Mkutano Mkuu
Maongezi Muhimu
Mkutano mkuu wa Aprili 2021


Maongezi Muhimu

Hatuwezi kusubiri kwa kuongoka kutokea kiepesi tu kwa watoto wetu. Kuongoka kwa bahati mbaya sio kanuni ya injili ya Yesu Kristo.

Umewahi kujiuliza kwa nini tunaliita darasa la Msingi “Msingi”? Wakati jina linamaanisha mafunzo ya kiroho ambayo watoto wanayapata katika miaka yao ya awali, kwangu mimi pia ni kumbukumbu ya ukweli wenye nguvu. Kwa Baba yetu wa Mbinguni, watoto hawajawahi kuwa upili—wamekuwa daima ni “msingi.”1

Anatuamini sisi katika kuwathamini, kuwaheshimu, na kuwalinda kama watoto wa Mungu. Hii inamaanisha kamwe tusiwadhuru kimwili, kwa maneno, au kihisia kwa namna yoyote ile, hata wakati migogoro na mashinikizo vinapoongezeka. Badala yake tuthamini watoto, na kufanya yote tunayoweza kupambana na maovu ya udhalilishaji. Matunzo yao ni ya msingi kwetu—kama ilivyo kwa Mungu.2

Mama mmoja kijana na baba walikaa kwenye meza yao ya jikoni wakitafakari siku yao. Ndipo kutoka chumbani, walisikia mshindo. Mama akauliza, “Hicho kilikuwa nini?”

Kisha walisika sauti nyororo ya kilio ikitoka kwenye chumba cha mtoto wao wa kiume mwenye umri wa miaka minne. Walikimbia kuelekea chumbani. Alikuwa pale, amelala sakafuni karibu na kitanda chake. Mama alimnyanyua na kumuuliza nini kilikuwa kimetokea.

Alisema, “nilianguka kutoka kitandani.”

Mama akamuuliza,“Kwa nini ulianguka kutoka kitandani?”

Alipandisha mabega juu na kushusha na kusema, “Sijui. Nadhani sikuwa nimesonga mbali vya kutosha.”

Ni kuhusu hili la “kusonga mbali vya kutosha” ambako ningependa kuzungumzia asubuhi ya leo. Ni fursa na wajibu kwetu kuwasaidia watoto “kusonga mbali vya kutosha” kwenye injili ya Yesu Kristo. Na ni muhimu kuanza mapema mno.

Kuna wakati maalum katika maisha ya watoto wanapokuwa wamekingwa dhidi ya ushawishi wa Shetani. Ni wakati wanapokuwa hawana hatia na huru kutokana na dhambi.3 Ni wakati mtakatifu wa mzazi na watoto. Watoto lazima wafundishwe, kwa neno na mfano, kabla na baada ya “kufikia miaka ya kuwajibika kwa Mungu.”4

Rais Henry B. Eyring alifundisha: “Tunayo fursa kubwa zaidi kwa wadogo hawa. Wakati bora wa kufundisha ni wawapo wadogo, wakati bado wana kinga ya majaribu ya adui wa hapa duniani, na mapema kabla maneno ya kweli hayajawa magumu kwao kusikia katika kelele ya mapambano yao ya kibinafsi.”5 Mafundisho kama hayo yatawasaidia kutambua asili yao ya kiungu, lengo lao, na baraka tele zinazowasubiria pale wanapofanya maagano matakatifu na kupokea ibada takatifu katika njia ya agano.

Hatuwezi kusubiri kwa kuongoka kutokea kiepesi tu kwa watoto wetu. Kuongoka kwa bahati mbaya sio kanuni ya injili ya Yesu Kristo. Kuwa kama Mwokozi wetu hakutatokea tu bila mpangilio. Kuwa mwenye kusudi katika kupenda, kufundisha, na kushuhudia kunaweza kuwasaidia watoto kuanza katika umri mdogo kuhisi ushawishi wa Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu ni wa muhimu kwa shuhuda za watoto wetu na kuongoka katika Yesu Kristo; tunatamani kwamba wao “daima wamkumbuka yeye, ili Roho wake apate kuwa pamoja nao.”6

Picha
Mazungumzo ya familia.

Fikiria thamani ya mazungumzo ya familia juu ya injili ya Yesu Kristo, mazungumzo muhimu ambayo yanaweza kumwalika Roho. Tunapokuwa na mazungumzo kama hayo pamoja na watoto wetu, tunawasaidia kujenga msingi, “ambao ni msingi imara, msingi ambako watu wote wakijenga hawataanguka.”7 Tunapomuimarisha mtoto, tunaimarisha familia.

Majadiliano haya muhimu yanaweza kuwaongoza watoto kwenye:

  • Kuelewa mafundisho ya toba.

  • Kuwa na imani katika Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.

  • Kuchagua ubatizo na kipawa cha Roho Mtakatifu wafikapo umri wa miaka nane.8

  • Na kusali na “kutembea katika haki mbele za Bwana”.9

Mwokozi aliasa, “Kwa hiyo ninakupeni amri, kuyafundisha mambo haya kwa uhuru kwa watoto wenu.”10 Na ni kitu gani Alitutaka sisi tufundishe kwa uhuru sana?

  1. Anguko la Adamu

  2. Upatanisho wa Yesu Kristo

  3. Umuhimu wa kuzaliwa mara ya pili11

Mzee D. Todd Christofferson alisema, “Kwa hakika adui anapendezwa wakati wazazi wanapopuuza kuwafundisha na kuwafunza watoto wao kuwa na imani katika Kristo na kuzaliwa tena kiroho.”12

Kinyume chake, Mwokozi anatutaka sisi kuwasaidia watoto “kuweka matumaini [yao] katika Roho yule anayeongoza kutenda mema.”13 Ili kufanya hivyo, tunaweza kuwasaidia watoto kutambua wakati wanapohisi Roho na katika kutambua ni matendo yapi husababisha Roho kuondoka. Hivyo hujifunza kutubu na kurejea katika nuru kwa kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo. Hii husaidia kuhamasisha uthabiti wa kiroho.

Tunaweza kufurahia kuwasaidia watoto wetu kujenga uthabiti wa kiroho katika umri wowote. Haitakiwi kuwa jambo gumu au la kutumia muda mwingi. Mazungumzo ya kawaida, na yenye kujali yanaweza kuwaongoza watoto kujua sio tu kile wanachokiamini, ila cha msingi, kwa nini wanakiamaini. Mazungumzo yenye kujali, yafanyikayo kwa hali ya kawaida na mara kwa mara, huweza kupelekea katika uelewa mzuri na majibu. Tusiruhusu uwepo wa vifaa vya kielektroniki kutuondoa katika kufundisha na kuwasikiliza watoto wetu na kuwaangalia machoni mwao.

Picha
Mazungumzo ya mama na binti

Fursa za ziada kwa ajili ya mazungumzo muhimu zinaweza kutokea kupitia kuigiza tukio. Wanafamilia wanaweza kuigiza hali za kujaribiwa au kusukumwa kufanya uchaguzi mbaya. Igizo kama hilo linaweza kuwaimarisha watoto kujiandaa katika hali za changamoto. Kwa mfano, tunaweza kuigiza na pia kuzungumzia igizo hilo wakati tunawauliza watoto ni nini wangefanya:

  • Ikiwa wamejaribiwa kuvunja Neno la Hekima.

  • Kama wamekumbana na picha za ponografia.

  • Kama wanajaribiwa kudanganya, kuiba, au kutokuwa waaminifu.

  • Ikiwa watasikia jambo kutoka kwa rafiki au mwalimu shuleni ambalo linapingana na imani yao au maadili.

Kadiri wanavyoigiza na kulizungumzia igizo, kuliko kukutwa bila kujiandaa katika mazingira ya kundi rika ovu, watoto wanaweza kulindwa na “ngao ya imani ambayo kwa hiyo [wao] wataweza kuizima mishale yote yenye moto ya adui.”14

Rafiki binafsi wa karibu alijifunza somo hili muhimu akiwa na umri wa miaka 18. Alijiandikisha katika jeshi la Marekani wakati wa mgogoro kati ya Marekani na Vietinam. Alipangwa katika mafunzo ya msingi ya jeshi la watembea kwa miguu. Alielezea kwamba mafunzo yalikuwa magumu. Alimwelezea mkufunzi wake wa mazoezi kama mtu mkatili na asiye na ubinadamu.

Siku moja mahsusi kundi lake lilikuwa limevalia mavazi kamili ya kivita, wakipanda mlima katika joto kali. Mkufunzi wa mazoezi ghafla alitoa amri za kuanguka chini na kutosogea. Mkufunzi alikuwa anaangalia hata hatua ndogo tu. Mtikisiko wa aina yoyote ule ungepelekea kwenye matokeo mabaya baadae. Kundi lilitaabika kwa zaidi ya saa mbili katika joto na hasira na chuki iliongezeka dhidi ya kiongozi wao.

Miezi mingi baadaye, rafiki yetu alijikuta akiongoza kikosi chake kupitia misitu ya Vietinam. Hii ilikuwa ni kweli, na sio mafunzo tu. Milio ya risasi ilianza kusikika kutokea juu katika miti iliyowazunguka. Mara moja kikosi chote kilianguka ardhini.

Adui alikuwa anatafuta nini? Mienendo yao. Hatua yoyote ile ingeleteleza moto. Rafiki yangu alinambia kwamba alivyokuwa amelala akitokwa jasho na bila kusogea katika sakafu ya msitu, akisubiria giza kwa masaa mengi, mawazo yake yalirejelea nyuma katika mafunzo ya msingi. Alikumbuka alivyokuwa hampendi mkufunzi wake. Sasa, alihisi shukrani kubwa—kwa kile alichokuwa amemfundisha na jinsi alivyokuwa amemwandaa kwa ajili ya nyakati hizi ngumu. Mkufunzi wa mazoezi kwa hekima alikuwa amemhami rafiki yetu na kikosi chake na uwezo wa kujua nini cha kufanya wakati mapigano yakiendelea. Alikuwa, kimsingi, ameokoa maisha ya rafiki yetu.

Je, ni kwa namna gani sisi tunaweza kufanya vivyo hivyo kiroho kwa watoto wetu? Mapema kabla ya kuingia katika uwanja wa vita ya maisha, kwa jinsi gani tunaweza kujitahidi zaidi kuwafunza, kuwaimarisha na kuwaandaa?15 Ni kwa jinsi gani tunaweza kuwaalika “kusonga mbali vya kutosha”? Si tungeweza kuwafanya “watoe jasho” katika mazingira salama ya kujifunza ya nyumbani kuliko kuvuja damu katika uwanja wa vita wa maisha?

Ninapotazama nyuma, kuna nyakati wakati mume wangu na mimi tulijihisi kama wakufunzi wa mazoezi katika bidii yetu ya kuwasaidia watoto wetu kuiishi injili ya Yesu Kristo. Nabii Yakobo alionekana kutamka hisia kama hizi aliposema: “ninajali ustawi wa nafsi zenu. Ndio, wasiwasi wangu ni mkubwa kwenu; na nyinyi mnajua imekuwa hivyo tangu mwanzo.”16

Kadiri watoto wanavyojifunza na kukua, imani yao itajaribiwa. Lakini kama watalindwa vizuri, wanaweza kukua kiimani, kiujasiri, na kujiamini, hata katikati ya upinzani mkubwa.

Alma alitufundisha sisi “kutayarisha akili [za] watoto.”17 Tunakiandaa kizazi kinachoinukia kuwa walinzi wa baadaye wa imani, kuelewa “kwamba mko huru kujitendea—kuchagua njia ya kifo kisicho na mwisho au njia ya uzima wa milele.”18 Watoto wanastahili kuelewa ukweli huu mkuu: ni jambo baya kutojua kuhusu umilele.

Basi mazungumzo yetu ya kawaida lakini ya muhimu na watoto wetu yawasaidie “kufurahia maneno ya uzima wa milele” sasa, ili waweze kufurahia “uzima wa milele katika ulimwengu ujao, hata utukufu usio na mwisho.”19

Kadiri tunavyowatunza na kuwaandaa watoto wetu, tunaruhusu uhuru wao wa kuchagua, tunawapenda kwa moyo wetu wote, tunawafundisha amri za Mungu na Zawadi Yake ya toba, na kamwe, hata siku moja, hatutawaacha. Hata hivyo, hii si ndio njia ya Bwana kwa kila mmoja wetu?

Acha “tusonge mbele tukiwa imara katika Kristo,” tukijua kwamba tunaweza kuwa na “mng’aro halisi wa tumaini”20 kupitia kwa Mwokozi wetu mpendwa.

Ninashuhudia kwamba daima Yeye ni jibu. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. (Ona 3 Nefi 5:23–24.)

  2. Ona Michaelene P. Grassli, “Behold Your Little Ones,” Ensign, Nov. 1992, 93: “To me, the word behold is significant. It implies more than just ‘look and see.’ Wakati Bwana alipowaagiza Wanefi kutazama wachanga wao, ninaamini aliwaambia kuwa makini kwa watoto wao, kuwatafakari wao, kutazama zaidi ya nyakati hizi na kuona uwezekano wao wa milele.”

    Ona pia Russell M. Nelson, “Listen to Learn,” Ensign, May 1991, 22: “To rule children by force is the technique of Satan, not of the Savior. Hapana, hatumiliki watoto wetu. Fursa yetu kama wazazi ni kuwapenda, kuwaongoza, na kuwaacha waende.”

  3. Ona Mafundisho na Maagano 29:46–47.

  4. Mafundisho na Maagano 20:71.

  5. Henry B. Eyring, “The Power of Teaching Doctrine,” Liahona, July 1999, 87.

  6. Mafundisho na Maagano 20:79.

  7. Helamani 5:12

  8. Ona Mafundisho na Maagano 68:25; ona pia Mafundisho na Maagano 1:4.

  9. Mafundisho na Maagano 68:28.

  10. Musa 6:58; msisitizo umeongezewa.

  11. Ona Musa 6:59; ona pia Mafundisho na Maagano 20:29–31.

  12. D. Todd Christofferson, “Why Marriage, Why Family?,” Liahona, May 2015, 52.

  13. Ona Mafundisho na Maagano 11:12–13; ona pia Mafundisho na Maagano 93.

  14. Mafundisho na Maagano 27:17; msisitizo umeongezwa; ona pia Marion G. Romney, “Home Teaching and Family Home Evening,” Improvement Era, June 1969, 97: “Satan, our enemy, is making an all-out assault upon righteousness. His well-marshaled forces are legion. Our children and youth are the targets of his main thrust. They are everywhere subjected to wicked and vicious propaganda. Every place they turn, they are buffeted with evil, cunningly devised to deceive and to destroy every sacred thing and every righteous principle. … If our children are to be sufficiently strengthened to stand against this satanic onslaught, they must be taught and trained in the home, as the Lord has directed.”

  15. See Russell M. Nelson, “Children of the Covenant,” Ensign, May 1995, 32:

    “Miaka iliyopita nikiwa mwanafunzi mchanga wa udaktari niliona wagonjwa wengi wakisumbuliwa na maradhi ambayo sasa yanaweza kuzuilika. Leo inawezekana kuwakinga watu binafisi dhidi ya hali ambazo zilikuwa zinalemaza—hata kifa Njia moja ambayo udhaifu wa kinga ya mwili hutolewa ni chanjo. Msemo chanjo ni wakuvutia. Unatoka katika mizizi miwili ya kilatini: in, ikimaanisha ‘ndani ya’; na oculus, ikimaanisha ‘jicho.’ Kitenzi kuchanja, kwa hiyo, kiuhalisia humaniisha ‘kuweka jicho ndani ya’—kufuatilia dhidi ya madhara.

    “Maumivu kama ya polio yanaweza kufanya mtu kupooza au kuharibu mwili. Maumivu kama ya dhambi yanaweza kulemaza au kuharibu roho. Madhara ya polio sasa yanaweza kuzuiliwa kwa chanjo, lakini madhara ya dhambi yanahitaji njia nyingine za kuzuia. Madaktari hawawezi kuchanja dhidi ya uovu. Ulizi wa Kiroho unatoka pekee kwa Bwana—na katika njia yake. Yesu hachagui kuchanja, bali kufundisha. Njia yake haihusishi chanjo; inatumia mafundisho ya mafundisho ya kiungu—‘jicho linaloongoza kwa ndani’—kulinda roho za milele za watoto wake.”

  16. 2 Nefi 6:3.

  17. Alma 39:16

  18. 2 Nefi 10:23.

  19. Musa 6:59; msisitizo umeongezewa.

  20. 2 Nefi 31:20.