2010–2019
Thamani bila kifani
Oktoba 2017


Thamani Isiyo na Kifani

Twaweza kila mara kufurahia mnong’ono mtamu wa Roho Mtakatifu, akithibitisha ukweli wa thamani yetu ya kiroho.

Nikiwa nazuru nchi ya Sierra Leone, Afrika Magharibi, nilishiriki katika mkutano ulioongozwa na kiongozi wa Msingi wa kigingi. Mariama aliongoza kwa upendo, madaha, na ujasiri kiasi cha kuamini ya kwamba alikuwa muumini wa Kanisa kwa muda mrefu. Mariama, hata hivyo, alikuwa mwongofu mpya sana wa Kanisa.

Picha
Mariama na bintiye

Dadake mdogo alijiunga na Kanisa na kumualika Mariama ahudhurie darasa la Kanisa pamoja naye. Mariama alivutiwa sana na ujumbe. Somo lilihusu sheria ya usafi wa kimwili. Aliomba afundishwe zaidi na wamisionari na punde alipokea ushuhuda kumhusu Nabii Joseph Smith. Alibatizwa mnamo 2014, na bintiye alibatizwa mwezi uliopita. Hebu fikiria, mafundisho mawili ya msingi ambayo yalichangia kuongoka kwa Mariama yalikuwa sheria ya usafi wa kimwili na Nabii Joseph Smith, hoja mbili ambazo dunia mara nyingi huona kama sio za maana, zimepitwa na wakati, au hazifai. Lakini Mariama alishuhudia kwamba alikuwa ni kama nondo aliyevutiwa na mwangaza. Alisema, “wakati nilipopata injili, nilijifahamu. Aligundua thamani yake kupitia kanuni takatifu. Thamani yake kama binti wa Mungu ilifunuliwa kwake kupitia Roho Mtakatifu.

Sasa hebu tukutane na kina dada wa Singh kutoka India. Renu, upande wa kulia kabisa, wa kwanza kati ya kina dada watano kujiunga na Kanisa, alishiriki mawazo haya:

Picha
Kina dada wa Singh

“Kabla ya kuanza kuchunguza Kanisa, sikuhisi ya kwamba nilikuwa maalum sana. Nilikuwa tu mmoja kati ya watu wengi, na jamii na utamaduni wangu kweli haikunifunza kwamba nilikuwa na thamani yoyote. Nilipojifunza injili na nikajifunza ya kwamba nilikuwa binti wa Baba wa Mbinguni, ilinibadili. Ghafla nilijihisi maalum—Mungu kwa kweli alikuwa ameniumba na kuumba nafsi yangu na maisha yangu kuwa yenye thamani na kusudi.

“Kabla ya kupokea injili maishani mwangu, daima nilikuwa nikijaribu kuwathibitishia wengine ya kwamba nilikuwa mtu maalum. Lakini nilipojifunza ukweli, kwamba mimi ni binti wa Mungu, sikuhitaji tena kuthibitisha chochote kwa mtu yeyote. Nilijua ya kwamba nilikuwa maalum. Kamwe usidhanie kwamba wewe si kitu.”

Rais Thomas S. Monson aliisema kikamilifu aliponukuu maneno haya: “Thamani ya nafsi ni uwezo wake wa kuwa kama Mungu.”1

Picha
Taiana

Nilibarikiwa hivi karibuni kukutana na msichana mwingine anayeelewa ukweli huu. Jina lake ni Taiana. Nilikutana naye kule Primary Children’s Hospital Jijini Salt Lake. Taiana alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika shule ya upili wakati alipobainiwa kuwa na saratani. Alipigana kwa ujasiri kwa miezi 18 kabla ya kuaga dunia wiki chache zilizopita. Taiana alikuwa amejawa na mwanga na upendo. Alijulikana kwa tabasamu lake la kuambukiza na ishara yake ya “vidole gumba viwili juu.” Wakati wengine walipouliza, “Kwa nini wewe, Taiana?” alijibu, “Kwa nini isiwe mimi?” Taiana alitafuta kuwa kama Mwokozi wake, ambaye alimpenda kwa dhati. Wakati wa matembezi yetu, nilielewa kwamba Taiana alielewa thamani yake. Kufahamu kwamba alikuwa binti wa Mungu kulimpa amani na ujasiri kupambana na majaribu yake ya kuangamiza kwa njia chanya kama alivyofanya.

Mariama, Renu, na Taiana wanatufundisha kwamba Roho atamthibitishia kila mmoja wetu binafsi thamani yetu takatifu. Kufahamu kwa hakika kwamba wewe ni binti wa Mungu kutaathiri kila sehemu ya maisha yako na kukuongoza katika huduma unayotoa kila siku. Rais Spencer W. Kimball alielezea kupitia maneno haya matukufu:

“Mungu ni Baba yako. Anakupenda. Yeye na mama yako wa mbinguni wanakuthamini kupita kiasi. … Wewe u wa kipekee. Mmoja wa aina yake, umeumbwa kutokana na kiumbe-akili-asilia cha milele ambayo inakuwezesha kudai maisha ya milele.

“Basi pasiwe na shaka yoyote akili mwako kuhusu thamani yako kama mtu binafsi. Lengo kamili la mpango wa injili ni kutoa nafasi kwa kila mmoja wenu ya kufikia uwezo wenu wote, ambao ni maendeleo ya milele na uwezekano wa uungu.”2

Niruhusu nionyeshe haja ya kutofautisha maneno mawili muhimu: thamani na ustahiki. Hayalingani. Thamani ya kiroho ina maana kujithamini sisi binafsi jinsi Baba wa Mbinguni anavyotuthamini, sio jinsi dunia inavyotuthamini. Thamani yetu iliamuliwa kabla ya kuzaliwa kwetu hapa duniani. “Upendo wa Mungu hauna mwisho na utadumu milele.”3

Kwa upande mwingine, ustahiki unapatikana kupitia utiifu. Tunapotenda dhambi, tunakuwa si wastahiki kamili, lakini kamwe hatukosi thamani! Tunaendelea kutubu na kujitahidi kuwa kama Yesu, thamani yetu ikiwa ingali kamili. Kama Rais Brigham Young alivyofundisha: “Roho mdogo zaidi, aliye duni sana humu duniani … ana thamani kupindukia.”4 Haijalishi chochote, daima tunayo thamani mbele ya macho ya Baba wa Mbinguni.

Licha ya ukweli huu wa ajabu, ni wangapi kati yetu wanapambana, mara kwa mara, na fikra au hisia hasi juu yetu. Mimi pia. Ni mtego rahisi. Shetani ni baba wa uwongo wote, hasa inapohusu taswira isiyo ya kweli kabisa kuhusu asili yetu ya uungu na lengo letu. Kujidunisha hakutustahilii. Badala yake kunaturudisha nyuma. Jinsi ambavyo tumefundishwa mara kwa mara, “Hakuna awezaye kukufanya ujihisi mtu duni bila ya idhini yako.”5 Tunaweza koma kulinganisha udhaifu wetu na ubora wa mwingine. “Kulinganisha ni mwizi wa furaha.”6

Tofauti na hayo, Bwana anatuhakikishia kwamba wakati ambapo tunayo mawazo mema, atatubariki na kujiamini, hata tukajiamini tukajua sisi haswa ni kina nani. Hakujawahi kuwa na wakati muhimu zaidi wa kutii maneno Yake. “Na wema uyapambe mawazo yako bila kukoma,” Alisema. “Ndipo kujiamini kwako kutakuwa imara katika uwepo wa Mungu; na … Roho Mtakatifu atakuwa mwenzi wako daima.”7

Bwana alifunua ukweli huu wa ziada kwa Nabii Joseph Smith: “Yule ambaye hupokea vya Mungu, na avihesabu kuwa ni vya Mungu; na afurahi kwamba Mungu humhesabu kuwa mwenye kustahili kupokea.”8 Tunapomhisi Roho, kama aya hii inavyoeleza, tunatambua ya kwamba kile tunachohisi kinatoka kwa Baba yetu wa Mbinguni mwenye upendo. Tunamtambua Yeye na kumsifu Yeye kwa kutubariki. Kisha tunafurahia ya kwamba tunahesabika kuwa wenye kustahili kupokea.

Hebu fikiria ya kwamba unasoma maandiko asubuhi moja na Roho anakunong’onezea ya kwamba yale unayosoma ni ya kweli. Je, unaweza kutambua Roho na kufurahia ya kwamba ulihisi upendo Wake na ulistahili kupokea?

Akina mama, mwaweza kuwa mmepiga magoti kando ya mwanao wa miaka minne akisema sala yake kabla ya kulala. Hisia fulani inakuzingira huku ukimsikiliza. Unahisi upendo na amani. Hisia hii ni fupi, lakini unatambua ya kwamba, katika kipindi hicho, unahesabika mstahiki kupokea. Twaweza kwa nadra, ikiwa itafanyika, tukapokea madhihirisho makubwa ya kiroho maishani mwetu: lakini twaweza mara kwa mara tukafurahia mnong’ono mtamu wa Roho Mtakatifu, akithibitisha ukweli wa thamani yetu ya kiroho.

Bwana alifafanua uhusiano baina ya thamani yetu na dhabihu Yake kuu ya upatanisho wakati aliposema:

“Kumbuka thamani ya nafsi ni kubwa mbele za Mungu;

“Kwani, tazama, Bwana Mkombozi wako aliteseka hadi kifo katika mwili; kwa hiyo aliteseka maumivu ya watu wote, ili kwamba watu wote waweze kutubu na kuja kwake.”9

Kina dada, kwa sababu ya kile alichotutendea, “tumeunganishwa kwake kupitia uhusiano wa upendo.”10 Alisema, “Na Baba yangu alinituma ili nipate kuinuliwa juu kwenye msalaba; na baada ya kuinulia juu kwenye msalaba, kwamba ningeleta watu wote kwangu.”11

Mfalme Benjamini pia alielezea kuhusu uhusiano huu unaotuunganisha na Mwokozi wetu: “Na lo, atavumilia majaribu, na maumivu ya mwili, njaa, kiu, na uchovu, hata zaidi ya vile mtu anaweza kuteseka, ila tu hadi kifo; kwani tazama, damu inatiririka kutoka kwa kila kinyweleo, mateso yake yatakuwa makuu kwa sababu ya uovu na machukizo ya watu Wake.”12 Mateso hayo na matokeo ya mateso hayo yanajaza mioyo yetu na upendo na shukrani. Mzee Paul E. Koelliker alifundisha, “Tunapoondoa vikwazo ambavyo vinatuvuta kwa upande wa dunia na kutumia uhuru wetu kumtafuta, tunafungua mioyo yetu kwa nguvu za selestia ambazo zinatuvuta Kwake.”13 Ikiwa upendo tulio nao kwa Mwokozi na yale ambayo alitufanyia ni mkuu kuliko nguvu tunayoupa udhaifu, shaka za kibinafsi, au tabia mbaya, basi atatusaidia kushinda yale mambo ambayo huleta mateso katika maisha yetu. Anatuokoa kutokana na sisi wenyewe.

Niruhusu nisisitize tena: ikiwa mvuto wa dunia una nguvu zaidi kuliko imani na tumaini tulilonalo katika Mwokozi, basi mvuto wa dunia utashinda kila wakati. Ikiwa tutachagua kuangazia fikra hasi na kuwa na shaka kuhusu thamani yetu, badala ya kushikamana kwa Mwokozi, inakuwa vigumu zaidi kuhisi misukumo ya Roho Mtakatifu.

Kina dada, hebu tusichanganyikiwe kuhusu sisi ni kina nani! Huku ikiwa mara nyingi ni rahisi kuwa mbatili kiroho kuliko kufanya jitihada za kiroho kukumbuka na kukubali utambulisho wetu mtakatifu, hatuwezi mudu kuwa na mtazamo huo katika siku hizi za mwisho. Kama kina dada, na “tuwe waminifu katika Kristo; … na Kristo atuinue [sisi] juu na kuumia kwake na kifo chake, … na rehema yake na uvumiivu, na matumaini ya utukufu wake na uzima wa milele, yawe katika [akili zetu] milele.”14 Mwokozi anapotuinua hadi kiwango cha juu, tunaweza kuona vyema zaidi sio tu sisi ni kina nani bali kwamba sisi tu karibu Naye zaidi ya tunavyofikiria. Katika jina takatifula Yesu Kristo, amina.