2018
Nyosha Mkono kwa Huruma
July 2018


Picha
Ministering

Kanuni za Kuhudumu, Julai 2018

Nyosha Mkono kwa Huruma

Unapofuata mfano wa Mwokozi wa huruma, utaona kwamba unaweza kuleta tofauti katika maisha ya wengine.

Huruma ni kuwa na ufahamu wa dhiki ya wengine pamoja na hamu ya kufanya iwe rahisi au kufariji. Agano la kumfuata Mwokozi ni agano la huruma la “kubeba mizigo ya mmoja na ya mwingine” (Mosia 18:8). Kazi ya kuwatunza wengine ni fursa ya kuhudumu kama ambavyo Mwokozi angehudumu kwa “huruma, akileta tofauti” (Yuda 1:22). Bwana aliamuru, “Kila mtu na amwonee ndugu yake rehema na huruma” (Zakaria 7:9).

Huruma ya Mwokozi

Huruma ilikuwa ni kichocheo katika huduma ya Mwokozi (ona maandishi ya pembeni mtandaoni: “Mwokozi Mwenye Huruma”). Huruma Yake kwa mwanadamu mwenzake ilimfanya Yeye kuwafikia wale waliomzunguka kwa nafasi zisizohesabika. Akitambua mahitaji ya watu na hamu zao, Yeye angeweza kuwabariki na kuwafundisha katika njia ambazo zilikuwa na maana zaidi kwao. Hamu ya Mwokozi ya kutuinua juu ya dhiki yetu ilipelekea hatimaye kwenye tendo kuu la huruma: Upatanisho Wake kwa dhambi na mateso ya mwanadamu.

Uwezo Wake wa kuitikia mahitaji ya watu ndicho kitu ambacho tunaweza kujitahidi kukipata tunapohudumu. Tunapoishi kwa haki na kusikiliza mnong’ono wa Roho, tutapata muongozo wa kiungu kunyosha mkono katika njia za maana.

Agano Letu la Huruma

Baba wa Mbinguni anawataka watoto Wake kuwa wenye huruma (ona 1 Wakorintho 12:25–27). Ili kuwa wafuasi wa kweli, lazima tukuze na kuonyesha huruma kwa wengine, hasa kwa wale wenye uhitaji (M&M 52:40).

Kujichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo kupitia agano letu la ubatizo, tunashuhudia kwamba tuko radhi kuonyesha huruma. Rais Henry B. Eyring, Mshauri wa Pili katika Urais wa Kwanza, alifundisha kwamba kipawa cha Roho Mtakatifu hutusaidia kufanya hivyo: “Wewe ni muumini wa agano wa Kanisa la Yesu Kristo.

“Hii ndiyo sababu una mawazo ya kutaka kumsaidia anayetaabika kusonga mbele chini ya mzigo wa huzuni na mateso. Uliahidi kwamba ungemsaidia Bwana kuifanya mizigo yao iwe miepesi na kufarijiwa. Ulipewa uwezo wa kuwasaidia kupunguza uzito wa mizigo hiyo pale ulipopokea kipawa cha Roho Mtakatifu.”1

Kwa mfano, dada huko Russia alikuwa na hali ngumu ya kifamilia ambayo ilimfanya kutohudhuria kanisani kwa zaidi ya mwaka mmoja. Dada mwingine katika tawi alinyoosha mkono kwa huruma kila Jumapili kwa kumpigia simu kumwambia kuhusu mahubiri, masomo, miito ya kwenda misheni, watoto waliozaliwa, na taarifa nyingine za tawi. Wakati hali ya kifamilia ya dada iliyomweka ndani ilipotatuliwa, alihisi kana kwamba alikuwa bado sehemu ya tawi kwa sababu ya simu alizopigiwa na rafiki yake kila wiki.

Muhtasari

  1. Henry B. Eyring, “Mfariji ,” Liahona, Mei 2015, 18.