2010–2019
Maneno ya Kutamatisha
Mkutano Mkuu wa Aprili 2019


Maneno ya Kutamatisha

Na acha tuweke wakfu na kuweka wakfu upya maisha yetu ili kumtumikia Mungu na watoto Wake—pande zote za pazia.

Kaka zangu na dada zangu wapendwa, tunapokaribia tamati ya mkutano huu wa kihistoria, tunamshukuru Bwana kwa uvuvio na ulinzi Wake. Jumbe zimetuelekeza na kutuinua.

Mada hazikutolewa kwa wazungumzaji. Kila mmoja aliomba kwa ajili ya ufunuo binafsi katika kutayarisha jumbe zao. Kwangu mimi, ni ya kusifika jinsi mada hizo zinavyoonekana kuendana vyema. Unapozisoma, tafuta kujifunza kile Bwana anachojaribu kukufunza wewe kupitia watumishi Wake.

Muziki umekuwa wa kupendeza. Tunatoa shukrani za dhati kwa wanamuziki ambao wameunganisha karama zao kuleta Roho wa Bwana kwenye kila kikao. Na Yeye amebariki sala na mkusanyiko katika kila kikao. Hakika, mkutano umekuwa tena karamu ya kiroho kwetu sote.

Tunatumaini na kuomba kwamba kila nyumba ya muumini itakuwa mahali patakatifu pa imani, ambapo Roho wa Bwana atakaa. Licha ya mabishano yanayotuzunguka, nyumba ya mtu inaweza kuwa mahali pa kimbingu, ambapo usomaji, sala, na imani vinaweza kuunganishwa na upendo. Tunaweza hakika kuwa wafuasi wa Bwana, tukisimama na kuzungumza kwa ajili Yake popote tulipo.

Lengo la Mungu linapaswa kuwa lengo letu. Yeye anataka watoto Wake kuchagua kurejea Kwake, wakiwa wamejitayarisha, wenye kustahili, wamepata endaumenti, wameunganishwa, na waaminifu kwenye maagano yaliyofanywa ndani ya mahekalu matakatifu.

Kwa sasa tunayo mahekalu 162 yaliyowekwa wakfu. Yale ya mwanzo kabisa yanasimama kama ukumbusho kwenye imani na ono la waanzilishi wetu wapendwa. Kila hekalu lililojengwa na wao lilikuwa matokeo ya dhabihu kuu na juhudi binafsi. Kila moja linasimama kama kito cha kupendeza katika taji la mafanikio la waanzilishi.

Letu sisi ni jukumu takatifu la kuyatunza. Kwa hivyo, mahekalu haya ya waanzilishi punde yatapitia kipindi cha matengenezo na kufanywa upya na, kwa baadhi, urejesho mkubwa. Juhudi zitafanyika kuhifadhi uhalisia wa kipekee wa kila hekalu kadiri iwezekanavyo, kuhifadhi uzuri wa kuvutia na ufundistadi wa kipekee wa vizazi vilivyopita kitambo sana.

Taarifa za Hekalu la St. George Utah tayari zimekwisha tolewa. Mipango ya ukarabati wa Hekalu la Salt Lake, Temple Square, na uwanda unaopakana karibu na Jengo la Ofisi ya Kanisa itatangazwa mnamo Ijumaa, Aprili 19, 2019.

Mahekalu ya Manti na Logan pia yatakarabatiwa katika miaka ijayo. Mipango hiyo itakapokuwa imeandaliwa, nayo pia itatangazwa.

Kazi hii itahitaji kwamba kila hekalu lifungwe kwa kipindi cha muda. Waumini wa Kanisa wanaweza kuendelea kufurahia ibada na shughuli za hekaluni kwenye mahekalu mengine ya karibu. Pale kila mradi utakapokamilika, kila hekalu la kihistoria litawekwa wakfu upya.

Akina kaka na akina dada, tunachukulia hekalu kama jengo takatifu zaidi katika Kanisa. Wakati tunapotangaza mipango ya kujenga hekalu jipya linakuwa sehemu ya historia yetu takatifu. Sasa, tafadhali sikilizeni kwa makini na kwa unyenyekevu. Ikiwa ninatangaza hekalu katika eneo ambalo ni maalumu kwako, naomba nipendekeze kwamba uinamishe tu kichwa chako kwa sala ya kimya kimya ya shukrani katika moyo wako. Hatutataka mlipuko wa maneno kupunguza thamani kwenye asili takatifu ya mkutano huu na mahekalu matakatifu ya Bwana.

Leo tunafurahia kutangaza mipango ya kujenga mahekalu zaidi, yatakayojengwa katika maeneo yafuatayo:

Pago Pago, American Samoa; Okinawa City, Okinawa; Neiafu, Tonga; Tooele Valley, Utah; Moses Lake, Washington; San Pedro Sula, Honduras; Antofagasta, Chile; Budapest, Hungary.

Asanteni, kaka zangu na dada zangu wapendwa.

Tunapozungumzia mahekalu yetu ya zamani na mapya, acha kila mmoja wetu aonyeshe kwa matendo yetu kwamba sisi ni wafuasi wa Bwana Yesu Kristo. Acha turekebishe maisha yetu kupitia imani yetu na uaminifu wetu Kwake. Acha tufikie nguvu ya Upatanisho Wake kwa toba yetu kila siku. Na acha tuweke wakfu na kuweka wakfu upya maisha yetu ili kumtumikia Mungu na watoto Wake—pande zote za pazia.

Ninawaachieni upendo na baraka zangu juu yenu, nikiwahakikishia kwamba ufunuo unaendelea hapa, katika Kanisa la Bwana. Utaendelea mpaka “malengo ya Mungu yatakapotimizwa, na Yehova Mkuu atasema kazi imekamilika.”1

Ninawabariki hivyo na kutoa ushuhuda wangu kwamba Mungu yu hai! Yesu ndiye Kristo! Hili ni Kanisa Lake. Sisi ni watu Wake. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Mafundisho ya Marais wa Kanisa: Joseph Smith (2007), 142.