Mkutano Mkuu
Falme za Utukufu
Mkutano mkuu wa Oktoba 2023


Falme za Utukufu

Tuna Baba wa Mbinguni mwenye upendo ambaye atahakikisha kwamba tunapokea kila baraka na kila faida ambayo matamanio yetu na chaguzi zetu huruhusu.

Waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho huulizwa mara kwa mara, “Kanisa lenu lina tofauti gani na makanisa mengine ya Kikristo?” Miongoni mwa majibu tunayotoa ni utimilifu wa mafundisho ya Yesu Kristo. Jambo kuu kati ya fundisho hilo ni ukweli kwamba Baba yetu wa Mbinguni anawapenda sana watoto Wake wote hata kwamba anataka sisi sote tuishi katika ufalme wa utukufu milele. Zaidi ya hayo, anataka tuishi pamoja Naye na Mwanawe, Yesu Kristo, milele. Mpango Wake hutupa sisi mafundisho na fursa ya kufanya maamuzi ambayo yatatuhakikishia hatma na maisha tunayochagua.

I.

Kutokana na ufunuo wa siku za leo tunajua kwamba hatma ya mwisho ya wote wanaoishi duniani sio wazo la mbinguni kwa wenye haki na mateso ya milele ya kuzimu kwa wengine. Mpango wa upendo wa Mungu kwa watoto Wake unajumuisha uhalisia huu uliofundishwa na Mwokozi wetu, Yesu Kristo: “Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi.”1

Mafundisho yaliyofunuliwa ya Kanisa lililorejeshwa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho yanafundisha kwamba watoto wote wa Mungu—isipokuwa wachache sana kuwafikiria hapa—hatimaye watarithi mojawapo ya falme tatu za utukufu, hata falme ndogo zaidi kati yake “zinapita ufahamu wote.”2 Baada ya kipindi ambacho wasiotii wanateseka kwa ajili ya dhambi zao, mateso ambayo yanawatayarisha kwa yale yatakayofuata, wote watafufuliwa na kuendelea hadi kwenye Hukumu ya Mwisho ya Bwana Yesu Kristo. Hapo, Mwokozi wetu mwenye upendo, ambaye, tumefundishwa, “humtukuza Baba, na kuziokoa kazi zote za mikono yake,”3 atawaweka watoto wote wa Mungu kwenye mojawapo ya falme hizi za utukufu kulingana na matamanio yanayodhihirishwa kupitia chaguzi zao.

Fundisho lingine la kipekee na utendaji wa Kanisa lililorejeshwa ni amri na maagano yaliyofunuliwa ambayo yanawapa watoto wote wa Mungu fursa takatifu ya kufuzu daraja la juu zaidi la utukufu katika ufalme wa selestia. Hatma hiyo ya juu zaidi—kuinuliwa katika ufalme wa selestia—ndio lengo la Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Kutokana na ufunuo wa siku za leo, Watakatifu wa Siku za Mwisho wana ufahamu huu wa kipekee wa mpango wa Mungu wa furaha kwa watoto Wake. Mpango huo unaanza na maisha yetu kama roho kabla hatujazaliwa, na hufunua madhumuni na masharti ya safari yetu tuliyochagua katika maisha ya duniani na mwisho wetu tunaotamani baada ya hapo.

II.

Tunajua kutokana na ufunuo wa siku za leo kwamba “falme zote zina sheria iliyotolewa”4 na kwamba ufalme wa utukufu tunaopokea katika Hukumu ya Mwisho unaamuliwa na sheria tunazochagua kufuata katika safari yetu ya duniani. Chini ya mpango huo wa upendo, kuna falme nyingi—makao mengi—ili watoto wote wa Mungu warithi ufalme wa utukufu ambao sheria zake wanaweza bila shida “kuziishi.”

Tunapoelezea asili na mahitaji ya kila moja ya falme tatu katika mpango wa Baba, tunaanza na ya juu zaidi, ambayo ni lengo la amri takatifu na maagizo ambayo Mungu amefunua kupitia Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Katika utukufu wa “selestia”5 kuna daraja tatu,6 ambapo la juu zaidi ni kuinuliwa katika ufalme wa selestia. Haya ndiyo makao ya wale “waliopokea utimilifu wake na utukufu wake,” kwa hiyo, “wao ni miungu, wana [na binti] wa Mungu”7 na “wanakaa mbele za Mungu na Kristo milele na milele.”8 Kupitia ufunuo, Mungu amefunua sheria za milele, ibada, na maagano ambayo lazima yazingatiwe ili kukuza sifa za kiungu zinazohitajika ili kufikia uwezo huu mtakatifu. Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho linafokasi juu ya haya kwa sababu lengo la Kanisa hili lililorejeshwa ni kuwatayarisha watoto wa Mungu kwa ajili ya wokovu katika utukufu wa selestia na, zaidi hasa, kwa ajili ya kuinuliwa katika daraja la juu kabisa.

Mpango wa Mungu, uliojengwa juu ya ukweli wa milele, unahitaji kwamba kuinuliwa kunaweza kupatikana tu kupitia uaminifu kwa maagano ya ndoa ya milele kati ya mwanamume na mwanamke katika hekalu takatifu,9 ndoa ambayo hatimaye itapatikana kwa waaminifu wote. Hiyo ndiyo sababu tunafundisha kwamba “jinsia ni hulka muhimu ya utambuzi wa milele wa maisha kabla ya maisha ya duniani, maisha ya duniani na utambulisho na lengo la milele.”10

Mafundisho ya thamani ya kipekee ya kutusaidia kujitayarisha kwa ajili ya kuinuliwa ni tangazo kwa familia.11 Matamko yake yanafafanua mahitaji ambayo hututayarisha kuishi na Mungu Baba na Mwanawe, Yesu Kristo. Wale ambao hawauelewi kikamilifu mpango wa upendo wa Baba kwa ajili ya watoto Wake wanaweza kufikiria tangazo hili la familia kama maelezo ya sera ambazo zinapaswa kubadilishwa. Badala yake, tunathibitisha kwamba tangazo kwa familia, lililopatikana kutokana na mafundisho yasiyobadilika, linafafanua mahusiano ya familia ya duniani ambapo sehemu muhimu sana ya maendeleo yetu ya milele inaweza kutokea.

Mtume Paulo anaeleza falme tatu za utukufu, akizifananisha na utukufu wa jua, mwezi, na nyota.12 Anaiita ile ya juu kabisa “selestia” na ya pili ya “terestria.”13 Hataji ulio chini kabisa, lakini ufunuo kwa Joseph Smith uliongeza jina lake: “telestia.”14 Ufunuo mwingine pia unaeleza asili ya watu watakaopangiwa katika kila moja ya hizi falme za utukufu. Wale wasiochagua “kuitii sheria ya ufalme wa selestia”15 watarithi ufalme mwingine wa utukufu, mdogo kuliko ule wa selestia lakini unaofaa kwa sheria walizochagua na wanaweza bila shida “kuziishi.” Neno hilo kaa, ambalo ni la kawaida sana katika maandiko, linamaanisha mahali pa usalama.16 Kwa mfano, wale walio katika ufalme wa terestria—ukilinganisha na dhana maarufu kuhusu mbingu—“ndio wale wanaopokea uwepo wa Mwana, lakini si utimilifu wa Baba.”17 Walikuwa “watu wema duiani, ambao waliopofushwa na hila za wanadamu,”18 lakini “sio mashujaa katika ushuhuda wa Yesu.”19

Maelezo ya ufunuo ya wale waliowekwa kwenye falme za chini kabisa za utukufu, telestia, ni “yeye asiyeweza kuishi … utukufu wa terestria.”20 Hiyo inaelezea wale wanaomkataa Mwokozi na hawajazingatia mipaka ya kiungu kwenye tabia zao. Huu ndio ufalme ambao waovu hukaa, baada ya kuteswa kwa ajili ya dhambi zao. Hawa wanaelezewa katika ufunuo wa siku za leo kama “ndiyo wale ambao hawakuipokea injili ya Kristo, wala ushuhuda wa Yesu. …

“Hawa ndiyo wale waongo, na wachawi, na wazinzi, na makahaba, na yeyote apendaye na kufanya uwongo.”21

Akizungumzia falme tatu za utukufu na ono lake la kinabii, Rais Russell M. Nelson hivi karibuni aliandika: “Muda wa maisha ya mwanadamu ni kidogo tu ikilinganishwa na umilele. Lakini ni jinsi gani ulivyo muda mchache muhimu sana! Fikiria kwa makini jinsi inavyofanya kazi: Wakati wa maisha haya ya duniani unapata kuchagua ni sheria zipi uko tayari kutii—zile za ufalme wa selestia, au terestria, au telestia—na, kwa hivyo, katika ufalme gani wa utukufu utaishi milele. Ni mpango ulioje! Ni mpango ambao unaheshimu kabisa haki yako ya kujiamulia.”22

III.

Mtume Paulo alifundisha kwamba mafundisho na amri za Bwana zilitolewa ili kwamba sisi sote tupate “cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.”23 Mchakato huo unahitaji zaidi ya kupata maarifa. Haitoshi hata kusadikishwa kuhusu injili; lazima tutende ili tuongoke kwayo. Tofauti na mahubiri mengine, ambayo yanatufundisha kujua jambo fulani, injili ya Yesu Kristo inatupa changamoto ya kuwa kitu fulani.

Kutokana na mafundisho hayo tunahitimisha kwamba hukumu ya Mwisho si tu tathmini ya majumuisho ya matendo mema na mabaya—yale tuliyofanya. Inazingatia athari ya mwisho ya matendo na mawazo—kile ambacho tumekuwa. Tunastahili kupata uzima wa milele kupitia mchakato wa uongofu. Kama lilivyotumiwa hapa, neno hili lenye maana nyingi huashiria mabadiliko makubwa ya asili. Haitoshi tu kwa mtu kupitia wazo. Amri, ibada, na maagano ya injili siyo orodha ya amana inayohitajika kuwekwa kwenye akaunti fulani ya mbinguni. Injili ya Yesu Kristo ni mpango ambao hutuonyesha jinsi ya kuwa kile Baba yetu wa Mbinguni anatamani sisi tuwe.24

IV.

Kwa sababu ya Yesu Kristo na Upatanisho Wake, tunapokosea katika maisha haya, tunaweza kutubu na kujiunga tena na njia ya agano ambayo inaongoza kwenye kile ambacho Baba yetu wa Mbinguni anatamani kwa ajili yetu.

Kitabu cha Mormoni hufundisha kwamba maisha haya ndiyo wakati wa watu kujitayarisha kukutana na Mungu.”25 Lakini changamoto hiyo ya “maisha haya” ilitolewa muktadha wa tumaini (angalau kwa kiasi fulani kwa baadhi ya watu) kwenye yale ambayo Bwana alifunua kwa Rais Joseph F. Smith, ambayo sasa yameandikwa katika Mafundisho na Maagano sehemu ya 138. “Niliona,” nabii aliandika, “kwamba wazee waaminifu wa kipindi hiki, wakati wakiondoka kutoka maisha katika mwili wenye kufa, huendelea na kazi zao katika kuhubiri injili ya toba na ukombozi, kupitia dhabihu ya Mwana Pekee wa Mungu, miongoni mwa wale walio gizani, na chini ya utumwa wa dhambi katika ulimwengu mkuu wa roho za wafu.

“Wafu wanaotubu watakombolewa, kwa njia ya utii kwa ibada za nyumba ya Mungu,

“Na baada ya kulipia adhabu ya uvunjaji wao wa sheria, na kuoshwa safi, watapokea thawabu kulingana na matendo yao, kwa kuwa wao ni warithi wa wokovu.”26

Kwa kuongezea, tunajua kwamba Milenia, ile miaka elfu inayofuata Ujio wa Pili wa Mwokozi, itakuwa ni wakati wa kufanya ibada zinazohitajika kwa wale ambao hawajazipokea katika maisha yao ya duniani.27

Kuna mengi ambayo hatujui kuhusu vipindi vitatu vikuu katika mpango wa wokovu na uhusiano kati yao: (1) ulimwengu wa roho kabla ya kuzaliwa, (2) maisha ya duniani, na (3) maisha yanayofuata. Lakini tunajua kweli hizi za milele: “Wokovu ni jambo binafsi, lakini kuinuliwa ni jambo la famiia.”28 Tunaye Baba wa Mbinguni mwenye upendo ambaye atataka kwamba tupokee kila baraka na kila faida ambayo matamanio yetu na chaguzi zetu huruhusu. Pia tunajua kwamba Yeye hatamlazimisha mtu yeyote kuingia katika uhusiano wa kuunganishwa tofauti na mapenzi ya mtu huyo. Baraka za uhusiano wa kuunganishwa zimehakikishwa kwa wote wanaotii maagano yao lakini kamwe si kwa kulazimisha uhusiano wa kuunganishwa kwa mtu mwingine ambaye hana haki au hataki.

Akina kaka na akina dada, ninashuhudia kuhusu ukweli wa vitu hivi. Ninashuhudia juu ya Bwana wetu Yesu Kristo, “mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu,”29 ambaye Upatanisho wake, chini ya mpango wa Baba yetu wa Mbinguni, unawezesha yote, katika jina la Yesu Kristo, amina.