Maandiko Matakatifu
Ushuhuda wa Nabii Joseph Smith


Ushuhuda wa Nabii Joseph Smith

Maneno yenyewe ya Nabii Joseph Smith kuhusu ufunuo wa Kitabu cha Mormoni ni haya:

“Na kisha, jioni ya siku … yaani tarehe ishirini na moja ya Septemba [1823] … nilifanya sala na maombi kwa Mwenyezi Mungu. …

“Wakati nikiwa katika kumlingana Mungu, niligundua mwangaza ukitokeza chumbani mwangu, mwangaza ambao uliendelea kuongezeka hadi chumba chote kikawa na mwanga mkali zaidi kuliko jua la saa sita mchana, na hatimaye mara mtu alionekana kuwa amesimama kando ya kitanda changu, amesimama hewani, kwani miguu yake haikugusa sakafu.

“Alikuwa amevaa joho kubwa jeupe zuri sana. Weupe wake ulikuwa weupe upitao kitu chochote cha kidunia nilichopata kukiona; wala siamini kwamba kitu chochote cha kidunia chaweza kufanywa kionekane cheupe na kiangavu kama hilo. Viganja vyake vilikuwa wazi, na mikono yake pia, juu kidogo ya kifundo; hivyo, pia, nyayo zake zilikuwa wazi, kama ilivyokuwa miguu yake, hadi juu kidogo ya vifundo. Kichwa chake na shingo pia vilikuwa wazi. Niliweza kugundua kuwa hakuwa na nguo nyingine aliyoivaa ila joho hili, kwa sababu lilikuwa wazi, kwani niliweza kuyaona maungo yake.

“Siyo tu joho lake lilikuwa jeupe zaidi, lakini hata kiwiliwili chake kilikuwa na utukufu usioelezeka, na uso wake hakika ulingʼara kama radi. Chumba kikajawa na mwangaza, lakini siyo sana kama ilivyokuwa kuzunguka pale alipokuwa yeye. Mara ya kwanza nilipomwangalia, niliogopa; lakini mara woga ukanitoka.

“Aliniita kwa jina, na kuniambia kwamba alikuwa mjumbe aliyetumwa kwangu kutoka uwepo wa Mungu, na kwamba jina lake lilikuwa Moroni; kwamba Mungu alikuwa na kazi ambayo mimi ningefanya; na kwamba jina langu litafikiriwa kwa mema na maovu miongoni mwa mataifa yote, makabila, na lugha, au lingetajwa kwa wema na kwa uovu miongoni mwa watu wote.

“Alisema kulikuwepo na kitabu kilichohifadhiwa, kilichoandikwa kwenye mabamba ya dhahabu, chenye kutoa historia ya wakazi wa zamani wa bara hili, na asili yao walikotokea. Yeye pia alisema kwamba utimilifu wa Injili isiyo na mwisho ulikuwepo ndani yake, kama ilivyoletwa na Mwokozi kwa wakazi hao wa kale;

“Pia, kwamba yalikuwepo mawe mawili katika pinde za fedha—na mawe haya, yalifungwa kwenye dera ya kifua, yalifanya kitu kinachoitwa Urimu na Thumimu—yamehifadhiwa pamoja na mabamba; na umiliki na utumiaji wa mawe haya ndiyo yalifanya watu waitwe ‘waonaji’ katika nyakati za kale au zilizopita; na kwamba Mungu alikuwa ameyatengeneza kwa ajili ya madhumuni ya kutafsiri kitabu. …

“Tena, akanieleza, kwamba nitakapoyapata mabamba hayo ambayo ameyasema—kwa maana wakati ambao yanapaswa kupatikana ulikuwa bado haujatimia—nisiyaonyeshe kwa mtu yeyote; wala dera ya kifua pamoja na Urimu na Thumimu; isipokuwa kwa wale tu ambao nitaamriwa niwaonyeshe; kama nitayaonyesha nitaangamizwa. Wakati alipokuwa akizungumza nami juu ya mabamba, ono lilifunguliwa akilini mwangu kwamba nikaweza kuona mahali ambapo mabamba yale yalihifadhiwa, na kwamba kila kitu nilikiona vizuri na kwa uwazi zaidi kiasi kwamba nilipajua mahali pale tena wakati nilipopatembelea.

“Baada ya mazungumzo haya, nikaona mwanga katika chumba ukianza mara moja kumzingira mtu ambaye alikuwa akizungumza nami, na ukaendelea kufanya hivyo, hadi chumba kikawa tena na giza, isipokuwa tu mahali alipokuwa amesimama, mara, nikaona, ni kama njia imefunguka hadi mbinguni, na yeye akapanda nayo hadi akatoweka kabisa, na chumba kikaachwa kama vile kilivyokuwa kabla ya mwanga huu wa mbinguni haujatokea.

“Nililala huku nikiwaza juu ya upekee wa hilo jambo, na nikishangazwa sana na yale niliyokuwa nimeambiwa na huyu mjumbe asiye wa kawaida; na halafu, katikati ya tafakuri yangu, nikagundua kwa ghafla kwamba chumba changu kilianza tena kuangazwa, na ikawa kwamba mara moja, kama ilivyokuwa, mjumbe yule yule wa mbinguni alikuwa tena kando ya kitanda changu.

“Akaanza, kuniambia tena vitu vile vile kama alivyofanya hapo awali, bila tofauti yoyote; baada ya kufanya hivyo, akanijulisha kuhusu hukumu kali ambazo zilikuwa zinakuja ulimwenguni, pamoja na ukiwa mkubwa utakaoletwa na njaa, upanga, na tauni; na kwamba hizi hukumu kali zitakuja ulimwenguni katika kizazi hiki. Baada ya kusimulia vitu hivi, akapanda juu tena kama alivyokuwa amefanya hapo awali.

“Kwa wakati huu, mawazo mazito yalikuwa yamejengwa akilini mwangu, kiasi kwamba usingizi ulitoroka machoni mwangu, nami nililala nikiwa nimezidiwa na mshangao kwa yale niliyokwisha kuyaona na kusikia. Lakini mshangao wangu ulikuwa ni wakati nilipomwona tena mjumbe yule yule kando ya kitanda changu, na nikamsikia akirejea au kurudia tena kwangu mambo yale yale kama hapo awali; na kuongeza tahadhari kwangu, akinieleza kwamba Shetani angejaribu kunishawishi (kutokana na hali ya ufukara wa familia ya baba yangu), ili kupata mabamba haya kwa madhumuni ya kupata utajiri. Hili alinikataza, akisema kwamba ni lazima nisiwe na lengo jingine lolote katika nia ya kupata mabamba haya isipokuwa kwa ajili ya kumtukuza Mungu, na nisichochewe na nia nyingine yoyote zaidi ya ile ya kuujenga ufalme wake; vinginevyo nisingeliweza kuyapata.

“Baada ya kuja mara hii ya tatu, akapaa tena mbinguni kama hapo mwanzo, na mimi tena nikaachwa nikitafakari juu ya ugeni wa yale ambayo nilikuwa nimeyashuhudia; ambapo punde tu baada ya mjumbe yule wa mbinguni kupaa mara ya tatu, jogoo akawika, na nikafahamu kwamba siku mpya ilikuwa inapambazuka, hivyo basi mahojiano yetu lazima yalikuwa yamechukua huo usiku wote.

“Muda mfupi baadaye niliamka kutoka kitandani pangu, na, kama kawaida, nilienda kufanya kazi muhimu za siku hiyo; lakini, katika kujaribu kufanya kazi kama nyakati zingine, nilijiona kuwa nguvu zangu zimeniishia hata kunifanya nisijiweze kabisa. Baba yangu, ambaye alikuwa akifanya kazi pamoja nami, aligundua kwamba nilikuwa na matatizo, na akaniambia niende nyumbani. Nilianza kwa dhamira ya kwenda nyumbani; lakini, katika kujaribu kuvuka ukingo wa shamba ambamo tulikuwepo, nguvu zangu ziliniishia kabisa, nami nilianguka chini kabisa, na kwa muda nilikuwa sijiwezi kabisa kwa chochote.

“Kitu cha kwanza ambacho ninaweza kukikumbuka kilikuwa ni sauti ikinisemesha, ikiniita kwa jina. Niliangalia juu, na nikamwona mjumbe yule yule akiwa amesimama juu ya kichwa changu, akiwa amezungukwa na mwanga kama vile awali. Kisha akayarudia tena yale yote aliyonieleza usiku uliopita, na akaniamuru niende kwa baba yangu na kumwambia juu ya lile ono na amri nilizozipokea.

“Nilitii; nikarudi kwa baba yangu shambani, na kumweleza jambo lile lote. Yeye alinijibu kwamba lilikuwa la Mungu, na akaniambia niende na kufanya kama nilivyoamriwa na yule mjumbe. Niliondoka shambani, na kwenda mahali ambapo yule mjumbe alinieleza kwamba mabamba yamehifadhiwa; na kwa sababu ya uwazi wa lile ono ambalo nililipata juu yake, nilipajua mahali pale mara baada ya kufika hapo.

“Karibu na kijiji cha Manchester, wilaya ya Ontario, New York, kimesimama kilima cha ukubwa wa wastani, na ndicho kilima kirefu kuliko chochote katika maeneo ya jirani. Upande wa magharibi ya kilima hiki, siyo mbali kutoka kileleni, chini ya jiwe la ukubwa wa wastani, yalilala mabamba, yakiwa yamehifadhiwa ndani ya kisanduku cha jiwe. Jiwe hili lilikuwa nene na la mviringo katikati juu ya upande wa juu, na jembamba zaidi kuelekea kwenye kingo, hivyo sehemu yake ya katikati ilikuwa ikionekana juu ya udongo, lakini kingo zake zote kuzunguka zilifunikwa kwa udongo.

“Baada ya kuondoa udongo, nilipata wenzo, ambayo niliitia chini ya kingo za lile jiwe, na kwa kutumia nguvu kidogo nililiinua. Niliangalia ndani, na humo hakika niliona mabamba hayo, Urimu na Thumimu, na dera ya kifuani, kama ilivyoelezwa na yule mjumbe. Lile sanduku ambalo ndani yake yaliwekwa lilitengenezwa kwa kuyapanga mawe pamoja kwa aina fulani ya saruji. Ndani, chini ya sanduku yaliwekwa mawe mawili yakikingama na sanduku, na juu ya mawe haya yaliwekwa mabamba hayo na vitu vingine pamoja nayo.

“Nilifanya jaribio la kuvitoa nje, lakini nilikatazwa na yule mjumbe, na tena niliarifiwa kuwa wakati wa kuvichukua ulikuwa bado haujafika, wala haungefika, hadi miaka minne kutoka wakati huo; lakini alinieleza kwamba yanipasa kuja mahali pale baada ya mwaka mmoja barabara kutoka wakati ule, na kwamba atakutana nami pale, na kwamba itanipasa kuendelea kufanya hivyo hadi wakati utakapofika wa kuyapata mabamba yale.

“Hivyo, kulingana na nilivyokuwa nimeamriwa, nilikwenda kila ilipofika mwisho wa mwaka, na kila wakati nilimkuta mjumbe yule pale, na nikapokea maelekezo na maarifa kutoka kwake katika kila mahojiano yetu, juu ya yale Bwana atakayoyafanya, na namna gani na kwa jinsi gani ufalme wake utaendeshwa katika siku za mwisho. …

“Hatimaye wakati ulifika wa kuyachukua mabamba, Urimu na Thumimu, na dera ya kifuani. Tarehe ishirini na mbili ya Septemba, elfu moja mia nane na ishirini na saba, ikiwa nimeenda kama kawaida mwishoni mwa mwaka mwingine mahali vilipokuwa vimehifadhiwa, mjumbe yule yule wa mbinguni alinipa pamoja na amri hii: kwamba nitawajibika juu yake; kwamba kama nitayaacha yaende kwa kukosa uangalifu, au kwa uzembe wangu, nitakatiliwa mbali; lakini kama nitatumia uwezo wangu wote kuyalinda, hadi yeye, yule mjumbe, atakapoyataka, yatalindwa.

“Muda si mrefu nilitambua sababu ya mimi kupokea amri ile kali ya kuyatunza kwa usalama, na kwa nini ilikuwa mjumbe aseme hivyo kwamba nitakapokuwa nimefanya yale yaliyotakiwa kutoka kwangu, atayataka. Kwani haikuwa muda mrefu ilijulikana kwamba nilikuwa nayo, juhudi ya nguvu nyingi zaidi ilitumika ili kuyapata kutoka kwangu mimi. Kila hila ambayo iliweza kubuniwa ilitumiwa kwa dhumuni hili. Mateso yakawa machungu zaidi na makali kuliko mwanzoni, na umati ulikuwa uko tayari daima kuyachukua kutoka kwangu kama ikiwezekana. Lakini kwa hekima ya Mungu, yalibaki salama mikononi mwangu, hadi nilipoyamalizia kazi ile iliyotakiwa kutoka kwangu. Hatimaye, kulingana na mipangilio, mjumbe yule akayataka, nikampa; naye anayo katika himaya zake hadi siku hii, ikiwa siku ya pili ya Mei, elfu moja mia nane na thelathini na nane.”

Kwa historia kamili, angalia Joseph Smith—Historia ya katika Lulu ya Thamani Kuu.

Historia hiyo ya kale ilitolewa kwenye ardhi kama sauti ya watu wakizungumza kutoka mavumbini, na ikatafsiriwa kwa lugha ya kisasa kwa karama na uwezo wa Mungu kama ilivyoshuhudiwa na Ushuhuda mtakatifu, ulichapishwa mara ya kwanza ulimwenguni kwa Kiingereza mwaka wa 1830 kama The Book of Mormon.