Mkutano Mkuu
Sifa kwa Aliyenena na Bwana
Mkutano mkuu wa Oktoba 2023


Sifa kwa Aliyenena na Bwana

Ni kwa kiasi gani tumebarikiwa kujua yote tunayoyajua kwa sababu tunaye Joseph Smith, nabii wa kipindi hichi cha mwisho cha utimilifu wa nyakati.

Wapendwa akina kaka na akina dada, ni heshima kuwa nanyi asubuhi hii ya leo. Ninaomba kwamba Bwana atanibariki.

Macho yangu si kama yalivyokuwa hapo awali. Nilikwenda na kumuona daktari wa macho, na kusema “siwezi kuona mashine ya kusomea.”

Na akasema, “Sawa, macho yako yamezeeka. Hayatabadilika.”

Hivyo nitafanya kwa kadiri ya uwezo wangu.

Ningependa kushiriki nanyi baadhi ya vitu ambavyo vimekuwa mawazoni mwangu. Nimetokea kuwa na Nabii Joseph katika mawazo yangu kwa miezi kadhaa iliyopita. Nimekaa na kutafakari jukumu lake takatifu la kuwa nabii wa wakati huu, wa utimilifu wa nyakati.

Nafikiria ni jinsi gani tulivyo na shukrani kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kwamba Joseph Smith, mvulana ambaye alitamani kujua kile alichotakiwa kufanya ili dhambi zake zisamehewe, alipata ujasiri wa kwenda kwenye kijisitu karibu na nyumbani kwake huko Palmyra, New York, na huko alipiga magoti na kusali, na—kwa maneno yake mwenyewe—kusali kwa sauti kwa mara ya kwanza (ona Joseph Smith—Historia ya 1:14).

Katika tukio hilo, wakati Joseph akiwa amepiga magoti mahali ambapo tunapaita Kijisitu Kitakatifu, mbingu zilifunguka. Watu wawili, wenye mng’aro zaidi ya jua la mchana, walimtokea. Mmoja wao alizungumza naye akisema, “[Joseph,] Huyu ni Mwanangu Mpendwa. Msikilize Yeye!” (Joseph Smith—Historia ya 1:17). Hivyo ukaanza Urejesho wa utimilifu wa injili isiyo na mwisho ya Yesu Kristo.

Kwa sababu Yesu, Mwokozi na Mkombozi wetu, alizungumza na mvulana Jospeh na kufungua utimilifu wa wakati huu ambao sasa tunaishi, tunaimba, “Sifa kwa Aliyenena na Bwana!” (“Sifa kwa Aliyenena na Bwana,” Nyimbo za Dini, na. 17). Tunamshukuru Bwana kwa ajili ya Joseph Smith na kwa ujasiri wake wa kwenda kwenye kijisitu mnamo 1820, karibu na nyumbani kwake huko Palmyra, New York.

Nimekuwa nikitafakari vitu vyote vya kushangaza ambavyo tunavijua na vyote ambavyo tunavyo. Wapenda akina kaka na dada zangu, ushuhuda wangu kwenu asubuhi hii ni kuhusu jinsi ambavyo tumebarikiwa kwa wingi kujua vyote tujuavyo kwa sababu ya Joseph Smith, nabii wa wakati huu wa mwisho wa utimilifu wa nyakati.

Tunao uelewa wa dhumuni la maisha, uelewa wa sisi ni nani.

Tunajua Mungu ni nani; tunajua Mwokozi ni nani, kwa sababu tunaye Joseph, ambaye alikwenda kwenye kijisitu kama mvulana, akitafuta msamaha wa dhambi zake.

Nadhani ni moja ya vitu vitukufu na vizuri ambavyo mtu yeyote ulimwenguni anaweza kujua—kwamba Baba yetu wa Mbinguni na Bwana Yesu Kristo Wamejionesha Wenyewe katika siku hizi za mwisho na kwamba Joseph alikuzwa ili kurejesha utimilifu wa injili isiyo na mwisho ya Yesu Kristo.

Tuna kitabu cha Mormoni. Kitabu cha Mormoni ni zawadi ya kupendeza na ya kustaajabisha kiasi gani kwa uumini wa Kanisa. Ni ushahidi mwingine, ushuhuda mwingine kwamba Yesu ndiye Kristo. Tunacho kwa sababu Joseph alikuwa mstahiki wa kwenda na kuchukua bamba, alipata msukumo wa kimbingu kuzitafsiri kwa kipawa na nguvu za Mungu na kukileta kitabu ulimwenguni.

Ingawa ujumbe wangu asubuhi hii ni rahisi, ni wa kina, na umejaa upendo kwa sababu ya Nabii Joseph Smith na kwa wale wote, akina kaka na dada zangu, ambao wamemuunga mkono na walikuwa tayari kumuunga mkono kwenye ujana wake.

Ningependa kutoa shukrani asubuhi hii kwa mama yake. Mara zote nimekuwa nikiwaza jinsi ilivyokuwa ya kupendeza wakati Joseph alipotoka kupitia uzoefu huo kwenye Kijisitu Kitakatifu na kumwambia mama yake kile ambacho kilitokea, Lucy Mack Smith alimwamini.

Nina shukrani kwa baba yake na kaka na dada zake na familia yake, ambao walimuunga mkono kwenye jukumu hili kubwa ambalo Bwana aliliweka juu yake la kuwa nabii ili kurejesha utimilifu wa injili ya Yesu Kristo mara nyingine tena duniani.

Kwa hiyo ushuhuda wangu asubuhi ya leo ni kwamba ninajua Yesu Kristo ndiye Mwokozi na Mkombozi wa ulimwengu. Pia ninajua kwamba Baba yetu wa Mbinguni na Bwana Yesu Kristo walimtokea na kuzungumza na Joseph Smith na kumuandaa ili awe nabii.

Ninashangazwa na naamini ni vivyo hivyo kwa wengi wenu, juu ya jinsi gani ambavyo tumebarikiwa kujua kile tunachokijua na kujua kuhusu dhumuni letu kwenye maisha, kwa nini tuko hapa, kipi tunatakiwa kujitahidi kukifanya na kukikamilisha kwenye maisha yetu ya kila siku. Tuko kwenye mchakato wa kujaribu kujiandaa, siku hadi siku, kuwa bora zaidi, wakarimu zaidi, waliojiandaa zaidi kwa ajili ya siku ile, ambayo kwa hakika itakuja, ambapo tutapita kwenye uwepo wa Baba yetu wa Mbinguni na Bwana Yesu Kristo.

Siku hiyo inasonga karibu sana kwangu mimi. Karibuni nitakuwa na miaka 95. Watoto wangu wananiambia wanadhani nimekuwa mzee zaidi kuliko baadhi ya siku, lakini hiyo ni SAWA. Ninafanya kadiri niwezavyo.

Lakini kwa takribani miaka 50, akina kaka na akina dada, nimekuwa na fursa ya kutembelea ulimwengu nikiwa kwenye jukumu langu kama Kiongozi Mkuu mwenye mamlaka wa Kanisa. Imekuwa ni baraka ya kupendeza. Nadhani nimefika karibu sehemu zote za ulimwengu. Nimekutana na waumini wa Kanisa ulimwenguni kote.

Oo, ni jinsi gani ninawapenda. Imekuwa ni uzoefu mtukufu kiasi gani—kutazama nyuso zenu, kuwa kwenye uwepo wenu, na kuhisi upendo wenu ambao mnao kwa Bwana na kwa Urejesho wa injili ya Yesu Kristo.

Na Baba yetu wa Mbinguni atulinde sasa na kubariki matangazo yote ya mkutano. Na tuwe na Roho wa Bwana kikamilifu mioyoni mwetu, na upendo wetu wa injili ya Yesu Kristo—Mwokozi wetu mpendwa, Bwana Yesu Kristo—uongezeke kadiri tunavyojitahidi kumtumikia Yeye na kushika amri Zake na kuwa zaidi kama Yeye kama matokeo ya uhudhuriaji wetu kwenye mkutano mkuu. Popote pale mlipo katika ulimwengu huu, Mungu awabariki. Na Roho wa Bwana awe nasi. Na tuhisi nguvu za mbinguni wakati tukiabudu kwa pamoja kwenye kikao hiki cha mkutano.

Ninawaachia ushahidi wangu na ushuhuda kwamba ninajua Yesu ndiye Kristo. Yeye ni Mwokozi wetu, Mkombozi wetu. Ni rafiki yetu wa kweli. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.