2000–2009
Kukusanywa kwa Israeli Waliotawanyika
Oktoba 2006


Kukusanywa kwa Israeli Waliotawanyika

Tunasaidia kukusanya wateule wa Bwana kwenye pande zote mbili za pazia.

Wapendwa kaka na dada zangu, asanteni sana kwa imani yenu, sala zenu, na upendo wenu. Tunashirikiana wajibu mkubwa wa kuwa watu wale ambao Bwana anatutaka tuwe na kufanya kile anachotaka sisi tufanye Sisi ni sehemu ya mabadiliko makubwa—kukusanya Israeli walio tawanyika. Ninazungumzia juu ya mafundisho haya leo kwa sababu ya umuhimu wake wa kipekee katika mpango wa milele wa Mungu.

Agano la Ibrahimu

Hapo kale, Bwana alimbariki Baba Ibrahimu kwa ahadi ya kufanya uzao wake kuwa wa watu wateule.1 Marejeo kwenye agano hili yanaonekana katika maandiko yote. Zilizojumuishwa zilikuwa ahadi kwamba Mwana wa Mungu angekuja kupitia ukoo wa Ibrahimu, kwamba nchi fulani zitarithiwa, kwamba mataifa na ndugu wa dunia watabarikiwa kupitia uzao wake, na zaidi.2 Wakati baadhi ya vipengele vya agano lile tayari vimekamilishwa, Kitabu cha Mormoni kinafundisha kwamba agano hili la Ibrahimu litatimizwa tu katika siku hizi za mwisho!3 Pia linasisitiza kwamba sisi ni miongoni mwa watu wa agano wa Bwana.4 Yetu ni heshima ya ushiriki binafsi katika utimilifu wa ahadi hizi. Wakati gani wa kusisimua kuwa hai!

Israeli Wakawa Wametawanywa

Kama wazao wa Ibrahimu, makabila ya Israeli ya kale yalikuwa na fursa ya kupata mamlaka ya ukuhani na baraka za injili, lakini hatimaye watu waliasi. Waliwaua manabii na wakaadhibiwa na Bwana. Makabila kumi yalichukuliwa mateka kwenda Assyria. Kutoka kule wakawa wamepotea kwenye kumbukumbu ya wanadamu. (Ni dhahiri, makabila yale kumi hayajapotea kwa Bwana.) Makabila mawili yaliyobaki yaliendelea kwa muda mfupi na kisha, kwa sababu ya uasi wao, walichukuliwa mateka kwenda Babeli.5 Wakati waliporudi, walipendelewa na Bwana, lakini tena hawa kumheshimu Yeye. Walimkataa na kumkashifu. Baba mwenye upendo lakini aliye huzunishwa aliahidi, “Nitawatawanya miongoni mwa watu wa ulimwengu,”6 na hilo alifanya—kwenye mataifa yote.

Israeli Kukusanywa

Ahadi ya Mungu kwa ajili ya kukusanywa kwa Israeli ilikuwa yenye nguvu vile vile.7 Isaya, kwa mfano, aliona mapema, kwamba katika siku za mwisho Bwana atatuma “wajumbe wa haraka” kwa watu hawa ambao walikuwa “ “wametawanyika na kuambuka.”8

Ahadi hii ya kukusanywa, iliyofumwa kupitia kitambaa cha maandiko, itatimizwa kwa hakika kama vile ilivyokuwa unabii wa kutawanywa kwa Israeli.9

Kanisa la Yesu Kristo katika Wakati wa Meridiani na Ukengeufu

Kabla ya Kusulibiwa Kwake, Bwana Yesu Kristo alikuwa amelianzisha Kanisa Lake. Lilijumuisha mitume, manabii, sabini, waalimu, na kadhalika.10 Na Bwana aliwatuma wanafunzi Wake kwenda ulimwenguni ili kuhubiri injili Yake.11

Baada ya muda Kanisa kama lililvyoanzishwa na Bwana liliangukia kwenye uozo wa kiroho. Mafundisho Yake yaligeuzwa; ibada Zake zilibadilishwa. Ukengeufu Mkuu ulikuja kama ilivyotabiriwa na Paulo, aliyejua kwamba Bwana hatakuja tena “isipokuwa kuje kuanguka kwanza.”12

Ukengeufu huu Mkuu ulifuata mpangilio ambao ulimalizia kila kipindi kilichotangulia. Cha kwanza kabisa kilikuwa katika wakati wa Adamu. Kisha vikaja vipindi vya Henoko, Nuhu, Ibrahimu, Musa, na wengine. Kila nabii alikuwa na wajibu mtukufu kufundisha juu ya uungu na mafundisho ya Bwana Yesu Kristo. Katika kila kipindi mafundisho haya yalikusudiwa kuwasaidia watu. Lakini kutotii kwao kulisababisha ukengeufu. Hivyo, vipindi vyote vilivyopita vilikuwa na vikomo katika muda na eneo. Vilikuwa na vikomo katika muda kwa sababu kila kimoja kiliisha katika ukengeufu. Vilikuwa na vikomo katika eneo kwa kiasi kidogo cha sehemu ya sayari ya dunia.

Urejesho wa Vitu Vyote

Hivyo urejesho kamili ulihitajika. Mungu Baba na Yesu Kristo walimwita Nabii Joseph Smith kuwa nabii wa kipindi hiki. Nguvu zote za kiungu za vipindi vilivyopita zilikuwa zirejeshwe kupitia Yeye.13 Kipindi hiki cha utimilifu wa nyakati hakitakuwa na kikomo katika muda au eneo. Hakitamalizika katika ukengeufu, na kitajaza ulimwengu.14

Kukusanywa kwa Israeli—ni Sehemu Muhimu ya Urejesho wa Vitu Vyote

Kama ilivyotolewa unabii na Petro na Paulo, vitu vyote vitarejeshwa katika kipindi hiki. Kwa hiyo, lazima uje, kama sehemu ya ule urejesho, kukusanywa kulikosubiriwa kwa muda mrefu wa Israeli iliyo tawanyika.15 Ni utangulizi muhimu kwa Ujio wa Pili wa Bwana.16

Mafundisho haya ya ukusanyaji ni mojawapo ya mafunzo muhimu ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Bwana ametangaza: Ninawapatia ishara … kwamba nitawakusanya ndani, kutoka kipindi chao kirefu, watu wangu, Ee nyumba ya Israeli, na nitaanzisha tena miongoni mwao Sayuni yangu.”17 Kutokea kwa Kitabu cha Mormoni ni ishara kwa ulimwengu mzima kwamba Bwana ameanza kukusanya Israeli na kutimiza maagano Aliyoyafanya kwa Ibrahimu, Isaka, na Yakobo.18 Hatufundishi tu kanuni hii, lakini tunaishiriki pia. Tunafanya hivyo tunaposaidia kuwakusanya wateule wa Bwana kutoka pande zote mbili za pazia.

Kitabu cha Mormoni ni kitovu cha kazi hii. Inatangaza mafundisho ya kukusanywa.19 Kinasababisha watu kujifunza kuhusu Yesu Kristo, kuamini injili yake, na kujiunga na Kanisa Lake. Kwa kweli, kama kusingekuwa na Kitabu cha Mormoni, mkusanyiko ulioahidiwa wa Israeli haungetokea.20

Kwa sisi jina linaloheshimika la Ibrahimu ni muhimu. Limetajwa katika mistari mingi zaidi ya maandiko ya Urejesho kuliko katika mistari yote ya Biblia.21 Ibrahimu ameunganishwa kwa waumini wote wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.22 Bwana alisisitiza tena agano la Ibrahimu katika siku yetu kupitia Nabii Joseph Smith.23 Ndani ya hekalu tunapokea baraka zetu za msingi, kama wa uzao wa Ibrahimu, Isaka, na Yakobo.24

Kipindi cha Maongozi ya Mungu cha Utimilifu wa Nyakati

Kipindi hiki cha maongozi ya Mungu cha utimilifu wa nyakati kilitabiriwa na Mungu kama ni wakati wa kukusanya, kote mbinguni na duniani. Petro alijua kwamba baada ya muda wa ukengeufu, urejesho ungekuja. Yeye, aliyekuwa pamoja na Bwana juu ya Mlima wa Kugeuka Sura,alitamka:

Kwa hiyo nyie tubuni, na mwongoke,ili dhambi zenu ziweze kufutiliwa mbali, wakati nyakati za kuburudishwa zitapokuja kutoka kwenye uwepo wa Bwana; …

“Ambaye ilimpasa kupokewa mbinguni hata zije zamani za kufanywa upya vitu vyote, zilizonenwa na Mungu kwa kinywa cha manabii wake wote watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu.”25

Katika nyakati za sasa Mitume Petro, Yakobo, na Yohana walitumwa na Bwana wakiwa na “funguo za ufalme [Wake], na kipindi cha injili kwa ajili ya nyakati za mwisho; na kwa ajili ya utimilifu wa nyakati,” ambao atawakusanya pamoja mambo yote, yaliyoko mbinguni na yaliyoko duniani.”26

Mnamo mwaka 1830 Nabii Joseph Smith alijifundisha juu ya mjumbe wa mbinguni aliyeitwa Eliasi, aliyekuwa na funguo za kuleta “urejesho wa vitu vyote.”27

Miaka sita baadae hekalu la Kirtland liliwekwa wakfu. Baada ya Bwana kukubali nyumba ile takatifu, wajumbe wa mbinguni walikuja na funguo za ukuhani. Musa alitokea28 “na kutukabidhi … funguo za kukusanywa kwa Israeli kutoka pande nne za dunia, na kuongozwa kwa makabila kumi kutoka nchi ya kaskazini.

“Baada ya hili, Eliasi alitokea, na kukabidhi kipindi cha injili ya Ibrahimu, akisema kwamba kupitia sisi na uzao wetu vizazi vyote baada yetu vitabarikiwa.”2929

Kisha Eliya nabii alikuja na kutangaza, “Tazama, muda,umekamilika, ambao ulisemwa kwa kinywa cha Malaki—akishuhudia kwamba yeye [Eliya] atapaswa kutumwa, kabla haijaja siku ile ya Bwana iliyo kuu na ya kuogofya —ili kugeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana.”30

Matukio haya yalitokea Aprili 3, 1836,31 na hivyo kutimilika kwa unabii wa Malaki.32 Funguo takatifu za kipindi hiki zilirejeshwa.33

Kukusanya Roho Upande Mwingine wa Pazia

Kwa huruma, mwaliko wa “kuja kwa Kristo”34 unaweza pia kutolewa kwa wale waliofariki bila ufahamu wa injili.35 Sehemu ya matayarisho yao, yana hitaji juhudi za wengine duniani. Tunakusanya chati za ukoo, tunatengeneza makartasi ya vikundi vya familia, na kufanya kazi ya hekaluni kwa niaba ili kuwakusanya watu kwa Bwana na katika familia zao.36

Ili Kushiriki katika Ukusanyaji: Sharti na Agano

Hapa duniani, kazi ya umisionari ni muhimu kwa ukusanyaji wa Israeli. Injili ilikuwa ipelekwe kwanza kwa “kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.”37 Kwa hiyo,watumishi wa Bwana wamesonga mbele wakitangaza Urejesho. Katika mataifa mengi wamisionari wetu wamewatafuta wale wa Israeli waliotawanyika; wamewawinda “kutoka kwenye mapango za majabali”; na wamewavua, kama katika siku za kale.38

Chaguo la kuja kwa Kristo sio swala la kieneo; ni swala la sharti la mtu binafsi. Watu wanaweza “kuletwa kwenye ufahamu wa Bwana”39 bila ya kuondoka kwenye ardhi zao za nyumbani. Kweli, katika siku za mwanzo za Kanisa, uongofu mara nyingi ulimaanisha pia uhamiaji. Lakini sasa kukusanyika kunafanyika katika kila taifa. Bwana ameagiza kuanzishwa kwa Sayuni40 katika kila ufalme ambapo Amewapa Watakatifu Wake uzaliwa wao na utaifa. Maandiko yanatabiri kwamba watu “watakusanywa nyumbani kwenye nchi zao za urithi, na wataimarishwa katika nchi zao zote za ahadi.”41 “Kila taifa ni mahali pa kukusanyikia kwa watu Wake.”42 “Mahali pa kukusanyika kwa Watakatifu wa Brazili ni katika Brazili; mahali pa kukusanyika kwa Watakatifu wa Nigeria ni katika Nigeria; mahali pa kukusanyika kwa Watakatifu wa Korea ni katika Korea; na kadhalika Sayuni ni “wasafi katika moyo.”43 Sayuni ni popote pale walipo Watakatifu wenye haki. Machapisho, mawasiliano, na mikusanyiko sasa ni kama vile karibu waumini wote wanaweza kupata mafundisho, funguo, ibada na baraka za injili, bila kujali eneo lao.

Usalama wa kiroho daima utategemea jinsi mtu anavyoishi, sio pale mtu anapoishi. Watakatifu katika kila nchi wana madai sawa juu ya baraka za Bwana.

Kazi hii ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Yu hai. Yesu ndiye Kristo. Hili ni Kanisa Lake, lililorejeshwa ili kutimiza hatima yake ya kiungu, ikijumuisha kukusanywa kwa Israeli kulikoahidiwa. Rais Gordon B. Hinckley ni nabii wa Mungu leo. Mimi nashuhudia hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.