Maandiko Matakatifu
Utangulizi


Utangulizi

Lulu ya Thamani Kuu ni uteuzi wa nyenzo bora zinazohusu vipengele muhimu vya imani na mafundisho ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Vipengele hivi vilitafsiriwa na kutolewa na Nabii Joseph Smith na vingi vilichapishwa katika majarida ya Kanisa katika siku za uhai wake.

Mkusanyiko wa kwanza wa maandiko uliobeba jina la Lulu ya Thamani Kuu ulifanywa mwaka 1851 na Mzee Franklin D. Richards, wakati huo akiwa mshiriki wa Baraza la wale Kumi na Wawili na Rais wa Misheni ya Uingereza. Madhumuni yake yalikuwa ni kurahisisha upatikanaji wa baadhi ya kanuni muhimu ambazo usambazaji wake ulikuwa mdogo katika wakati wa Joseph Smith. Wakati idadi ya waumini wa Kanisa ilipoongezeka kote Ulaya na Marekani, palikuwa na haja ya kuzifanya makala hizi kuweza kupatikana. Lulu ya Thamani Kuu kilipata matumizi makubwa sana na hatimaye kikawa kitabu cha maandiko matakatifu cha Kanisa kwa kauli ya Urais wa Kwanza na mkutano mkuu uliofanyika Jijini Salt Lake tarehe 10 Oktoba 1880.

Mapitio kadhaa yamekwisha fanyika katika yale yaliyomo kadri ya mahitaji ya Kanisa yalivyohitaji. Katika mwaka 1878 sehemu za kitabu cha Musa ambazo hazikuwepo katika toleo la kwanza ziliongezwa. Katika mwaka 1902 sehemu fulani za Lulu ya Thamani Kuu ambazo pia zilikuwa zimerudiwa kuchapishwa katika Mafundisho na Maagano ziliondolewa. Mpangilio katika milango na mistari, pamoja na tanbihi, ulifanywa katika mwaka 1902. Chapisho la kwanza katika kurasa yenye safu mbili, pamoja na faharasa, ilifanyika mwaka 1921. Hakuna mabadiliko mengine yaliyofanywa hadi Aprili 1976, wakati vipengele viwili vya ufunuo vilipoongezwa. Katika mwaka 1979 vipengee hivyo viwili viliondolewa kutoka kwenye Lulu ya Thamani Kuu na kuwekwa katika Mafundisho na Maagano, ambayo sasa yanaonekana kama sehemu ya 137 na 138. Katika toleo la sasa mabadiliko fulani yamefanywa ili kuyaweka maandiko katika maafikiano na nyaraka za awali.

Ufuatao ni utangulizi mfupi kwa yaliyomo kwa sasa:

  1. Teuzi kutoka katika Kitabu cha Musa. Kiziduo kutoka kitabu cha Mwanzo cha tafsiri ya Joseph Smith ya Biblia, ambayo aliianza Juni 1830.

  2. Kitabu cha Ibrahimu. Ni tafsiri yenye uvuvio uliotokana na maandishi ya Ibrahimu. Joseph Smith alianza tafsiri hiyo mnamo mwaka wa 1835 baada ya kupata mafunjo ya Kimisri. Tafsiri hiyo ilichapwa kwa mfululizo katika Times and Seasons kuanzia tarehe 1 Machi 1842, huko Nauvoo, Illinois.

  3. Joseph Smith—Mathayo. Kiziduo kutoka ushuhuda wa Mathayo katika tafsiri ya Joseph Smith ya Biblia (ona Mafundisho na Maagano 45:60–61 kwa ajili ya amri takatifu ya kuanza tafsiri ya Agano Jipya).

  4. Joseph Smith—Historia ya. Dondoo kutoka ushuhuda na historia rasmi ya Joseph Smith, ambayo aliiandika katika mwaka 1838 na ambayo yeye na waandishi wake waliitayarisha mwaka 1838–1839 na ambayo ilichapishwa mfululizo katika Times and Seasons huko Nauvoo, Illinois, kuanzia 15 Machi 1842.

  5. Makala ya Imani ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Ni maelezo yaliyotolewa na Joseph Smith na kuchapishwa katika Times and Seasons 1 Machi 1842, yaliyoambatana na historia fupi ya Kanisa ambayo kwa umaarufu yalijulikana kama Barua ya Wentworth.