2000–2009
Simama katika Mahali Pako Ulipopangiwa
Aprili 2003


Simama katika Mahali Pako Ulipopangiwa

Na tuwafikie na kuwaokoa wale walioanguka kando ya njia, ili isiwepo hata nafsi moja ya thamani itakayopotea.

Tumekutanika jioni hii kama mkusanyiko wenye nguvu wa ukuhani, kote hapa katika Kituo cha Mkutano na katika maeneo mbalimbali ulimwenguni kote. Baadhi wanashikilia Ukuhani wa Haruni, wakati wengine wanashikilia Ukuhani wa Melkizedeki.

Rais Stephen L. Richards, ambae alihudumu kama mshauri wa Rais David O. McKay, alitangaza, “Ukuhani kwa kawaida kirahisi unafafanuliwa kama ‘nguvu ya Mungu iliyonaibishwa kwa binadamu.” Anaendelea: “Ufafanuzi huu, Nafikiri, ni sahihi. Bali kwa ajili ya azma ya utendaji napenda kufafanua Ukuhani katika hali ya huduma na mara kwa mara nauita ‘mpango mkamilifu wa huduma.’ … Ni chombo cha huduma … na mtu anayeshindwa kuutumia anaelekea kuupoteza, kwani tumeelezwa wazi kwa ufunuo kwamba yule anayeudharu ‘hata hesabiwa kustahili kusimama.’”1

Katika Kigingi cha Pioneer, kilicho katika Jiji la Salt Lake na ambako nilipokea vyote Ukuhani wa Haruni na Melkizedeki, tulifunzwa kuwa na uzoefu wa maandiko, ikiwa ni pamoja na sehemu ya 20, 84, na 107 ya Mafundisho na Maagano. Katika sehemu hizi tunajifunza kuhusu ukuhani na utawala wa Kanisa.

Usiku huu ningependa kusisitiza mstari mmoja kutoka Sehemu ya 107: “Kwa sababu hiyo, sasa acha kila mtu na ajifunze wajibu wake, na kutenda kazi katika ofisi ambayo ameteuliwa, kwa bidii yote.”2

Rais Harlod B. Lee mara kwa mara alifundisha: “Wakati mtu anapokuwa na ukuhani, anakuwa wakala wa Bwana. Anatakiwa afikirie wito wake kama vile alikuwa kwenye wito wa Bwana.”3

Pia tunajifunza kutoka kwenye sehemu hizi kazi za akidi za urais na ukweli kwamba tuna majukumu kwa ajili ya wengine zaidi ya sisi wenyewe.

Kiuthabiti ninaamini kwamba Kanisa leo ni imara kuliko ambavyo limewahi kuwa. Kiwango cha shughuli za vijana wetu kinashuhudia kwamba huu ni uzao wa imani na wenye moyo wa kujitolea kwenye ukweli. Hata hivyo wapo baadhi wanaoanguka kando ya njia, wanaopata vivutio vingine ambavyo vinawashawishi kupuuza majukumu yao ya Kanisa. Lazima tusipoteze roho za thamani kama hizi.

Kuna idadi inayoongezeka miongoni mwa wazee watarajiwa ambao hawapo katika mikutano ya Kanisa wala hawatimizi majukumu yao ya Kanisa. Hali hii inaweza na lazima irekebishwe. Kazi ni yetu. Jukumu linahitaji kutolewa na juhudi kuwekwa mbele bila kuchelewa.

Urais katika akidi za ukuhani wa Haruni, chini ya uongozi wa uaskofu na washauri wa akidi, unaweza kuongezewa nguvu kufikia na kuokoa.

Alisema Bwana, “Kumbuka thamani ya nafsi ni kubwa mbele za Mungu; … na ni shangwe kubwa kiasi gani kwake katika nafsi ambayo hutubu!”4

Wakati mwingine kazi inaonekana ngumu mno. Tunaweza kuwa na ujasiri mpya kutokana na uzoefu wa Gideoni wa kale, ambaye, pamoja na jeshi lake la kadiri, alikuwa apigane na Wamidiani na Waamaleki. Mtakumbuka jinsi Gideoni na jeshi lake walivyokabiliana na nguvu kubwa mno ya majeshi makubwa na bora katika silaha na idadi. Kitabu cha Waamuzi katika Agano la Kale kinaandika kwamba jeshi lililoungana, Wamidiani na Waamaleki, “walikuwa wametua bondeni, mfano wa nzige kwa wingi; na ngamia zao walikuwa hawana hesabu; mfano wa mchanga wa ufuoni, kwa wingi.”5 Gideoni alikwenda kwa mwenyezi Mungu kwa ajili ya nguvu zake.

Kwa mshangao wake, Gideoni alishauriwa na Bwana kwamba idadi ya majeshi yake ilikuwa kubwa mno kwa ajili ya Bwana kumkabidhi adui kwenye mikono yao, wasije wakasema, “Mkono wangu mwenyewe ndio ulioniokoa.”6 Gideoni aliamriwa kutangaza kwa watu wake: “Mtu awaye yote anayeogopa na kutetemeka, na arudi aondoke … katika mlima wa Gileadi. Ndipo wakarudi watu ishirini na mbili elfu; na wakabaki elfu kumi,”7

Kisha Bwana alisema, “Hata sasa watu hawa ni wengi mno.”8 Alimwamuru Gideoni kuwapeleka watu kwenye maji kuangalia jinsi ambavyo wangeyanywa maji. Wale ambao waliramba maji waliwekwa katika kundi moja, na wale ambao walipiga magoti kunywa waliwekwa katika kundi lingine. Bwana alimwambia Gideoni “Kwa watu hawa mia tatu walioyaramba nitawaokoa, nami nitawatia Wamidiani katika mikono yako: lakini watu hawa wote wengine na waende zao kila mtu mahali pake.”9

Gideoni alirudi kwenye majeshi yake na kuwaambia, “Inukeni; kwa maana Bwana amelitia jeshi la Midiani mikononi mwenu.”10 Na aliwagawa wale watu mia tatu kwenye kombania tatu, na aliweka tarumbeta katika mkono wa kila mtu, pamoja na mitungi isiyo maji na mienge ndani ya hiyo mitungi. Na aliwaambia:

“Nitazameni, na mkafanye kama nifanyavyo mimi: na angalieni, nitakapofika mwisho wa kambi, itakuwa, nifanyavyo mimi nanyi fanyeni kadhalika.

“Nitakapopiga tarumbeta, Mimi na wote walio pamoja nami, basi nyinyi nanyi zipigeni tarumbeta pande zote za kambi … mkaseme, Upanga wa Bwana, na wa Gideoni,” Kisha alisema kwa kweli, “Nifuate.” Maneno yake hasa yalikuwa, “Kama nifanyavyo mimi, nanyi fanyeni kadhalika.”11

Kwa ishara ya kiongozi, jeshi la Gideoni walipiga tarumbeta zao na walivunja mitungi yao na waligumia, “Upanga wa Bwana, na wa Gideoni.” Maandiko yanarekodi matokeo ya vita hii ya uamuzi: “Na walisimama kila mtu katika mahali pake,” na ushindi ulipatikana.12

Mafundisho ya nyumbani ni sehemu ya mpango wa leo wa kuokoa. Wakati ulipotambulishwa na Rais David O. McKay kwa Viongozi wakuu wote wenye Mamlaka, alishauri, “Mafundisho ya Nyumbani ni moja wapo ya nafasi zetu muhimu na zenye thawabu kubwa za kutunza na kuvutia, kushauri na kuwaongoza watoto wa Baba yetu. … [Ni] huduma takatifu, wito mtakatifu. Ni wajibu wetu kama Walimu wa Nyumbani kupeleka roho takatifu kwenye kila nyumba na moyo,”13.

Katika maeneo fulani ambako nguvu ya kutosha ya Ukuhani wa Melkizedeki haipo, marais wa vigingi na maaskofu, wakishirikiana na rais wa misheni, wanaweza kuwatumia wamisionari wa muda wote kuwatembelea wasioshiriki kikamilifu na familia zenye muumini mmoja. Sio tu hii inaamsha tena roho ya umisionari katika nyumba, bali pia inatoa nafasi iliyo bora kwa ajili ya wale watambulishwao kwa wamisionari kuweza kupatikana.

Miaka yote nilipotembelea vigingi vingi ulimwenguni kote, pamekuwa na vigingi vile ambapo viongozi wa kata na vigingi, kwa kuona umuhimu au katika kuitikia wajibu, waliacha kuminya mikono yao, wakakunja mikono ya mavazi yao, na, kwa msaada wa Bwana, walikwenda kufanya kazi na kuleta watu wenye thamani kustahili kwa ajili ya Ukuhani wa Melkizedeki pamoja na wake zao na watoto, kuingia hekalu takatifu kwa ajili ya endaumenti zao na kuunganishwa.

Kwa ufupi nitataja baadhi ya mifano:

Kwenye ziara yangu ya Kigingi cha Millcreek katika Jiji la Salt Lake miaka michache iliyopita, nilijifunza kwamba takribani zaidi ya akina kaka 100 waliokuwa wazee watarajiwa walikuwa wametawazwa kuwa wazee mwaka uliotangulia. Nilimwuliza Rais James Clegg siri ya mafaniko yake. Ingawa alikuwa pia asiyejivuna kupokea sifa, mmoja wa washauri wake alionesha kwamba Rais Clegg, akitambua changamoto, aliamua kibinafsi kupiga simu na kupanga miadi binafsi na kila mzee mtarajiwa. Wakati wa miadi, Rais Clegg angelitaja hekalu la Bwana, ibada za wokovu na maagano yanayosisitizwa pale, na angehitimisha na swali hili: “Je, usinge tamani kumchukuwa mkeo kipenzi na watoto wako wa thamani kwenye nyumba ya Bwana, ili muweze kuwa familia daima milele yote?” Makubaliano yalifuata, mchakato wa uhamasishaji tena ulifuatia, na lengo lilifikiwa.

Katika mwaka 1952 familia nyingi katika Kata ya Tatu ya Rose Park walikuwa waumini ambao akina baba au waume walikuwa na Ukuhani wa Haruni tu, badala ya Ukuhani wa Melkizedeki. Kaka L.Brent Goates aliitwa kuhudumu kama askofu. Alimwalika kaka asiyeshiriki kikamilifu katika kata, Ernest Skinner, kusaidia katika kuwachochea akina kaka 29 wakubwa katika kata waliokuwa wakishikilia ofisi ya mwalimu katika Ukuhani wa Haruni na kuwasaidia wanaume hawa na familia zao kwenda hekaluni. Kama muumini asiyeshiriki kikamilifu mwenyewe, Kaka Skinner alisita hapo mwanzo lakini hatimaye alionesha kwamba angefanya kile ambacho angeweza. Alianza kibinafsi kutembelea walimu wakubwa wasioshiriki kikamilifu, akijaribu kuwasaidia kuona wajibu wao kama viongozi wa ukuhani katika nyumba zao na kama waume na akina baba kwenye familia zao. Hatimaye aliwaorodhesha baadhi ya akina kaka wasioshiriki kikamilifu kumsaidia katika kazi yake. Mmoja mmoja walianza kuwa tena washiriki kikamilifu na walichukuwa familia zao kwenda hekaluni.

Siku moja karani wa kata alitoka nje ya mstari wa kulipa wa duka la vyakula kusalimia kundi la mwisho la kwenda hekaluni. Akitoa maoni juu ya nafasi yake kama wa mwisho, yule mtu alisema: “Nilisimama na kuangalia wakati kundi lile lote wakiwa washiriki kikamilifu katika kata yetu na kwenda hekaluni. Kama tu ningeweza kufikiria jinsi gani inavyopendeza ndani ya hekalu, na jinsi gani ingeweza kubadili maisha yangu milele, kamwe nisingekuwa wa mwisho kwa watu 29 kuunganishwa katika hekalu.”

Katika kila moja ya maelezo haya, kulikuwa na ishara nne ambazo ziliwaongoza kwenye mafanikio:

  1. Nafasi ya uhamasishaji alifuatiliwa kwenye ngazi ya kata.

  2. Askofu wa kata alihusika.

  3. Walimu wenye weledi na wenye uvuvio waliandaliwa.

  4. Uangalifu ulitolewa kwa kila mmoja.

Akina Kaka, acha tukumbuke ushauri wa Mfalme Benyamini: “Mnapowatumukia wanadamu wenzenu mnamtumikia tu Mungu wenu.”14

Na tunyooshe mkono kuwaokoa wale wanaohitaji msaada wetu na tuwainue kwenye barabara ya juu na njia bora zaidi. Na tulenge mawazo yetu kwenye mahitaji ya wanaoshikilia ukuhani na wake zao na watoto walioteleza kutoka kwenye njia ya kushiriki kikamilifu. Na tusikilize jumbe zisizosemwa kutoka mioyoni mwao:

Niongoze, kaa nami, tembea karibu nami,

Nisaidie kuipata njia.

Nifundishe yote ambayo minapaswa kuyafanya

Kuishi pamoja naye siku moja.15

Kazi ya uhamasishaji sio kazi kwa ajili ya mvivu au mwota ndoto. Watoto wanakua, wazazi wanazeeka, na muda haumsubiri mtu. Usiahirishe msukumo; bali, ufanyie kazi, na Bwana atafungua njia.

Mara kwa mara uvumilivu wa maadili ya kimbingu unahitajika. Kama askofu nilihisi msukumo siku moja kumpigia simu mtu ambaye mkewe kwa kiasi fulani alikuwa akishiriki kikamilifu, wakati walikuwa watoto. Mtu huyu, hata hivyo, kamwe hakujibu. Ilikuwa siku ya joto wakati wa majira ya joto nilipogonga kisitiri cha mlango cha Harold G. Gallacher. Niliweza kumwona Kaka Gallacher amekaa katika kiti chake akisoma gazeti. “Ni nani huyo?” aliuliza bila kuangalia.

“Askofu wako,” nilijibu. “Nimekuja tufahamiane na kusihi sana mahudhurio yako pamoja na familia yako kwenye mikutano yetu.”

“Hapana, nina shughuli nyingi,” likaja jibu lake la dharau. Kamwe hakunitazama. Nilimshukuru kwa kusikiliza na niliondoka kutoka ngazi za mlango wake.

Familia ya Gallacher ilihamia California muda mchache baadaye. Miaka mingi ilipita. Kisha, kama mshiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, nilikuwa nafanya kazi ofisini kwangu siku moja wakati katibu muhtasi wangu alipopiga simu, akisema: “Kaka Gallacher ambaye mwanzo aliishi katika kata yako angependa kuzungumza nawe. Yupo hapa katika ofisi yangu.”

Nilijibu, “Muulize kama jina lake ni Harold G. Gallacher ambaye, pamoja na familia yake, waliishi Vissing Place kwenye West Temple na Fifth South.”

Alisema, “Yeye ndiye”

Nikamwomba amlete ndani. Tulikuwa na mazungumzo mazuri pamoja kuhusu familia yake. Aliniambia, “Nimekuja kuomba radhi kwa kutokuinuka kutoka kwenye kiti na kukuruhusu katika mlango siku ile ya majira ya joto miaka mingi iliyopita.” Nilimwuliza kama alikuwa akishiriki kikamilifu Kanisani. Kwa tabasamu la kulazimisha, alijibu: “Mimi sasa ni mshauri wa pili katika uaskofu wa kata yangu. Mwaliko wako wa kujitokeza kwenda Kanisani, na jibu langu hasi, lilinisumbua sana kiasi kwamba niliamua kufanya kitu fulani kuhusu hilo.

Harold na Mimi tulitembeleana pamoja katika matukio kadhaa kabla hajafariki. Akina Gallacher na watoto wao walitumika miito mingi Kanisani. Mmoja wa wajukuu wadogo sasa anahudumia umisionari wa muda wote.

Kwa wamisionari wengi ambao mtakuwa mnasikiliza jioni hii, ninashiriki ugunduzi kwamba mbegu za ushuhuda mara kwa mara hazioti mizizi na kuchanua kwa haraka. Mkate uliotupwa juu ya maji unarudi, wakati mwingine, baada tu ya siku nyingi. Lakini unarudi.

Nilijibu muito wa simu yangu jioni moja kusikia sauti ikiuliza, “Je, una uhusiano na Mzee Monson ambaye miaka iliyopita alihudumia katika Misheni ya New England?”

Nilijibu kwamba hivyo sivyo ilivyo. Mpiga simu alijitambulisha mwenyewe kama Kaka Leonardo Gambardella na kisha alitaja kwamba Mzee Monson na mzee Bonner walipiga simu nyumbani kwake siku nyingi zilizopita na kutoa ushuhuda wao kwake na kwa mke wake. Walisikiliza lakini hawakufanya chochote zaidi kutumia mafundisho yao. Baadaye walihamia California, ambako, kiasi cha miaka 13 baadaye, walipata tena ukweli na waliongoka na kubatizwa. Kaka Gambardella kisha aliuliza kama kulikuwa na njia yoyote angeweza kuwafikia Wazee ambao mwanzo waliwatembelea, ili aweze kuonyesha shukrani zake za dhati kwa ajili ya ushuhuda wao, ambao umebakia pamoja naye na mke wake.

Nilichunguza kumbukumbu. Nilipata walipo wazee. Unaweza kufikiri mshangao wao wakati, sasa wameoa na wana familia zao wenyewe, niliwapigia simu na kuwaeleza habari njema—hata hitimisho la juhudi zao za mwanzo. Mara moja waliwakumbuka akina Gambardella. Nilipanga mkutano kupitia simu ili waweze kibinafsi kuwapa hongera na kuwakaribisha Kanisani. Walifanya hivyo. Kulikuwa na machozi, bali yalikuwa machozi ya furaha.

Edwin Marham aliandika mistari hii:

Kuna takdiri ambayo hutufanya sisi kuwa ndugu;

Hakuna yeyote ambaye huenda njia yake pake yake:

Yale yote tunayotuma katika maisha ya wengine

Hurudi tena kwetu wenyewe.16.

Usiku huu ninaomba kwamba sisi sote tunaoshikilia ukuhani tuweze kuhisi wajibu wetu, ili sisi, kama Gideoni wa kale, tuweze kusimama kila mtu katika mahali pake alipopangiwa na kama wamoja, tumfuate kiongozi wetu—hata Bwana Yesu Kristo—na nabii wake, Rais Gordon B. Hinckley. Na tuwafikie na kuwaokoa wale walioanguka kando ya njia, ili isiwepo hata nafsi moja ya thamani itakayopotea.

Katika Jina la Yesu Kristo, amina.