Maandiko Matakatifu
Yakobo (KM) 7


Mlango wa 7

Sheremu anamkana Kristo, anabishana na Yakobo, anadai ishara, na anapigwa na Mungu—Manabii wote wamezungumza kuhusu Kristo na Upatanisho Wake—Wanefi waliishi maisha yao kama wahamaji, wakizaliwa matesoni na kuchukiwa na Walamani. Karibia mwaka 544–421 K.K.

1 Na sasa ikawa kwamba baada ya miaka kadhaa kupita, palitokea mtu miongoni mwa watu wa Nefi, aliyeitwa Sheremu.

2 Na ikawa kwamba alianza kuhubiri miongoni mwa wale watu, na kuwatangazia kwamba hakutakuwa na Kristo. Na akahubiri vitu vingi ambavyo vilikuwa vya kupendeza kwa watu; na alifanya hivi ili apindue mafundisho ya Kristo.

3 Na akatumika kwa bidii ili apotoshe mioyo ya watu, hadi akapotosha mioyo mingi; na yeye akijua kwamba mimi, Yakobo, nilikuwa na imani kwa Kristo atakayekuja, alitafuta nafasi ili anijie.

4 Na alikuwa ameelimika, hata kwamba alifahamu kikamilifu lugha ya wale watu; kwa hivyo, angerairai, na alikuwa na uwezo wa kuzungumza sana, kulingana na nguvu ya ibilisi.

5 Na alikuwa anatumaini kwamba ataniondoa kutoka imani, ingawa nilikuwa na ufunuo mwingi na vitu vingi ambavyo nilikuwa nimeona kuhusu vitu hivi; kwani kwa kweli nilikuwa nimewaona malaika, na walikuwa wamenihudumia. Na pia, nilikuwa nimesikia sauti ya Bwana ikinizungumzia kwa maneno dhahiri, mara kwa mara; kwa hivyo, singetetemeshwa.

6 Na ikawa kwamba alinijia, na akanizungumzia hivi, akisema: Kaka Yakobo, nimetafuta nafasi ili nikuzungumzie; kwani nimesikia na pia ninajua kwamba wewe unasafiri sana, ukihubiri ile ambayo unaiita injili, au mafundisho ya Kristo.

7 Na umepotosha watu hawa wengi kwamba wamegeuza njia ile sawa ya Mungu, na hawatii amri ya Musa ambayo ndiyo njia sawa; na kubadili sheria ya Musa kuwa ibada ya mtu ambaye unasema kwamba atakuja baada ya miaka mia na mia. Na sasa tazama, mimi, Sheremu, nakutangazia wewe kwamba huu ni ukufuru; kwani hakuna mtu anayejua vitu hivi; kwani hawezi kuzungumza kuhusu vitu vile vitakavyokuwepo. Na Sheremu alibishana na mimi katika njia hii.

8 Lakini tazama, Bwana Mungu alinishushia Roho wake katika nafsi yangu, hadi nikamfadhaisha katika maneno yake yote.

9 Na nikamwambia: Je, wewe unamkana Kristo ambaye atakuja? Na akasema: kama Kristo atakuwepo, singemkana; lakini najua kwamba hakuna Kristo, wala hajakuwepo, wala hatakuwepo.

10 Na nikamwambia: Je, wewe unaamini maandiko? Na akasema, Ndiyo.

11 Na nikamwambia: Basi hauyafahamu; kwani yanashuhudia Kristo kwa kweli. Tazama, nakuambia kwamba hakuna manabii walioandika, wala kutoa unabii, bila kuzungumza kuhusu huyu Kristo.

12 Na haya sio yote—imedhihirishwa kwangu mimi, kwani nimesikia na kuona; na pia imedhihirishwa kwangu kwa nguvu za Roho Mtakatifu; kwa hivyo, najua kama hakuna upatanisho wanadamu wote watapotea.

13 Na ikawa kwamba aliniambia: Nionyeshe ishara kwa nguvu hizi za Roho Mtakatifu ambazo zinakuwezesha kujua haya mengi.

14 Na nikamwambia: Mimi ni nani ili nimjaribu Mungu akuonyeshe ishara kwa kitu unachokijua kwamba ni kweli? Lakini bado wewe unalikana, kwa sababu wewe ni wa ibilisi. Walakini, nia yangu isitendeke; lakini kama Mungu atakupiga, hebu hiyo na iwe ishara kwako kwamba ana nguvu, mbinguni na duniani; na pia, kwamba Kristo atakuja. Na nia yako, Ewe Bwana, itendeke, sio yangu.

15 Na ikawa kwamba wakati mimi, Yakobo, nilizungumza maneno haya, nguvu za Bwana zikamshukia, hadi akainama kwenye ardhi. Na ikawa kwamba alilishwa kwa muda wa siku nyingi.

16 Na ikawa kwamba aliwaambia watu: Kusanyikeni pamoja hapo kesho, kwani nitafariki; kwa hivyo, natamani kuzungumza na watu kabla sijafariki.

17 Na ikawa kwamba umati ulikusanyika pamoja kesho yake; na akazungumza kwao wazi wazi na akakana vile vitu alivyokuwa amewafundisha, na akamkiri Kristo, na nguvu za Roho Mtakatifu, na huduma ya malaika.

18 Na akawazungumzia wazi, kwamba alikuwa amedanganywa na nguvu ya ibilisi. Na akazungumza kuhusu jehanamu, na umilele, na adhabu ya milele.

19 Na akasema: Nahofia kwamba nimetenda dhambi isiyosamehewa, kwani nimesema uwongo mbele ya Mungu; kwani nilimkana Kristo, na nikasema kwamba niliamini maandiko; na kwa kweli yanamshuhudia yeye. Na kwa sababu nimemdanganya Mungu naogopa kwamba hali yangu itakuwa mbaya; lakini ninatubu kwa Mungu.

20 Na ikawa kwamba baada ya kusema maneno haya hakuweza tena kusema mengine, na akafariki.

21 Na umati uliposhuhudia kwamba alizungumza vitu hivi akiwa karibu ya kufariki, walishangazwa sana; hadi nguvu za Mungu zikawashukia, na wakazidiwa na kuinama ardhini.

22 Sasa, kitu hiki kilinifurahisha mimi, Yakobo, kwani nilikuwa nimemwomba Baba yangu aliye mbinguni; kwani alisikia kilio changu na kujibu sala yangu.

23 Na ikawa kwamba amani na upendo wa Mungu ulirejeshwa tena miongoni mwa watu; na wakasoma maandiko, na hawakutii tena maneno ya huyu mtu mwovu.

24 Na ikawa kwamba mbinu nyingi zilitumiwa kuwarejesha Walamani ili wapate ufahamu wa kweli; lakini yote yalikuwa ni bure, kwani walifurahia vita na umwagaji wa damu, na walikuwa na chuki ya milele kwetu sisi, ndugu zao. Na wakataka kwa uwezo wao wa silaha kutuangamiza daima.

25 Kwa hivyo, watu wa Nefi wakajiimarisha dhidi yao kwa silaha zao, na kwa nguvu zao zote, wakimwamini Mungu na mwamba wa wokovu wao; kwa hivyo, wakawa, washindi wa maadui zao.

26 Na ikawa kwamba mimi, Yakobo, nilianza kuzeeka; na maandishi ya watu hawa yakiwa yameandikwa katika yale mabamba mengine ya Nefi, kwa hivyo, namaliza historia hii, nikikiri kwamba nimeandika kulingana na ufahamu wangu kamili, na kusema kwamba wakati ulipita pamoja nasi, na pia maisha yetu yalipita kama ndoto, sisi tukiwa watu wenye upweke na unadhiri, wahamaji, tuliotupwa nje kutoka Yerusalemu, tukizaliwa kwenye mateso, kwenye nyika, na kuchukiwa na ndugu zetu, ambao walisababisha vita na mabishano; kwa hivyo, tuliomboleza maisha yetu.

27 Na mimi, Yakobo, nikafahamu kwamba lazima hivi karibu niende kaburini; kwa hivyo, nikamwambia mwana wangu Enoshi: Chukua mabamba haya. Na nilimwambia vile vitu ambavyo kaka yangu Nefi aliniamuru, na akaahidi kutii zile amri. Na ninamaliza kuandika katika mabamba haya, uandishi ambao umekuwa mfupi; na kwa msomaji nakuaga kwa heri, nikitumaini kwamba ndugu zangu wengi watasoma maneno haya. Ndugu, Mungu awe nanyi.