Mkutano Mkuu
Kristo Amefufuka; Imani Kwake Itahamisha Milima
Mkutano mkuu wa Aprili 2021


Kristo Amefufuka; Imani Kwake Itahamisha Milima

Imani katika Yesu Kristo ni nguvu kubwa zaidi inayopatikana kwetu katika maisha haya. Vitu vyote vinawezekana kwa wale waaminio.

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, ninashukuru kwa fursa hii ya kuzungumza nanyi katika siku hii ya Jumapili ya Pasaka.1 Dhabihu ya kulipia dhambi na Ufufuko wa Yesu Kristo vimebadilisha maisha ya kila mmoja wetu milele. Tunampenda na kwa shukrani tunamwabudu Yeye na Baba yetu wa Mbinguni.

Katika miezi sita iliyopita, tumeendelea kupambana na janga la ulimwengu. Ninashangaa kwa uthabiti wako na nguvu ya kiroho mbele ya ugonjwa, kupoteza, na kutengwa. Ninaomba kila wakati kwamba, kupitia hayo yote, utahisi upendo wa Bwana usiokwisha kwako. Ikiwa umejibu majaribio yako kwa ufuasi wenye nguvu, mwaka huu uliopita hautakuwa bure.

Asubuhi ya leo, tumesikia kutoka kwa viongozi wa Kanisa ambao huja kutoka kila bara linalokaliwa duniani. Kweli, baraka za injili ni kwa kila kabila, lugha, na watu. Kanisa la Yesu Kristo ni kanisa la ulimwengu. Yesu Kristo ni kiongozi wetu.

Na kwa bahati nzuri, hata ugonjwa huu haujaweza kupunguza mwendo wa kuendelea kwa ukweli wa injili Yake. Injili ya Yesu Kristo ndiyo hasa inahitajika katika ulimwengu huu wa kuchanganyikiwa, ugomvi, na kuchoka.

Kila mmoja wa watoto wa Mungu anastahili fursa ya kusikia na kukubali ujumbe wa uponyaji, ukombozi wa Yesu Kristo. Hakuna ujumbe mwingine muhimu zaidi kwa furaha yetu—sasa na hata milele.2 Hakuna ujumbe mwingine uliojazwa zaidi na tumaini. Hakuna ujumbe mwingine unaoweza kuondoa ubishi katika jamii yetu.

Imani katika Yesu Kristo ni msingi wa imani yote na ni mfereji wa nguvu za kimungu. Kulingana na Mtume Paulo, “Pasipo imani haiwezekani kumpendeza [Mungu]: kwa maana yeye amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba yeye huwapa thawabu wale wamtafutao kwa bidii.”3

Kila kitu kizuri maishani—kila baraka inayowezekana ya umuhimu wa milele—huanza na imani. Kuruhusu Mungu atawale katika maisha yetu huanza na imani kwamba Yuko tayari kutuongoza. Toba ya kweli huanza na imani kwamba Yesu Kristo ana uwezo wa kutusafisha, kutuponya na kutuimarisha.4

“Msikatae uwezo wa Mungu,” nabii Moroni alitangaza, “kwani hufanya kazi kwa uwezo, kulingana na imani ya binadamu.”5 Ni imani yetu inayofungulia nguvu za Mungu katika maisha yetu.

Na bado, kuifanyia kazi imani kunaweza kuonekana kutuzidi uwezo. Wakati mwingine tunaweza kushangaa kama tunaweza kupata imani ya kutosha kupokea baraka ambazo tunahitaji sana. Walakini, Bwana alituliza hofu hizo kupitia maneno ya nabii wa Kitabu cha Mormoni Alma.

Picha
Mbegu ya haradali

Alma anatuomba kujaribu juu ya neno na “kutumia chembe ya imani, ndio, hata kama [hatuwezi] zaidi ya kutamani kuamini.”6 Msemo “chembe ya imani” unanikumbusha ahadi ya Bwana ya kibiblia kwamba ikiwa “tuna imani kama punje ya haradali,” tutaweza “kuuambia mlima huu, Ondoka hapa kwenda mahali pale; nao utaondoka; na hakuna jambo litakaloshindwa [kwetu].”7

Picha
Ndege miongoni mwa mbegu za haradali

Bwana anaelewa udhaifu wetu wa kimwili. Sisi sote tunashindwa wakati mwingine. Lakini pia Anajua uwezo wetu mkubwa. Mbegu ya haradali huanza kidogo lakini hukua kuwa mti mkubwa wa kutosha kwa ndege kutua kwenye matawi yake. Mbegu ya haradali inawakilisha imani ndogo lakini inayokua.8

Bwana hahitaji imani kamilifu kwetu ili kufikia uwezo Wake mkamilifu. Lakini anatuomba tuamini.

Ndugu na dada zangu wapendwa, wito wangu kwenu asubuhi hii ya Pasaka ni kuanzia leo kuongeza imani yako. Kupitia imani yako, Yesu Kristo ataongeza uwezo wako wa kuhamisha milima katika maisha yako,9 ingawa changamoto zako za kibinafsi zinaweza kuonekana kama Mlima Everest.

Milima yako inaweza kuwa upweke, shaka, magonjwa, au shida zingine za kibinafsi. Milima yako itatofautiana, na bado jibu kwa kila changamoto yako ni kuongeza imani yako. Hiyo inahitaji kazi. Wanafunzi wavivu na wanafunzi wazembe watapambana kila wakati kukusanya hata chembe ya imani.

Kufanya kitu vizuri kunahitaji juhudi. Kuwa mwanafunzi wa kweli wa Yesu Kristo hakuna chaguzi. Kuongeza imani yako na uaminifu Kwake kunahitaji juhudi. Napenda kutoa maoni sita kukusaidia kukuza imani hiyo na uaminifu.

Kwanza, soma. Kuwa mwenye kujifunza zaidi. Jifunze maandiko kwa kina ili kuelewa vyema utume na huduma ya Kristo. Yajue mafundisho ya Kristo ili uelewe nguvu yake kwa ajili ya maisha yako. Husisha ukweli ambao Upatanisho wa Yesu Kristo unafanya kazi kwako. Alijichukulia Mwenywe mateso yako, makosa yako, udhaifu wako, na dhambi zako Alilipa fidia na akakupa nguvu ya wewe kuhamisha kila mlima utakao kumbana nao. Unapata nguvu hiyo kwa imani yako, uaminifu, na utayari wa kumfuata Yeye.

Kuhamisha milima yako inaweza kuhitaji muujiza. Jifunze kuhusu miujiza. Miujiza huja kulingana na imani yako kwa Bwana. Kiini cha imani hiyo ni kuamini mapenzi Yake na ratiba—ni jinsi gani na lini atakubariki na msaada wa kimiujiza unaotamani. Ni kutoamini kwako ambako kutamfanya Mungu asikubariki na miujiza ya kuhamisha milima katika maisha yako.10

Kadri unavyojifunza zaidi juu ya Mwokozi, ndivyo itakavyokuwa rahisi kutumaini rehema Yake, upendo Wake usio na kikomo, na uimarisho Wake, uponyaji, na ukombozi. Mwokozi kamwe hayuko karibu na wewe kama wakati unapokabiliana na au kupanda mlima kwa imani.

Pili, chagua kuamini katika Yesu Kristo. Ikiwa una mashaka juu ya Mungu Baba na Mwanawe Mpendwa, au uhalali wa Urejesho au ukweli wa wito wa kimungu wa Joseph Smith kama nabii, chagua kuamini11 na baki kuwa mwaminifu. Chukua maswali yako kwa Bwana na kwa vyanzo vingine vya uaminifu. Jifunze kwa hamu ya kuamini badala ya kuwa na tumaini kwamba unaweza kupata kasoro katika maisha ya nabii au tofauti katika maandiko. Acha kuongeza mashaka yako kwa kuyarudia na wengine wenye mashaka. Ruhusu Bwana akuongoze kwenye safari yako ya ugunduzi wa kiroho.

Tatu, tenda kwa imani. Ungefanya nini kama ungekuwa na imani zaidi? Fikiria kuhusu hilo. Andika kuhusu hilo. Kisha pokea zaidi imani kwa kufanya kitu ambacho kinahitaji zaidi imani.

Nne, shiriki ibada takatifu kwa ustahiki. Amri hufungua nguvu za Mungu kwa maisha yako.12

Na tano, muombe Baba yako wa Mbinguni, katika Jina la Yesu Kristo, kwa ajili ya msaada.

Imani inahitaji matendo. Kupokea ufunuo kunahitaji matendo. Lakini “kila mmoja ambaye huuliza, hupata; na yule anayetafuta, huvumbua; na yule ambaye hubisha, hufunguliwa.”13 Mungu anajua nini kitasaidia imani yako kukua. Omba, na kisha omba tena.

Mtu asiyeamini anaweza kusema kuwa imani ni ya wanyonge. Lakini madai haya hayazingatii nguvu ya imani. Je, Mitume wa Mwokozi wangeendelea kufundisha mafundisho Yake baada ya kifo Chake, katika hatari ya maisha yao, ikiwa walikuwa wamemtilia shaka?14 Je, Joseph na Hyrum Smith wangepata vifo vya mashahidi kwa kutetea Urejesho wa Kanisa la Bwana kama wasingekuwa na ushuhuda wa kweli kwamba ni kweli? Je, Watakatifu takribani 2,000 wangekufa kando ya njia ya msafra wa waanzilishi15 ikiwa hawakuwa na imani kwamba injili ya Yesu Kristo ilikuwa imerejeshwa? Kweli, imani ni nguvu ambayo inawezesha uwezekano wa kutimiza yasiyowezekana.

Usipunguze imani ambayo tayari unayo. Inahitaji imani kujiunga na Kanisa na kubaki mwaminifu. Inahitaji imani kuwafuata manabii badala ya wataalam na maoni maarufu. Inahitaji imani kuhudumu misheni wakati wa janga lililoenea ulimwenguni. Inahitaji imani kuishi maisha safi wakati ulimwengu unapiga kelele kwamba sheria ya Mungu ya usafi wa mwili sasa imepitwa na wakati. Inahitaji imani kufundisha injili kwa watoto katika ulimwengu wa kidunia. Inahitaji imani kuombea maisha ya mpendwa, na imani zaidi kukubali jibu la kukatisha tamaa.

Miaka miwili iliyopita Dada Nelson na mimi tulitembelea Samoa, Tonga, Fiji, na Tahiti. Kila moja ya mataifa ya kisiwa hicho yalikuwa yamepata mvua kubwa kwa siku nyingi. Waumini walifunga na kuomba kwamba mikutano yao ya nje ilindwe kutokana na mvua.

Katika Samoa, Fiji, na Tahiti, mara tu mkutano ulipoanza, mvua ilikatika. Lakini Tonga, mvua haikukatika. Walakini Watakatifu waaminifu 13,000 walikuja mapema saa nyingi ili kupata kiti, walisubiri kwa uvumilivu kwenye mvua, na kisha wakakaa kwenye mkutano wa saa mbili wakiwa wameloana sana.

Picha
Watakatifu wa Tonga wakiwa kwene vua

Tuliona imani thabiti ikifanya kazi miongoni mwa kila mmoja wa wenyeji wa kisiwa hicho—imani ya kutosha kuzuia mvua, na imani ya kuvumilia wakati mvua ikinyeesha.

Milima katika maisha yetu sio kila wakati inasonga jinsi au vile tupendavyo. Lakini imani yetu mara zote itatupeleka mbele. Imani mara zote inaongeza ufikiaji wetu wa nguvu za kimungu.

Tafadhali tambua hili: ikiwa kila kitu na kila mtu ulimwenguni ambaye unamwamini atashindwa, Yesu Kristo na Kanisa Lake kamwe hawatashindwa. Bwana hasinzii kwamwe, wala Halali.16 Yeye ni “yule yule jana, na leo, na hata [kesho].”17 Hatasahau maagano Yake,18 ahadi Zake, au upendo wake kwa watu Wake. Yeye hufanya miujiza leo na Atafanya miujiza kesho.19

Imani katika Yesu Kristo ndiyo nguvu kubwa zaidi inayopatikana kwa ajili yetu sisi katika maisha haya. Vitu vyote vinawezekana kwa wale waaminio.20

Imani yako inayoongezeka Kwake itahamisha milima—sio milima ya mwamba ambayo huipamba dunia—lakini milima ya taabu katika maisha yako. Imani yako inayostawi itakusaidia kuzigeuza changamoto kuwa ukuaji unaoendana na fursa.

Katika Jumapili hii ya Pasaka, pamoja na hisia zangu za kina za upendo na shukrani, ninatoa ushuhuda wangu kwamba Yesu Kristo amefufuka. Amefufuka ili aliongoze Kanisa Lake. Amefufuka kubariki maisha ya watoto wote wa Mungu, popote wanapoishi. Kwa imani Kwake, tunaweza kusogeza milima katika maisha yetu. Ninashuhudia hivyo, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.