Mkutano Mkuu
Ni Kipi Tunachojifunza na Kamwe Hatutakisahau
Mkutano mkuu wa Aprili 2021


Ni Kipi Tunachojifunza na Kamwe Hatutakisahau

Kama utatazama maisha yako kwa sala, ninaamini utaona njia nyingi ambazo Bwana amekuwa akikuongoza kupitia wakati huu wa shida.

Ndugu zangu wapendwa, nimekuwa nikitazamia kuwa pamoja nanyi katika mkutano huu kwa njia ya mtandao. Mara ya mwisho kuwa na kikao cha ukuhani cha mkutano mkuu ilikuwa Aprili 2019. Mengi yametokea katika miaka miwili iliyopita! Baadhi yenu mmepoteza wapendwa wenu. Wengine wamepoteza kazi, riziki, au afya. Bado wengine wamepoteza hisia za amani au matumaini kwa siku za baadaye. Moyo wangu umfikie kila mmoja wenu ambaye ameteseka na haya au hasara zingine. Ninaomba daima kwamba Bwana awafariji Mnapoendelea kumwacha Mungu ashinde katika maisha yenu, ninajua kwamba Yeye ana mategemeo kuhusu siku zenu za baadaye kama ambayo amekuwa.

Katikati ya upotevu tulioupata, pia kuna baadhi ya vitu tulivyovipata. Baadhi wamepata imani ya kina zaidi kwa Baba Yetu wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo. Wengi wamepata taswira mpya juu ya maisha—hata taswira ya milele. Unaweza kuwa umepata mahusiano yenye nguvu kubwa na wapendwa wako na pamoja na Mungu. Ninatumaini umepata uwezo mkubwa wa Kumsikia Yeye na kupokea ufunuo binafsi. Majaribu magumu mara nyingi yanatoa fursa ya kukua ambayo isingekuja katika njia nyingine yoyote.

Fikiria nyuma kwenye miaka miwili iliyopita. Ni jinsi gani ulivyokua? Umejifunza nini? Unaweza hapo mwanzo ukatamani ungerudi nyuma mpaka mwaka 2019 na kubaki pale! Lakini kama utatazama maisha yako kwa sala, ninaamini utaona njia nyingi ambazo Bwana amekuwa akikuongoza kupitia wakati huu wa shida, akikusaidia kuwa mwaminifu sana, mtu mwongofu sana—mtu mkweli wa Mungu.

Ninajua Bwana ana mipango mikubwa na ya ajabu kwa ajili yetu—kibinafsi na kwa pamoja. Kwa huruma na subira, Anasema:

“Ninyi ni watoto wadogo, nanyi bado hamjaelewa jinsi baraka kuu Baba … amezitayarisha kwa ajili yenu;

“Na hamwezi kustahimili mambo yote kwa sasa; hata hivyo, changamkeni, kwa kuwa nitawaongoza.”1

Akina kaka, ninashuhudia kwamba Amekuwa, na yupo, kwa hakika anatuongoza, tunapotafuta kumsikiliza Yeye. Anatutaka kukua na kujifunza, hata kupitia—pengine hususani kupitia—dhiki.

Dhiki ni mwalimu mkuu. Umejifunza nini wewe katika miaka miwili iliyopita ambayo siku zote unapenda kukumbuka? Majibu yenu yatakuwa ya kipekee kwenu, lakini naomba nipendekeze masomo manne ambayo natumaini sote tumejifunza na kamwe hatutasahau.

Somo la 1: Nyumbani ndipo Mahali pa Kitovu cha Imani na ibada

Mara nyingi wakati Bwana anapotuonya kuhusu hatari kubwa za siku za mwisho, Anajumuisha ushauri huu: “Simameni katika sehemu takatifu, na wala msiondoke.”2 Hizi “sehemu takatifu” kwa hakika zinajumuisha mahekalu ya Bwana na nyumba za mikutano. Lakini kwa vile uwezo wetu wa kukusanyika katika sehemu hizi umezuiwa kwa viwango tofauti, tumejifunza kwamba moja ya sehemu takatifu mno duniani ni nyumbani—ndiyo, hata nyumbani kwako.

Ndugu, mnashikilia ukuhani wa Mungu. “Haki za ukuhani ukuhani zimeunganishwa na hazitenganishwi na nguvu za mbinguni.”3 Wewe na wanafamilia wako mmepokea ibada za ukuhani. Ni “katika ibada [za ukuhani, kwamba] nguvu za ucha mungu zimedhihirishwa.”4 Nguvu hiyo inapatikana kwako na familia yako katika nyumba yako mwenyewe kadiri utunzavyo maagano uliyoyaweka.5

Miaka 185 iliyopita, siku kama hii ya leo, Aprili 3, 1836, Eliya alirejesha funguo za ukuhani ambazo zinaruhusu familia zetu kuunganishwa pamoja milele. Hiyo ndio maana ilikuwa vyema sana kuhudumia sakramenti nyumbani mwako. Ni kwa jinsi gani iliathiri jinsi wanafamilia wanavyokuona—baba yao, babu, mume, mwana, au kaka—ukihudumia ibada hii takatifu? Utafanya nini kubakia na hisia hiyo takatifu katika familia yako?

Unaweza kuhisi kwamba bado kuna mengi zaidi ya kufanya ili kuiweka nyumba yako mahali patakatifu pa imani. Kama ndivyo, tafadhali fanya hivyo! Kama umeoa, shauriana na mkeo kama mwenza wako katika kazi hii muhimu sana. Hili ni la muhimu sana kuliko malengo machache mengine. Kati ya sasa na muda ambao Bwana atakuja tena, sote tunahitaji nyumba zetu ziwe mahali palipo safi na penye usalama.6

Tabia na vitendo vinavyomwalika Roho vitaongeza utakatifu wa nyumba yako. Katika ukweli sawa na huo ni ukweli kwamba utukufu utatoweka kama kuna chochote katika tabia yako au mazingira ambayo yanamchukiza Roho Mtakatifu, kwani “mbingu hujitoa zenyewe.”7

Umewahi kujiuliza kwa nini Bwana anatutaka kufanya nyumba zetu kitovu cha kujifunza na kuishi injili? Sio tu kutuandaa kwa ajili ya, na kutusaidia kupita maradhi haya ya ulimwengu. Vizuizi vya sasa vya kukusanyika hatimaye vitaisha. Hata hivyo, dhamira yako ya kufanya nyumba yako sehemu ya msingi ya imani haipaswi kamwe kwisha. Wakati imani na utukufu unapopungua katika ulimwengu huu ulioanguka, hitajio lako la mahali patakatifu litaongezeka. Ninawasihi kuendelea kufanya nyumba yako mahali patakatifu pa kweli “na msiondolewe8 kutoka lengo hilo muhimu.

Somo 2: Tunahitajiana Sisi kwa Sisi

Mungu anatutaka sisi kufanya kazi kwa pamoja na kusaidiana. Hiyo ndiyo sababu Ametutuma duniani katika familia na kutuweka kwenye kata na vigingi. Hiyo ndiyo sababu Anatutaka kutumikiana na kuhudumiana. Hiyo ndiyo sababu Anatutaka tuishi katika ulimwengu lakini sio kuwa wa ulimwengu.9 Tunaweza kutimiza mengi mno zaidi pamoja kuliko tunavyoweza kipekee.10 Mpango wa Mungu wa furaha ungekuwa pasipo maana kama watoto Wake wangebaki wametengana.

Janga la ulimwengu la hivi karibuni limekuwa la kipekee kwani limemuathiri kila mmoja ulimwenguni kwa wakati mmoja. Wakati baadhi wameteseka zaidi kuliko wengine, sisi sote tumepigwa na changamoto kwa njia fulani. Kwa sababu ya hili, jaribu letu la pamoja lina uwezo wa kusaidia kuwaunganisha watoto wa Mungu kuliko hapo awali. Kwa hiyo, nauliza, je, jaribu hili la pamoja limewasogeza karibu zaidi kwa majirani zenu—kwa kaka na dada zenu mtaa wa pili na ulimwengu mzima?

Kwa swala hili, amri kuu mbili zinaweza kutuongoza: kwanza, kumpenda Mungu na, pili, kuwapenda jirani zetu.11 Tunaonyesha upendo wetu kwa kuhudumia.

Kama unamjua yeyote aliye mpweke, mwendee—hata kama unajihisi mpweke pia! Huhitaji kuwa na sababu au ujumbe au biashara ya kushughulikia. Toa salamu zako na onyesha upendo wako. Teknolojia inaweza kukusaidia. Kuwepo na janga la ulimwengu au la, kila mtoto wa Mungu anahitaji kujua kwamba yeye hayupo peke yake!

Somo 3: Akidi Yenu ya Ukuhani Imenuiwa kuwa zaidi ya Kukutana tu

Wakati wa janga hili la ulimwenguni kote, mikutano ya Jumapili ya akidi ilifutwa kwa muda. Baadhi ya akidi sasa zinaweza kukutana kwa njia ya mtandao. Hata hivyo, kazi ambayo Bwana ameitoa kwa akidi za ukuhani kamwe hazikuwekwa kuishia kwenye mkutano. Mikutano ni sehemu ndogo tu ya kile akidi imenuiwa na kile inachoweza kufanya.

Ndugu zangu wa akidi za Ukuhani wa Haruni na akidi ya wazee, panueni uoni wenu wa kwa nini tuna akidi. Ni kwa jinsi gani Bwana anatamani nyie mngetumia akidi zenu kukamilisha kazi Yake—sasa? Tafuta ufunuo kutoka kwa Bwana. Jinyenyekeze! Uliza! Sikiliza! Kama umeitwa kuongoza, shauriana kama urais pamoja na washiriki wa akidi. Bila kujali ofisi yako ya ukuhani au wito, acha Mungu atawale katika dhamira zenu kama mshiriki wa akidi yenu na katika huduma zenu. Kuwa na uzoefu wenye furaha kwa haki utakayoileta wakati unapojishughulisha “kwa shauku katika kazi njema.”12 Akidi zipo katika nafasi ya kipekee ya kuongeza kasi ya kusanyiko la Israeli kwenye pande zote mbili za pazia.

Somo 4: Tunamsikia Yesu Kristo Vyema Wakati tupo Kimya

Tunaishi katika muda uliotabiriwa miaka mingi iliyopita, wakati “vitu vyote vitakuwa katika vurugu; na hakika, watu watavunjika mioyo; kwa kuwa hofu itakuja juu ya watu wote.”13 Hiyo ilikuwa kweli kabla ya janga la ulimwengu na itakuwa kweli hata baada yake. Vurugu katika ulimwengu itaendelea kuongezeka. Kinyume chake, sauti ya Bwana sio “sauti kubwa ya kuchanganya, lakini … [ni] sauti tulivu, [kama] mnong’ono, na [inapenya] hata kwenye roho.”14 Ili kuweza kuisikia sauti hii tulivu, wewe pia lazima uwe mtulivu!15

Kwa muda, ugonjwa huu wa ulimwenguni kote umefuta shughuli ambazo kwa kawaida ni sehemu ya maisha yetu. Karibuni tutaweza kuchagua kuujaza muda huo tena na kelele na vurugu za ulimwengu. Au tunaweza kutumia muda wetu kusikiliza sauti ya Bwana ikinon’gona mwongozo Wake, faraja, na amani. Muda wa ukimya ni muda mtakatifu—muda ambao utasaidia ufunuo binafsi na kuleta amani.

Jiwekee nidhamu ya kuwa na muda wa peke yako na muda pamoja na uwapendao. Fungua moyo wako kwa Mungu katika maombi. Tenga muda wa kujifunza zaidi maandiko na kuabudu katika hekalu.

Ndugu zangu wapendwa, kuna mambo mengi Bwana anatutaka kujifunza kutoka katika uzoefu wetu wakati wa ugonjwa huu wa ulimwenguni kote. Nimeorodhesha manne tuu. Ninawaalika kutengeneza orodha yenu wenyewe, kuitafakari kwa uangalifu, na kuishiriki na wale unaowapenda.

Yajayo ni angavu kwa watu wa Mungu watunzao maagano.16 Bwana kwa wingi atawaita watumishi Wake ambao wanashikilia ukuhani kwa kustahili kwa ajili ya kubariki, kufariji, na kuimarisha wanadamu na kusaidia kuutayarisha ulimwengu na watu wake kwa ajili ya Ujio Wake wa Pili. Inatupasa kila mmoja wetu kujipima kwa utawazo mtakatifu tulioupokea. Tunaweza kufanya hili! Nashuhudia hayo, kwa kuonyesha hisia zangu za upendo kwa kila mmoja wenu, kaka zangu wapendwa, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.