2010–2019
Manabii Wanazungumza kwa Uwezo wa Roho Mtakatifu;
Aprili 2018


Manabii wanazungumza kwa Uwezo wa Roho Mtakatifu

Kuwa na manabii ni ishara ya upendo wa Mungu kwa watoto Wake. Wanafanya zijulikane ahadi na asili ya kweli ya Mungu na Yesu Kristo kwa watu Wao.

Wapendwa akina kaka na akina dada, popote mnapoweza kuwa, ningependa kuelezea shukrani zangu za dhati na za kina kwa kura zenu za kukubali jana. Ingawa ninahisi kukosa ufasaha na nina kigugumizi kama Musa, ninajipa moyo kwa maneno ya Bwana kwake:

“Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kuwa kipofu? Si mimi, Bwana?

“Basi sasa, enenda, nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na kukufundisha utakalolinena” (Kutoka 4:11–12; ona pia mstari wa 10).

Ninajipa moyo pia katika upendo na msaada wa mke wangu mpendwa. Yeye amekuwa mfano wa wema, upendo, na kujitoa kikamilifu kwa Bwana kwa ajili yangu na familia yangu. Ninampenda kwa kila wakia ya moyo wangu, na ninashukuru kwa ushawishi chanya ambao amekua nao kwetu.

Akina kaka na akina dada, ninashuhudia kwenu kwamba Rais Russell M. Nelson ni nabii wa Mungu duniani. Kamwe sijawahi kumuona yeyote mkarimu na mwenye upendo zaidi ya alivyo. Japo nilihisi nisiyestahili kwa wito huu mtakatifu, maneno yake na mtazamo wake wa upole katika macho yake wakati alipotoa jukumu hili vilinifanya nihisi kukumbatiwa na upendo wa Mwokozi. Asante, Rais Nelson. Ninakuhidhinisha na kukupenda.

Akina kaka na akina dada, je, hii si baraka kuwa na manabii, waonaji, na wafunuzi duniani katika siku hizi ambazo tunaishi, wanaotafuta kujua mapenzi ya Bwana na kuyafuata? Inatia faraja kujua kwamba hatuko peke yetu katika ulimwengu, licha ya changamoto tunazopata katika maisha. Kuwa na manabii ni ishara ya upendo wa Mungu kwa watoto Wake. Wanafanya zijulikane ahadi na asili ya kweli ya Mungu na Yesu Kristo kwa watu Wao. Nimejifunza hivyo kupitia uzoefu wangu mwenyewe.

Miaka kumi na minane iliyopita, mimi na mke wangu tulipokea simu kutoka kwa Rais James E. Faust, wakati huo Mshauri wa Pili katika Urais wa Kwanza. Aliniita kutumikia kama rais wa misheni na mwenza wangu katika Ureno. Alituambia kwamba tulikuwa na wiki sita tu kabla ya kuanza misheni yetu. Japokuwa tulihisi kutokuwa tayari na kuwa na mapungufu, tulikubali wito. Wasiwasi wetu mkubwa wakati huo ulikuwa kupata viza iliyohitajika kutumikia katika nchi hiyo kwa sababu, kulingana na uzoefu wa nyuma, tulijua mchakato ulichukua miezi sita mpaka nane kumalizika.

Rais Faust kisha aliuliza kama tulikuwa na imani kwamba Bwana angetenda muujiza na kwamba tungeweza kutatua suala la viza haraka. Jibu letu lilikuwa “ndiyo” kubwa, na tulianza kufanya mipangilio mara moja. Tuliandaa hati zilizohitajika kwa ajili ya viza, tulichukua familia yetu changa, na kwenda ubalozi mdogo haraka kadiri tulivyoweza. Mwanamke mwema alikutana nasi pale. Katika kupitia karatasi zetu na kutaka kujua kile tulichokuwa tukienda kukifanya Ureno, alituuliza, “Hivi ni kweli mnakwenda kuwasaidia watu wa nchi yangu?” Kwa ujasiri tulijibu “ndiyo” na kuelezea kwamba tungemwakilisha Yesu Kristo na kushuhudia kuhusu Yeye na wito Wake mtakatifu ulimwenguni. Tulirudi pale wiki nne baadaye, tulipokea viza zetu, na tulifika kwenye eneo la misheni ndani ya wiki sita, kama nabii wa Bwana alivyotuomba kufanya.

Akina kaka na akina dada, kutoka kwa ndani ya moyo wangu, inashuhudia kwamba manabii wanazungumza kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Wanashuhudia kuhusu Kristo na wito Wake mtakatifu duniani. Wanawakilisha wazo na moyo wa Bwana na wameitwa kumwakilisha Yeye na kutufundisha kile tunapaswa kufanya kurudi kuishi katika uwepo wa Mungu na Mwana Wake, Yesu Kristo. Tunabarikiwa tunapoonyesha imani yetu na kufuata mafundisho yao. Kwa kuwafuata, maisha yetu yana furaha na changamoto kidogo, magumu yetu na matatizo yetu yanakuwa rahisi kuvumilika, na tunatengeneza ngao ya kiroho kutuzunguka ambayo itatulinda kutokana na mashambulizi ya adui katika siku yetu.

Katika hii siku ya Pasaka ninashuhudia kwa dhati kwamba Yesu Kristo alifufuka, Yu hai na Anaongoza Kanisa Lake duniani kupitia manabii Wake, waonaji, na wafunuzi. Ninashuhudia kwamba Yeye ni Mwokozi na Mkombozi wa ulimwengu na kwamba kupitia Yeye tunaweza kuokolewa na kuinuliwa katika uwepo wa Mungu wetu mpendwa. Ninampenda; ninamhusudu. Ninataka kumfuata na kufanya mapenzi Yake na kuwa zaidi kama Yeye. Ninasema mambo haya kwa unyenyekevu katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.