2010–2019
Nguvu za Ukuhani
Aprili 2018


Nguvu za Ukuhani

Kukuza ukuhani mtakatifu ambao mnao ni muhimu katika kazi ya Bwana katika familia zenu na miito yenu kanisani.

Ndugu zangu wapendwa, tumesikia kuhusu tangazo la ufunuo kutoka kwa Rais Russell M. Nelson. Tumesikia kuhusu ufafanuzi muhimu toka kwa Wazee Christofferson na Rasband na Rais Eyring. Kile ambacho bado kitasemwa, ikijumuisha zaidi kutoka kwa Rais Nelson, kitafafanua kile ninyi, viongozi mlioitwa na Bwana na wenye ukuhani, mtafanya katika majukumu yenu. Kusaidia katika hilo, nitafanya marejeo katika baadhi ya kanuni muhimu zinazosimamia ukuhani mlionao.

I. Ukuhani:

Ukuhani wa Melkizedeki ni mamlaka matakatifu aliyoyatoa Mungu ili kufanikisha kazi Yake ya “kuleta kutokufa na uzima wa milele wa wanadamu” (Musa 1:39). Katika mwaka 1829, yalitolewa kwa Joseph Smith na Oliver Cowdery kupitia Mitume wa Mwokozi Petro, Yakobo na Yohana (ona Mafundisho na Maagano 27:12). Ni matakatifu na yana nguvu kuliko uwezo wa nguvu zetu kuelezea.

Funguo za ukuhani ni nguvu za kuongoza utumiaji wa mamlaka ya ukuhani. Hivyo, wakati Mitume walipowapa Ukuhani wa Melkizedeki Joseph na Oliver, waliwapa pia funguo za kuongoza utumiaji wake (ona Mafundisho na Maagano 27:12–13). Lakini si funguo zote walipewa wakati ule. Funguo zote muhumu kwa ajili ya “kipindi cha utimilifu wa nyakati” (M&M 128:18) zinatolewa “mstari juu ya mstari” (mstari wa 21). Funguo zaidi zilitolewa kwenye Hekalu la Kirtland miaka saba baadae (ona Mafundisho na Maagano110:11–16). Funguo hizi zilitolewa kuongoza mamlaka ya ukuhani katika kazi za ziada zilizotolewa wakati huo, kama vile ubatizo kwa niaba ya wafu.

Ukuhani wa Melkizedeki si hali au alama. Ni nguvu tukufu inayomilikiwa kwa ajili ya manufaa ya kazi ya Mungu kwa watoto Wake. Lazima mara zote tukumbuke kwamba wanaume wenye ukuhani si “ukuhani.” Si sahihi kutumia “ukuhani na wanawake.” Tunatakiwa kutumia “wenye ukuhani na wanawake.”

II. Kazi ya Huduma

Sasa tufikirie kile Bwana Yesu Kristo anatarajia kutoka kwa wale wenye ukuhani Wake—jinsi ya kuleta nafsi Kwake.

Rais Joseph F. Smith alifundisha “Ni kweli imesemwa kwamba Kanisa limepangwa kikamilifu. Tatizo pekee ni kwamba jumuiya kama hizi haziko hai kikamilifu katika wajibu ulioko juu yake. Wakati zitaamshwa kikamilifu katika yale yanayohitajika toka kwao, zitatimiza majukumu yao kwa uaminifu zaidi, na kazi ya Bwana itakuwa imara zaidi na ya nguvu zaidi na ya kuleta athari duniani.”1

Rais Smith pia alitoa tahadhari:

“Vyeo vya heshima vilivyotolewa na Mungu … vinayohusiana na baadhi ya ofisi ndani ya na katika utaratibu wa Ukuhani Mtakatifu, havitakiwi kutumika au kuchukuliwa kama vyeo vitokanavyo na mwanadamu, si vya ubwana au kujikweza, lakini ni uteuzi wa huduma nyenyekevu katika kazi ya Bwana mmoja ambaye tunadai kumtumikia. …

“… Tunafanya kazi kwa ajili ya ukombozi wa nafsi, na tunatakiwa kuhisi kwamba hili ni jukumu kubwa sana ambalo liko juu yetu. Hivyo ni lazima tuhisi utayari kujitolea kila kitu, kama itahitajika, kwa sababu ya upendo kwa Mungu, ukombozi wa mwanadamu, na ushindi wa ufalme wa Mungu Duniani.”2

III. Ofisi za Ukuhani

Katika Kanisa la Bwana, ofisi katika ukuhani wa Melkizedeki zina kazi tofauti. Mafundisho na Maagano hurejea kuhani mkuu kama “marais wasimamizi au watumishi juu ya vigingi mbalimbali vilivyoenea ng’ambo” (Mafundisho na Maagano 124:134). Inarejea kuhusu wazee kama “wahudumu wa kudumu kwa kanisa la [Bwana]” (Mafundisho na Maagano 124:137). Hapa kuna mafundisho mengine kuhusu kazi hizo tofauti

Kuhani mkuu anasimamia na kuhudumia katika mambo ya kiroho (ona Mafundisho na Maagano 107:10, 12). Pia, kama alivyosema Rais Joseph F. Smith, ikiwa kama ametawazwa kuwa kuhani mkuu, [ana] takiwa ahisi kwamba ana jukumu … la kuwa mfano stahiki wa kufuatwa, mbele ya wakubwa na wadogo, na kuwa mwalimu wa utakatifu, si tu kwa kanuni lakini hususan zaidi kwa mfano—akiwanufaisha wadogo kwa uzoefu wa umri, na hivyo kuwa mtu wa nguvu katika jamii anayoishi.”3

Kuhusu majukumu ya mzee, Mzee Bruce R. McConkie wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alifundisha: “Mzee ni mtumishi wa Bwana Yesu Kristo. … Amewepa mamlaka ya kusimama katika nafasi kwa niaba ya Bwana wake … katika kuwatumikia wenzake. Yeye ni wakala wa Bwana.”4

Mzee McConkie alikosoa wazo la kwamba mtu ni “mzee tu.” Kila mzee Kanisani ana ukuhani sawa na Rais wa Kanisa … ,” alisema. “Mzee ni nani? Ni mchungaji, mchungaji anayetumikia katika zizi la Mchungaji Mwema.”5

Katika shughuli hii muhimu ya kuhudumu katika zizi la Mchungaji Mwema, hakuna tofauti kati ya ofisi ya kuhani mkuu na mzee katika ukuhani wa Melkizedeki. Katika mlango wa 107 wa Mafundisho na Maagano, Bwana anatangaza, “Makuhani wakuu kwa mfano wa Ukuhani wa Melkizedeki wanayo haki ya kutenda kazi katika nafasi yao wenyewe, chini ya maelekezo ya urais, katika kuhudumu katika mambo ya kiroho, na pia katika ofisi ya mzee [au ofisi katika Ukuhani wa Haruni]” (Mafundisho na Maagano 107:1; ona pia mstari wa 12).

Kanuni muhimu kwa wenye ukuhani wote ni kanuni iliyofundishwa na nabii Yakobo wa Kitabu cha Mormoni. Baada ya yeye na Yusufu kaka yake kutawazwa kuwa makuhani na waalimu wa watu, alitangaza, “na tuliadhimisha ofisi yetu kwa Bwana, tukijichukulia jukumu, na wajibu wa dhambi za watu vichwani mwetu kama hatungewafunza neno la Mungu kwa bidii yote” (Yakobo 1:19).

Ndugu, wajibu wetu kama wenye ukuhani ni jambo la muhimu. Jumuiya zingine zinaweza kuridhika na viwango vya kiutendaji vya dunia katika kutoa ujumbe wao na ufanyaji kazi wao wenyewe. Lakini sisi ambao tuna ukuhani wa Mungu tuna nguvu tukufu ambayo inaongoza katika lango la ufalme wa selestia wa Mungu. Tuna dhumuni na wajibu ambao Bwana ametaja katika utangulizi uliofunuliwa katika Mafundisho na Maagano. Tunatakiwa kutangaza kwa ulimwengu:

“Kwamba kila mwanadamu aweze kuongea katika jina la Mungu Bwana, hata Mwokozi wa ulimwengu;

“Kwamba imani pia ipate kuongezeka katika dunia;

“Kwamba agano langu lisilo na mwisho liweze kuanzishwa;

“Kwamba utimilifu wa injili yangu uweze kutangazwa na watu walio dhaifu na wa kawaida hata mwisho wa dunia”(Mafundisho na Maagano 1:20–23).

Ili kutimiza agizo hili tukufu, lazima tuwe waaminifu katika “kukuza” ukuhani wetu na majukumu (ona Mafundisho na Maagano 84:33). Rais Harlod B. Lee alifafanua inamaanisha nini kukuza ukuhani: “Wakati mtu anapokuwa na ukuhani anakuwa wakala wa Bwana. Anatakiwa afikirie wito wake kama vile alikuwa kwenye kazi ya Bwana. Hii ndio maana ya kukuza ukuhani.”6

Kwa hivyo, ndugu, kama Bwana Mwenyewe angekuomba kumsaidia mmoja wa wana au binti Zake—ambavyo amekwisha fanya kupitia watumishi Wake—je, ungefanya hivyo? Na kama ungefanya hivyo, je, ungefanya kama wakala Wake, “katika kazi yake,” ukitegemea msaada Alioahidi?

Rais Lee alikuwa na fundisho lingine kuhusu kukuza wito wa ukuhani: “Wakati unabeba kiookuzi juu ya kitu, inakifanya kitu hicho kuonekana kikubwa kuliko ambavyo ungekiona kwa macho ya kawaida; hicho ndiyo kiookuzi. Sasa … kama mtu yoyoye anakuza wito wa ukuhani—hiyo ni, kuufanya kuonekana mkubwa kuliko walivyofikiri hapo awali na muhimu zaidi kuliko mtu yoyote mwingine alivyodhani ulikuwa—hiyo ndio njia unavyokuza wito wako wa ukuhani.”7

Hapa kuna mfano wa mwenye ukuhani akikuza majukumu yake ya ukuhani. Nilisikia kutoka kwa mwenzangu Mzee Jeffrey D. Erekson, katika mkutano wa kigingi huko Idaho. Kama kijana aliyeoa hivi karibuni, akiwa masikini na kuhisi hawezi kumaliza mwaka wake wa mwisho chuoni, Jeffrey aliamua kuacha chuo na kukubali kazi ya kuvutia. Siku chache baadaye rais wake wa akidi ya wazee alikuja nyumbani kwake. “Unaelewa umuhimu wa funguo za ukuhani ambazo ninazo?” rais wa akidi aliuliza. Wakati Jeffrey alipojibu kuwa alijua, rais akamwambia kwamba tangu aliposikia nia yake ya kuacha chuo, Bwana amekuwa akimsumbua usiku asiweze kulala ili ampe ujumbe huu Jeffrey: “Kama rais wako wa akidi ya wazee, nakushauri kutoacha chuo. Huo ni ujumbe kwako kutoka kwa Bwana.” Jeffrey alibaki shuleni. Miaka baadae nilikutana nae akiwa kama mfanya biashara mwenye mafanikio na nilimsikia akiliambia kusanyiko la wenye ukuhani, “kwamba [ushauri] ule umeleta tofauti yote katika maisha yangu.”

Mwenye ukuhani alikuza ukuhani na wito, na hiyo ilileta “tofauti yote” katika maisha ya mtoto mwingine wa Mungu.

IV. Ukuhani katika Familia

Mpaka sasa, nimekuwa nikizungumzia kuhusu kazi za ukuhani katika Kanisa. Sasa nitazungmzia kuhusu ukuhani katika familia. Ninaanza na funguo. Kanuni ya kwamba mamlaka ya ukuhani yanaweza tu kutumika chini ya uongozi wa mmoja ambaye ana funguo kwa ajili ya kazi hiyo ni muhimu katika Kanisa lakini haitumiki katika kutumia mamlaka ya ukuhani katika familia.8 Baba mwenye ukuhani anaongoza katika familia yake kwa mamlaka ya ukuhani aliyonayo. Haitaji kuwa na mwongozo au ruhusa ya funguo za ukuhani ili kuweza kushauri wanafamilia wa familia yake, kuwa na mikutano ya familia, kutoa baraka za ukuhani kwa mkewe na watoto, au kutoa baraka za uponyaji kwa mwanafamilia au wengine.

Picha
Familia ikijifunza pamoja

Kama akina baba wangekuza ukuhani wao katika familia yao, ingesogeza mbele kazi ya Kanisa zaidi ya kingine chochote ambacho wangeweza kufanya. Akina baba wenye Ukuhani wa Melkizedeki lazima watii amri ili waweze kuwa na nguvu za ukuhani kutoa baraka kwa wanafamilia wao. Akina baba lazima pia wakuze mahusiano yenye upendo ya familia ili kwamba wanafamilia watataka kuwaomba baba zao baraka. Na wazazi lazima wahimize kupata baraka zaidi za kikuhani katika familia.

Picha
Baraka za Ukuhani

Akina baba hufanya kazi kama “wenzi sawa” wa wake zenu, kama tangazo la familia linavyofundisha.9 Na, akina baba wakati umepata fursa ya kutumia nguvu na ushawishi wa mamlaka ya ukuhani wako, fanya hivyo “kwa ushawishi, kwa uvumilivu, kwa upole na unyenyekevu, na kwa upendo usio unafiki” (Mafundisho na Maagano 121:41). Hicho kiwango cha juu kwa ajili ya utumiaji wa mamlaka ya ukuhani ni muhimu zaidi katika familia. Rais Harold B. Lee alitoa ahadi hii baada tu ya kuwa Rais wa Kanisa: “Kamwe nguvu za ukuhani, ambao mnao, hazijawa nzuri zaidi kama wakati ambapo kuna tatizo katika nyumba zenu, maradhi makali, au kufanya baadhi ya chaguzi muhimu. … Zikivikwa kwenye nguvu za ukuhani, ambazo ni nguvu za Mwenyezi Mungu, ni nguvu za kufanya miujiza kama ni mapenzi ya Bwana, lakini ikiwa tunataka kutumia ukuhani huo, lazima tuwe wastahiki kuutumia. Kushindwa kuelewa kanuni hii ni kushindwa kupokea baraka ya kuwa wenye ukuhani huo mkuu.”10

Ndugu zangu wapendwa, kukuza ukuhani mtakatifu ambao mnao ni muhimu katika kazi ya Bwana katika familia zenu na miito yenu Kanisani.

Namshuhudia Yeye ambaye huu ukuhani ni wake. Kupitia mateso ya upatanisho Wake na ufufuko, wanaume wote na wanawake wamehakikishiwa kutokufa na nafasi kwa ajili ya uzima wa milele. Kila mmoja wetu lazima awe mwaminifu na mwenye bidii katika kutenda sehemu yetu katika kazi hii kuu ya Mungu Baba Yetu wa Milele, katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Teachings of Presidents of the Church: Joseph F. Smith(1998), 343.

  2. Teachings: Joseph F. Smith, 340, 343.

  3. Joseph F. Smith, Gospel Doctrine, 5th ed. (1939), 182.

  4. Bruce R. McConkie, “Only an Elder,” Ensign, June 1975, 66; emphasis in original not preserved.

  5. Bruce R. McConkie, “Only an Elder,” 66; emphasis in original not preserved.

  6. Teachings of Presidents of the Church: Harold B. Lee (2000), 93.

  7. The Teachings of Harold B. Lee, ed. Clyde J. Williams (1996), 499.

  8. Ona Dallin H. Oaks, “Priesthood Authority in the Family and the Church,” Ensign or Liahona, Nov. 2005, 24–27.

  9. Ona “Familia: Tamko kwa Ulimwengu,” Liahona, Mei. 2017, 145.

  10. Teachings: Harold B. Lee, 97.