Maandiko Matakatifu
Musa 2


Mlango wa 2

(Juni–Oktoba 1830)

Mungu huumba mbingu na dunia—Aina zote za uhai zinaumbwa—Mungu anamuumba mwanadamu na kumpa utawala juu ya vingine vyote.

1 Na ikawa kwamba Bwana akamwambia Musa, akisema: Tazama, ninakufunulia wewe kuhusu mbingu hii, na dunia hii; andika maneno ninenayo. Mimi ni Mwanzo na Mwisho, Mungu Mwenyezi; kwa njia ya Mwanangu wa Pekee niliviumba vitu hivi; ndiyo, hapo mwanzo niliumba mbingu, na dunia ambayo juu yake wewe umesimama.

2 Na dunia ilikuwa bila mpangilio, na tupu; nami nikafanya giza kuja juu ya uso wa vilindi; na Roho yangu ikazunguka zunguka juu ya uso wa maji; kwa maana Mimi ni Mungu.

3 Na Mimi, Mungu, nikasema: Na uwepo mwanga; na mwanga ukawa.

4 Na Mimi, Mungu, nikauona mwanga; na mwanga ukawa mwema. Na mimi, Mungu, nikaugawa mwanga na giza.

5 Na Mimi, Mungu, nakauita mwanga Mchana; na giza, nikaliita Usiku; na hii nilifanya kwa njia ya neno la uwezo wangu, na ikafanyika kama nilivyosema; na jioni na asubuhi ikawa siku ya kwanza.

6 Na tena, Mimi, Mungu, nikasema: Na liwe anga katikati ya maji, na ikawa hivyo, hata kama nilivyosema; nami nikasema: Na likayatenge maji na maji; na ikawa hivyo.

7 Na Mimi, Mungu, nikalifanya anga na kuyagawanya maji, ndiyo, maji mengi chini ya anga na maji yale yaliyo juu ya anga, na ikawa hivyo hata kama nilivyosema.

8 Na Mimi, Mungu, nikaliita anga Mbingu; na jioni na asubuhi ikawa siku ya pili.

9 Na Mimi, Mungu, nikasema: Na maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, na ikawa hivyo; na Mimi, Mungu, nikasema: Na pawepo nchi kavu; na ikawa hivyo.

10 Na Mimi, Mungu, nikapaita pale pakavu Nchi; na makusanyiko ya maji, nikayaita Bahari; na Mimi, Mungu, nikaona kwamba vitu vyote nilivyofanya kuwa ni vyema.

11 Na Mimi, Mungu, nikasema: Nchi na itoe majani, mche utoao mbegu, na mti wa matunda uzaao matunda, kwa jinsi yake, na mti uzaao matunda, ambao mbegu yake iwe ndani yake, juu ya nchi, na ikawa hivyo hata kama nilivyosema.

12 Na nchi ikatoa majani, kila mche utoao mbegu kwa jinsi yake, na mti uzaao matunda, ambao mbegu zake zimo ndani yake, kwa jinsi yake; na Mimi, Mungu, nikaona kwamba vitu vyote nilivyovifanya vilikuwa vyema;

13 Na jioni na asubuhi ikawa siku ya tatu.

14 Na Mimi, Mungu, nikasema: Na iwe mianga katika anga la mbingu, ili itenge kati ya mchana na usiku, nayo iwe ndiyo dalili, na kwa majira, na kwa siku, na kwa miaka;

15 Na iwe ndiyo mianga katika anga la mbingu itie mwanga juu ya dunia; na ikawa hivyo.

16 Na Mimi, Mungu, nikaifanya mianga miwili mikuu; ule mwanga mkubwa zaidi utawale mchana, na ule mwanga mdogo zaidi utawale usiku, na ule mwanga mkubwa ulikuwa ndiyo jua, na ule mwanga mdogo ndiyo mwezi; na nyota nazo pia zilifanywa hata kulingana na neno langu.

17 Na Mimi, Mungu, nikaziweka katika anga la mbingu ili zitoe mwanga juu ya dunia.

18 Na jua litawale mchana, na mwezi utawale usiku, na kugawanya mwanga na giza; na Mimi, Mungu, nikaona kwamba vitu vyote nilivyofanya kuwa ni vyema;

19 Na jioni na asubuhi ikawa siku ya nne.

20 Na Mimi, Mungu, nikasema: Maji na yalete kwa wingi viumbe vitembeavyo ambavyo vina uhai, na ndege ambao wanaweza kuruka juu ya nchi katika anga lililo wazi la mbingu.

21 Na Mimi, Mungu, nikaumba nyangumi wakubwa, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho, ambacho maji yalikileta kwa wingi, kwa jinsi zao, na kila ndege mwenye mabawa kwa jinsi yake; na Mimi, Mungu, nikaona kwamba vitu vyote nilivyoviumba vilikuwa vyema.

22 Na Mimi, Mungu, nikavibariki, nikisema: Zaeni, na mkaongezeke, na mkayajaze maji ya baharini; ndege na waongezeke katika nchi;

23 Na jioni na asubuhi ikawa siku ya tano.

24 Na Mimi, Mungu, nikasema: Dunia na izae kiumbe hai kwa jinsi yake, wanyama wa kufugwa, na vitu vitambaavyo, nao wanyama wa mwituni wa dunia kwa jinsi zao, na ikawa hivyo;

25 Na Mimi, Mungu, nikafanya wanyama wa mwituni wa dunia kwa jinsi zao, na wanyama wa kufugwa kwa jinsi yao, na kila kitu kitambaacho juu ya dunia kwa jinsi yake; na Mimi, Mungu, nikaona kwamba vitu hivi vyote kuwa ni vyema.

26 Na Mimi, Mungu, nikamwambia Mwanangu wa Pekee, ambaye alikuwa nami tangu mwanzo: Na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; na ikawa hivyo. Na Mimi, Mungu, nikasema: Na watawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama wafugwao, na juu ya dunia yote, na kila kitu chenye kutambaa kitambaacho juu ya dunia.

27 Na Mimi, Mungu, nikamuumba mtu kwa mfano wangu mwenyewe, kwa mfano wa Mwanangu wa Pekee nikamwumba; mwanamume na mwanamke nikawaumba.

28 Na Mimi, Mungu, nikawabariki, na kuwaambia: Zaeni, na mkaongezeke, na mkaijaze dunia, na kuitiisha, na mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya dunia.

29 Na Mimi, Mungu, nikamwambia mwanadamu: Tazama, nimekupa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wa dunia yote, na kila mti ambao matunda yake yana mbegu; kwenu vitakuwa ndicho chakula chenu.

30 Na kwa kila mnyama wa mwitu, na kila ndege wa angani, na kwa kila kitambaacho juu ya dunia, ambacho nimekipa uhai, kutatolewa kila mche safi kwa chakula; na ikawa hivyo, hata kama nilivyosema.

31 Na Mimi, Mungu, nikaona vitu vyote nilivyovifanya, na tazama, vitu vyote nilivyovifanya vilikuwa vyema sana; na jioni na asubuhi ikawa siku ya sita.