2010–2019
Mtazame Mtu Huyo!
Aprili 2018


Mtazame Mtu Huyo!

Wale wanaopata njia ya kweli ya kumwona Mtu huyo wanapata mlango wa maisha yenye furaha zaidi na faraja katika dhiki za maisha za kukatisha tamaa

Ndugu na dada zangu wapendwa, marafiki wapendwa, nina furaha ya kuwa nanyi katika mkutano huu mkuu wa wikiendi. Harriet nami tunafurahia pamoja nanyi katika kuwaidhinisha Wazee Gong na Soares na kina ndugu na kina dada wengi ambao wamepokea wito mpya katika mkutano mkuu huu.

Ijapokuwa ninamkosa rafiki yangu mkubwa Rais Thomas S. Monson, ninampenda, nina muidhinisha na ninamuunga mkono nabii na Rais wetu, Russell M. Nelson, na washauri wake.

Pia ninashukuru na kwa heshima kufanya tena kazi kwa karibu zaidi na Ndugu zangu wapendwa wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili.

Zaidi ya yote, nimenyenyekezwa sana na nina furaha kubwa kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, ambako mamilioni ya wanaume, wanawake, na watoto wapo tayari kuinua pale wanaposimama—katika uwezo au wito wao—na kujitolea kwa mioyo yao yote kumtumikia Mungu na watoto Wake, kuujenga ufalme wa Mungu.

Leo ni siku takatifu. Ni Jumapili ya Pasaka, tunaposherehekea asubuhi ile tukufu wakati Mwokozi wetu alipokishinda kifo1 na kufufuka toka kaburini.

Siku Kubwa katika Historia

Hivi majuzi niliuliza interneti, “ni siku gani imebadilisha mwelekeo wa historia?”

Majibu, yalijipanga toka ya kushangaza na ya ajabu hadi ya umaizi na hisia za kusisimua shauku. Miongoni mwa hayo, ni siku ambayo sayari ndogo ya kihistoria ilipoanguka katika Peninsula ya Yucatan; au wakati mwaka 1440 Johannes Gutenberg alipomaliza kazi yake ya uchapaji; na hakika siku katika mwaka 1903 wakati ndugu wa Wright walipoonyesha kuwa mtu anaweza kupaa.

Kama swali hilo hilo litaulizwa kwako, wewe ungesema nini?

Katika akili yangu jibu ni wazi.

Kujua siku muhimu zaidi katika historia, lazima turudi nyuma kwenye jioni ile karibu miaka 2000 iliyopita katika Bustani la Gethsemane wakati Yesu Kristo alipopiga magoti kuomba na kujitoa Yeye Mwenyewe dhabihu kama malipo ya dhambi zetu. Ilikuwa ni kipindi hiki cha dhabihu kubwa na isiyo na mwisho ya mateso yasiyo na kifani ya kimwili na kiroho kwamba Yesu Kristo, hata Mungu, alivuja damu kila kinyweleo. Kutokana na upendo wa kweli, Alitoa vyote ili tuweze kupokea vyote. Dhabihu Yake ya kutoka juu, ngumu kuelewa, inaweza kuhisiwa tu na mioyo yetu na akili zetu, inatukumbusha deni la ulimwengu tunalodaiwa na Kristo kwa ajili ya zawadi Yake takatifu.

Baadaye jioni ile, Yesu aliletwa mbele ya viongozi wa dini na kisiasa ambao walimcheka, walimpiga na walimhukumu Yeye kwa kifo cha aibu. Alininginia msalabani na maumivu makali hadi, mwisho, “[ikawa] imekwisha.”2 Mwili Wake usio na uhai uliwekwa ndani ya kaburi la kuazima. Na kisha, asubuhi ya siku ya tatu, Yesu Kristo, Mwana wa Mungu Mkuu, aliinuka kutoka kaburini akiwa kiumbe aliyetukuka, aliyefufuka mwenye furaha, nuru na utukufu.

Ndio, kuna matukio mengi katika historia ambayo yameathiri kwa kina mwelekeoo wa mataifa na watu. Lakini ukiunganisha yote, na hayawezi kuanza kulinganishwa na umuhimu wa kile kilichotokea katika siku ile ya asubuhi ya kwanza ya Pasaka.

Nini kinaifanya dhabihu isiyo na mwisho na Ufufuko wa Yesu Kristo kuwa tukio muhimu zaidi katika historia—la kuvutia zaidi kuliko vita vya ulimwengu, janga la mafuriko, na mabadiliko ya kisayansi ya uvumbuzi?

Kwa Sababu ya Yesu Kristo, Tunaweza Kuishi Tena

Jibu lipo katika sehemu mbili, za changamoto zisizoweza kushindwa ambazo kila mmoja wetu anakumbana nazo.

Kwanza, sote tutakufa. Bila kujali udogo, uzuri, afya njema, au unachukua tahadhari kiasi gani, siku moja mwili wako hautakuwa na uzima. Marafiki na familia watakuomboleza. Lakini hawawezi kukurudisha.

Hata hivyo, kwa sababu ya Yesu Kristo, kifo chako kitakuwa cha muda. Roho yako siku moja itaungana na mwili wako. Mwili huu uliofufuka hautaonja mauti,3 na utaishi katika umilele, bila kuwa na maumivu na mateso ya kimwili.4

Hii itatokea kwa sababu ya Yesu Kristo, Aliyeyatoa maisha Yake na kuyachukua tena.

Alifanya hivi kwa ajili ya wote ambao wanamwamini Yeye.

Alifanya hivi kwa ajili ya wote ambao hawaamini katika Yeye.

Alifanya hivi hata kwa ajili ya wale ambao walimdhihaki, kumtukana, na kulaani jina Lake.5

Kwa sababu ya Yesu Kristo, Tunaweza Kuishi na Mungu

Pili, sote tumetenda dhambi. Dhambi zetu zingetufanya tusiweze kuishi na Mungu, kwa sababu “hakuna kitu kichafu kinaweza kuingia katika ufalme wake.”6

Kama matokeo, kila mwanamume, mwanamke, na mtoto waliondolewa toka kwenye uwepo Wake—hii ni kwamba, hadi Yesu Kristo, Mwana Kondoo asiye na mawaa, alipotoa dhabihu ya maisha Yake kwa ajili ya dhambi zetu. Kwa sababu Yesu hakuwa na deni katika haki, Angeweza kulipa deni letu na kutimiza hitaji la haki kwa kila nafsi. Na hiyo inajuisha wewe na mimi.

Yesu Kristo alitoa dhamana kwa ajili ya dhambi zetu.

Zote.

Siku ile muhimu sana katika historia, Yesu Kristo alifungua milango ya kifo na kuvitupilia mbali vizuizi ambavyo vilituzuia kuingia katika nyumba takatifu za uzima wa milele. Kwa sababu ya Bwana na Mwokozi wetu, wewe na mimi tumepewa zawadi ya thamani na ya gharama kuu—bila kujali mambo yetu ya kale, tunaweza kutubu na kufuata njia ambayo inayoongoza katika nuru na utukufu wa selestia, tukizungukwa na watoto wa Baba wa Mbinguni.

Kwa nini Tunafurahi

Hiki ndicho tunachokisherehekea katika Jumapili ya Pasaka—tunasherehekea uzima!

Kwa sababu ya Yesu Kristo, tutafufuka toka kwenye dhiki ya kifo na kuwakumbatia wale tuwapendao katika mikono yetu, tukibubujikwa na machozi ya furaha na shukurani. Kwa sababu ya Yesu Kristo, tutaishi kama viumbe wa milele, hata mwisho wa dunia.

Kwa sababu ya Yesu Kristo, dhambi zetu haziwezi tu kufutwa, zinaweza kusahaulika.

Tunaweza kuwa kusafishwa na kuhuishwa.

Takatifu.

Kwa sababu ya Mwokozi wetu mpendwa, tunaweza kunywa toka kisima cha uzima ambacho kinamiminikia kwenye uzima wa milele.7 Tunaweza kuishi milele katika nyumba za Mfalme wetu wa milele, katika utukufu usioelezeka na furaha kamili.

Je, “Tunamtazama Mtu Huyo”?

Licha ya haya yote, kuna wengi katika ulimwengu huu leo ambao huenda hawajui au hawaamini katika zawadi ya thamani ambayo Yesu Kristo ametupa. Huenda wamesikia juu ya Yesu Kristo na kumjua Yeye kama picha ya kihistoria, lakini hawamwoni Yeye ni nani hasa.

Ninapofikiria hili, ninakumbushwa Mwokozi akisimama mbele ya Mrumi wa Kiyahudi, Pontio Pilato, saa kadhaa kabla ya kifo Chake.

Pilato alimwona Yesu kwa mtazamo hasa wa kilimwengu kawaida. Pilato alikuwa na kazi ya kufanya, na ilijumuisha kazi kuu mbili: kukusanya ushuru kwa Warumi na kuweka amani. Sasa Mkutano wa Makuhani wa Kiyahudi walikuwa wameleta kwake mtu aliyetuhumiwa alikuwa mpingaji wa vyote.8

Baada ya kumhoji mfungwa wake, Pilato alitangaza,“sioni kosa lake hata kidogo.”9 Lakini alihisi kuwaridhisha washitaki wa Yesu, hivyo Pilato akafuata desturi kwamba mfungwa mmoja aachiliwe wakati wa Pasaka. Kwa nini hawakumfungulia Yesu badala ya mnyanganyi na muuaji Baraba?10

Lakini makelele ya umati yalitaka kwamba Pilato awafungulie Baraba na wamsulubishe Yesu.

“Kwa nini?” Pilato akauliza. “Ametenda maovu gani?”

Lakini waliendelea kupaza sauti. “Asulubiwe!”11

Katika juhudi zake za mwisho kuuridhisha umati, Pilato aliamuru watu wake wampige mjeledi Yesu.12 Wakafanya hivyo, wakimwacha akitokwa na damu na michubuko. Walimdhihaki, walimvisha taji la miba katika kichwa Chake, na wakamvisha kanzu la zambarao.13

Huenda Pilato alifikiri kwamba hii ingeweza kukidhi tamaa ya damu ya wale watu. Huenda watamhurumia mtu huyo. “Tazama, ninamleta nje kwenu,” Pilato alisema, “kwa maana mimi sikuona hatia yoyote kwake. … Mtazameni mtu huyo!”14

Mwana wa Mungu alisimama kimwili mbele ya watu wa Yerusalemu.

Wangeweza kumwona Yesu, lakini hawakuweza kumtazama Yeye.

Hawakuwa na macho ya kuona.15

Kwa namna ya mfano, sisi pia tunaalikwa “kumtazama mtu huyo.” Maoni kumhusu Yeye yanatofautiana katika ulimwengu. Manabii wa kale na wa sasa wanashuhudia kwamba Yeye ni Mwana wa Mungu. Mimi pia. Ni dhahiri na muhimu kwamba kila mmoja wetu atakuja kujua mwenyewe. Hivyo, unapotafakari maisha na utumishi wa Yesu Kristo, unaona nini?

Wale wanaopata njia ya kweli ya kumtazama Mtu huyo anauona mlango wa maisha yenye furaha zaidi na Zeri katika maisha yanayokatisha tamaa.

Hivyo, wakati unapozungukwa na masikitiko na huzuni, mtazame Mtu huyo.

Unapohisi umepotea au kusahaulika, mtazame Mtu huyo.

Wakati unapokuwa umekata tamaa, umeachwa, una shaka, umeharibiwa, au umeshindwa, mtazame Mtu huyo.

Atakufariji.

Atakuponya na kukupa maana ya safari yako. Yeye atamimina Roho Yake na kujaza moyo wako kwa furaha isiyo na kifani.16

Yeye huwapa “nguvu walioanguka, na kwa wale wasio na nguvu huwaongezea.”17

Tunapomtazama Mtu huo, tunajifunza juu Yake na kutaka kuyaweka maisha yetu pamoja Naye. Tunatubu na tunajaribu kuitakasa asili yetu na kumkaribia kidogo Yeye. Tunamwamini Yeye. Tunaonesha upendo wetu Kwake kwa kutii Amri Zake na kuishi katika maagano yetu matakatifu.

Kwa maneno mengine, tunakuwa wafuasi Wake.

Nuru Yake ya kusafisha hujaa nafsini mwetu. Neema Yake inatuinua. Mizigo yetu inapunguzwa, amani yetu inaongezeka. Wakati kweli tunapomtazama Mtu huyo, tuna ahadi ya maisha mazuri ambayo yanahamasisha na kutushikilia kwenye kona na matuta katika safari ya maisha. Tukiangalia nyuma, tutagundua kwamba kuna mpango mtakatifu, kwamba nukta zinaunganika.18

Unapokubali dhabihu Yake, kuwa mfuasi Wake, na hatimaye kufika mwisho wa safari yako ya duniani, huzuni zako ambazo umevumilia katika maisha haya zitakuwa nini?

Zitakuwa zimekwenda.

Je, kukata tamaa, usaliti, mateso uliyokumbana nayo?

Yameenda.

Je, taabu, huzuni kubwa, hatia, aibu, na maumivu makali ambayo umeyapitia?

Yameenda.

Yamesahaulika.

Hii ndiyo maana tunazungumza kuhusu Kristo, tunafurahia katika Kristo, tunahubiri kuhusu Kristo, tunatoa unabii kumhusu Kristo … ili watoto wetu wajue asili ya kutegemea kwa msamaha wa dhambi zao”?19

Je, kuna ajabu yoyote kwamba tunajitahidi kwa mioyo yetu yote kumtazama Mtu Huyo?

Ndugu na dada zangu wapendwa, ninashuhudia kwamba siku iliyo muhimu katika historia ya mwanadamu ilikuwa ni siku ambayo Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai, alishinda vita dhidi ya kifo na dhambi kwa ajili ya watoto wote wa Mungu. Na siku muhimu zaidi katika maisha yako na yangu ni siku ambayo tulijifunza “kumtazama Mtu Huyu”; wakati tunapomwona Yeye kama vile alivyo; tunapouchukua kwa moyo na akili zetu zote nguvu za upatanisho; wakati kwa matamanio na nguvu, tunaahidi kumfuata Yeye. Naomba siku hiyo iwe siku ambayo inajitokeza tena na tena katika maisha yetu.

Ninawaachia ushuhuda na baraka zangu kwamba “tunapomtazama mtu huyu,” tutapata maana, furaha, na amani katika ulimwengu huu, na uzima wa milele katika ulimwengu ujao. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona Mosia 3:23

  2. Yohana 7:30.

  3. Ona Alma 11:45.

  4. Ona Ufunuo 21:4.

  5. Ona 1 Wakorintho 15:21–23.

  6. 3 Nefi 27:19.

  7. Ona Yohana 4:14.

  8. Ona Luka 23:2.

  9. Yohana 18:38. Kuepuka kumhukumu Yesu, Pilato alijaribu kuisukumakesi kwa Herode Antipas. Kama Herode, ambaye aliamulu kifo cha Yohana Mbatizaji (ona Mathayo 14:6-11), angemshutumu Yesu, Pilato angeweza kubadirisha hukumu na kudai lilikuwa jambo la kijamii ambalo alikubali ili kuleta amani. Lakini Yesu hakumjibu neno Herode (ona Luka 23:6-12.), na Herode akamrudisha kwa Pirato.

  10. Ona Marko 15:6–7; John 18:39–40. Mwandishi mmoja wa Agano Jipya aliandika, “Ilioneka kuwa desturi, kwamba wakati wa PasakaGavana wa Kirumi alimwachilia kwa umma wa Wayahudi baadhi ya wafungwa jeuri ambao walihukumiwa kifo” (Alfred Edersheim, The Life and Times of Jesus the Messiah [1899], 2:576). Jina Baraba linamaana “mwana wa baba.” Jambo la kuwapa watu wa Yerusalemu chaguo kati ya watu hawa wawili linafurahisha.

  11. Ona Marko 15:11–14.

  12. Mjeledi huu ulikuwa hatari uliitwa “kifo cha haraka” (Edersheim, Jesus the Messiah, 2:579).

  13. Ona Yohana 19:1-3.

  14. Yohana 19:4–5.

  15. Mwanzo Yesualiona kwamba,“moyo wa watu hawa ulishupaa, na masikio yao yameziba kusikia, na macho yao yamefumba; ili wakati wowote waweze kuona kwa macho yao, na kusikia kwa masikio yao, na kufahamu kwa moyo wao, na waweze kuongoka, na nitawaponya. Na kisha kwa wema Aliwaambia wafuasi Wake,“Lakini heri macho yenu, kwa kuwa yanaona: na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia” (Mathayo 13:15–16). Tutaiacha mioyo yetu iwe migumu, au au tutafumbua macho na mioyo yetu ili tuweze kumwona Mtu huyo?

  16. Ona Mosia 4:20

  17. Isaya 40:29.

  18. Ona Dieter F. Uchtdorf, “The Adventure of Mortality” (worldwide devotional for young adults, Jan. 14, 2018), broadcasts.lds.org.

  19. 2 Nefi 25:26.