Mkutano Mkuu
Songa Mbele kwa Imani
Mkutano mkuu wa Aprili 2020


Songa Mbele kwa Imani

Ninawabariki kwa amani na ongezeko la imani katika Bwana.

Kaka zangu na dada zangu wapendwa, tunapokaribia tamati ya mkutano huu wa kihistoria, tunatoa shukrani zetu kwa Bwana. Muziki umekuwa mzuri, na jumbe ni za kuinua.

Wakati wa mkutano huu, tumepata maelekezo mengi. Katika maadhimisho haya ya miaka mia mbili, tumetambulisha tangazo kwa ulimwengu likitangaza uhalisia wa Urejesho wa injili ya Yesu Kristo katika utimilifu wake.

Tumefanya kumbukizi ya Urejesho kwa Shangwe za Hosana.

Tumefunua alama mpya inayoashiria imani yetu katika Bwana Yesu Kristo na kwa utambuzi wa kuonekana wa taarifa maalumu na nyaraka za Kanisa.

Tumeweka siku ya ulimwegu wote kufunga na kuomba, kwamba gonjwa ambukizi la sasa liweze kutulizwa, watoa huduma kulindwa, uchumi kuimarishwa, na maisha kurejea kawaida. Mfungo huu utafanyika katika Ijumaa Kuu, Aprili 10. Na hiyo itakuwa Ijumaa ya kupendeza sana!

Jumapili ijayo ni Jumapili ya Pasaka, ambapo tutafanya tena kumbukizi ya Upatanisho na Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa sababu ya Upatanisho wake, Zawadi yake ya ufufuko itakuja kwa wote waliopata kuishi. Na zawadi yake ya uzima wa milele itakuja kwa wote wanaokidhi kwa uaminifu kwenye ibada na maagano yaliyofanywa katika mahekalu Yake matakatifu.

Maneno mengi ya kuinua ya huu mkutano mkuu wa Aprili 2020—na wiki takatifu ambayo sasa tunaianza—vinaweza kufupishwa kwa maneno mawili yenye utukufu yaliyotangazwa: “Msikilize Yeye.”1 Tunaomba kwamba fokasi yenu kwa Baba wa Mbinguni, aliyeongea maneno hayo, na kwa Mwanaye Mpendwa, Yesu Kristo, vitazidi kuongezeka katika kumbukumbu zenu kwa yale yote yaliyotukia. Tunaomba kwamba mtaanza upya kwa dhati kusikia, kusikiliza, na kufuata maneno ya Mwokozi.2 Ninaahidi kwamba upungufu wa woga na ongezeko la imani vitafuatia.

Asanteni kwa hamu yenu ya kufanya nyumba zenu kuwa sehemu takatifu za kweli za imani, ambapo Roho wa Bwana anaweza kukaa. Mtaala wetu wa kujifunza injili, Njoo, Unifuate, utaendelea kubariki maisha yenu. Juhudi zako zisizokoma katika swala hili—hata katika nyakati hizo ambapo unaweza kuhisi kwamba haufanikiwi—zitabadili maisha yako, yale ya familia yako, na ya ulimwengu. Tutaimarishwa tunapoendelea kuwa wafuasi hodari wa Bwana, tukisimama na kuongea kwa niaba Yake, popote tulipo.

Sasa, tuzungumzie kuhusu mahekalu. Tuna mahekalu 168 yaliyowekwa wakfu duniani kote. Mengine yapo katika hatua mbalimbali za mipango na ujenzi. Wakati mipango inapotangazwa kwa ajili ya ujenzi wa hekalu jipya, linakuwa sehemu ya historia yetu tukufu.

Inaweza kuonekana mzaha kutangaza mahekalu mapya wakati mahekalu yetu yote yamefungwa kwa muda.

Zaidi ya karne iliyopita, Rais Wilford Woodruff aliona hali kama za kwetu leo, kama ilivyorekodiwa katika sala yake ya uwekaji wakfu wa Hekalu la Salt Lake, iliyotolewa mnamo 1893. Baadhi yenu hivi karibuni mnaweza kuwa mmeona dondoo kutoka katika sala hii isiyo ya kifani katika mitandao ya kijamii.

Sikiliza maombi haya kutoka kwa nabii mkuu wa Mungu: “Wakati watu Wako watakapokuwa hawana fursa ya kuingia katika nyumba hii takatifu … na wanakandamizwa na wako matatizoni, wakizungukwa na magumu … na watakapogeuza nyuso zao kuelekea nyumba Yako hii takatifu na Kukuomba kwa ajili ya ukombozi, kwa msaada, kwa nguvu Zako kuonekana kwa niaba yao, tunakuomba, kuangalia chini kutoka katika makazi Yako matukufu kwa rehema … na kusikiliza vilio vyao. Au wakati watoto wa watu Wako, katika miaka ijayo, watatengwa, kwa sababu yoyote, mbali na sehemu hii, … na watakapokulilia kutoka katika vilindi vya mateso yao na huzuni ili kupata msaada na ukombozi wao, kwa unyenyekevu tunakuomba … usikilize vilio vyao, na uwapatie baraka wanazoziomba.”3

Akina kaka na akina dada, katika vipindi vyetu vya dhiki wakati mahekalu yatakuwa yamefungwa, bado mnaweza kuita nguvu za maagano yenu ya hekaluni na endaumenti pale mnapotii maagano yenu. Tafadhali tumia muda huu wakati mahekalu yamefungwa kuendelea kuishi maisha ya kustahili hekaluni, au kuwa mwenye kustahili kwa ajili ya hekalu.

Zungumza kuhusu hekalu pamoja na familia yako na marafiki. Kwa sababu Yesu Kristo ni kiini cha kila kitu tunachokifanya hekaluni, unapofikiria zaidi kuhusu hekalu utazidi kufikiria zaidi kumhusu Yeye. Jifunze na omba kujua zaidi kuhusu nguvu na maarifa ambayo umetunukiwa—au ambayo utatunukiwa.

Leo tunafurahia kutangaza mipango ya kujenga mahekalu mapya manane katika maeneo yafuatayo: Bahía Blanca, Argentina; Tallahassee, Florida; Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; Pittsburgh, Pennsylvania; Benin City, Nigeria; Syracuse, Utah; Dubai, United Arab Emirates; na Shanghai, Jamhuri ya Watu wa China.

Katika maeneo yote manane, wasanifu majengo wa Kanisa watafanya kazi pamoja na viongozi wa serikali wa maeneo husika ili kwamba hekalu liweze kuendana na, na kuwa nyongeza ya kupendeza kwa kila jamii.

Mpango wa hekalu huko Dubai unakuja kutokana na mwitikio wa mwaliko wao mzuri, ambao tunautambua kwa shukrani.

Muktadha kwa ajili ya mpango wa Shanghai ni muhimu sana. Kwa zaidi ya miongo miwili, waumini wanaostahili kwenda hekaluni katika Jamhuri ya Watu wa China wamekuwa wakihudhuria Hekalu la Hong Kong China. Lakini mnamo Julai 2019, hekalu hilo lilifungwa kwa ajili ya marekebisho yaliyopangwa kitambo na yaliyohitajika kwa kiasi kikubwa.

Huko Shanghai, mahali penye staha na panapokidhi mahitaji mbalimbali patatoa njia kwa waumini wa China kuendelea kushiriki katika ibada za hekalu—katika Jamhuri ya Watu wa China—kwa ajili yao na kwa ajili ya mababu zao.4

Katika kila nchi, Kanisa hili linawafunza waumini wake kuheshimu, kutii, na kuunga mkono sheria.5 Tunafundisha umuhimu wa familia, wa kuwa wazazi wema na raia wa mifano ya kuigwa. Kwa sababu tunaheshimu sheria na taratibu za Jamhuri ya Watu wa China, Kanisa halipeleki wamisionari wanaohubiri huko; wala hatutafanya hivyo sasa.

Mikusanyiko ya wahamiaji na Wachina itaendelea kufanywa tofauti. Hadhi rasmi ya Kanisa huko itabaki bila kubadilishwa. Katika hatua ya mwanzo ya matumizi ya nyenzo, kuingia kutakuwa kwa ahadi ya kuonana tu. Nyumba ya Bwana kule Shanghai haitakuwa mahali kwa ajili ya watalii kutoka nchi zingine.

Mahekalu haya mapya manane yatabariki maisha ya watu wengi katika pande zote za pazia la kifo. Mahekalu ni sehemu ya kilele ya Urejesho wa utimilifu wa injili ya Yesu Kristo. Katika wema na ukarimu wa Mungu, anasogeza baraka za hekalu karibu na watoto Wake kila mahali.

Kadiri Urejesho unavyoendelea, ninajua kwamba Mungu ataendelea kufunua vitu vingi vikubwa na vya muhimu kuhusu ufalme Wake hapa duniani.6 Ufalme huo ni Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Wapendwa akina kaka na akina dada, ninaelezea upendo wangu kwenu. Katika kipindi hiki cha wasiwasi na mashaka, na kwa mamlaka ya kusihi niliyonayo, ningependa kuwapatia baraka ya kitume.

Ninawabariki kwa amani na ongezeko la imani katika Bwana.7

Ninawabariki kwa hamu ya kutubu na kuwa zaidi kama Yeye kila siku ipitayo.8

Ninawabariki kujua kwamba Nabii Joseph Smith ni nabii wa Urejesho wa injili ya Yesu Kristo katika utimilifu wake.

Kama kuna ugonjwa miongoni mwenu au kwa wale mnaowapenda, ninawaachia baraka ya uponyaji, kulingana na mapenzi ya Bwana.

Ninawabariki hivyo, nikiongezea tena hisia zangu za upendo kwa kila mmoja wenu, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.