi kwenye wimbo wa Urejesho.

Inatia moyo kiasi gani kujua, japo sisi siyo wakamilifu, kama mioyo yetu itamgeukia Mungu, atakuwa mwenye ukarimu na mwenye neema na kututumia kwa makusudi Yake.

Wale wanaompenda na kumtumikia Mungu na wengine, na kwa upole na kushiriki kikamilifu katika kazi Yake, wataona mambo ya ajabu yakitokea katika maisha yao na wale wanaowapenda.

Milango inayoonekana kufungwa itafunguliwa.

Malaika wataenda mbele zao kutayarisha njia.

Bila kujali nafasi yako katika jamii au, katika Kanisa, Mungu atakutumia kama u tayari. Atakuza tamaa zako za haki na kugeuza matendo ya fadhila uliyoyapanda kuwa mavuno tele ya wema.

Hatuwezi Kufika Kule Bila Rubani

Sisi, kila mmoja wetu,“ni mgeni na hujaji”14 katika ulimwengu huu. Katika njia nyingi, tupo mbali na nyumbani. Lakini hilo halimaanishi tunatakiwa kuhisi tumepotea au wapweke.

Baba yetu wa Mbinguni mpendwa ametupa nuru ya Kristo. Na ndani ya kila mmoja wetu, kichochea cha mbinguni kinatuhimiza kugeuza macho na mioyo yetu kumwelekea Yeye tunapofanya safari ya kurudi kwenye mji wetu wa selestia.

Hii inahitaji juhudi. Huwezi kufika kule bila ya kujitahidi kujifunza kuhusu Yeye, kuelewa miongozo Yake, kuifanyia kazi kwa bidii, na kuweka mguu mmoja mbele ya mwingine.

Hapana, maisha si kama gari linayojiendesha lenyewe. Siyo ndege inayojiongoza bila rubani kufanya chochote.

Huwezi tu kuelea juu ya maji ya maisha na kuamini kwamba mkondo utakuchukua kwenda utakako siku moja.Uanafunzi unahitaji hiari yetu ya kuogelea dhidi ya mkondo inapohitajika.

Hakuna anayewajibika kwa safari yako binafsi. Mwokozi atakusaidia wewe na kukuandalia njia, lakini kujituma kumfuata Yeye na kutii amri kutokane na wewe. Huo ndio mzigo wako, nafasi yako pekee.

Hili ni tukio lako kubwa.

Tafadhali tii wito wa Mwokozi wako.

Mfuate Yeye.

Bwana ameanzisha Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ili kusaidia katika sharti la kumtumikia Mungu na wanadamu wenzetu. Lengo lake ni kuhimiza, kufundisha, kuinua, na kuhuisha. Hili Kanisa la ajabu hutoa nafasi za kuonyesha huruma, kuwafikia wengine, na kuyafanya upya na kuyashika maagano matakatifu. Limewekwa ili kubariki maisha yako na kuimarisha nyumba yako, jamii, na taifa lako.

Njoo, ungana nasi na mwamini Bwana. Onyesha talanta zako katika kazi Yake ya ajabu. Wafikie, wahimize, waponye, na waunge mkono wote wanaotaka kujisikia na kuitii hamu ya nyumba yetu ya juu. Acheni tuungane pamoja katika safari hii ya utukufu kwenda kwenye hali ya mbinguni.

Injili ni ujumbe wa matumaini, furaha na shangwe. Ni njia ambayo inaturudisha nyumbani.

Tunapokumbatia injili kwa imani na vitendo, kila siku na kila saa, tutajongea karibu na Mungu wetu. Maisha yetu yatakuwa mazuri, na Bwana atatutumia sisi kwa njia za ajabu kuwabariki wale wanaotuzunguka na kuleta malengo ya milele. Juu ya haya nashuhudia na kuwaachieni baraka zangu katika jina la Yesu Kristo, amina.