Mkutano Mkuu
Tenga Muda kwa ajili ya Bwana
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2021


Tenga Muda kwa ajili ya Bwana

Ninawasihi leo kupambana na mitego na majaribu ya ulimwengu kwa kutenga muda kwa ajili ya Bwana katika maisha yako—kila siku ipitayo.

Kaka zangu na dada zangu wapendwa, kwa siku mbili tumefunzwa vyema na watumishi wa Bwana ambao wametafuta kwa bidii kujua kile ambacho Bwana angewataka waseme.

Tumepewa agizo letu la miezi sita ijayo. Sasa swali ni, ni jinsi gani tutakuwa tofauti kwa sababu ya kile tulichosikia na kuhisi?

Janga la ulimwengu limeonesha jinsi kwa haraka maisha yanavyoweza kubadilika, nyakati zingine kutoka kwenye hali zilizo nje ya uwezo wetu kudhibiti. Hata hivyo, kuna mambo mengi tunayoweza kudhibiti. Tunaweka vipaumbele vyetu na kuamua jinsi tunavyotumia nguvu, muda na nyenzo. Tunaamua jinsi tutakavyotendeana kila mmoja. Tunawachagua wale ambao kwao tutawageukia kwa ajili ya ukweli na mwongozo.

Sauti na mashinikizo ya ulimwengu ni ya kuvutia na ni mengi. Lakini sauti nyingi sana ni za uongo, zenye kuhadaa na zinaweza kutuvuta kutoka kwenye njia ya agano. Ili kuepuka kuvunjika moyo kusikoepukika kunakofuatia, ninawasihi leo kupambana na mitego na majaribu ya ulimwengu kwa kutenga muda kwa ajili ya Bwana katika maisha yenu—kila siku ipitayo.

Ikiwa wingi wa taarifa unazopata zinatoka kwenye mitandao ya kijamii au mingine, uwezo wako wa kusikia minong’ono ya Roho utapungua. Ikiwa pia humtafuti Bwana kupitia sala na usomaji wa injili kila siku, unajiacha kuwa muhanga wa filosofia ambazo zinaweza kuwa za kuvutia lakini si za kweli. Hata Watakatifu ambao pengine waaminifu wanaweza kuvutiwa na mdundo wa mara kwa mara wa bendi ya Babeli.

Kaka zangu na dada zangu, ninawasihi mtenge muda kwa ajili ya Bwana! Fanya msingi wako mwenyewe wa kiroho kuwa imara na unaoweza kuhimili majaribu ya kila wakati kwa kufanya mambo yale ambayo yanamruhusu Roho Mtakatifu kuwa pamoja nawe daima.

Kamwe usipuuze ukweli mkuu kwamba “Roho huzungumza … kuhusu vile vitu kama vilivyo na vile vitu kama vitavyo kuwa.”1 “Atawaonyesha vitu vyote ambavyo mnastahili kutenda.”2

Hakuna kinachomwalika Roho zaidi ya kukita fokasi yako juu ya Yesu Kristo. Zungumzeni kuhusu Kristo, furahieni katika Kristo, kuleni na kusherehekea maneno ya Kristo na msonge mbele mkiwa na uimara katika Kristo.3 Ifanyeni Sabato yenu kuwa ya furaha pale mnapomwabudu Yeye, kupokea sakramenti na kuifanya siku Yake kuwa takatifu.4

Kama nilivyosisitiza asubuhi ya leo, tafadhali tengeni muda kwa ajili ya Bwana katika nyumba Yake takatifu. Hakuna kitakachoimarisha msingi wako wa kiroho kama huduma ya hekaluni na kuabudu hekaluni.

Tunawashukuru wote ambao wanafanyia kazi mahekalu yetu mapya. Yanajengwa kote ulimwenguni. Leo ninayo furaha kutangaza mipango yetu ya kujenga mahekalu zaidi kwenye maeneo au karibu na maeneo yafuatayo: Kaohsiung, Taiwan; Tacloban, Philippines; Monrovia, Liberia; Kananga, Democratic Republic of the Congo; Antananarivo, Madagascar; Culiacán, Mexico; Vitória, Brazil; La Paz, Bolivia; Santiago West, Chile; Fort Worth, Texas; Cody, Wyoming; Rexburg North, Idaho; Heber Valley, Utah; na kujengwa upya kwa Hekalu la Provo, Utah baada ya kuweka wakfu Hekalu la Orem Utah.

Ninawapenda, wapendwa akina kaka na akina dada. Bwana anawajua na anawapenda. Yeye ni Mwokozi wenu na Mkombozi wenu. Anaelekeza na kuliongoza Kanisa Lake. Atakuelekeza na kukuongoza wewe katika maisha yako binafsi ikiwa utatenga muda kwa ajili Yake katika maisha yako—kila siku ipitayo.

Mungu awe nanyi mpaka tutakapokutana tena, ninaomba katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.