2010–2019
Kufundisha Nyumbani—Wajibu Wenye Shangwe na Mtakatifu
Aprili 2018


Kufundisha Nyumbani—Wajibu Wenye Shangwe na Mtakatifu

Ninaomba msaada wa mbinguni tunapojitahidi kuwa walimu kama Kristo katika nyumba zetu.

Mke wangu, Julie, nami tumewalea watoto sita wenye thamani, na hivi majuzi tumekuwa viota vitupu. Jinsi gani ninawakosa kuwa na watoto wetu katika nyumba yetu wakati wote. Ninakosa kujifunza kutoka kwao na kuwafundisha.

Leo ninaelekeza mazungumzo yangu kwa wazazi wote na wote wanaotaka kuwa wazazi. Wengi wenu mnawalea watoto sasa. Kwa wengine, wakati huo unaweza kuja hivi karibuni. Na kwa wengine bado, uzazi unaweza kuwa baraka za baadaye. Ninaomba sisi sote tutambue wajibu wenye shangwe na mtakatifu ni kufundisha mtoto.1

Kama wazazi, tunawasilisha watoto wetu kwa Baba wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo. Tunawasaidia watoto wetu kusema sala zao za kwanza. Tunatoa mwongozo na msaada wanapoingia njia ya agano2 kupitia kwa ubatizo. Tunawafundisha kutii amri za Mungu. Tunawaelimisha kuhusu mpango Wake kwa watoto Wake, na tunawasaidia kutambua, ushawishi wa Roho Mtakatifu. Tunawaambia hadithi za manabii wa kale na kuwahimiza kufuata walio hai. Tunaomba kwa ajili ya ushindi wao na kulia nao wakati wa majaribio yao. Tunawashuhudia watoto wetu juu ya baraka za hekalu, na tunajitahidi kuwaandaa vizuri kutumikia misheni. Tunatoa ushauri wa upendo watoto wetu wanapokuwa wazazi wenyewe. Lakini—hata wakati huo—hatuwezi kuacha kuwa wazazi wao. Hatuwezi kuacha kuwa walimu wao. Hatuwezi kuachiliwa kutoka kwenye miito hii ya milele.

Leo hebu tufikirie baadhi ya fursa za ajabu ambazo tunazo za kuwafundisha watoto wetu katika nyumba zetu.

Ufundishaji wa Jioni ya Familia Nyumbani

Hebu tuanze na jioni ya familia nyumbani, ambayo ilikuwa kipaumbele cha juu katika nyumba iliyojaa imani kule ambapo nililelewa. Sikumbuki masomo maalum yaliyofundishwa katika jioni ya familia nyumbani, lakini ninakumbuka kuwa hatukukosa kila wiki.3 Nilijua kilicho muhimu kwa wazazi wangu.4

Nakumbuka mojawapo ya shughuli zangu nipendazo za jioni za familia nyumbani. Baba angemwalika mmoja wa watoto wake kufanya “Mtihani.” Angempa mtoto mfululizo wa maelekezo kama, “Kwanza, nenda jikoni na ufungue na ufunge friji. Kisha kimbia ndani ya chumba changu cha kulala na unyakue jozi ya soksi kutoka kwa kabati langu. Kisha urudi kwangu, uruke juu na chini mara tatu, na useme, ‘Baba, nimetimiza!’”

Nilipenda wakati ilipokuwa ni zamu yangu. Nilitaka kupata kila hatua sawa, na nilithamini wakati ambapo ningeweza kusema, “Baba, nimetimiza!” Shughuli hii ilisaidia kuimarisha ujasiri wangu na kuifanya rahisi kwa kijana asiye na utulivu kuzingatia wakati mama au baba alipofundisha kanuni ya injili.

Rais Gordon B. Hinckley alishauri: “Ukiwa una shaka yoyote juu ya wema wa jioni ya familia nyumbani, ijaribu. Wakusanye watoto wako karibu na wewe, wafundishe, watolee ushuhuda, someni maandiko pamoja na kuwa na wakati wa furaha pamoja.”5

Daima kutakuwa na upinzani wa kufanya jioni ya familia nyumbani.6 Bila kujali, nakualika kutafuta njia katikati ya vikwazo na kuipa kipaumbele jioni ya familia nyumbani—na kuweka burudani kiungo muhimu.

Ufundishaji wa Maombi ya Familia

Maombi ya familia ni fursa nyingine kubwa ya kufundisha.

Ninapenda jinsi baba ya Rais N. Eldon Tanner alivyomfundisha wakati wa sala ya familia. Rais Tanner alisema hivi:

“Ninakumbuka jioni moja tulipokuwa tukipiga magoti kwa sala ya familia, baba yangu alimwambia Bwana, ‘Eldon alifanya kitu leo ambacho hakupaswa kufanya; ameomba msamaha, na kama utamsamehe, hatakifanya tena.

“Hilo lilinifanya kutokufanya tena—zaidi kuliko vile kichapo kingefanya.”7

Kama mvulana, wakati mwingine ningekasirishwa na sala zetu za familia zilizoonekana kuwa nyingi, nikifikiri kwa nafsi yangu, “Je! Hatukuomba tu dakika chache zilizopita?” Sasa, kama mzazi, najua hatuwezi kuomba sana kama familia.8

Nimevutiwa daima na jinsi Baba wa Mbinguni anavyomtambulisha Yesu Kristo kama Mwana Wake Mpendwa.9 Ninafurahia kuwaombea watoto wangu kwa majina huku wakinisikiliza nikielezea Baba wa Mbinguni jinsi walivyo wapendwa kwangu mimi. Inaonekana hakuna wakati mzuri wa kuwasilisha upendo kwa watoto wetu kuliko wakati wa kuomba pamoja nao au kuwabariki. Wakati familia zinapokusanyika kwa maombi ya unyenyekevu, masomo yenye nguvu na ya kudumu yanafundishwa.

Ufundishaji wa Dharura

Mafundisho ya wazazi ni kama kuwa daktari wa dharura. Daima tunatakiwa kuwa tayari kufundisha watoto wetu kwa sababu hatujui wakati fursa itajitokeza.

Picha
Yesu na mwanamke Msamaria kisimani

Sisi ni kama Mwokozi, ambaye mafundisho yake mara nyingi “hayakufanyika katika sinagogi lakini katika mazingira ya kila siku yasiyo rasmi—akila chakula na wanafunzi Wake, kuchota maji kisimani, au kupita kando ya mti wa mtini.10

Miaka iliyopita, mama yangu alishiriki mazungumzo yake mawili mazuri ya injili pamoja na ndugu yangu mkubwa, Matt, wakati mmoja alipokuwa akikunja nguo na wakati mwingine alipokuwa akimpeleka kwa daktari wa meno. Mojawapo ya mambo mengi niliyotamani kuhusu mama yangu ilikuwa ni utayari wake wa kufundisha watoto wake.

Ufundishaji wake kama mzazi haujawahi kukoma. Nilipokuwa nikihudumu kama askofu, mama yangu, akiwa wa umri wa miaka 78, aliniambia nilihitaji kunyolewa. Alijua kwamba nilihitaji kuwa mfano, na hakusita kuniambia hivyo. Nakupenda, Mama!

Kama baba, nimehamasishwa kujifunza na kutafakari maandiko ili niweze kujibu wakati watoto wangu au wajukuu wanapowasilisha mwito wa ufundishaji wa dharura.11 “Baadhi ya nyakati bora zaidi za kufundisha huanza kama swali au wasiwasi katika moyo wa mwana [familia].”12 Je! Tunasikiliza wakati huo?13

Ninapenda mwaliko wa Mtume Petro, “Muwe tayari siku zote kumjibu kila mtu [na naongeza, mtoto] awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu.14

Nilipokuwa kijana, baba yangu na mimi tulifurahia kupatiana changamoto ili tuone ni nani ambaye alikuwa na nguvu nyingi zaidi ya kushikilia. Tungefinyilia mkono wa mwingine kwa nguvu iwezekanavyo kwa jitihada za kumfanya mwingine kuhisi maumivu. Haionekani kuwa burudani sana sasa, lakini kwa namna fulani ilikuwa wakati huo. Baada ya mapambano kama hayo, baba aliniangalia machoni na kusema, “Una mikono yenye nguvu, mwanangu. Natumaini mikono yako itakuwa na nguvu daima ili usiweze kamwe kugusa mwanamke mdogo vibaya.” Kisha akanialika nikae msafi kimaadili na kuwasaidia wengine kufanya hivyo.

Mzee Douglas L. Callister alishiriki haya kuhusu baba yake: “Nilipokuwa nikisafiri nyumbani kutoka kazini siku moja Baba alisema kwa hiari, ‘Nililipa zaka yangu leo. Niliandika “asante” juu ya fungu la kumi. Ninamshukuru Bwana kwa kuibariki familia yetu.

Mzee Callister alitoa ushuhuda huu juu ya baba yake-mwalimu: “Alifundisha vitendo na mtazamo wa utii.”15

Ninadhani ni busara kujiuliza mara kwa mara, “Nitafundisha nini, au ninafundisha nini, watoto wangu kwa vitendo na mtazamo wangu wa utii?”

Ufundishaji wa Maandiko kwa Familia

Kujifunza maandiko kwa familia ni jukwaa bora la kufundisha mafundisho nyumbani.

Rais Russell M. Nelson alisema, “Si eti tu wazazi wanapaswa kushikilia neno la Bwana, lakini wana jukumu takatifu la kuifundisha kwa watoto wao.”16

Julie nami tulivyowalea watoto wetu, tulijaribu kuwa thabiti na ubunifu. Mwaka mmoja, tuliamua kusoma Kitabu cha Mormoni kwa Kihispania kama familia. Inaweza kuwa ndiyo sababu Bwana aliwaita kila mmoja wa watoto wetu ambao walitumikia misheni katika misheni ya Kihispania? Es posible.

Niliguswa sana wakati Ndugu Brian K. Ashton aliposhiriki nami kwamba yeye na baba yake waliisoma kila ukurasa wa Kitabu cha Mormoni pamoja wakati wa mwaka wake mwisho wa shule ya sekondari. Ndugu Ashton anapenda maandiko. Yameandikwa katika akili yake na kwa moyo wake. Baba yake alipanda mbegu wakati Ndugu Ashton alipokuwa kijana, na mbegu hio17 imekua kuwa mti wa kweli wenye mizizi imara. Ndugu Ashton amefanya vivyo hivyo na watoto wake wakubwa.18 Mwanawe mwenye umri wa miaka minane hivi majuzi alimwuliza, “Baba, ni lini nitasoma Kitabu cha Mormoni?”

Ufundishaji kwa Mfano

Hatimaye, ufundishaji wetu wazazi wenye matokeo ni mfano wetu. Tunashauriwa kuwa “kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.”19

Wakati wa safari ya hivi majuzi, Julie nami tulihudhuria kanisa na tuliona aya hii kwa vitendo. Kijana, ambaye anaondoka hivi karibuni kwenda misheni yake, alizungumza katika mkutano wa sakramenti.

Alisema, “Ninyi nyote mnafikiri baba yangu ni mtu mzuri sana kanisani, lakini …” Alisita, na mimi nilishangaa ni nini kinachofuata ataweza kusema. Aliendelea na kusema, “Yeye ni mtu mzuri nyumbani.”

Picha
Familia ya Stewart

Nilimshukuru kijana huyu baadaye kwa ajili ya sifa ya msukumo aliyomtolea baba yake. Kisha niligundua kwamba baba yake alikuwa askofu wa kata. Ingawa askofu huyu alikuwa akihudumia kata yake kwa uaminifu, mwanawe alihisi kuwa kazi yake bora ilifanyika nyumbani.20

Mzee D. Todd Christofferson anashauri: “Tuna fursa nyingi za kufundisha … kizazi kinachoinukia, na tunapaswa kutoa mawazo yetu bora na jitihada za kupata faida kamili kwao. Zaidi ya yote, ni lazima tuendelee kuwahimiza na kuwasaidia wazazi kuwa walimu bora na thabiti … hasa kwa mfano.”21

Hivyo ndivyo Mwokozi anavyofundisha.22

Wakati wa likizo wa hivi majuzi na watoto wetu wawili wadogo, Julie alipendekeza tufanye ubatizo wa wakala katika Hekalu kote St. George na San Diego. Nilijinung’unikia—binafsi—nikifikiria, “Tunahudhuria hekalu nyumbani, na sasa tuko kwenye likizo. Kwa nini usifanye kitu kama cha likizo zaidi?” Baada ya ubatizo, Julie alitaka kuchukua picha nje ya hekalu. Nilinung’unika kimya kimya—tena. Unaweza kukisia ni nini kilichotokea tena-tulipiga picha.

Picha
Kina Durrant katika Hekalu la San Diego
Picha
Kina Durrant katika Hekalu la St. George

Julie anataka watoto wetu wawe na kumbukumbu za jinsi tulivyowasaidia babu zetu, na hivyo mimi pia. Hatukuhitaji somo rasmi juu ya umuhimu wa hekalu. Tuliishi—shukrani kwa mama ambaye anapenda hekalu na anataka watoto wake washiriki upendo huo.

Wakati wazazi wanapotunzana na kutoa mifano mema, watoto wanabarikiwa milele.

Hitimisho

Kwa ninyi nyote mnaojitahidi kufanya kazi nzuri ya kufundisha katika nyumba zenu, na muweze kupata amani na furaha katika jitihada zenu. Na kama unahisi kuwa una nafasi ya kuboresha au unahitaji maandalizi makubwa, tafadhali jibu kwa unyenyekevu uvuvio wa Roho anavyokuhimiza na ujifunge kutenda.23

Mzee L. Tom Perry alisema, “Afya ya jamii yoyote, furaha ya watu wake, mafanikio yao, na amani yao yote hupata mizizi ya kawaida katika mafundisho ya watoto nyumbani.”24

Ndiyo, kiota changu cha nyumbani sasa ni tupu, lakini bado niko kwa mwito, tayari na hamu ya kupata fursa za ziada za kufundisha watoto wangu wazima, watoto wao, na siku moja, natumaini, watoto wao.

Ninaomba msaada wa mbinguni tunapojitahidi kuwa walimu kama Kristo katika nyumba zetu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona Mafundisho na Maagano 68:25; 93:40.

    Mzee L. Tom Perry alifundisha: “Ushawishi wa adui ni mkubwa sana na yeye ni hushambulia, kujaribu kumomomyoa na kuharibu msingi wa jamii yetu, hata familia. Wazazi wanapaswa kuamua kwamba kufundisha nyumbani ni jukumu takatifu zaidi na muhimu” (“Mothers Teaching Children in the Home,” Liahona, May 2010, 30).

    Urais wa Kwanza na Jamii ya Mitume Kumi na Wawili wamefundisha: “Mume na mke wana jukumu muhimu la kupenda na kutunzana mmoja na mwingine na watoto wao. “Watoto ni urithi wa Bwana” (Zaburi 127:3). Wazazi wana jukumu takatifu la kulea watoto wao katika upendo na utakatifu, kukimu mahitaji yao ya kimwili na kiroho, na kuwafundisha kupenda na kutumikiana mmoja na mwingine, kutii amri za Mungu, na kuwa wananchi wenye kutii sheria popote wanapoishi. Wanaume na wanawake—kina mama na kina baba—watawajibika mbele za Mbungu kwa kufanya majukumu haya” (“The Family: A Proclamation to the World,” Liahona, May 2017, 145).

  2. Ona Russell M. Nelson, “,” Liahona, Apr. 2018, 7.

  3. Mzee David A. Bednar alisema: “Leo ikiwa unaweza kuuliza wana wetu wazima wanachokumbuka kuhusu sala ya familia, kusoma maandiko, na jioni ya familia nyumbani, naamini ninajua jinsi watakavyojibu. Huenda hawatatambua sala maalum au mfano maalum wa masomo ya maandiko au somo la jioni ya familia nyumbani la maana sana kama wakati wa ajabu katika maendeleo yao ya kiroho. Kile wangeweza kusema wanakumbuka ni kwamba kama familia tulikuwa thabiti” (“More Diligent and Concerned at Home,” Liahona, Nov. 2009, 19).

  4. Ona “Home Can Be a Heaven on Earth,” Hymns, no. 298.

  5. Teachings of Presidents of the Church: Gordon B. Hinckley (2016), chapter 171.

  6. Ona 2 Nefi 2:11.

  7. N. Eldon Tanner, “Never Be Ashamed of the Gospel of Christ,” Ensign, Feb. 1980, 4.

  8. Ona 3 Nefi 18:21.

  9. Ona Mathayo 3:16–17; 3 Nefi 11:6–8; Mafundisho na Maagano 18:34–36; Joseph Smith—Historia 1:17.

  10. “Take Advantage of Spontaneous Teaching Moments,” Teaching in the Savior’s Way (2016), 16. Kufundisha katika Njia ya Mwokozi inajumuisha mbinu na rasmali kadha kwa kufundisha nyumbani.

  11. Ona Mafundisho na Maagano 11:21; 84:85.

  12. Kufundisha katika Njia ya Mwokozi, 16.

  13. OnaPreach My Gospel: A Guide to Missionary Service (2004), 185-86.

  14. 1 Petro 3:15.

  15. Douglas L. Callister, “Most Influential Teacher—Emeritus Seventy Pays Tribute to Father,” Aug. 29, 2016, news.lds.org.

  16. Ona Russell M. Nelson, “Set in Order Thy House,” Liahona, Jan. 2002, 81.

  17. Ona Alma 32:28-43.

  18. Sister Melinda Ashton pinch-hits when her husband, Brother Ashton, is out of town.

  19. 1 Timotheo 4:12; ona pia Alma 17:11.

  20. Askofu Jeffrey L. Stewart anahudumu katika kata ya Pili ya Southgate huko St. George, Utah. Samuel, mwanawe, sasa anahudumu katika misheni ya Colombia Medellín.

  21. D. Todd Christofferson, “Strengthening the Faith and Long-Term Conversion of the Rising Generation,” in General Conference Leadership Meeting, Sept. 27, 2017.

  22. (Ona 3 Nefi 27:21, 27.)

  23. Ona Mafundisho na Maagano 43:8-9.

  24. L. Tom Perry, “Mothers Teaching Children in the Home,” 30.