Maandiko Matakatifu
3 Nefi 24


Mlango wa 24

Mjumbe wa Bwana atatayarisha njia kwa Ujio wa Pili—Kristo ataketi kwenye hukumu—Israeli inaamrishwa kulipa zaka na matoleo—Kitabu cha ukumbusho kinahifadhiwa—Linganisha Malaki 3. Karibia mwaka 34 B.K.

1 Na ikawa kwamba aliwaamuru kwamba waandike maneno ambayo Baba alimkabidhi Malaki, ambayo angewaambia. Na ikawa kwamba baada ya kuandikwa, aliyaeleza. Na haya ndiyo maneno aliyowaambia akisema: Baba alimwambia Malaki hivi—Tazama, nitamtuma mjumbe wangu, na atatayarisha njia kabla yangu, na Bwana mnayemgojea atakuja kwa ghafla kwenye hekalu lake, hata yule mjumbe wa agano ambaye mnafurahia ndani; tazama atakuja, asema Bwana wa Majeshi.

2 Lakini ni nani atakayestahili siku ya kuja kwake, na ni nani atakayesimama atakapotokea? Kwani yeye yuko kama moto usafishao fedha, na kama sabuni ya dobi.

3 Na ataketi kama asafishaye fedha na kuitakasa, na atawatakasa wana wa Lawi, atawasafisha kama dhahabu na fedha, ili dhabihu kwa Bwana liwe toleo kwa haki.

4 Ndipo dhabihu ya Yuda na Yerusalemu zitapendeza mbele ya Bwana, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani.

5 Na nitawakaribia kwa hukumu; na nitakuwa shahidi mwepesi dhidi ya wachawi, na dhidi ya wazinzi, na dhidi ya waapao uwongo, na dhidi ya wale wamwoneao mwenye kuajiriwa kwa ajili ya mshahara wake, mjane na yatima, na wale wanaompoteza mgeni, na hawaniogopi, asema Bwana wa Majeshi.

6 Kwa kuwa mimi ni Bwana, sibadiliki; kwa hivyo enyi wana wa Yakobo hamwangamizwi.

7 Hata kutoka siku za babu zenu, mmegeuka upande kutoka kwa maagizo yangu, na hamjayashika. Nirudieni na nitarudi kwenu, asema Bwana wa Majeshi. Lakini ninyi mwasema: Tutarudi kwa namna gani?

8 Je, mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini mmeniibia. Lakini mnasema: Tumekuibia kwa namna gani? Katika zaka na madhabihu.

9 Mmelaaniwa na laana, kwani mmeniibia, hata hili taifa lote.

10 Leteni zaka kamili ghalani, ili kuweko chakula katika nyumba yangu; na mnijaribu sasa hivi, asema Bwana wa Majeshi, kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagia baraka, kwamba kusiwe na nafasi ya kutosha ya kuipokea.

11 Na nitamkemea mlaji kwa ajili yenu, na hataharibu matunda ya ardhi yenu; wala mizabibu wenu hautapukutisha matunda yake katika ardhi kabla ya wakati wake huko shambani, asema Bwana wa Majeshi.

12 Na mataifa yote yatawaita wenye heri, kwani mtakuwa nchi ya kupendeza, asema Bwana wa Majeshi.

13 Maneno yenu yamekuwa magumu juu yangu, asema Bwana. Lakini mnasema: Tumesema nini dhidi yako?

14 Mmesema ni bure kumtumikia Mungu, na tumepata faida gani kwa kuzishika ibada zake, na kwamba tumetembea kwa huzuni mbele ya Bwana wa Majeshi.

15 Na sasa tunawaita wenye kiburi ndiyo walio heri; ndiyo, wale wanaotenda maovu na kunufaika; ndiyo, wanaomjaribu Mungu ndiyo wanaookolewa.

16 Ndipo wale wanaomcha Bwana, walisemezana wao kwa wao, na Bwana akasikiliza na kusikia; na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele yake kwa wao wanaomcha Bwana, na kulitafakari jina lake.

17 Na watakuwa wangu, asema Bwana wa Majeshi, katika siku ile nitakapofanya vito vyangu; na nitawaachilia vile mtu huachilia mwana wake amtumikiaye.

18 Ndipo mtakaporudi, na kupambanua miongoni mwa wenye haki na waovu, na miongoni mwa yule amtumikiaye Mungu na yule asiyemtumikia.