Maandiko Matakatifu
3 Nefi 25


Mlango wa 25

Katika Ujio wa Pili, wenye kiburi na waovu watateketezwa kama makapi—Eliya atarejea kabla ya ile siku kubwa na ya kutisha—Linganisha Malaki 4. Karibia mwaka 34 B.K.

1 Kwani tazama, ile siku inakuja ambayo itawaka kama tanuru; na wote wenye kiburi, ndiyo, na wote wanaotenda maovu, watakuwa makapi; na ile siku inayokuja itawateketeza, asema Bwana wa Majeshi, kwamba haitawaachia shina wala tawi.

2 Lakini kwenu mnaolicha jina langu, yule Mwana wa Haki atawashukia na uponyaji katika mabawa yake; na ninyi mtaenda mbele na kukua kama ndama zizini.

3 Na mtakanyaga waovu; kwani watakuwa majivu chini ya nyayo za miguu yenu katika siku nitakayofanya hivi, asema Bwana wa Majeshi.

4 Kumbukeni ninyi sheria ya Musa, mtumishi wangu, niliyemwamuru huko Horebu kwa ajili ya Waisraeli wote, na amri za hukumu.

5 Tazama, nitawatumia Eliya nabii kabla ya kuja kwa ile siku kubwa na ya kutisha ya Bwana.

6 Na atageuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, nisije na kupiga dunia na laana.