Maandiko Matakatifu
Mormoni 9


Mlango wa 9

Moroni anawahimiza wale ambao hawaamini katika Kristo watubu—Anamtangaza Mungu wa miujiza, ambaye hutoa unabii na anayetoa vipawa na ishara juu ya waumini—Miujiza hukoma kwa sababu ya kutoamini—Ishara hutolewa kwa wale ambao huamini—Watu wanashauriwa kuwa na busara na kutii amri. Karibia mwaka 401–421 B.K.

1 Na sasa, ninazungumza pia kuhusu wale ambao hawaamini katika Kristo.

2 Tazama, mtaamini katika siku ya hukumu yenu—tazama, wakati Bwana atakapokuja, ndiyo, hata ile siku kuu wakati dunia itakunjwa pamoja kama karatasi, na vitu vya asili vitayeyuka kwa joto kubwa, ndiyo, katika siku ile kuu wakati mtaletwa kusimama mbele ya Mwanakondoo wa Mungu—ndipo mtasema kwamba hakuna Mungu?

3 Ndipo mtaendelea kumkana Kristo, au mnaweza kumtazama Mwanakondoo wa Mungu? Mnadhani kwamba mtaishi na yeye chini ya ufahamu wa makosa yenu? Mnadhani ya kwamba mngekuwa na furaha kuishi na kile Kiumbe kitakatifu, wakati nafsi zenu zina msukosuko na ufahamu wa makosa kwamba daima mmetusi sheria zake?

4 Tazama, ninawaambia kwamba mtakuwa na huzuni sana kuishi na Mungu aliye mtakatifu na wa haki, chini ya ufahamu wa uchafu wenu mbele yake, kuliko kuishi na nafsi zilizolaaniwa katika jehanamu.

5 Kwani tazama, wakati mtaletwa kuona uchi wenu mbele ya Mungu, na pia utukufu wa Mungu, na utakatifu wa Yesu Kristo, itawasha mwale wa moto usiozimika juu yenu.

6 Ee basi ninyi msioamini, mgeukieni Bwana; lieni kwa Baba kwa nguvu katika jina la Yesu, kwamba pengine mpatikane bila waa, safi, warembo, na weupe, mkiwa mmeoshwa na damu ya Mwanakondoo, katika ile siku kuu na ya mwisho.

7 Na tena ninawazungumzia ninyi ambao hukataa unabii wa Mungu, na kusema kwamba haifanyiki tena, kwamba hakuna ufunuo, wala unabii, wala vipawa, wala uponyaji, wala kuzungumza kwenye lugha za kigeni, na kutafsiri lugha;

8 Tazama nawaambia, yule anayekana vitu hivi hajui injili ya Kristo; ndiyo, hajasoma maandiko; na ikiwa ameyasoma, hayaelewi.

9 Kwani si tunasoma kwamba Mungu ni yule yule jana, na leo, na hata milele, na kwake hakuna kubadilika wala kivuli cha kubadilika?

10 Na sasa, kama mmejiwazia, mungu anayebadilika, na ambaye ana kivuli cha kubadilika, aidha mmejidhania mungu ambaye si Mungu wa miujiza.

11 Lakini tazama, nitawaelezea Mungu wa miujiza, hata Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo; na yule yule Mungu aliyeumba mbingu na dunia, na vitu vyote vilivyomo.

12 Tazama, alimuumba Adamu, na kupitia kwa Adamu kukatokea mwanguko wa binadamu. Na kwa sababu ya mwanguko wa binadamu Yesu Kristo alikuja, ambaye ni Baba na Mwana; na kwa sababu ya Yesu Kristo ukombozi wa binadamu ulitokea.

13 Na kwa sababu ya ukombozi wa binadamu, ambao ulifika kupitia kwa Yesu Kristo, wanarudishwa kwenye uwepo wa Bwana; ndiyo, hii ndiyo njia ambayo kwake watu wote wanakombolewa, kwa sababu kifo cha Kristo husababisha kutimizwa kwa ufufuko, ambao husababisha kutimizwa kwa ukombozi kutoka kwa usingizi wa milele, usingizi ambao watu wote wataamshwa kwa uwezo wa Mungu wakati tarumbeta itakapolia; na watatoka nje, wote wadogo na wakubwa, na wote watasimama mbele ya hukumu yake, wakikombolewa na kufunguliwa kutoka kwenye kamba hii ya kifo cha milele, kifo ambacho ni kifo cha mwili.

14 Na ndipo kutatokea hukumu ya Yule Mtakatifu juu yao; na ndipo kutatokea wakati ambao yule ambaye ni mchafu ataendelea kuwa mchafu; na yule ambaye ni mwenye haki ataendelea kuwa mwenye haki; yule ambaye ana furaha ataendelea kuwa na furaha; na yule asiye na furaha ataendelea kuwa bila furaha.

15 Na sasa, Ee ninyi nyote ambao mmejiwazia mungu ambaye hawezi kufanya miujiza, ningewauliza, je, vitu hivi vyote ambavyo nimezungumzia, vimefanyika? Je, mwisho umefika? Tazama nawaambia, Hapana; na Mungu hajakoma kuwa Mungu wa miujiza.

16 Tazama, si vitu ambavyo Mungu amefanya ni vya ajabu machoni mwetu? Ndiyo, na ni nani anayeweza kufahamu kazi za ajabu za Mungu?

17 Ni nani atasema kwamba haikuwa miujiza ambayo kwa neno lake mbingu na dunia vipo; na kwa uwezo wa neno lake mtu aliumbwa kutoka kwa mavumbi ya dunia; na kwa uwezo wa neno lake miujiza imefanyika?

18 Na ni nani atasema kwamba Yesu Kristo hakufanya miujiza mingi mikubwa? Na kulikuwa na miujiza mingi mikubwa iliyofanywa na mitume.

19 Na ikiwa miujiza ilifanyika wakati huo, kwa nini Mungu amekoma kuwa Mungu wa miujiza na bado awe kiumbe kisichobadilika? Na tazama, nawaambia habadiliki; ikiwa hivyo angekoma kuwa Mungu; na hakomi kuwa Mungu, na ni Mungu wa miujiza.

20 Na sababu ambayo inamfanya kukoma kufanya miujiza miongoni mwa watoto wa watu ni kwa sababu kwamba wamefifia katika kutoamini, na kutoka kwa njia ya kweli, na hawamjui Mungu ambaye wanapaswa kumwamini.

21 Tazama, ninawaambia kwamba yeyote aaminiye katika Kristo bila tashwishi, chochote atakachomwomba Baba katika jina la Kristo kitatolewa kwake; na hii ahadi iko kwa wote, hata mpaka mwisho wa dunia.

22 Kwani tazama, hivi anasema Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, kwa wanafunzi wake ambao watabaki nyuma, ndiyo, na pia kwa wanafunzi wake wote, kundi lilipokuwa likisikiliza: Nendeni ninyi katika ulimwengu wote, na mhubiri injili kwa kila mtu;

23 Na yule anayeamini na kubatizwa ataokolewa, lakini yule ambaye haamini atalaaniwa;

24 Na ishara hizi zitafuatana nao ambao huamini—katika jina langu watawatupa nje mashetani; watazungumza kwa lugha ngeni; watainua nyoka; na ikiwa watakunywa kitu cha kuhatarisha hakitawadhuru; wataweka mikono yao kwa wagonjwa na watapona;

25 Na yeyote atakayeamini katika jina langu, bila kuwa na shaka, kwake nitamhakikishia maneno yangu yote, hata kwa sehemu zote za dunia.

26 Na sasa, tazama, ni nani anaweza kuzuia kazi ya Bwana? Ni nani anayeweza kukana misemo yake? Ni nani atakayesimama dhidi ya uwezo usio na kipimo wa Bwana? Ni nani atachukia kazi za Bwana? Ni nani atachukia watoto wa Kristo? Tazama, nyote ambao mnachukia kazi za Bwana, kwani mtatangatanga na kuangamia.

27 Ee basi msidharau, na msishangae, lakini sikilizeni maneno ya Bwana, na mmwombeni Baba katika jina la Yesu kwa vitu vyote mtakavyohitaji. Msiwe na shaka, lakini muwe mkiamini, na muanze kama wakati wa kale, na mje kwa Bwana na mioyo yenu yote, na mtimize wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka mbele yake.

28 Muwe na hekima katika siku zenu za majaribio; jiondoeni kutoka kwenye uchafu; msiulize, ili mle kwa tamaa yenu, lakini ulizeni kwa uthabiti usiotingishika, kwamba msilegee kwa majaribu yoyote, lakini kwamba mheshimu Mungu wa kweli na aishiye.

29 Oneni kwamba hambatizwi bila kustahili; oneni kwamba msile sakramenti ya Kristo bila kustahili; lakini mhakikishe kwamba mnafanya vitu vyote katika ustahilifu, na mvifanye katika jina la Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aishiye; na mkifanya hivi, na mvumilie hadi mwisho, hamtatupwa nje kamwe.

30 Tazama, ninawazungumzia kama ninayezungumza kutoka kwa wafu; kwani najua kwamba mtapokea maneno yangu.

31 Msinilaani kwa sababu ya upungufu wangu, wala baba yangu, kwa sababu ya upungufu wake, wala wale ambao wameandika mbele yake; walakini mshukuruni Mungu kwa sababu amewaonyesha upungufu wetu, ili mjifunze kuwa na hekima zaidi yetu.

32 Na sasa, tazama, tumeandika maandiko haya kulingana na kujua kwetu, katika herufi ambazo zinaitwa miongoni mwetu Kimisri kilichogeuzwa, ambacho kilitolewa na kugeuzwa nasi, kulingana na njia yetu ya kuongea.

33 Na ikiwa mabamba yetu yangekuwa kubwa za kutosha tungeandika katika Kihebrania, lakini Kihebrania kimegeuzwa nasi pia; na ikiwa tungeandika katika Kihebrania; tazama, hamngekuwa na upungufu katika maandishi yetu.

34 Lakini Bwana anajua vitu ambavyo tumeandika, na pia kwamba watu wengine hawajui lugha yetu; na kwa sababu hakuna watu wengine wajuao lugha yetu, kwa ajili hii ametayarisha njia ya kutafsiri.

35 Na vitu hivi vimeandikwa ili tuwe huru kutoka kwa jukumu la dhambi zilizofanywa na ndugu zetu, ambao wamefifia kwa kutoamini.

36 Na tazama, vitu hivi ambavyo tumetaka kuhusu ndugu zetu, ndiyo, hata kurudishwa kwao kwa ufahamu wa Kristo, vipo kulingana na sala za watakatifu ambao waliishi katika nchi.

37 Na ninaomba Bwana Yesu Kristo awakubalie kwamba sala zao zijibiwe kulingana na imani yao; na namwomba Mungu Baba akumbuke lile agano ambalo amefanya na nyumba ya Israeli; na ninaomba awabariki milele, kupitia kwa imani kwa jina la Yesu Kristo. Amina.