2010–2019
Kuhudumu kama Mwokozi
Aprili 2018


Kuhudumu Kama Mwokozi Anavyohudumu

Na tuonyeshe shukrani zetu na upendo kwa Mungu kwa kuwahudumia kwa upendo akina dada na kaka zetu wa milele.

Ni baraka nzuri iliyoje kuishi katika wakati wa muendelezo wa ufunuo kutoka kwa Mungu! Tunapotazamia na kupokea “kufanywa upya vitu vyote,”1 ambako kumekuja na kutakuja kupitia matukio yaliyotabiriwa ya wakati wetu, tunakuwa tunaandaliwa kwa Ujio wa Pili wa Mwokozi.2

Na ni njia ipi nzuri ya kujiandaa kumpokea Yeye zaidi ya kujitahidi kuwa kama Yeye kupitia kuhudumiana kwa upendo! Kama Yesu Kristo alivyofundisha wafuasi Wake mwanzoni mwa kipindi hiki cha maongozi ya Mungu, “Kama wanipenda utanitumikia.”3 Huduma yetu kwa wengine ni dhihirisho la ufuasi na shukrani yetu na upendo kwa Mungu na Mwanawe, Yesu Kristo.

Wakati mwingine tunadhani tunapaswa kufanya kitu kikubwa na cha kishujaa “kuhesabika” kama tumewatumikia jirani zetu. Bado matendo madogo ya huduma yanaweza kuwa na athari kubwa kwa wengine—vilevile kwetu wenyewe. Mwokozi alifanya nini? Kupitia kwa zawadi Zake za kiungu za Upatanisho na Ufufuo—ambazo tunasherehekea katika Jumapili hii nzuri ya Pasaka—“hakuna mwingine aliyekuwa na ushawishi mkubwa [juu ya] wote ambao wameishi na ambao bado wataishi juu ya dunia.”4 Lakini Yeye pia alitabasamu, alizungumza, alitembea , alisikiliza, alitenga muda, aliwatia moyo, alifundisha, kulisha na kusamehe. Alitumikia familia na marafiki, majirani na asiyowajua sawia, na Aliwaalika asiowajua na wapendwa wao kufurahia baraka tele za injili Yake. “Matendo” hayo rahisi ya huduma na upendo huweka kigezo kwa huduma yetu leo.

Unapopata fursa ya kumwakilisha Mwokozi katika juhudi zako za kuhudumu, jiulize, “Ni vipi ninavyoweza kushiriki nuru ya injili na mtu huyu au familia hii? Roho ananishawishi kufanya nini?”

Kuhudumu kunaweza kufanywa katika njia kuu tofauti za kibinafsi. Kwa hivyo kunaoneka vipi?

Kuhudumu kunaonekana kama urais wa akidi ya wazee na Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama kwa sala wakishauriana kuhusu majukumu. Badala ya viongozi kutoa vijikaratasi, kunaonekana kama kushauriana kuhusu watu binafsi na familia ana kwa ana pale majukumu yanapotolewa kuhudumia akina kaka na kina dada. Kunaonekana kama kwenda matembezini, kukutana pamoja kwa mchezo wa usiku, kutoa huduma, au hata kuhudumu pamoja. Kunaonekana kama kutembelea kwa kufika mwenyewe au kuzungumza kwenye simu au kupitia kwa chati mtandaoni au kutuma arafa. Kunaonekana kama kupeleka kadi ya siku ya kuzaliwa na kushangilia kwenye mchezo wa mpira. Kunaonekana kama kushiriki andiko au nukuu kutoka kwenye ujumbe wa mkutano ambao utakuwa na maana kwa mtu huyu. Kunaonekana kama kujadili swali la injili na kushiriki ushuhuda kuleta ufafanuzi na amani. Kunaonekana kama kuwa sehemu ya maisha ya mtu na kumjali. Kunaonekana pia kama huduma ya usahili ambapo mahitaji na nguvu hujadiliwa kwa hisia na kwa kufaa. Kunaonekana kama baraza la kata likipanga kufanyia kazi hitaji kubwa.

Aina hii ya kuhudumu ilimuimarisha dada mmoja aliyehamia mbali sana na nyumbani wakati mumewe alipoanza shule ya elimu ya uzamili. Bila simu iliyofanya kazi na mtoto mdogo wa kumlea, alihisi kukanganywa katika eneo jipya, kupotea kabisa na mpweke. Bila kutoa taarifa awali, dada wa Muungano wa Usaidizi wa akina mama alikuja mlangoni akiwa na jozi ya viatu kwa ajili ya mtoto, akawaweka wote wawili ndani ya gari lake, na kuwapeleka kutafuta duka la vyakula. Dada mwenye shukrani alisema, “Alikuwa ni tegemeo langu!”

Kuhudumu kwa kweli kunadhihirishwa na dada mzee huko Afrika aliyepangiwa kumtafuta dada ambaye hakuwa anahudhuria mikutano ya Kanisa kwa muda mrefu. Alipokwenda nyumbani kwa dada huyo, alikuta kwamba alikuwa amepigwa na kuporwa, alikuwa na kidogo cha kula, na hakuwa na nguo ambazo alihisi zilikuwa za kufaa kwa ajili ya mikutano ya Kanisa Jumapili. Mwanamke aliyepangiwa kumhudumia alikwenda na sikio la kusikiliza, mazao kutoka bustanini mwake, maandiko ya kusoma, na urafiki. Dada “aliyepotea” punde alirudi kanisani na sasa ana wito kwa sababu anajua anapendwa na kuthaminiwa.

Kujumuisha juhudi hizi za Muungano wa Usaidizi wa akina mama na akidi ya wazee mpya sasa kutaleta umoja ambao utaleta matokeo ya kustaajabisha. Kuhudumu kunakuwa juhudi moja sawa ya kutimiza jukumu la ukuhani la “kutembelea nyumba ya kila muumini” na “kulichunga kanisa daima, na kuwa nao na kuwaimarisha,”5 vilevile kufikia lengo la Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama la kusaidiana kujiandaa kwa baraka za uzima wa milele.6 Kufanya kazi pamoja chini ya maelekezo ya askofu, urais wa akidi ya wazee na Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama kunaweza kuvutia wanapotafuta njia bora za kulinda na kutunza kila mtu binafsi na familia.

Acha niwape mfano. Mama aligundulika kuwa na saratani. Punde alianza matibabu, na mara moja, akina dada wa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama walikwenda kazini, wakipanga jinsi ya kumsaidia vizuri zaidi kwa chakula, usafiri kwenye miadi ya tiba, na msaada mwingine. Walimtembelea kila mara, wakitoa wenza wa matumaini. Wakati huo huo, akidi ya Ukuhani wa Melkizedeki walijitokeza vitendo. Walifanya kazi katika kubadilisha chumba cha kulala na maliwato kufanya iwe rahisi kumtunza dada mgonjwa. Wavulana walitoa mikono yao na migongo kushiriki katika juhudi ile ya muhimu. Na wasichana walijihusisha: kwa furaha walipanga kwa uaminifu kumtembeza mbwa kila siku. Muda ulivyokwenda, kata iliendeleza huduma yao, ikiongeza na kubadili pale palipohitajika. Ilikuwa dhahiri huduma ya upendo, kila muumini akijitoa mwenyewe, kwa muungano wakionyesha kujali katika njia binafsi ambazo zilimbariki siyo tu dada mgonjwa bali kila mmoja wa familia yake.

Baada ya juhudi za kishujaa, dada hatimaye alishindwa na saratani na alipumzishwa. Je, kata ilivuta pumzi ya faraja na kuchukulia kuwa kazi ilikuwa imefanywa vizuri na kuisha vizuri? Hasha, wasichana waliendelea kumtembeza mbwa kila siku, akidi za makuhani ziliendelea kumhudumia baba na familia ile, na Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama waliendelea kufika kwa upendo kuhakikisha uwezo na mahitaji. Akina kaka na akina dada, huku ndiko kuhudumu—huku ndiko kupenda kama Mwokozi anavyopenda!

Baraka nyingine ya matangazo haya yenye ushawishi ni fursa ya wasichana wa miaka 14 mpaka 18 kushiriki katika kuhudumu kama wenza kwa akina dada wa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama, kama vile wavulana wa umri wao kuhudumu kama wenza wahudumiaji kwa wenye Ukuhani wa Melkizedeki. Vijana wanaweza kushiriki vipaji vyao vya kipekee na kukua kiroho wanapotumika pembeni mwa watu wazima katika kazi ya Wokovu. Kuwashirikisha vijana katika majukumu ya kuhudumu kunaweza pia kuongeza ufikiaji wa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama na akidi ya wazee kuwajali wengine kwa kuongeza idadi ya waumini wanaoshiriki.

Ninapofikiria kuhusu wasichana wazuri niliopata kuwajua, ninapata msisimko kwa ajili ya hao akina dada wa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama ambao watapata fursa ya kubarikiwa na shauku ya wasichana, vipaji, na hisia za kiroho wanapohudumu kando yao au kuhudumiwa na wao. Na ninafurahishwa vilevile na nafasi ambayo wasichana watapata ya kuwa na mnasihi na kufundishwa na kuimarishwa na dada zao katika Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama. Fursa hii ya kushiriki katika kuujenga ufalme wa Mungu itakuwa ya manufaa makubwa kwa wasichana, ikiwasaidia kujiandaa vizuri zaidi kutimiza majukumu yao kama viongozi Kanisani na kwenye jamii na kama wenzi wenye mchango katika familia zao. Kama Dada Bonnie L. Oscarson alivyoshiriki jana, wasichana “wanataka kuwa kwenye huduma. Wanahitaji kujua kuwa wanathaminiwa na ni wa muhimu katika kazi ya wokovu!”7

Kwa kweli, wasichana tayari wanawahudumia wengine, bila kupangiwa au matangazo. Familia ninayoifahamu ilihamia mamia ya maili katika eneo jipya ambapo hawakumjua mtu yeyote. Ndani ya juma la kwanza, msichana wa miaka-14 kutoka kwenye kata yao mpya alikuja mlangoni kwao akiwa na sahani ya biskuti, akiwakaribisha kwenye eneo hilo. Mama yake alisimama nyuma yake akitabasamu kama dereva aliye tayari, akiunga mkono hamu ya binti yake ya kuhudumu.

Mama mwingine alionyesha kujali siku moja kwamba binti yake wa miaka-16 hakuwa nyumbani katika muda wa kawaida. Hatimaye msichana alipofika, mama yake alimuuliza kwa wasiwasi kuhusu wapi alipokuwa. Msichana wa miaka-16 kwa haya alijibu kwamba alikuwa amempelekea maua mjane aliyeishi karibu. Aligundua dada mzee alionekana mpweke na alihisi kuvuviwa kumtembelea. Kwa ruhusa kamili ya mama yake, msichana aliendelea kumtembelea yule mwanamke mkongwe. Walikuwa marafiki wazuri, na ushirikiano wao wa kuvutia uliendelea kwa miaka.

Kila mmoja wa wasichana hawa, na wengine wengi kama wao, waligundua hitaji la mtu na walilishughulikia. Wasichana wana hamu ya asili kujali na kushiriki ambayo inaweza kuelekezwa vyema kupitia kuhudumu kwa kushirikiana na dada mkubwa.

Haijalishi umri wetu, tunapofikiria jinsi ya kuhudumu kikamilifu, tunauliza, “Je, anahitaji nini?” Kuunganisha swali hilo na nia ya dhati ya kuhudumu, ndipo hapo tunaongozwa na Roho kufanya kile kinachofaa na kumuimarisha mtu. Nimesikia hadithi zisizo na idadi za akina kaka na akina dada ambao walibarikiwa kwa tendo dogo la kujumuishwa na kukaribishwa kanisani, barua pepe ya kujali au arafa, mawasiliano ya mtu katika wakati mgumu, mwaliko wa kushiriki katika shughuli ya kikundi, au kujitolea kusaidia kwenye hali ya changamoto. Mzazi mmoja, waongofu wapya, waumini wasioshiriki kikamilifu, wajane na wagane, au kijana anayehangaika wanaweza kuhitaji umakini wa ziada na msaada wa kipaumbele kutoka kwa akina kaka na akina dada wanaowahudumia Uratibu kati ya urais wa akidi ya wazee na Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama huruhusu majukumu sahihi kufanywa.

Hatimaye, kuhudumu kwa kweli hutimizwa mmoja baada ya mwingine kwa upendo kama motisha. Thamani na sifa na muujiza wa kuhudumia kwa dhati ni kwamba kiukweli hubadilisha maisha! Wakati mioyo yetu imefunguliwa na iko radhi kupenda na kujumuisha, kutia moyo na faraja, nguvu ya kuhudumia kwetu itakuwa isiyozuilika. Upendo ukiwa motisha, miujiza itafanyika, na tutapata njia za kuwaleta dada zetu na kaka zetu “waliopotea” kwenye mjumuisho-wa pamoja wa injili ya Yesu Kristo.

Mwokozi ni mfano wetu katika kila kitu—siyo tu katika kile tunachopaswa kufanya lakini kwa nini tukifanye.8 “Maisha yake duniani yalikuwa mwaliko kwetu—kuinua uoni wetu juu zaidi, kusahau matatizo yetu wenyewe na kuwafikia wengine.”9 Tunapokubali nafasi ya kuwahudumu kwa moyo wote kina dada na kina kaka zetu, tunabarikiwa kuwa wenye kutakaswa zaidi kiroho, kwenye tuni zaidi na mapenzi ya Mungu, na kuweza zaidi kuelewa mpango Wake wa kumsaidia kila mmoja kurudi Kwake. Tutakuwa tayari zaidi kutambua baraka Zake na kuwa na ari zaidi ya kunyoosha baraka hizo kwa wengine. Mioyo yetu itaimba kwa pamoja na sauti zetu:

Mwokozi, niweze kumpenda ndugu yangu

Kama ninavyojua wanipenda,

Nipate kwako nguvu yangu, nguzo yangu,

Kwani mtumishi wako nitakuwa.

Mwokozi, niweze kumpenda ndugu yangu—

Bwana, Nitakufuata wewe.10

Na tuonyeshe shukrani na upendo wetu kwa Mungu kwa kuhudumu kwa upendo kwa dada na kaka zetu wa milele.11 Matokeo yatakuwa umoja wa hisia kama vile watu wa Amerika ya kale walivyofurahia miaka 100 baada ya kutokea kwa Mwokozi katika ardhi yao.

“Na ikawa kwamba hakukuwa na ubishi … kwa sababu ya mapenzi ya Mungu ambayo yaliishi katika mioyo ya watu.

“… Na hakukuwa na wivu, wala ubishi, … na kwa kweli hakujakuwa na watu ambao wangekuwa na furaha zaidi miongoni mwa watu wote ambao waliumbwa na mkono wa Mungu.”12

Kwa furaha ninatoa ushahidi wangu kwamba mabadiliko haya ya ufunuo yametoka kwa Mungu na kwamba, tunapoyapokea kwa mioyo iliyo radhi, tutakuwa tumeandaliwa vizuri zaidi kukutana na Mwanawe, Yesu Kristo, katika ujio Wake. Tutakuwa karibu ya kuwa watu wa Sayuni na kuhisi furaha isiyo kifani na wale ambao tumewasaidia katika njia ya ufuasi. Kwamba na tufanye hivyo ndiyo sala yangu ya unyenyekevu katika jina la Yesu Kristo, amina.