2010–2019
Yote ni Kwa Ajili ya Watu
Aprili 2018


Yote ni Kwa Ajili ya Watu

Kanisa lipo kwa ajili yenu, wafuasi wa Bwana—wale wanaompenda na kumfuata na ambao wamejichukulia jina Lake juu yao.

Wakati wa matayarisho ya ujenzi wa Hekalu la ajabu la Paris France, nilikuwa na uzoefu ambao sitausahau kamwe. Katika mwaka wa 2010 wakati ardhi ya hekalu ilipopatikana, meya wa jiji aliomba kukutana nasi ili apate kujua zaidi kuhusu Kanisa letu. Mkutano huu ulikuwa hatua muhimu katika kupata kibali cha ujenzi. Tuliandaa kwa uangalifu mkubwa uwasilisho ambao ulijumuisha picha kadhaa za kuvutia za Mahekalu ya Watakatifu wa Siku za Mwisho. Tumaini langu kubwa zaidi lilikuwa kwamba uzuri wa usanifu wa majengo ungemshawishi meya kuunga mkono mradi wetu.

Kushangaza, meya aliashiria kwamba badala ya kutathmini uwasilisho wetu, yeye pamoja na timu yake walipendelea kufanya uchunguzi wao wenyewe ili kugundua sisi tulikuwa kanisa la aina gani. Mwezi uliofuata, tulialikwa tena kusikiliza ripoti ambayo ilitolewa na mwanabaraza wa jiji ambaye pia alikuwa profesa wa historia ya kidini. Alisema, “Zaidi ya mengine yote, tulitaka kuelewa waumini wa kanisa lenu ni watu wa aina gani. Kwanza, tulihudhuria mojawapo ya mikutano yenu ya sakramenti. Tuliketi katika sehemu ya nyuma ya jengo lenu na kwa makini tukachunguza wale watu waliokuwa katika mkutano na kile walikuwa wakifanya. Kisha tulifanya mikutano na majirani wenu—wale wanaoishi karibu na kituo cha kigingi—na tukawauliza nyinyi Wamormoni ni watu wa aina gani.”

“Kwa hivyo, hitimisho lenu ni lipi?” Niliuliza, nikihisi wasiwasi kidogo. Alijibu, “Tuligundua ya kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni Kanisa linalokaribia sana kufanana na Kanisa la asili la Yesu Kristo kuliko makanisa mengine tunayoyafahamu.” Nilikuwa karibu kupinga kwa kusema, “Huo si ukweli kamili! Sio kanisa linalokaribia sana; ni Kanisa la Yesu Kristo—Kanisa lile lile, Kanisa la kweli!” Lakini nilijizuia na badala yake nikasali kimoyomoyo kutoa shukrani. Kisha meya na timu yake walitushauri ya kwamba, kulingana na matokeo ya uchunguzi wao, yeye na timu yake hawakuwa na pingamizi yoyote kuhusu ujenzi wa hekalu katika jumuia yao.

Leo, ninapowaza kuhusu uzoefu huo wa kimiujiza, ninakuwa na shukrani kwa hekima ya meya na roho wa umaizi. Alielewa kwamba jambo la muhimu katika kuelewa Kanisa sio kulitazama kupitia umbo la majengo yake au hata jumuiya iliyopangika vizuri lakini kupitia mamilioni ya waumini wake waaminifu, ambao kila siku wanajaribu kuiga mfano wa Yesu Kristo.

Ufafanuzi wa Kanisa unaweza ukatolewa kutoka fungu katika Kitabu cha Mormoni ambalo linasema, “Na wale [akimaanisha wanafunzi wa Bwana] ambao walibatizwa katika jina la Yesu waliitwa kanisa la Kristo.”1

Kwa maneno mengine, kila kitu juu ya Kanisa kinahusu watu. Kila kitu ni juu yenu, wafuasi wa Bwana—wale wanaompenda na kumfuata na ambao wamejichukulia jina Lake juu yao kupitia agano.

Rais Russell M. Nelson wakati mmoja alifananisha Kanisa na gari nzuri. Sisi sote tunafurahia wakati gari letu ni safi na linang’aa. Lakini lengo la gari sio kuonekana kama mashine yenye kupendeza; ni kuwasafirisha watu walio ndani ya gari.2 Katika namna sawa, sisi, kama waumini wa Kanisa, tunashukuru kuwa na mahali pazuri pa kuabudu ambapo ni pasafi na ambapo pametunzwa vyema, na pia tunafurahia kuwa programu zinazofanya kazi vyema. Lakini hii ni mifumo ya kutegemeza tu. Lengo letu kuu ni kualika kila mwana na binti wa Mungu aje kwa Kristo na aongozwe katika njia ya agano. Hakuna kitu muhimu zaidi. Kazi yetu inahusu tu watu na maagano.

Je, si ajabu kwamba jina lililopewa Kanisa la urejesho kupitia ufunuo linaunganisha vitu viwili muhimu zaidi katika kila agano la injili? Kwanza ni jina Yesu Kristo. Kanisa hili ni Lake, na Upatanisho Wake wa kutakasa na maagano ni njia ya pekee inayoelekea kwenye wokovu na kuinuliwa. Jina la pili linatutaja sisi: Watakatifu, au kwa namna nyingine, mashahidi Wake na wafuasi Wake.

Nilijifunza umuhimu wa kuzingatia juu ya watu wakati nilipohudumu kama rais wa kigingi kule Ufaransa. Mwanzoni mwa huduma yangu, akilini mwangu nilikuwa na malengo makuu zaidi kwa ajili ya kigingi: uanzishwaji wa kata mpya, ujenzi wa nyumba mpya za mikutano, na hata ujenzi wa hekalu katika eneo letu. Nilipopumzishwa miaka sita baadaye, hakuna hata moja kati ya malengo haya yalikuwa yamefikiwa. Hii inaweza kuwa ilionekana kama kushindwa kabisa isipokuwa ya kwamba, wakati wa muda huo wa miaka sita, malengo yangu yalikuwa yamebadilika.

“Nikiwa nimekaa kwenye jukwaa siku yangu ya kupumzishwa, nilizidiwa na hisia kubwa za shukrani na ufanikishaji. Nilitazama katika nyuso za mamia ya waumini waliokuwa katika mkutano. Niliweza kukumbuka uzoefu wa kiroho ambao ulihusiana na kila mmoja wao.

Kulikuwa na akina kaka na akina dada ambao walikuwa wameingia katika maji ya ubatizo, wale ambao nilikuwa nimeweka saini kwenye vibali vyao vya hekaluni ili waweze kupokea ibada takatifu za hekaluni, na vijana na wanandoa niliokuwa nimewasimika au kuwapumzisha kama wamisionari. Kulikuwa na wengine wengi ambao nilikuwa nimewahudumia walipokuwa wakipitia majaribu na shida katika maisha yao. Nilihisi upendo wa dhati wa kindugu kwa kila mmoja wao. Nilikuwa nimepata furaha ya kweli katika kuwahudumia na nilifurahia katika uaminifu wao uliozidi, na imani katika Mwokozi.

Rais M. Russell Ballard alifundisha, “Kilicho muhimu zaidi katika majukumu yetu ya Kanisa sio takwimu zinazoripotiwa au mikutano inayofanyika lakini ni ikiwa au isipokuwa watu binafsi—wanaohudumiwa mmoja baada ya mwingine jinsi tu Mwokozi alivyofanya—wameinuliwa na kutiwa moyo na hatimaye wamebadilika.”3

Wapendwa kaka na dada zangu, je tunashiriki kikamilifu katika injili au tunashughulika tu Kanisani? Jambo muhimu ni kufuata mfano wa Mwokozi katika mambo yote. Ikiwa tutafanya hivyo, kiasili tutazingatia katika kuwaokoa watu binafsi badala ya kutekeleza majukumu na kufanikisha programu.

Umewahi kujiuliza jinsi inavyoweza kuwa ikiwa Mwokozi angetembelea kata yako Jumapili ijayo? Angefanya nini? Je, angekuwa na wasiwasi kujua ikiwa vielelezo vilikuwa vizuri au ikiwa viti vilikuwa vimepangwa vyema ndani ya darasa? Au angempata mtu wa kumpenda, kumfundisha, na kumbariki? Pengine angemtafuta mshiriki mgeni au rafiki wa kumkaribisha, kaka mgonjwa au dada anayehitaji faraja, kijana anayeyumbayumba anayehitaji kuinuliwa na kutiwa moyo.

Ni madarasa gani Yesu angeyatembelea? Nisingeshangaa kama angetembelea kwanza watoto wa Msingi. Pengine angepiga magoti na kuzungumza nao ana kwa ana. Angeonyesha upendo Wake kwao, angewasimulia hadithi, angewapongeza kwa michoro yao, na kushuhudia kuhusu Baba Yake wa Mbinguni. Tabia yake ingekuwa rahisi, ya kweli, na bila ya kujifanya. Je, Tunaweza kufanya sawa na hivyo?

Ninakuahidi ya kwamba ukiendelea kujitahidi kuwa kwenye ajenda ya Bwana, hakuna kitu kitakachokuwa muhimu zaidi kuliko kuwatafuta wale watu ambao unaweza kuwasaidia na kuwabariki. Kanisani utazingatia katika kufundisha watu binafsi na kugusa mioyo yao. Shauku yako itakuwa ni kukuza uzoefu wa kiroho kuliko kupanga shughuli kamilifu, kuhudumia washiriki wenzako badala ya kujaza idadi ya matembezi ambayo umefanya. Haitakuwa kwa ajili yako bali kwa ajili yao ambao tunawaita kaka zetu na dada zetu.

Wakati mwingine tuzungumza kuhusu kwenda kanisani. Lakini Kanisa ni zaidi ya jengo au mahali fulani. Ni kweli na hai katika makazi nyenyekevu katika maeneo madogo zaidi duniani kama ilivyo hapa katika Makao Makuu ya Kanisa Jijini Salt Lake. Bwana Mwenyewe alisema, “Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, mimi nipo papo hapo katikati yao.”4

Tunakwenda na kanisa popote tuendapo: kazini, shuleni, likizoni, na hasa nyumbani kwetu. Uwepo wetu hasa na ushawishi wetu unaweza kuwa wa kutosha kufanya popote tulipo kuwa mahali patakatifu.

Ninakumbuka mazungumzo niliyokuwa nayo na rafiki ambaye si wa imani yetu. Alishangaa kujifunza kuwa mwanaume yeyote mstahiki katika Kanisa letu anaweza kupokea ukuhani. Akauliza, “Lakini ni makuhani wangapi mlio nao katika kata yako?”

Nilijibu, “Kati ya 30 na 40.”

Akiwa amekanganywa, aliendelea, “Katika mkusanyiko wangu, tunaye kuhani mmoja. Je, kwa nini mnahitaji makuhani wengi hivyo Jumapili asubuhi?

Nikiwa nimevutiwa sana na swali lake, nilihisi msukumo kujibu, “Nakubaliana nawe. Sidhani tunahitaji makuhani kiasi hicho kanisani Jumapili. Lakini tunahitaji kuhani katika kila nyumba. Na wakati ambapo hakuna mwenye ukuhani katika nyumba fulani, makuhani wengine wanaitwa kulinda na kutumikia familia hiyo.”

Letu si Kanisa la Jumapili tu. Kuabudu kwetu kunaendelea kila siku ya wiki, mahali popote tulipo na katika kila tufanyacho. Nyumba zetu hasa ni “sehemu takatifu ya msingi ya imani yetu.”5 Mara nyingi ni katika nyumba zetu ambapo tunasali, tunabariki, tunajifunza, tunafundisha neno la Mungu, na tunahudumu kwa upendo msafi. Ninaweza kushuhudia kutokana na uzoefu wa kibinafsi ya kwamba nyumba zetu ni mahali patakatifu ambapo Roho anaweza kudumu—zaidi, na mara nyingine zaidi ya, sehemu zetu rasmi za kuabudu.

Ninashuhudia ya kamba Kanisa hili ni Kanisa la Yesu Kristo. Nguvu na uhai wake unatokana na vitendo vya kila siku vya mamilioni ya wafuasi Wake ambao wanajitahidi kila siku kufuata mfano Wake bora zaidi kwa kuwajali wengine. Kristo yu hai na anaongoza Kanisa hili. Rais Russell M. Nelson ni nabii ambaye amemchagua atuongoze na kutuelekeza katika wakati wetu. Kwa haya nashuhudia katika jina la Yesu Kristo, amina.