Maandiko Matakatifu
2 Nefi 33


Mlango wa 33

Maneno ya Nefi ni ya kweli—Yanamshuhudia Kristo—Wale ambao wanamwamini Kristo wataamini maneno ya Nefi, ambayo yatasimama kama shahidi mbele ya baraza la hukumu. Karibia mwaka 559–545 K.K.

1 Na sasa mimi, Nefi, siwezi kuandika vitu vyote ambavyo vilifundishwa miongoni mwa watu wangu; wala mimi sio shujaa kwa kuandika, kama nilivyo katika mazungumzo; kwani mwanadamu anapozungumza kwa uwezo wa Roho Mtakatifu uwezo wa Roho Mtakatifu huyapeleka katika mioyo ya watoto wa watu.

2 Lakini tazama, kuna wengi wanaoshupaza mioyo yao dhidi ya Roho Mtakatifu, kwamba hana nafasi ndani yao; kwa hivyo, wanatupa vitu vingi ambavyo vimeandikwa na kuvichukua kama vitu visivyofaa.

3 Lakini mimi, Nefi, nimeandika yale ambayo nimeandika, na kuyachukua kuwa yenye thamani kuu, na zaidi kwa watu wangu. Kwani nawaombea siku zote kwa mchana, na macho yangu huitia mto maji usiku, kwa sababu yao; na ninamlilia Mungu wangu kwa imani, na ninajua kwamba atasikia kilio changu.

4 Na ninajua kwamba Bwana Mungu ataweka wakfu sala zangu kwa faidha ya watu wangu. Na maneno ambayo nimeandika kwa unyonge yatatiwa nguvu kwao; kwani inawashawishi kutenda mema; inawafahamisha wao kuhusu babu zao; na inazungumza kuhusu Yesu, na kuwashawishi kumwamini, na kuvumilia hadi mwisho, ambao ni uzima wa milele.

5 Na inazungumza kwa ukali dhidi ya dhambi, kulingana na vile ukweli ulivyo wazi; kwa hivyo, hakuna mtu yeyote atakayekasirikia maneno ambayo nimeandika ila tu awe na roho ya ibilisi.

6 Nafurahia kwa uwazi; nafurahia ukweli; namfurahia Yesu wangu, kwani ameikomboa nafsi yangu kutoka jehanamu.

7 Nina hisani kwa watu wangu, na imani kuu katika Kristo kwamba nitakutana na nafsi nyingi zisizokuwa na mawaa katika kiti chake cha hukumu.

8 Nina hisani kwa Myahudi—nasema Myahudi, kwa sababu nina maana kwamba nilitoka huko.

9 Na pia nina hisani kwa Wayunani. Lakini tazama, siwezi kuwatumainia ila tu wao wapatanishwe na Kristo, na kuingia katika lile lango jembamba, na watembee katika njia ile iliyosonga inayoelekeza uzima wa milele, na waendelee katika njia hiyo hadi mwisho wa siku ya majaribio.

10 Na sasa, ndugu zangu wapendwa, na pia Myahudi, na ninyi nyote mlio pande zote za ulimwengu, sikilizeni maneno haya na mwamini katika Kristo; na kama hamwamini katika maneno haya aminini katika Kristo. Na kama mtamwamini Kristo mtaamini katika maneno haya, kwani ni maneno ya Kristo, na ameyapatia kwangu; na yanafundisha wanadamu wote kwamba wafanye mema.

11 Na kama sio maneno ya Kristo, amueni ninyi—kwani Kristo atawaonyesha, kwa uwezo na utukufu mkuu, kwamba ni maneno yake, katika siku ya mwisho; na wewe na mimi tutasimama uso kwa uso kwenye baraza lake; na utajua kwamba nimeamriwa na yeye kuandika vitu hivi, ingawa mimi ni mnyonge.

12 Na ninamuomba Baba kwa jina la Kristo kwamba wengi wetu, kama sio wote, waokolewe katika ufalme wake siku ile kuu ya mwisho.

13 Na sasa, ndugu zangu wapendwa, wale wote ambao ni wa nyumba ya Israeli, na nyote hadi mwisho wa ulimwengu, nawazungumzia kama sauti inayolia kutoka mavumbini: Kwa herini hadi siku ile kuu itakapofika.

14 Na wewe usiyekubali kupokea wema wa Mungu, na kuheshimu maneno ya Wayahudi, na pia maneno yangu, na maneno yatakayotoka kutoka kinywa cha Mwanakondoo wa Mungu, tazama, nakupigia kwaheri isiyo na mwisho, kwani maneno haya yatakuhukumu siku ya mwisho.

15 Kwani yale ambayo ninayatia muhuri duniani, yataletwa dhidi yako katika baraza la hukumu; kwani Bwana ameniamuru hivi, na ni lazima nitii. Amina.