2000–2009
Kanuni Mbili kwa Uchumi Wowote
Oktoba 2009


Kanuni Mbili kwa Uchumi Wowote

Mara nyingi ni katika jaribio la taabu kwamba tunajifunza masomo yale yenye upeo wa juu ambayo yanatengeneza tabia zetu na kuipa umbo hatima yetu.

Katika ziara zetu kutembelea waumini wa Kanisa kote ulimwenguni na kwa njia ya ngazi zilizoanzishwa za ukuhani, tunapokea mwitikio wa moja kwa moja juu ya hali na changamoto za waumini wetu. Kwa miaka mingi wengi wa waumini wetu wamekumbwa na maafa ya ulimwengu, yote ya asili na yaliyotengenezwa na watu. Pia tunaelewa kwamba familia nyingi zimelazimika kupunguza gharama za maisha na wana wasiwasi kuhusu kuvumilia nyakati hizi za changamoto.

Ndugu, tunajihisi karibu sana na nyinyi. Tunawapenda na tunawaombea kila wakati. Nimeona panda shuka za kutosha kote katika maisha yangu kuweza kujua ya kwamba kwa hakika wakati mgumu huleta matumaini ya wakati mzuri. Mimi nina matumaini makubwa kuhusu siku zijazo. Ndugu, kwa upande wetu, lazima tuwe na uthabiti katika tumaini, tufanye kazi kwa nguvu zetu zote na tumtumaini mungu.

Hivi karibuni nimekuwa nikiwaza kuhusu wakati katika maisha yangu wakati uzito wa wasiwasi na masikitiko juu ya wakati ujao wenye mashaka ulipoonekana daima kuwepo. Nilikuwa na umri wa miaka 11 na niliishi na familia yangu darini kwenye nyumba ya mkulima karibu na Frankfurt, Ujerumani. Tulikuwa wakimbizi kwa mara ya pili katika muda wa miaka michache sana, na tulikuwa tunajitahidi kujiimarisha wenyewe katika eneo jipya mbali kabisa kutoka nyumba yetu ya hapo awali. Ningesema kwamba tulikuwa masikini, lakini hayo yangekuwa maelezo pungufu. Sote tulilala pamoja katika chumba kimoja kilichokuwa kidogo kiasi kwamba hakukuwa na nafasi ya kuzunguka kando ya vitanda. Katika chumba kingine kidogo, tulikuwa na vipande vichache vya samani nzuri na jiko la mafuta ambalo mama alitumia kupikia chakula. Kutoka chumba kimoja hadi kingine, ilitubidi tupite kwenye chumba cha ghala ambacho mkulima aliweka vifaa vyake pamoja na nyenzo, sambamba na nyama na soseji zilizopangwa vizuri zikining’inia kwenye kombamoyo. Harufu nzuri kila wakati ilinifanya nihisi njaa sana. Hatukuwa na maliwato lakini tulikuwa na banda la uwani—chini ya ngazi na umbali wa futi 50 (mita 15), ingawa ilionekana mbali kidogo wakati wa majira ya baridi.

Kwa sababu nilikuwa mkimbizi na kwa sababu ya lafudhi yangu ya Ujerumani Mashariki, watoto wengine mara kwa mara walinicheka na kuniita majina ambayo yalinikera sana. Katika nyakati zote za ujana wangu, ninaamini hili linaweza kuwa la kukatisha tamaa zaidi.

Sasa, miongo kadhaa baadaye, naweza kukumbuka hizo siku kupitia chujio laini la uzoefu. Ingawa ningali nakumbuka maumivu na kukata tamaa, naweza kuona sasa kile ambacho sikuweza kuona wakati ule: hiki kilikuwa kipindi cha ukuaji binafsi mkubwa. Katika wakati huu, familia yetu iliungana pamoja. Nilitazama na kujifunza kutoka kwa wazazi wangu. Nilipendezwa na ushupavu wao na msimamo wao. Kutoka kwao nilijifunza kwamba taabu, ikikabiliwa kwa imani, ujasiri, na ushupavu, inaweza kushindwa.

Nikijua kwamba baadhi yenu mnapitia vipindi vyenu vya mahangaiko na kukata tamaa, leo nilitaka kuzungumza kuhusu kanuni mbili muhimu ambazo zimenihimili kupita kipindi hiki cha ukuaji maishani mwangu.

Kanuni ya Kwanza: Kazi

Mpaka leo, napendezwa sana na jinsi familia yangu ilivyofanya kazi baada ya kupoteza kila kitu kufuatia vita ya pili ya dunia! Namkumbuka baba yangu—Mfanyakazi wa serikali kwa kusomea na kwa uzoefu—akifanya kazi kadhaa ngumu, zikiwemo kuchimba madini ya makaa ya mawe, kuchimba madini ya urani, makanika na dereva wa lori. Alitoka mapema asubuhi na kila mara alirudi usiku sana ili kuikimu familia yetu. Mama yangu alianza kazi ya kufua nguo na alifanya kazi za mikono kwa masaa mengi. Alituandikisha mimi na dada yangu katika biashara yake. Kwa kutumia baisikeli yangu nilikuwa mtoa huduma ya kubeba na kuwasilisha. Nilihisi vizuri kuweza kusaidia familia yangu kwa njia ndogo, na ingawa sikulijua hilo wakati ule, kazi ya sulubu iligeuka kuwa baraka kwa afya yangu pia.

Haikuwa rahisi, lakini kazi ilituepusha na kujikita sana kwenye magumu ya hali zetu. Japokuwa hali yetu haikubadilika kwa siku moja, ilikuja kubadilika. Hili ndilo jambo kuhusu kazi. Kama tutazidi kuifanya—kwa uthabiti na siku zote—kwa hakika mambo yatazidi kuwa mazuri.

Jinsi gani ninapendezwa na wanaume, wanawake, na watoto wanaojua jinsi ya kufanya kazi! Jinsi gani Bwana anavyompenda mfanyakazi! Alisema “Kwa jasho la uso wako utakula chakula,”1 Na “Mfanyakazi anastahili ujira wake.”2 Na pia Yeye alitoa ahadi : “ingiza mundu yako kwa moyo wako wote na dhambi zako zitasamehewa.”3 Wale wasioogopa kufanya kazi na kujikita katika utafutaji wa malengo ya thamani ni baraka kwa familia zao, jamii, mataifa na kwa Kanisa.

Bwana hatarajii tufanye kazi kubwa kuliko uwezo wetu. Hapendi (wala hatupaswi) kulinganisha juhudi zetu na za wengine. Baba yetu wa mbinguni anaomba tu tufanye vizuri tuwezavyo—kwamba tufanye kazi kulingana na uwezo wetu wote, hata kama utakuwa mkubwa au mdogo.

Kazi ni kinyume cha wasiwasi, lihamu ya huzuni, na mlango kwenye uwezekano. Bila kujali hali yetu katika maisha, ndugu zangu wapendwa, na tufanye vizuri tuwezavyo na tupalilie heshima kwa ajili ya ubora katika yote tunayofanya. Acha tuweke mawazo yetu na miili yetu katika fursa tukufu kwa kazi ambayo huletwa na kila siku iliyo mpya.

Wakati magari yetu yanapokwama kwenye matope, Mungu atapendelea zaidi kumsaidia mtu ambaye atatoka nje kusukuma kuliko yule ambaye anapaza sauti tu katika sala—licha ya maneno yenye ushawishi. Rais Thomas S. Monson aliliweka hivi: “Haitoshi tu kutaka kuweka juhudi na kusema tutaweka juhudi. … Ni katika kutenda, si tu kufikiri, ambapo tunatimiza malengo yetu. Kama tutaendelea kuahirisha malengo yetu, hatutaona kamwe yakitimia.”4

Kazi inaweza kuadilisha na kuridhisha, lakini kumbuka onyo la Yakobo la “msitumie … nguvu zenu kwa yale yasiyotosheleza.”5 Kama tutajitoa kwenye kutafuta utajiri wa humu ulimwenguni na kutambuliwa na watu kwa hasara ya familia zetu na ukuaji wetu wa kiroho, punde tutagundua kwamba tulijihusisha na mambo ya kipumbavu. Kazi njema tunayofanya majumbani mwetu ni takatifu zaidi; Faida zake zina manufaa ya milele. Haiwezi kunaibishwa. Ni msingi wa kazi yetu kama wenye ukuhani.

Kumbuka, sisi ni wasafiri wa muda tu humu duniani. Tusitumie vipaji na nguvu tulizopewa na Mungu kwenye kuweka nanga za kidunia pekee, bali acha tutumie siku zetu kukua kiroho. Kwani kama wana wa Mungu aliye Juu, tuliumbwa kupaa katika upeo mpya.

Sasa, neno kwetu sisi wenye uzoefu: kustaafu si sehemu ya mpango mkuu wa Bwana wa furaha. Hakuna programu ya sabato au kustaafu kutoka kwenye majukumu ya ukuhani—licha ya umri na uwezo wa kimwili. Wakati maneno “nilishakuwa hapo, nishafanya hilo” yanaweza kuwa kama kisingizio cha kuepuka kuteleza kwenye barafu, kukataa mwaliko wa kuendesha pikipiki au kuepuka pilipili kwenye chakula cha kujipakulia mwenyewe, si kisingizio kinachokubalika kuepuka majukumu ya agano ya kuweka wakfu muda wetu, vipaji, na nyenzo katika kazi ya ufalme wa Mungu.

Kunaweza kuwa na wale ambao, baada ya kutumikia kanisa kwa miaka mingi, huamini kwamba wanastahili muda wa kupumzika wakati wengine wakifanya kazi. Nikiliweka wazi, ndugu, aina hii ya kufikiri haistahili kwa mfuasi wa Kristo. Sehemu kubwa ya kazi yetu hapa duniani ni kuvumilia kwa furaha hadi mwisho—kila siku ya maisha yetu.

Sasa, neno pia kwa kaka zetu vijana katika Ukuhani wa Melkizedeki, wanaotafuta malengo ya haki ya kupata elimu na kupata mwenza wa milele. Haya ni malengo sahihi, kaka zangu, lakini kumbukeni: kufanya kazi kwa bidii katika shamba la mizabibu la Bwana kutawaongezea sifa kwenye wasifu wenu binafsi na kuongeza uwezekano wa mafanikio katika juhudi hizi zote mbili zenye thamani.

Uwe shemasi mdogo zaidi au kuhani mkuu mzee kabisa, kuna kazi ya kufanya!

Kanuni ya Pili: Jifunze

Kipindi cha wakati mgumu wa hali za kiuchumi baada ya vita vya Ujerumani, fursa za elimu hazikuwa nyingi kama zilivyo leo. Lakini licha ya machaguo machache, daima nilihisi hamu ya kujifunza. Nakumbuka siku moja, wakati nikiwa naenda na baiskeli yangu kupeleka nguo, niliingia kwenye nyumba ya mwanafunzi mwenzangu. Katika moja ya vyumba, meza mbili ndogo zilikuwa zimeegeshwa ukutani. Yalikuwa mandhari ya kupendeza yaliyoje! Ni bahati ilioje hao watoto kuwa na meza zao wenyewe! Ningeweza kuwafikiria wakiwa wameketi na vitabu vyao vimefunguliwa wakijifunza masomo yao na kufanya kazi yao ya shuleni nyumbani. Kwangu mimi ilionekana kwamba kuwa na meza yangu ingekuwa jambo la kupendeza sana ulimwenguni.

Ilinibidi kusubiri kwa muda mrefu kabla ya matamanio yangu kutimizwa. Miaka mingi baadaye, nilipata kazi kwenye taasisi ya utafiti ambayo ilikuwa na maktaba kubwa sana. Nakumbuka kutumia muda wangu mwingi sana nilipomaliza kazi katika maktaba hiyo. Hapo hatimaye ningeweza kukaa kwenye meza—peke yangu—na kunywa kwenye habari na maarifa ambayo vitabu vinatoa. Jinsi gani nilivyopenda kusoma na kujifunza! Katika siku hizo, nilielewa fika maneno ya msemo wa kale: Elimu si kupata maarifa tu bali ni kufanya jambo na hayo maarifa.

Kwa waumini wa Kanisa, elimu si tu wazo zuri—ni amri. Tunapaswa kujifunza “juu ya mambo kote mbinguni na duniani, na chini ya dunia mambo yaliyokuwepo, mambo yaliyopo, mambo ambayo hayana budi kutokea upesi; mambo yaliyoko nyumbani, mambo yaliyoko ng’ambo.”6

Joseph Smith alipenda kusoma ingawa alikuwa na fursa chache sana za masomo ya darasani. Katika sharaja zake, alizungumza kwa furaha kuhusu siku alizozitumia kujifunza na kila mara alielezea upendo wake kuhusu kusoma.7

Joseph aliwafundisha watakatifu kwamba maarifa yalikuwa sehemu muhimu ya safari yetu ya duniani, kwa kuwa “Haiwezekani kwa mwanadamu kuokolewa katika ujinga,”8 na “kwamba kanuni yoyote ya akili tuipatayo … katika maisha haya, itafufuka nasi katika ufufuko.”9 Katika nyakati za changamoto, ni jambo la muhimu zaidi kujifunza. Nabii Joseph alifundisha, “Maarifa huondoa giza, [wasiwasi], na shaka; kwa kuwa haya hayawezi kuwepo mahali palipo na maarifa.”10

Ndugu, mna wajibu wa kujifunza kadiri muwezavyo. Tafadhali himizeni familia zenu, washiriki wa akidi zenu, kila mtu kujifunza na kuwa walio elimika vizuri. Kama elimu ya darasani haipatikani, usiruhusu hilo kukuzuia kupata maarifa yote unayoweza kupata. Katika hali kama hizo, vitabu vizuri zaidi kwa mantiki hiyo, vinaweza kuwa “chuo chako kikuu”—darasa ambalo liko wazi kila wakati na huwapokea wote watakaoomba. Jitahidi kuongeza maarifa yako kwa chochote kilicho “chema, chenye kupendeza, au chenye taarifa njema au chenye kustahili sifa.”11 Tafuteni maarifa “kwa kujifunza na pia kwa imani.”12 Tafuteni kwa roho ya unyenyekevu na moyo uliopondeka.13 Unapotumia mtazamo wa kiroho wa imani katika kujifunza kwako—hata kwa mambo ya kimwili—unaweza kuzidisha uwezo wa akili, kwa kuwa “kama macho yenu yatakuwa katika utukufu wa [Mungu] pekee, [miili] yenu yote itajazwa na nuru, … na [mtafahamu] mambo yote.”14

Katika kujifunza kwetu tusipuuze chemichemi ya ufunuo. Maandiko na maneno ya mitume na manabii wa siku hizi ndiyo vyanzo vya hekima, elimu takatifu, na ufunuo binafsi kutusaidia kutafuta majibu ya changamoto za maisha. Acha tujifunze juu ya Kristo; acha tutafute yale maarifa ambayo yanaelekeza kwenye amani, ukweli, na siri tukufu za milele.15

Hitimisho

Ndugu, nafikiria nyuma kwa yule mvulana wa miaka 11 huko Frankfurt, Ujerumani, aliyekuwa na wasiwasi kuhusu maisha yake ya baadaye na aliyehisi uchungu wa maneno ya kejeli. Nakumbuka wakati huu kwa kumbukumbu za huzuni kiasi. Wakati nisingependa kukumbuka hizo siku za majaribio na shida, nina uhakika mkubwa kwamba masomo niliyojifunza yalikuwa matayarisho muhimu kwa fursa zijazo. Sasa, miaka mingi baadaye, ninajua hili kwa uhakika: mara nyingi ni katika jaribio la taabu kwamba tunajifunza masomo yale yenye upeo wa juu ambayo yanatengeneza tabia zetu na kuipa umbo hatima yetu.

Ninaomba kwamba katika miezi na miaka ijayo tuweze kujaza muda na siku zetu kwa kazi za haki. Ninaomba kwamba tutatafuta kujifunza na kuboresha akili zetu na mioyo yetu kwa kunywa kwa kina kutoka kwenye chemichemi safi za ukweli. Ninawaachia upendo wangu na baraka katika jina la Yesu Kristo, amina.