2010–2019
Usiogope kutenda Mema
Oktoba 2017


Usiogope Kutenda Mema

Bwana anatuambia kwamba tunaposimama kwa imani katika mwamba Wake, shaka na uoga hupungua; hamu ya kufanya mema huongezeka.

Kaka na dada zangu, ninaomba kwa unyenyekevu kwamba Roho wa Bwana atakuwa nasi ninapoongea leo. Moyo wangu umejaa shukrani kwa Bwana, ambaye hili ni Kanisa Lake, kwa msukumo tuliosikia katika sala za dhati, mahubiri yenye mwongozo, na kuimba kama malaika katika mkutano huu.

Aprili iliyopita, Rais Thomas S. Monson alitoa ujumbe ambao ulichochea mioyo duniani kote, ikiwa ni pamoja na wangu. Aliongelea kuhusu uwezo wa Kitabu cha Mormoni. Alituhimiza kujifunza, kutafakari, na kutumia mafundisho yake. Aliahidi kuwa ikiwa tungetoa wakati wetu kila siku kusoma na kutafakari na kuzingatia amri zilizopo katika Kitabu cha Mormoni, tungeweza kuwa na ushuhuda muhimu wa ukweli wake, na ushuhuda wa kudhihirika wa Kristo aliye hai ungetupitisha hadi katika usalama wakati wa shida. (Ona “Nguvu ya Kitabu cha Mormoni,” Liahona, May 2017, 86 -87.)

Kama wengi wenu, nilisikia maneno ya Nabii kama sauti ya Bwana kwangu. Na, pia kama wengi wenu, niliamua kutii hayo maneno. Sasa, tangu nilipokuwa mvulana mdogo, nimehisi ushahidi kwamba Kitabu cha Mormoni ni neno la Mungu, kwamba Baba na Mwana walimtokea na kuongea na Joseph Smith, na kwamba Mitume wa kale walimjia Nabii Joseph kurejesha funguo za ukuhani katika Kanisa la Bwana.

Kwa ushuhuda huo, nimesoma Kitabu cha Mormoni kila siku kwa zaidi ya miaka 50. Kwa hiyo labda ningeweza kufikiri kimantiki kwamba maneno ya Rais Monson yalikuwa kwa mtu mwingine. Hata hivyo, kama wengi wenu, nilihisi hamasa ya nabii na ahadi yake ikinialika kufanya bidii zaidi. Wengi wenu mmefanya kile nilichofanya: kuomba kwa nia iliyoongezeka, mmetafakari maandiko kwa makini zaidi, na kujitahidi kwa bidii kumtumikia Bwana na wengine kwa ajili Yake.

Tokeo la furaha kwangu, na kwa wengi wenu, limekuwa kile nabii aliahidi. Wale wetu ambao walichukua ushauri wake wa mwongozo wamehisi Roho kwa udhahiri zaidi. Tumepata uwezo mkubwakushinda majaribu na kuhisi imani kuu katika Yesu Kristo aliyefufuka, Injili Yake, na Kanisa Lake lililo hai.

Katika msimu wa kuongezeka kwa machafuko ulimwenguni, ongezeko hilo katika ushuhuda limefukuza shaka na hofu na kutuletea hisia za amani. Kusikiliza ushauri wa Rais Monson kumekuwa na matokeo mawili ya ajabu kwangu: Kwanza, Roho aliyeahidi amezalisha hisia ya matumaini kuhusu kile kilichoko mbele, hata kama vurugu ulimwenguni inaonekana kuongezeka. Na, pili, Bwana amenipa mimi—na wewe—hisia kubwa zaidi ya upendo Wake kwa wale walio katika dhiki. Tumehisi ongezeko la hamu ya kwenda kwa uokoaji wa wengine. Tamaa hiyo imekuwa katika kitovu cha huduma na mafundisho ya Rais Monson.

Bwana aliahidi upendo kwa wengine na ujasiri kwa Nabii Joseph Smith na Oliver Cowdery wakati kazi mbele yao ingekuwa imeonekana kuwashinda kabisa. Bwana alisema kwamba ujasiri unaohitajika unatoka kwa imani yao ndani Yake kama mwamba wao:

“Msiogope kufanya mema, wana wangu, kwani chochote unachopanda, ndicho pia wewe utakacho kivuna; kwa hiyo kama utapanda mema pia utavuna mema kwa thawabu zenu.

“Kwa sababu hiyo, msiogope, enyi kundi dogo; tendeni mema; acha dunia na jahanamu ziungane dhidi yenu, kwani kama mmejengwa juu ya mwamba wangu, haziwezi kuwashinda.

“Tazama, siwahukumu ninyi; nendeni zenu na msitende dhambi tena; fanyeni kwa utaratibu kazi ambayo nimewaamuru.

“Nitegemeeni katika kila wazo; msitie shaka, msiogope.

“Tazama majeraha yaliyoko yaliotobolewa ubavuni mwangu, na pia alama za misumari katika mikono na miguu yangu; kuweni waaminifu, zishikeni amri zangu, na mtaurithi ufalme wa mbinguni” (M&M 6:33–37).

Bwana aliwaambia viongozi Wake juu ya Urejesho, na Anatuambia sisi, kwamba tunaposimama kwa imani katika mwamba Wake, shaka na uoga hupungua; hamu ya kufanya mema huongezeka. Tunapokubali mwaliko wa Rais Monson wa kupanda katika mioyo yetu ushuhuda wa Yesu Kristo, tunapata nguvu, hamu, na ujasiri wa kwenda kuwaokoa wengine bila kujali mahitaji yetu wenyewe.

Nimeona imani na ujasiri huo mara nyingi wakati Watakatifu wa Siku za Mwisho wanaoamini wamekabiliwa na majaribu ya kutisha. Kwa mfano, nilikuwa Idaho wakati bwawa la Teton lilipobomoka mnamo Juni 5, 1976. Ukuta wa maji ulianguka. Maelfu walikimbia kutoka kwenye nyumba zao. Maelfu ya biashara na nyumba zao ziliharibika. Kimiujiza, watu wachache chini ya 15 waliuawa.

Nilichoona huko, nimekiona kila wakati Watakatifu wa Siku za Mwisho wanaposimama imara juu ya mwamba wa ushuhuda wa Yesu Kristo. Kwa sababu hawana shaka Yeye anawalinda, wanakuwa hawana hofu. Wanakataa majaribu yao wenyewe kwenda kutoa msaada kwa wengine. Na wanafanya hivyo kwa kumpenda Bwana, pasipo kuomba malipo.

Kwa mfano, wakati Bwawa la Teton lilipobomoka, wanandoa wa Watakatifu wa Siku za Mwisho walikuwa safarini, maili nyingi mbali kutoka nyumbani kwao. Mara waliposikia habari katika redio, waliharakisha kurudi Rexburg. Badala ya kuenda nyumbani kwao kuona kama iliharibiwa, walienda kumtafuta Askofu wao. Alikuwa katika jengo ambalo lilikuwa linatumika kama kituo cha dharura. Alikuwa akisaidia kuongoza maelfu ya waliojitolea waliokuwa wakiwasili katika mabasi ya njano ya shule.

Wanandoa walienda hadi kwa askofu na kusema, “Tumerudi sasa hivi. Askofu, twende wapi kusaidia?” Aliwapatia majina ya familia. Wanandoa hao walikawia wakitoa matope na maji katika nyumba moja baada ya nyingine. Walifanya kazi tangu alfajiri hadi giza kwa siku kadhaa. Hatimaye walichukua mapumziko kwenda kuona nyumba yao wenyewe. Ilikuwa imesombwa na mafuriko, bila kuacha chochote. Kwa hiyo wakageuka haraka na kurudi kwa askofu wao. Wakamuuliza, “Askofu, una mtu ambaye tunaweza kumsaidia?”

Muujiza huo wa ujasiri na hisani tulivu—na upendo msafi wa Kristo—umerudiwa kwa miaka na ulimwenguni kote. Ilitokea katika siku za kutisha za mateso na majaribu wakati wa Nabii Joseph Smith huko Missouri. Ilitokea wakati Brigham Young aliongoza safari kutoka Nauvoo na kisha akawaita watakatifu kuacha maeneo yote ya magharibi mwa Marekani, ili kusaidiana kujenga Sayuni kwa ajili ya Bwana.

Ikiwa unasoma vitabu vya kumbukumbu vya waanzilishi hao, unaona muujiza wa imani unaondoa shaka na hofu. Na unasoma juu ya Watakatifu wakiacha maslahi yao wenyewe kumsaidia mtu mwingine kwa Bwana, kabla ya kurudi kwenye kondoo zao au kwa mashamba yao wenyewe ambayo hayajalimwa.

Niliona muujiza huo siku chache zilizopita baada ya kimbunga cha Irma huko Puerto Rico, Saint Thomas, na Florida, ambapo Watakatifu wa Siku za Mwisho waliungana na makanisa mengine, makundi ya jamii, na mashirika ya kitaifa ili kuanza juhudi za kusafisha.

Kama marafiki zangu huko Rexburg, wanandoa wasiokuwa waumini mjini Florida walizingatia kusaidia jamii badala ya kufanya kazi kwenye mali yao wenyewe. Wakati baadhi ya majirani wa Watakatifu wa Siku za Mwisho walipojitolea kusaidia kwa miti miwili mikubwa iliyokuwa ikizuia barabara yao, wanandoa walielezea kwamba walikuwa wameshindwa na hivyo waliamua kuwasaidia wengine, wakiwa na imani kwamba Bwana atatoa msaada waliohitaji nyumbani kwao.Mume kisha alishiriki haya kabla ya waumini wetu wa Kanisa kuwasili na matoleo ya misaada, waliokuwa wakiomba. Walikuwa wamepokea majibu kuwa msaada utakuja. Ulikuja ndani ya masaa ya uhakika huo.

Nimesikia kuhusu ripoti kwamba wengine wameanza kuwaita Watakatifu wa Siku za Mwisho wanaovalia Vesti za Helping Hands za rangi ya manjano “Malaika wa Manjano.” Mtakatifu mmoja wa siku za mwisho alipeleka gari lake kwa uangalizi wa kitaalamu, na bwana aliyekuwa akimhudumia alielezea “tukio la kiroho” alilohisi wakati watu waliovalia mashati ya manjano walipoondoa miti kutoka kwenye uga wake na kisha, alisema, “waliniimbia baadhi ya nyimbo kuhusu kuwa mtoto wa Mungu.”

Mkazi mwingine wa Florida—ambaye pia sio wa dini yetu—alielezea kwamba Watakatifu wa Siku za Mwisho walifika nyumbani kwake wakati alipokuwa akifanya kazi katika jengo lake lililoharibiwa na kujisikia kulemewa, kuchoshwa, na karibu kutoa machozi. Watu wa kujitolea walifanya, kwa maneno yake, “muujiza halisi.” Walihudumu si tu kwa bidii bali pia kwa kicheko na tabasamu, bila kukubali chochote kama malipo.

Niliona bidii hiyo na kusikia kicheko hicho wakati, Jumamosi moja jioni nilipotembelea kikundi cha Watakatifu wa Siku za Mwisho huko Florida. Watu wa kujitolea waliacha kazi zao za kusafisha kwa muda wa kutosha tu kuniruhusu kuwasalimia kwa mkono. Walisema kuwa waumini 90 wa kigingi chao huko Georgia walikuwa wameunda mpango wa kujiunga na uokoaji huko Florida tu usiku kabla ya kuondoka.

Kisha waliondoka nyumbani saa 10:00 asubuhi, wakaendesha kwa saa, wakafanya kazi usiku, na wakafanya kazi tena siku iliyofuata

Walinielezea yote kwa tabasamu na ucheshi mzuri. Dhiki tu niliyohisi ilikuwa kwamba walitaka kuacha kushukuriwa ili waweze kurudi kufanya kazi. Rais wa kigingi alikuwa ameanzisha tena msumeno wake wa minyororo na akaanza kazi kukata mti na askofu alikuwa akivuta matawi ya mti tulipoingia katika gari letu kuelekea kwenye timu nyingine ya uokoaji

Mapema siku hiyo, tulipoondoka kutoka sehemu nyingine, kuna mtu alikuja kwenye gari, akatoa kofia yake, na kutushukuru kwa waliojiolea. Alisema, “Mimi sio mshiriki wa kanisa lenu. Siwezi kuamini kile mlichotufanyia. Mungu awabariki.” Mtu wa kujitolea wa WSM akisimama kando yake akiwa na shati yake ya njano alitabasamu na kuinua mabega, kama kwamba hakutaka sifa.

Wakati watu wa kujitolea kutoka Georgia walipokuja kumsaidia mtu huyu ambaye hakuweza kuamini, mamia ya Watakatifu wa Siku za Mwisho kutoka sehemu hiyo iliyoharibiwa ya Florida walikuwa wamekwenda mamia ya maili kusini mahali pengine huko Florida ambapo walikuwa wamesikia watu walikuwa wamelemewa mno.

Siku hiyo, nilikumbuka, na kuelewa vyema, maneno ya kinabii ya Nabii Joseph Smith: “Mtu aliyejaa upendo wa Mungu, hatosheki na baraka za familia yake peke yake, lakini hupitia ulimwenguni pote, akijitahidi kubariki jamii yote ya binadamu” (Mafundisho ya Maraisi wa Kanisa:Joseph Smith[2007], 426).

Tunaona upendo kama huo katika maisha ya Watakatifu wa Siku za Mwisho kila mahali. Kila wakati kuna tukio la kutisha mahali popote ulimwenguni, Watakatifu wa Siku za Mwisho hutoa mchango na kujitolea katika jitihada za kibinadamu za Kanisa. Maombi hakika yanahitajika kwa nadra. Kwa kweli, wakati mwingine, tunapaswa kuuliza wale ambao wangejitolea kusubiri kusafiri kwenda kwenye kituo cha dharura mpaka wale wanaoongoza kazi wanapokuwa wamekwisha jiandaa kuwapokea.

Hamu hiyo ya kubariki ndilo tunda la watu wanaopata ushuhuda wa Yesu Kristo, Injili Yake, Kanisa Lake la urejesho, na Nabii Wake. Ndio maana watu wa Bwana hawana shaka wala hofu. Ndiyo sababu wamisionari wanajitolea kwa huduma katika kila kona ya dunia. Ndio sababu wazazi husali na watoto wao kwa ajili ya wengine. Hiyo ndiyo maana viongozi huwahimiza vijana wao kuchukua ombi la Rais Monson kujizamisha ndani ya Kitabu cha Mormoni moyoni. Tunda huja sio kwa kuhimizwa na viongozi lakini kwa vijana na waumini wakitenda kwa imani.Imani yao, iliyowekwa katika matendo, kupitia dhabihu, huleta mabadiliko ya moyo ambayo yanawawezesha kusikia upendo wa Mungu.

Mioyo yetu, hata hivyo, inabadilishwa tu almradi kama tutaendelea kufuata ushauri wa nabii. Ikiwa tunaacha kujaribu baada ya jitihada moja kubwa, mabadiliko yatafifia.

Watakatifu wa Siku za Mwisho waaminifu wameongeza imani yao katika Bwana Yesu Kristo, katika Kitabu cha Mormoni kama neno la Mungu, na katika kurejeshwa kwa ufunguo wa ukuhani katika Kanisa Lake la kweli. Ushuhuda huo ulioongezeka umetupa ujasiri mkubwa na kujali kwa watoto wengine wa Mungu. Lakini changamoto na fursa zijazo zitahitaji hata zaidi.

Hatuwezi kutambua maelezo, lakini tunajua picha kubwa. Tunajua kwamba katika siku za mwisho dunia itajawa na uovu. Tunajua kwamba katikati ya shida yoyote inayokuja, Bwana ataongoza Watakatifu wa Siku za Mwisho waaminifu kupeleka injili ya Yesu Kristo kwa kila taifa, jamaa, lugha, na watu. Na tunajua kwamba wafuasi wa kweli wa Bwana watastahili na kuwa tayari kumpokeaAtakapokuja tena. Hatuna haja kuogopa.

Kwa hiyo, kama vile tumejenga imani na ujasiri katika mioyo yetu, Bwana anatarajia zaidi kutoka kwetu—na kutokakwa vizazi baada yetu. Wao watahitaji kuwa na nguvu zaidi na wenye ujasiri kwa sababu watafanya mambo makubwa zaidi na magumu zaidi kuliko tuliyoyatenda. Na watakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa adui wa roho zetu.

Njia ya matumaini mema tunapoendelea mbele ilitolewa na Bwana: “Nitegemeeni katika kila wazo; msitie shaka, msiogope.” (M&M 6:36). Rais Monson alituambia jinsi ya kufanya hivyo. Tunapaswa kutafakari na kutumia Kitabu cha Mormoni na maneno ya manabii. Kusali daima. Kuendelea kuamini. Kumtumikia Bwana kwa moyo wetu wote, uwezo, akili, na nguvu. Tunapaswa kuomba kwa nguvu zote za mioyo yetu kwa ajili ya zawadi ya upendo, upendo msafi wa Kristo (ona Moroni 7:47–48). Na juu ya yote, tunapaswa kuwa thabiti na kuendelea katika kufuata ushauri wa nabii wetu.

Wakati njia ni ngumu, tunaweza kutegemea ahadi ya Bwana—ahadi ambayo Rais Monson ametukumbusha aliponukuu mara kwa mara maneno haya ya Mwokozi: “Na yeyote awapokeaye ninyi, hapo nitakuwepo pia, kwani nitakwenda mbele ya uso wenu. Nitakuwa mkono wenu wa kuume na wa kushoto, na Roho wangu atakuwa mioyoni mwenu, na malaika zangu watawazingira, ili kuwabeba juu” (M&M 84:88).

Ninashuhudia kuwa Bwana huenda mbele ya uso wako wakati wowote unapokuwa katika kazi Yake. Wakati mwingine utakuwa yule malaika Bwana humtuma kuwabeba wengine. Wakati mwingine utakuwa ndiye unayezungukwa na malaika ambao wanakubeba wewe juu. Lakini daima utakuwa na Roho Wake kuwa ndani ya moyo wako, kama ulivyoahidiwa katika kila ibada ya sakramenti. Tunahitaji tu kutii amri Zake.

Siku bora zipo mbele kwa ufalme wa Mungu duniani. Upinzani utaimarisha imani yetu katika Yesu Kristo, kama ilivyo kuwa tangu siku za Nabii Joseph Smith. Imani daima hushinda hofu. Kusimama pamoja huleta umoja. Na maombi yako kwa wale walio na mahitaji husikika na kujibiwa na Mungu mwenye upendo. Yeye halali wala kusinzia.

Ninatoa ushahidi wangu kwamba Mungu Baba yu hai na anataka wewe uje nyumbani Kwake. Hili ndilo Kanisa la kweli la Yesu Kristo. Anakujua; Anakupenda; Anakuangalia. Alifanya upatanisho kwa ajili ya dhambi zako na zangu na dhambi za watoto wote wa Baba wa Mbinguni. Kumfuata Yeye maishani mwako na kwa huduma yako kwa wengine ndio njia pekee ya uzima wa milele.

Ninashuhudia hivyo na kuwaachia baraka zangu na upendo wangu. Katika jina takatifula Yesu Kristo, amina.