Maandiko Matakatifu
Ibrahimu 4


Mlango wa 4

Miungu wanapanga uumbaji wa dunia na uhai wote juu yake—Mipango yao ya uumbaji kwa siku sita yaelezwa.

1 Na kisha Bwana akasema: Na tushuke chini. Nao wakashuka chini hapa mwanzo, na wale, ambao ni Miungu, kupanga na kutengeneza mbingu na dunia.

2 Na dunia, baada ya kuwa imetengenezwa, ilikuwa tupu na yenye ukiwa, kwa sababu hawakutengeneza chochote isipokuwa dunia; na giza lilitawala juu ya uso wa kilindi, na Roho za Miungu zilitulia juu ya uso wa maji.

3 Nao (Miungu) wakasema: Na uwepo mwanga; na mwanga ukawa.

4 Nao (Miungu) wakauona mwanga, kwani ulikuwa mwangavu; nao wakautenga mwanga, au wakaufanya utengane, na giza.

5 Na Miungu wakiita ile nuru Mchana, na giza wakaliita Usiku. Na ikawa kwamba kutoka jioni hadi asubuhi wakauita usiku; na kutoka asubuhi hadi jioni wakauita mchana; na hii ikawa ya kwanza, au mwanzo, wa ile waliyoiita mchana na usiku.

6 Na Miungu pia wakasema: Na liwe anga katikati ya maji, na likayatenge maji na maji.

7 Na Miungu wakaliagiza anga, ili liyatenge maji ambayo yalikuwa chini ya anga na maji yaliyokuwa juu ya anga; na ikawa hivyo, hata kama walivyoagiza.

8 Na Miungu wakaliita lile anga, Mbingu. Na ikawa kwamba ilikuwa kutoka jioni hadi asubuhi ile wakaiita usiku; na ikawa kwamba kutoka asubuhi hadi jioni ile wakaiita mchana; na hii ilikuwa ni mara ya pili kwamba wao wameita usiku na mchana.

9 Na Miungu wakaagiza, wakisema: Na maji yaliyo chini ya mbingu yakusanyike mahali pamoja, na acha dunia ipate kuonekana kavu; na ikawa hivyo kama walivyoagiza;

10 Na Miungu wakaiita ile ardhi kavu, Nchi; na kusanyiko la pamoja la maji, wao wakaliita Maji Makuu; na Miungu wakaona ya kuwa imewatii.

11 Na Miungu wakasema: Na tuitengeneze dunia ili ipate kutoa majani; mche utoao mbegu; mti wa matunda utoao matunda, kwa jinsi yake, ambao mbegu zake ziko ndani yake juu ya dunia; na ikawa hivyo, hata kama walivyoagiza.

12 Na Miungu wakaitengeneza dunia ili itoe majani kutokana na mbegu zake yenyewe, na mche utoao mche kutokana na mbegu zake wenyewe, utoe mbegu kwa jinsi yake; na dunia itoe mti kutokana na mbegu yake wenyewe, utoe matunda, mbegu ambayo yaweza kutoa matunda yake yenyewe, kwa jinsi yake; na Miungu wakaona kwamba imewatii.

13 Na ikawa kwamba wao wakazihesabu zile siku; kutoka jioni hadi asubuhi wakaita usiku; na ikawa, kutoka asubuhi hadi jioni wakaita mchana, na ikawa ni mara ya tatu.

14 Nao Miungu wakaipanga ile mianga katika anga la mbingu, na wakaifanya ziitenge mchana na usiku; na wakaipanga ili iwe kwa ishara na kwa majira, na kwa ajili ya siku na miaka;

15 Na wakaipanga ili ipate kuwa na nuru katika anga la mbingu na kutoa nuru juu ya dunia; na ikawa hivyo.

16 Na Miungu wakaipanga ile mianga mikuu miwili, mwanga mkubwa zaidi utawale mchana, na ule mwanga mdogo zaidi utawale usiku; pamoja na mwanga mdogo wakaziweka na nyota pia;

17 Na Miungu ikaiweka katika anga la mbingu, ili kutoa mwanga juu ya dunia, na kutawala mchana na usiku, na ili kutenganisha mwanga na giza.

18 Na Miungu wakaviangalia vitu hivyo walivyoviagiza hadi vikawa vinatii.

19 Na ikawa kwamba kutoka jioni hadi asubuhi hiyo ikawa usiku; na ikawa kwamba kutoka asubuhi hadi jioni hiyo ikawa mchana; na hiyo ilikuwa mara ya nne.

20 Na Miungu wakasema: Na tuyatengeneze maji yatoe kwa wingi viumbe vyenye uhai; na ndege, ili wapate kuruka juu ya dunia katika anga la wazi la mbingu.

21 Na Miungu wakayatengeneza maji ili yapate kutoa nyangumi wakubwa, na kila kiumbe chenye uhai kitembeacho, ambavyo maji yalijawa navyo kwa wingi kwa jinsi zao; na kila ndege arukaye kwa jinsi zao. Na Miungu wakaona ya kuwa vitawatii, na kwamba mpango wao ulikuwa mwema.

22 Na Miungu wakasema: Tutawabariki, na kuwafanya wazae na kuongezeka, na kuyajaza maji ya bahari au maji makuu; na kuwafanya ndege waongezeke katika nchi.

23 Na ikawa kwamba kutoka jioni hadi asubuhi hiyo wakaiita usiku; na ikawa kwamba kutoka asubuhi hadi jioni hiyo wakaiita mchana; na hiyo ilikuwa ni mara ya tano.

24 Na Miungu ikaitayarisha dunia ili itoe kiumbe chenye uhai kwa jinsi zake, mnyama wa kufugwa wa dunia navyo vitambaavyo, na wanyama wa mwitu kwa jinsi zake; na ikawa hivyo, kama wao walivyosema.

25 Na Miungu wakaitayarisha dunia ili itoe wanyama wa mwituni kwa jinsi zake, na mnyama wa kufugwa kwa jinsi zao; na kila kitu kitambaacho juu ya dunia kwa jinsi zao; na Miungu wakaona kuwa wangetii.

26 Na Miungu wakashauriana wenyewe na kusema: Na tushuke chini na tukamtengeneze mtu kwa mfano wetu, na kwa sura yetu; nasi tutawapa utawala juu ya samaki wa baharini, na juu ya ndege wa angani, na juu ya mnyama wa kufugwa, na juu ya dunia yote, na juu ya kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya ardhi.

27 Hivyo Miungu wakashuka chini ili kumuumba mtu kwa mfano wao, katika mfano wa Miungu wamfanye yeye, mme na mke wawafanye.

28 Na Miungu wakasema: Tutawabariki. Na Miungu wakasema: Tutawafanya wazaane na kuongezeka, na waijaze dunia, na kuitiisha, na kuwa na utawala juu ya samaki wa baharini, na juu ya ndege wa angani, na juu ya kila kitu chenye uhai kiendacho juu ya dunia.

29 Na Miungu wakasema: Tazama, tutawapa kila mche utoao mbegu utakao kuja juu ya uso wa dunia yote, na kila mti utakaotoa matunda juu yake; ndiyo, tunda la mti utoao mbegu kwao tutawapa, utakuwa kwa ajili ya chakula chao.

30 Na kwa kila mnyama wa mwituni wa dunia, na kwa kila ndege wa angani, na kwa kila kitu kitambaacho juu ya dunia, tazama, tutawapa uhai, na pia tutawapa kila mche wa kijani kwa ajili ya chakula, na mambo haya yote yatakuwa hivyo yalivyopangwa.

31 Na Miungu wakasema: Tutafanya kila kitu tulichokisema, na kuvitengeneza; na tazama, navyo vitakuwa vitiifu sana. Na ikawa kwamba kutoka jioni hadi asubuhi wakaita usiku; na ikawa kwamba kutoka asubuhi hadi jioni wakaita mchana; nao wakaihesabu kwa mara ya sita.