Maandiko Matakatifu
Etheri 3


Mlango wa 3

Kaka wa Yaredi anaona kidole cha Bwana Anapogusa mawe kumi na sita—Kristo anaonyesha mwili Wake wa kiroho kwa kaka wa Yaredi—Wale ambao wana elimu kamili hawawezi kuwekwa nyuma ya pazia—Zana za kufasiri zinatolewa kufanya kumbukumbu ya Wayaredi kujulikana.

1 Na ikawa kwamba kaka wa Yaredi, (sasa idadi ya boti ambazo zilikuwa zimetayarishwa zilikuwa nane) alienda mbele kwenye mlima, ambao waliuita mlima Shelemu, kwa sababu ya urefu wake mwingi, na akachonga mawe madogo kumi na sita kutoka kwenye mwamba; na yalikuwa meupe na safi, hata kama kioo kilicho wazi; na aliyabeba katika mikono yake hadi juu ya kilele cha mlima, na akaomba tena kwa Bwana, akisema:

2 Ee Bwana, umesema kwamba lazima tuzungukwe na mafuriko. Sasa tazama, Ee Bwana, na usiwe na hasira na mtumishi wako kwa sababu ya udhaifu wake mbele yako; kwani tunajua kwamba wewe ni mtakatifu na unaishi mbinguni, na sisi hatufai mbele yako; kwa sababu ya mwanguko maumbile yetu yamekuwa maovu siku zote; walakini, Ee Bwana, umetupatia amri kwamba tukulingane, kwamba kutoka kwako tungepokea mahitaji yetu.

3 Tazama, Ee Bwana, umetuadhibu kwa sababu ya uovu wetu, na umetusukuma mbele, na katika hii miaka mingi tumekuwa katika nyika; walakini, umekuwa mwenye huruma kwetu. Ee Bwana, nitazame na huruma, na ugeuze hasira yako kutoka kwa watu hawa, na usikubali kwamba wavuke hii bahari katika giza; lakini tazama vitu hivi ambavyo nimechonga kutoka katika mwamba.

4 Na ninajua, Ee Bwana, kwamba una uwezo wote, na unaweza kufanya chochote upendacho kwa faida ya binadamu; kwa hivyo gusa mawe haya, Ee Bwana, na kidole chako, na uyatayarishe kwamba yaangaze kwenye giza; na yatangʼaa kwetu ndani ya boti ambazo tumezitayarisha, ili tuweze kuwa na mwangaza tutakapovuka bahari.

5 Tazama, Ee Bwana, unaweza kufanya hivi. Tunajua kwamba unaweza kuonyesha mbele uwezo wako mkuu, ambao unaonekana mdogo katika macho ya watu.

6 Na ikawa kwamba baada ya kaka wa Yaredi kusema maneno haya, tazama, Bwana alinyoosha mbele mkono wake na kugusa yale mawe moja moja kwa kidole chake. Na pazia lilitolewa machoni mwa kaka wa Yaredi, na akaona kidole cha Bwana; na kilikuwa kama kidole cha mtu, sawa kama mwili na damu; na kaka wa Yaredi alianguka chini mbele ya Bwana, kwani alikumbwa na woga.

7 Na Bwana aliona kwamba kaka wa Yaredi alikuwa ameanguka chini; na Bwana akasema kwake: Amka, kwa nini umeanguka?

8 Na akamwambia Bwana: Niliona kidole cha Bwana, na nikaogopa asije akanipiga; kwani sikujua kama Bwana anao mwili na damu.

9 Na Bwana akamwambia: Kwa sababu ya imani yako umeona kwamba nitachukua juu yangu mwili na damu; na hakujakuwa na mtu aliyekuja kwangu mbeleni na imani kubwa vile umefanya; kwani kama hungekuwa hivyo hungeona kidole changu. Je, uliona zaidi ya hii?

10 Na akajibu: Hapana; Bwana, jidhihirishe kwangu.

11 Na Bwana akamwambia: utaamini maneno ambayo nitasema?

12 Na akajibu: Ndiyo, Bwana, najua kwamba wewe husema ukweli, kwani wewe u Mungu wa ukweli, na huwezi kudanganya.

13 Na baada ya kusema maneno haya, tazama, Bwana alijionyesha kwake, na kusema: Kwa sababu unajua vitu hivi umekombolewa kutoka kwenye mwanguko; kwa hivyo umerudishwa kwenye uwepo wangu; kwa hivyo ninajionyesha kwako.

14 Tazama, ni mimi yule aliyetayarishwa kutoka mwanzo wa dunia kuokoa watu wangu. Tazama, mimi ni Yesu Kristo. Mimi ni Baba na Mwana. Ndani yangu binadamu wote watapata maisha, na kwamba milele, hata wale watakaoamini kwa jina langu; na watakuwa wana wangu na mabinti zangu.

15 Na kamwe sijajionyesha kwa binadamu ambaye nilimuumba, kwani binadamu hajaamini kwangu vile umefanya. Je, unaona kwamba uliumbwa kwa mfano wangu? Ndiyo, hata watu wote waliumbwa katika mwanzo kwa jinsi ya kama maumbile yangu.

16 Tazama, huu mwili, ambao unauona sasa, ni mwili wa roho yangu; na nimemuumba mtu jinsi ya mwili wangu wa roho; na hata ninavyoonekana kwako kuwa katika roho ndivyo nitakavyoonekana kwa watu wangu katika mwili.

17 Na sasa, kwa vile mimi, Moroni, nilisema siwezi kuandika historia kamili ya vitu hivi ambavyo vimeandikwa, kwa hivyo, ninatosheka kusema kwamba Yesu alijionyesha kwa mtu huyu katika roho, hata jinsi alivyojionyesha kwa Wanefi.

18 Na alimhudumia kama alivyowahudumia Wanefi; na alifanya haya yote, ili huyu mtu ajue kwamba alikuwa Mungu, kwa sababu ya matendo mengi makubwa ambayo Bwana alikuwa amemwonyesha.

19 Na kwa sababu ya ufahamu wa huyu mtu hangeweza kuzuiwa kuona ndani ya pazia; na aliona kidole cha Yesu, ambacho, baada ya kukiona, alianguka kwa woga; kwani alijua kwamba kilikuwa kidole cha Bwana; na hakuwa na imani tena, kwani alijua, bila tashwishi.

20 Kwa hivyo, akiwa na hii elimu kamilifu ya Mungu, hangeweza kuwekwa kwenye pazia; kwa hivyo alimwona Yesu; na akamhudumia.

21 Na ikawa kwamba Bwana alimwambia kaka wa Yaredi: Tazama, hutaruhusu lolote la vitu hivi ambavyo umeona na kusikia kufunuliwa kwa ulimwengu, mpaka wakati utakapotimia nitakapolitukuza jina langu katika mwili; kwa hivyo, utaweka vitu hivi ambavyo umeviona na kusikia kwako, na usimwonyeshe mtu yeyote.

22 Na tazama, utakapokuja kwangu, utaviandika na kufunga, ili mtu yeyote asiweze kuvitafsiri; kwani utaviandika kwa lugha ambayo haiwezi kusomeka.

23 Na tazama, mawe haya mawili nitakukabidhi, nawe utayafunga pia pamoja na vitu utakavyoandika.

24 Kwani tazama, lugha ambayo utaandika nimeichanganya; kwa hivyo nitasababisha kwa wakati wangu unaonifaa kwamba mawe haya yatakuza macho ni pa binadamu vitu hivi ambavyo utaandika.

25 Na baada ya Bwana kusema maneno haya, alimwonyesha kaka wa Yaredi wakazi wote wa dunia ambao walikuwepo, na pia wote watakaokuwepo; na hakuwaficha kutoka kwenye uwezo wake wa kuona, hata hadi kwenye mwisho wa dunia.

26 Kwani alikuwa amemwambia mbeleni, ikiwa atamwamini kwamba angemwonyesha vitu vyote—kwamba ataonyeshwa; kwa hivyo Bwana hakuweza kumzuia lolote, kwani alijua kwamba Bwana angemwonyesha vitu vyote.

27 Na Bwana akamwambia: Andika vitu hivi na uvitie muhuri; na nitavidhihirisha kwa watoto wa watu katika muda wangu unaonifaa.

28 Na ikawa kwamba Bwana alimwamuru kwamba kuyafungia yale mawe mawili ambayo alikuwa amepokea, na asiyaonyeshe kwa yeyote, mpaka Bwana atakapoyadhihirisha kwa watoto wa watu.