Maandiko Matakatifu
Yakobo (KM) 1


Kitabu cha Yakobo
Mdogo wa Nefi

Maneno aliyowahubiria ndugu zake. Anamfadhaisha mtu aliyetaka kupindua mafundisho ya Kristo. Maneno machache kuhusu historia ya watu wa Nefi.

Mlango wa 1

Yakobo na Yusufu wanatafuta kuwashawishi wanadamu kumwamini Kristo na kushika amri Zake—Nefi anafariki—Uovu unazidi miongoni mwa Wanefi. Karibia mwaka 544–421 K.K.

1 Kwani tazama, ikawa kwamba miaka hamsini na mitano ilikuwa imepita tangu Lehi atoke Yerusalemu; kwa hivyo, Nefi alinipatia mimi, Yakobo, amri kuhusu mabamba yale madogo, ambako vitu hivi vimechorwa.

2 Na akanipatia mimi, Yakobo, amri kwamba niandike kwenye mabamba haya vitu vichache ambavyo nilivifikiria kuwa vyenye thamani; na kwamba nisiguse, ila kidogo tu, kuhusu historia ya hawa watu wanaoitwa watu wa Nefi.

3 Kwani alisema kwamba historia ya watu wake iandikwe kwenye yale mabamba yake mengine, na kwamba nihifadhi mabamba haya na kupokelezea uzao wangu, kutoka kizazi hadi kizazi.

4 Na kama kulikuwa na mahubiri yaliyo matakatifu, au ufunuo ulio mkuu, au kutoa unabii, kwamba nichore yaliyo muhimu katika mabamba haya, na niyagusie sana kama iwezekanavyo, kwa ajili ya Kristo, na kwa faida ya watu wetu.

5 Kwani kwa sababu ya imani na wasiwasi mwingi, kwa hakika tulidhihirishiwa, kuhusu vile vitu vitakavyowapata watu wetu.

6 Na pia tulikuwa na ufunuo mwingi, na roho ya unabii mwingi; kwa hivyo, tulijua kuhusu Kristo na ufalme wake, utakaokuja.

7 Kwa hivyo tulifanya kazi kwa bidii miongoni mwa watu wetu, kwamba tuwashawishi waje kwa Kristo, na waonje wema wa Mungu, ili waingie katika pumziko lake, na ili kwa njia yoyote asiape katika ghadhabu yake kwamba hawataingia ndani, kama walivyomtia hasira katika siku za majaribio wakati wana wa Israeli walipokuwa nyikani.

8 Kwa hivyo, tunatamani kutoka kwa Mungu kama ingewezekana kwamba tungewashawishi wanadamu wote wasimwasi Mungu, kumtia hasira, lakini kwamba watu wote wangemwamini Kristo, na kutafakari kuhusu kifo chake, na kubeba msalaba wake na kuchukua aibu ya ulimwengu; kwa hivyo, mimi, Yakobo, najichukulia kutimiza amri ya kaka yangu Nefi.

9 Sasa Nefi akaanza kuzeeka, na akajua kwamba anakaribia kufariki; kwa hivyo, akamtia mtu mafuta awe mfalme na mtawala juu ya watu wake sasa, kulingana na utawala wa wafalme.

10 Watu walikuwa wamempenda Nefi sana, kwa vile alikuwa mlinzi wao mkuu, na kuupunga upanga wa Labani kwa ulinzi wao, na alikuwa ametumikia kwa ustawi wao katika maisha yake yote—

11 Kwa hivyo, watu walitaka kulikumbuka jina lake. Na yeyote atakayetawala baada yake watu walimwita, Nefi wa pili, Nefi wa tatu, na kadhalika, kulingana na utawala wa wafalme; na hivyo ndivyo walivyoitwa na watu, haidhuru jina lolote walilokuwa nalo.

12 Na ikawa kwamba Nefi alifariki.

13 Sasa wale watu ambao hawakuwa Walamani walikuwa Wanefi; walakini, waliitwa Wanefi, Wayakobo, Wayusufu, Wazoramu, Walamani, Walemueli, na Waishmaeli.

14 Lakini mimi, Yakobo, hapa baadaye sitawapambanua kwa majina haya, lakini wale wanaotaka kuangamiza watu wa Nefi nitawaita Walamani, na wale ambao ni marafiki wa Nefi nitawaita Wanefi, au watu wa Nefi, kulingana na utawala wa wafalme.

15 Na sasa ikawa kwamba watu wa Nefi, chini ya utawala wa mfalme wa pili, walianza kuwa wagumu mioyoni mwao, na kujihusisha katika matendo maovu, kama vile Daudi wa kale wakitamani wake wengi na makahaba, na pia mwana wake, Sulemani.

16 Ndiyo, na hata pia wakaanza kutafuta dhahabu na fedha nyingi, na wakaanza kuinuliwa katika kiburi.

17 Kwa hivyo mimi, Yakobo, niliwapatia maneno haya nilipowafundisha katika hekalu, nikiwa nimepokea kwanza mwito wangu kutoka kwa Bwana.

18 Kwani mimi, Yakobo, na kaka yangu Yusufu tulikuwa tumetengwa tuwe makuhani na walimu kwa watu hawa, kwa mkono wa Nefi.

19 Na tuliadhimisha ofisi yetu kwa Bwana, tukijichukulia jukumu, na wajibu wa dhambi za watu vichwani mwetu kama hatungewafundisha neno la Mungu kwa bidii yote; kwa hivyo, tulitumikia kwa uwezo wetu ili damu yao isiwe katika mavazi yetu; la sivyo, damu yao ingekuwa katika mavazi yetu, na hatungepatikana bila alama katika siku ile ya mwisho.