2015
Ni Nani Shujaa Wako?
Aprili 2015


Ni nani shujaa Wako?

Mwandishi anaishi katika California, Marekani.

Ellie alijua shujaa wake ni nani, lakini alikuwa mwoga sana kusema.

“Simama na dhamiri yako, heshima yako, imani yako; simama kama shujaa” (Children’s Songbook, 158).

Ellie aliuma kucha la dolegumba lake kwa wasiwasi. Binti Fitz alikuwa anafuata safu ya madawati akiuliza kila mwanafunzi swali, mmoja baada ya mwingine.

“Nani shujaa wako?” Binti Fritz akamwuliza Jeremy.

Jeremy hakupoteza muda kujibu. “Baba yangu!” alisema kwa kujivunia.

Binti Fitz akatabasamu “Na wako Sara?”

Jibu lake likaja haraka vivyo. “Abraham Lincoln.”

Ellie alisikia mapigo ya moyo wake wakati Binti Fitz alipoendelea kwenye safu ya wanafunzi. Walikuwa wamezungumza juu ya mashujaa siku nzima na sasa kila mtu alipaswa kusema ni nani alikuwa shujaa wake—mbele ya darasa zima!

Amber na Justin walisema mama zao walikuwa mashujaa wao. Walter alisema wake alikuwa babu yake. Wanafunzi wengine wachache walisema shujaa wao alikuwa mfalme au rais.

Wanafunzi wachache walisalia kabla ya Binti Fitz kumfikia Ellie. Ilimbidi kufikiria shujaa—na kwa haraka.

Ellie alitazama chini kwenye viatu vyake, akiona haya. Kuamua nani alikuwa shujaa haikuwa shida hasa. Tayari alijua shujaa wake ni nani. Ilikuwa Yesu Kristo. Aliwaponya wagonjwa, alifufua wafu, na kulipa gharama ya dhambi ya kila mtu. Alikuwa shujaa mkuu aliyewahi kuishi! Aliogopa sana kusema hivyo.

Ellie aliuma kucha ya dolegumba lake tena na kufikiria kuliambia darasa zima kwamba Yesu Kristo alikuwa shujaa wake. Ingekuwaje kama Jeremy angemcheka? Na ingekuwaje kama Sara na Amber wangemsengenya wakati wa mapumziko?

Bila shaka alijua kuwa Yesu Kristo alikuwa shujaa wake Lakini hilo halikumaanisha kila mtu alihitaji kujua.

Binti Fitz alisimama hasa mbele ya dawati la Ellie na kutabasamu. “Na shujaa wako ni nani Ellie?”

Ellie alitazama kutoka safu ya wanafunzi waliokuwa karibu naye hadi kwa Binti Fitz. “Abraham Lincoln,” alinong’ona.

Binti Fitz akafurahi “Vyema” alisema alipoenda kwa mwanafunzi aliyefuata katika safu.

Mara tu alipoondoka, mabega ya Ellie yalitua kwa shime. Shukrani, hilo lilikuwa limepita. Jambo la mwisho alilohitaji ilikuwa ni kila mtu kujua ni nani aliyekuwa shujaa wake—

“Yesu Kristo,” sauti ikasema.

Macho ya Ellie yakapanuka alipogeuka pole pole. Pale—chini kidogo ya safu—alikaa mvulana mdogo aliyekuwa na nywele zilizokunjana. Alikuwa mwembamba na mwoga, na kila mara alikaa nyuma ya darasa. Ellie hata hakufahamu jina lake. Hakumkumbuka akisema hata neno moja—hadi sasa.

Wanafunzi wachache waligeuka ili kumkodolea macho yule mvulana lakini hakuwaona. Alimtazama tu Binti Fitz na kuzungumza tena. “Shujaa wangu ni Yesu Kristo.”

Binti Fitz alitabasamu sana na kuendelea kwenye safu. Lakini Ellie alimtazama yule mvulana kwa mshangao Alikuwa amekuwa na uoga wa kumwambia kila mtu kuhusu shujaa wake, lakini mvulana huyu hakuwa mwoga. Hata hakuenda katika kanisa lake! Lakini alijua ilivyokuwa muhimu kusimama kama mfano wa Yesu Kristo hata ilipokuwa vigumu.

Ellie alitabasamu kwa yule mvulana. Hangeogopa tena kusema ni nani aliyekuwa shujaa wake. Kwani, alikuwa na wawili sasa.