Vitabu vya Maelekezo na Miito
2. Kuwasaidia Watu Binafsi na Familia katika Kazi ya Wokovu na Kuinuliwa


“2. Kuwasaidia Watu Binafsi na Familia katika Kazi ya Wokovu na Kuinuliwa,” Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho (2020).

“2. Kuwasaidia Watu Binafsi na Familia,” Kitabu cha Maelezo ya Jumla.

Picha
picha ya familia

2.

Kuwasaidia Watu Binafsi na Familia katika Kazi ya Wokovu na Kuinuliwa

2.0

Utangulizi

Kama kiongozi katika Kanisa la Yesu Kristo, unawasaidia watu binafsi na familia katika kutimiza kazi ya Mungu ya wokovu na kuinuliwa (ona 1.2). Hatima ya lengo la kazi hii ni kuwasaidia watoto wote wa Mungu kupokea baraka za uzima wa milele na utimilifu wa shangwe.

Kazi kubwa ya wokovu na kuinuliwa inatimizwa kupitia familia. Kwa waumini wote wa Kanisa, kiini cha kazi hii ni nyumbani. Sura hii itakusaidia kupata ono la:

  • Wajibu wa familia katika mpango wa Mungu.

  • Kazi ya wokovu na kuinuliwa nyumbani.

  • Uhusiano kati ya nyumbani na Kanisani.

2.1

Wajibu wa Familia katika Mpango wa Mungu

Familia imetakaswa na Mungu na ni kiini cha mpango Wake. Kila mmoja wetu “ni mwana au binti mpendwa wa kiroho wa wazazi wa mbinguni [mwenye] asili takatifu na takdiri (“Familia: Tangazo kwa Ulimwengu,” ChurchofJesusChrist.org). Sisi ni sehemu ya familia yao. Tuliishi pamoja nao kabla hatujazaliwa duniani.

Kama sehemu ya mpango Wake, Baba wa Mbinguni ameanzisha familia duniani. Anakusudia familia zituletee furaha. Familia zinatoa fursa ya kujifunza, kukua, kuhudumu, kutubu, na kusamehe. Zinaweza kutusaidia kujiandaa kwa ajili ya uzima wa milele.

Katika maisha haya, watu wengi wana fursa chache za uhusiano wa kifamilia wenye upendo. Hakuna familia iliyo huru kutokana na changamoto, maumivu, na huzuni. Watu binafsi na familia huonyesha imani katika Bwana na kujitahidi kuishi kulingana na kweli Yeye alizozifunua kuhusu familia. Mwokozi ameahidi kwamba Atasaidia kubeba mizigo ya wote wanaokwenda Kwake (ona Mathayo 11:28–30).

Mpango wa Baba wa Mbinguni wa furaha unahakikisha kwamba watoto Wake wote watakuwa na fursa ya kuikubali injili Yake na kupokea baraka Zake kuu (ona Mafundisho na Maagano 137:7–10). Wote wanaofanya na kushika maagano na Mungu wanaweza kupata furaha na “amani katika ulimwengu huu, na uzima wa milele katika ulimwengu ujao” (Mafundisho na Maagano 59:23; ona pia Mosia 2:41).

Ahadi ya Mungu ya uzima wa milele inajumuisha ndoa ya milele, watoto, na baraka zingine zote za familia ya milele. Ahadi hii inatumika kwa wale ambao kwa sasa hawajafunga ndoa au hawana familia ndani ya Kanisa (ona 38.1.4). Ingawa muda sahihi na jinsi ambavyo baraka za kuinuliwa zinavyopokelewa haijulikani, baraka hizi zinaahidiwa kwa wale wanaojitahidi kuishi kama wafuasi wa Yesu Kristo.

2.1.1

Familia za Milele

Familia za milele zinaundwa wakati waumini wa Kanisa wanapofanya maagano pale wanapopokea ibada za kuunganishwa ndani ya hekalu. Baraka za familia ya milele huja pale waumini wanaposhika maagano hayo na kutubu wakati wanapokosea. Viongozi wa Kanisa wanawasaidia waumini kujiandaa kupokea ibada hizi na kuheshimu maagano yao.

Kila mtu anaweza kutimiza idadi kadhaa ya majukumu katika familia ya milele. Majukumu yote ya kifamilia ni matakatifu na muhimu. Majukumu haya yanaweza kuwajumuisha mama na baba, binti na mwana, dada na kaka, shangazi na mjomba, na bibi na babu. Kutimiza majukumu haya kwa upendo kunawasaidia watoto wa Mungu kupiga hatua kuelekea uzima wa milele.

Kipengele cha ziada cha kuanzisha familia za milele ni kufanya ibada katika hekalu zinazowaruhusu waumini kuunganishwa kwa mababu zao waliofariki.

Wakiwa na uelewa wa mpango wa Mungu, waumini wanatafuta baraka za familia ya milele. Hii inajumuisha kujiandaa kuwa mwenza na mzazi mwenye kustahili na mwenye upendo.

2.1.2

Mume na Mke

Ndoa kati ya mwanamume na mwanamke imetakaswa na Mungu (ona Mafundisho na Maagano 49:15). Mume na mke wanakusudiwa kuendelea kukua pamoja kuelekea uzima wa milele (ona 1 Wakorintho 11:11).

Moja ya vigezo kwa ajili ya kupata uzima wa milele ni kwa mwanamume na mwanamke kuingia katika agano la ndoa ya milele (ona Mafundisho na Maagano 131:1–4). Wanandoa wanafanya agano hili wakati wanapopokea ibada ya kuunganishwa katika ndoa ndani ya hekalu. Agano hili ni msingi wa familia ya milele. Likitunzwa kwa uaminifu, linaruhusu ndoa yao kudumu milele. Hatimaye, wanaweza kuwa kama Mungu (ona Mafundisho na Maagano132:19–20).

Mungu ameamuru waume na wake waambatane pamoja (ona Mwanzo 2:24; Mafundisho na Maagano 42:22). Katika muktadha huu, neno ambatana linamaanisha kujitoa kikamilifu na kuwa mwaminifu kwa mtu fulani. Wanandoa waliooana huambatana pamoja kwa kupendana na kuhudumiana.

Kuambatana pia kunajumuisha uaminifu kamili kati ya mume na mke. Mahusiano ya kimapenzi kati ya mume na mke yanakusudiwa kuwa ya kupendeza na matakatifu. Yameamriwa na Mungu kwa ajili ya uumbaji wa watoto na kwa ajili ya kuonyesha upendo kati ya mume na mke. Upole na heshima—sio ubinafsi—vinapaswa kuongoza uhusiano wao wa kimapenzi.

Mungu ameamuru kuwa kujamiiana kuhifadhiwe kwa ajili ya ndoa kati ya mwanamume na mwanamke. Kubaki safi kimapenzi kabla ya ndoa na kuwa mwaminifu katika ndoa kunawasaidia watu binafsi kuwa wenye furaha ya kweli na kuepuka madhara ya kiroho, kihisia, na ya kimwili. Wazazi na viongozi wa Kanisa wanahimizwa kufanya yote wawezayo ili kuimarisha mafundisho haya. (Ona 38.6:5.)

Wanandoa wanatafuta umoja katika kuanzisha familia yao (ona Mwanzo 2:24). Kuwa wamoja katika ndoa kunahitaji ubia kamili, kushirikiana majukumu. Mume na mke wako sawa machoni pa Mungu. Mmoja hapaswi kumtawala mwingine. Maamuzi yao yanapaswa kufanywa kwa umoja na upendo, pamoja na ushiriki mkamilifu wa wote.

Adamu na Hawa waliweka mfano kwa ajili ya waume na wake. Walifanya kazi, kusali, na kuabudu pamoja (ona Musa 5:1, 4). Waliwafundisha watoto wao injili na waliomboleza pamoja juu ya majaribu yao (ona Musa 5:12, 27). Waliungana wao kwa wao na pamoja na Mungu.

2.1.3

Wazazi na Watoto

Kabla watoto wa Mungu hawajapokea “kutokufa na uzima wa milele,” lazima wapate mwili wenye kufa (Musa 1:39). Amri ya kwanza ya Mungu kwa Adamu na Hawa kama mume na mke ilikuwa ni kupata watoto (ona Mwanzo 1:28). Manabii wa siku za mwisho wamefundisha kwamba “amri ya Mungu kwa watoto Wake ya kuongezeka na kuijaza dunia inabaki kuwa na nguvu” (“Familia: Tangazo kwa Ulimwengu”; ona pia Mafundisho na Maagano 49:16–17).

Ni fursa na ni wajibu mtakatifu kwa mume na mke kuwatunza watoto wanaoweza kuwazaa au kuwaasili. Wazazi wenye kuasili wana baraka na wajibu ule ule kama wa wazazi wa kibaiolojia.

Mume na mke wenye upendo kwa pamoja wanaweka mazingira yaliyo bora zaidi kwa ajili ya kuwalea na kuwafunza watoto. Hali binafsi zinaweza kuwazuia wazazi kuwalea watoto wao kwa pamoja. Hata hivyo, Bwana atawabariki wanapotafuta msaada Wake na wanapojitahidi kutunza maagano yao pamoja Naye.

Wazazi wana jukumu muhimu la kuwasaidia watoto wao kujiandaa kupokea baraka za uzima wa milele. Wanawafundisha watoto wao kumpenda na kumtumikia Mungu na wengine (ona Mathayo 22:36–40). Wanawafundisha kusali kwa Baba wa Mbinguni na kujifunza neno la Mungu (ona Alma 37:36–37, 44–46). Wanawasaidia watoto wao waelewe mafundisho ya imani katika Yesu Kristo, toba, ubatizo, na kipawa cha Roho Mtakatifu (ona Mafundisho na Maagano 68:25). Pia wanawasaidia wajiandae kufanya maagano wakati wanapopokea ibada za wokovu na kuinuliwa.

“Akina baba wanapaswa kusimamia familia zao katika upendo na haki na wana jukumu la kukimu mahitaji ya maisha na ulinzi kwa familia zao” (“Familia: Tangazo kwa Ulimwengu”). Wakati panapokuwa hakuna mume au baba katika nyumba, mama anaongoza katika familia.

Kuongoza katika familia ni jukumu la kusaidia kuwaongoza wanafamilia kurudi kuishi katika uwepo wa Mungu. Hii inafanyika kwa kuhudumu na kufundisha kwa upole, unyenyekevu, na upendo msafi, kwa kufuata mfano wa Yesu Kristo (ona Mathayo 20:26–28). Kuongoza katika familia kunajumuisha kuwaongoza wanafamilia katika sala za kila siku, kujifunza injili, na vipengele vingine vya kuabudu. Wazazi wanafanya kazi kwa umoja ili kutimiza majukumu haya.

“Akina mama wana jukumu la kimsingi kwa utunzaji wa watoto wao” (“Familia: Tangazo kwa Ulimwengu”). Kutunza maana yake ni kustawisha, kufundisha, na kuunga mkono, kwa kufuata mfano wa Mwokozi (ona 3 Nefi 10:4). Katika umoja na mume wake, mama anasaidia familia yake kujifunza kweli za injili na kujenga imani kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Kwa pamoja wanakuza mazingira ya upendo katika familia.

“Katika majukumu haya matakatifu, akina baba na akina mama wana wajibu wa kusaidiana wao kwa wao kama washiriki sawa” (“Familia: Tangazo kwa Ulimwengu”). Kwa sala wanashauriana pamoja na pia na Bwana. Wanafanya maamuzi kwa pamoja kwa umoja na upendo, kwa ushirikiano kamili wa wote wawili.

Picha
baba akiifundisha familia

2.2

Kazi ya Wokovu na Kuinuliwa Nyumbani

Urais wa Kwanza ulisema, “Nyumbani ni msingi wa maisha yenye uadilifu” (barua ya Urais wa Kwanza, Feb. 11, 1999). Katika nyumba zao, watu binafsi na familia wanashiriki katika kazi ya wokovu na kuinuliwa. Kazi hii ina majukumu manne matakatifu yaliyoainishwa:

  • Kuishi injili ya Yesu Kristo (ona 1.2.1)

  • Kuwatunza wale wenye uhitaji (ona 1.2.2)

  • Kuwaalika wote waipokee injili (ona 1.2.3)

  • Kuziunganisha familia milele (ona 1.2.4)

Ili kuwasaidia waumini katika kufanya kazi ya wokovu na kuinuliwa nyumbani, viongozi wa Kanisa wanawahimiza kuweka nyumba zao kuwa mahali ambapo Roho yupo. Pia wanawahimiza waumini kuheshimu siku ya Sabato, kujifunza na kusoma injili nyumbani, na kufanya jioni ya nyumbani kila wiki. Viongozi wanatilia mkazo maalum kwa kuwasaidia watu binafsi ambao wanaweza kukosa msaada au kutiwa moyo kutoka kwa wanafamilia.

2.2.1

Nyumba Ambapo Roho Yupo

Waumini wa Kanisa wanahimizwa kufanya nyumba zao kuwa mahala pa nguvu za kiroho na shangwe. Wanaweza kumwalika Roho wa Bwana katika nyumba zao kupitia juhudi za kawaida. Kila nyumba inaweza kuwa “nyumba ya sala, nyumba ya kufunga, nyumba ya imani, nyumba ya kujifunza, nyumba ya utukufu, nyumba ya utaratibu, nyumba ya Mungu” (Mafundisho na Maagano 88:119).

2.2.2

Kuitakasa Sabato

Mungu amewaamuru watoto Wake “kuikumbuka siku ya sabato, na kuitakasa” (Kutoka 20:8). Waumini wa Kanisa wanakusanyika siku ya Sabato ili kupokea sakramenti kwa ajili ya ukumbusho wa Yesu Kristo na Upatanisho Wake (ona Mafundisho na Maagano 59:12). Sabato ni siku ya kujifunza injili na kufundisha kanisani na nyumbani. Waumini wanaweza kuimarishwa siku ya Sabato pale wanaposhiriki katika shughuli kama vile:

  • Kuabudu binafsi kupitia sala na kufunga.

  • Kujifunza na kusoma injili.

  • Uhudumiaji na huduma kwa wengine.

  • Historia ya familia.

  • Muda wa kufurahi kama familia.

  • Mikusanyiko mingine inayofaa.

2.2.3

Kujifunza na Kusoma Injili Nyumbani

Kufundisha na kujifunza injili kunalenga nyumbani na kusaidiwa na Kanisa. Viongozi wa Kanisa wanawahimiza waumini wote kujifunza injili nyumbani siku ya Sabato na katika wiki yote. Kujifunza injili nyumbani kunawaimarisha watu binafsi na familia. Kunafanya uongofu kwa Baba wa Mbinguni na Bwana Yesu Kristo kuwa wa kina.

Mafunzo ya maandiko kama yalivyoelezwa kwa muhtasari kwenye Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia ni kozi iliyopendekezwa ya kujifunza ya injili nyumbani. Njoo, Unifuate imepanga masomo yaliyo sambamba katika Darasa la Watoto, Shule ya Jumapili, Wasichana, akidi za Ukuhani wa Haruni na seminari pamoja na mafunzo ya injili nyumbani.

Watu binafsi na familia wanatafuta mwongozo wa kiungu wanapochagua kujifunza kile kitakachoweza kwa kiasi kikubwa kukidhi mahitaji yao. Kwa nyongeza kwenye vifungu vya maandiko vilivyopendekezwa katika Njoo, Unifuate, watu wanaweza kwa sala kufikiria kujifunza:

  • Kitabu cha Mormoni na maandiko mengine.

  • Jumbe za mkutano mkuu.

  • Majarida ya Kanisa na maudhui mengine yenye kujenga.

2.2.4

Jioni ya Nyumbani na Shughuli Nyinginezo

Manabii wa siku za mwisho wamewashauri waumini wa Kanisa kuwa na jioni ya nyumbani kila wiki. Huu ni muda mtakatifu kwa ajili ya watu binafsi na familia kujifunza injili, kuimarisha shuhuda, kujenga umoja, na kuwa na furaha wao kwa wao.

Jioni ya nyumbani inaweza kubadilika kulingana na hali za waumini. Inaweza kufanyika siku ya Sabato au siku na muda mwingine. Inaweza kujumuisha:

  • Mafunzo na maelekezo ya injili (nyenzo za Njoo, Unifuate zinaweza kutumika kulingana na mapendeleo).

  • Kuwatumikia wengine.

  • Kuimba au kupiga nyimbo za Kanisa na nyimbo za Watoto (ona sura ya 19).

  • Kuwasaidia wanafamilia katika Maendeleo ya Watoto na Vijana.

  • Baraza la familia ili kuweka malengo, kutatua matatizo, na kuratibu ratiba.

  • Shughuli za burudani.

Waumini waseja na wengine wanaweza kukusanyika katika vikundi katika muda tofauti na ibada za kuabudu za Sabato ili kushiriki katika jioni ya nyumbani na kuimarishana kupitia kujifunza injili. Njoo, Unifuate inaweza kuwa nyenzo kwa ajili ya wale wanaotamani kujifunza pamoja.

Viongozi wanatoa umakini maalum ili kuwasaidia wale ambao ni wapya katika kuwa na jioni ya nyumbani na kujifunza injili.

Kwa kuongeza kwenye jioni ya nyumbani, viongozi wanahimiza familia kuweka kipaumbele kwa kutenga muda wa kuwa pamoja kwa wiki nzima. Hii inaweza kujumuisha kushiriki milo, kufanya kazi na kuhudumu pamoja, na shughuli za burudani.

Ili kutoa muda kwa ajili ya familia kuwa pamoja, viongozi wanapaswa kutenga siku za Jumatatu jioni ili kusiwe na mikutano na shughuli za Kanisa.

Viongozi wanawahimiza waumini kuwa endelevu katika kuwa na jioni ya nyumbani na kutumia muda pamoja kama familia (ona Mafundisho na Maagano 64:33).

2.2.5

Kuwasaidia Watu Binafsi

Viongozi wa Kanisa wanawasaidia waumini wanaokosa msaada wa kifamilia. Waumini ambao wanaweza kuhitaji msaada wa ziada ni pamoja na:

  • Watoto, vijana, na watu wazima ambao familia zao hazishiriki kikamilifu katika mikutano na shughuli za Kanisa.

  • Watu wazima waseja wa umri wowote, ikiwa ni pamoja na wazazi wasio na wenzi na wanaume wagane na wanawake wajane.

Viongozi wanawasaidia waumini hawa na familia zao kuwa na fursa za ushirika, uzoefu wa kijamii wenye siha, na ukuaji wa kiroho. Viongozi wanawahimiza na kuwasaidia katika juhudi zao za kujifunza na kuishi injili ya Yesu Kristo. Viongozi pia wanawapa fursa za kuhudumu katika Kanisa.

2.3

Uhusiano kati ya Nyumbani na Kanisani

Kazi ya wokovu na kuinuliwa inalenga nyumbani na kusaidiwa na Kanisa. Kanuni zifuatazo zinatumika katika uhusiano kati ya Nyumbani na Kanisani.

  • Viongozi na walimu wanaheshimu wajibu wa wazazi na kuwasaidia. Viongozi na walimu wanaanzisha na kudumisha mawasiliano yenye tija na wazazi.

  • Viongozi wanatafuta kuhakikisha kwamba mikutano ya Kanisa, shughuli, na programu vinawasaidia watu binafsi na familia katika kufanya kazi ya wokovu na kuinuliwa katika nyumba zao.

  • Baadhi ya mikutano ya Kanisa ni muhimu katika kila kata au tawi. Hii inajumuisha mikutano ya sakramenti na madarasa na mikutano ya akidi inayofanywa siku ya Sabato. Mikutano mingine mingi, shughuli, na programu sio muhimu. Viongozi wanaipangilia kama itavyohitajika ili kukidhi mahitaji ya watu binafsi na familia. Viongozi wanazingatia hali ya mahali husika na nyenzo.

  • Watu binafsi na familia wanafikiria hali zao wakati wanapofanya maamuzi kuhusu kushiriki katika programu za Kanisa ambazo si za lazima.

  • Huduma za Kanisa na ushiriki huitaji kiasi cha dhabihu. Bwana atawabariki waumini wakati wanapohudumu na kutoa dhabihu katika Kanisa Lake. Hata hivyo, kiasi cha muda kilichotengwa kwa ajili ya huduma ya Kanisa hakipaswi kupunguza uwezo wa waumini kutimiza wajibu wao nyumbani, kazini, na sehemu nyingine. Viongozi na waumini hawapaswi kuzidiwa na majukumu mengi ya Kanisa. Wala hawapaswi kutakiwa kufanya dhabihu za ziada ili kusaidia programu au shughuli za Kanisa.

Kadri waumini watakavyofuata kanuni hizi na misukumo ya Roho, Baba wa Mbinguni atabariki juhudi zao.

Picha
wenza wakicheka