2010
Baraka za Hekalu
Oktoba 2010


Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Oktoba 2010

Baraka za Hekalu

Hekalu linatupatia dhamira kwa maisha yetu. Linaleta amani kwa nafsi zetu—sio amani inayopeanwa na watu bali amani iliyoahaidiwa na Mwana wa Mungu aliposema, “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa.”

Katika hekalu tunaweza kuhisi karibu na Bwana

Nafikiri hakuna sehemu duniani ambapo nahisi nikiwa karibu na Bwana zaidi ya kuwa katika moja ya hekalu zake. Ili kufafanua shairi:

Mbinguni ni mbali kiasi gani?

Si mbali sana

Katika mahekalu ya Mungu,

Ni hapa mahali tulipo.

Bwana alisema:

“Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba:

“Bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi;

“Kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwa na moyo wako.”1

Kwa washiriki wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku Za Mwisho, Hekalu ndiyo sehemu takatifu zaidi duniani. Ndiyo nyumba ya Bwana, na kama vile mchoro wa muhuri kwenye nje ya hekalu inavyosema, hekalu ni “utakatifu kwa Bwana.”

Hekalu hutufariji na kutuinua

Katika hekalu, mpango wa thamani wa Mungu unafundishwa. Ni katika hekalu ambapo maagano ya milele yanafanywa. Hekalu hutufariji na kutuinua, linasimama kama mnara kwa wote kuona, na kutuelekeza kwenye utukufu wa selestia. Ni nyumba ya Mungu. Yote yanayofanyika ndani ya kuta za hekalu yanatia moyo ma kuvutia.

Hekalu ni la familia, moja ya hazina kuu tulionayo duniani. Bwana ameongea kwa udhahiri nasi akina baba,3 akitueleza kwamba tuna jukumu la kupenda wake zetu kwa mioyo yetu yote na kuwasaidia pamoja na watoto wetu. Ameelezea kwamba kazi kuu zaidi ambao sisi wazazi tunaweza kufanya inafanywa katika nyumba zetu, na nyumba zetu zinaweza kuwa mbinguni, haswa wakati ndoa zetu zimefunganishwa katika nyumba ya Mungu.

Marehemu Mzee Matthew Cowley, aliyekuwa mshiriki wa Jamii ya Wale Mitume Kumi na Wawili, aliwahi kusimulia tukio la Jumamosi jioni kama babu akishikilia mkono alimpeleka bintiye mdogo mjukuu kwenye matembezi ya siku ya kuzaliwa—sio kwenye hifadhi ya wanyama pori au kwenye maonyesho ya sinema bali kwenye bustani ya hekalu. Kwa ruhusa ya mlinda bustani, hao wawili watembea kwenye milango mikubwa ya hekalu. Alidokeza kwamba aiweke mikono yake kwenye kuta thabiti halafu kwenye mlango mkubwa. Kwa upendo alimwambia, “Kumbuka kwamba siku hii umegusa hekalu. Siku moja utaingia ndani.” Zawadi yake kwa mdogo huyu haikuwa peremende wala aiskrimu bali tukio muhimu zaidi na la kudumu—kujifahamisha nyumba la Bwana. Alikuwa amegusa hekalu, na hekalu likawa limemgusa.

Hekalu linaleta amani kwa nafsi zetu

Tunavyogusa hekalu na kupenda hekalu, maisha yetu yataonyesha1 imani yetu. Tunavyoenda kwenye nyumba takatifu, tunavyokumbuka maagano tunayoweka humo ndani, tutaweza kustahimili kila jaribio na kushinda jaribio. Hekalu linapeana dhamira kwa maisha yetu. Linaleta amani kwa nafsi zetu—sio amani inayopeanwa na watu bali amani iliyoahaidiwa na Mwana wa Mungu aliposema, “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa: niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.”2

Kuna imani kubwa miongoni mwa Watakatifu wa Siku za Mwisho. Bwana anatupatia fursa ili kuona ikiwa tutafuata sheria Zake, ikiwa tutafuata njia ambayo Yesu wa Nazareti alifuata, ikiwa tutampenda Bwana kwa moyo wetu wote, uwezo, akili na nguvu, 1 na kuwapenda majirani zetu kama sisi wenyewe.3

Naamini katika mithali “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe. Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.”4

Hivyo ndivyo ilivyo; hivyo ndivyo itakavyokuwa. Ikiwa tutatenda jukumu letu na kutumaini kamili katika Bwana, tutajaza mahekalu Yake, sio tu kwa kufanya kazi yetu ya agizo, bali pia kupata fursa ya kuwafanyia wengine kazi. Tutapiga magoti kwenye madhabahu takatifu ili kuweza kuwa wakala katika mifunganisho ambayo inaunganisha waume na wake na watoto kwa milele yote. Vijana wastahilifu na wasichana wenye umri wa miaka 12 wanaweza kuwa wakala kwa wale waliokufa bila baraka ya ubatizo. Hii inaweza kuwa mapenzi ya Baba yetu wa Mbinguni kwako na kwangu.

Miujiza ulitendeka

Miaka mingi iliyopita, babu mwaminifu na mnyenyekevu, Ndugu Percy K. Fetzer, aliitwa ili kupeana baraka za babu kwa washiriki wa Kanisa wanaoishi nyuma ya Pazia la Chuma.

Ndugu Fetzer alienda katika nchi ya Poland wakati huo wa siku za giza. Mipaka ilifungwa, na hakuna raia wowote walioruhusiwa kuondoka. Ndugu Fetzer alikutana na Watakatifu Wajerumani waliokuwa wamefungiwa pale wakati mipaka ilipobadilishwa kufuatia Vita Vya Pili vya Dunia na nchi ambako walikuwa wanaishi ilikuwa sehemu ya Poland.

Kiongozi wetu miongoni mwa Watakatifu hao Wajerumani alikuwa Ndugu Eric P. Konietz, aliyeishi huko pamoja na mkewe na watoto. Ndugu Fezter aliwapa Ndugu na Dada Konietz na watoto wazima baraka za babu.

Wakati Ndugu Fetzer aliporudi Marekani, alipiga simu na kuuliza ikiwa angekuja kunitembelea. Alivyoketi afisini mwangu, alianza kulia. Alisema, “Ndugu Monson, nilivyoweka mikono yangu juu ya vichwa vya wanafamilia wa Konietz, nilifanya ahadi ambazo haziwezi kutimizwa. Niliahidi Ndugu na Dada Konietz kwamba wataweza kurudi kwenye nchi yao ya asili ya Ujerumani, kwamba hawatakuwa wafungwa wa maamuzi dhalimu wa kuteka mataifa na kwamba watafunganishwa pamoja kama familia katika nyumba ya Bwana. Niliahidi mwanawe kwamba ataenda misheni, na niliahidi bintiye kwamba ataoleka katika hekalu takatifu ya Mungu. Wewe na mimi tunajua kwamba kwa sababu ya mipaka iliofungwa, hawataweza kupokea utimizo wa baraka hizo. Nimefanya nini?”

Nilisema, “Ndugu Fetzer, nakujua vyema kutosha kujua kwamba umefanya yale ambayo Baba yetu wa Mbinguni alitaka ufanye.” Tulipiga magoti chini kando ya meza yangu na kuomba kwa Baba yetu wa Mbinguni, tukielezea kwamba ahadi zilikuwa zimepeanwa kwa familia takatifu kuhusu hekalu la Mungu na baraka zingine ambazo sasa wamenyimwa. Ni Yeye tu angewezesha miujiza tuliohitaji.

Miujiza ulitendeka. Mkataba ulitiwa sahihi na viongozi wa serikali ya Poland na viongozi wa Taifa ya Shirikisho ya Ujerumani, unayowaruhusu wenyeji wa Ujerumani waliokwama katika eneo hilo ili kuenda Ujerumani Magharibi, na Ndugu Konietz akawa askofu wa kata ambako waliishi.

Familia yote ya Konietz ilienda kwenye hekalu takatifu huko Switzerland. Na ni nani aliyekuwa rais wa hekalu aliyewasalimia akivalia suti nyeupe kwa mikono wazi? Sio mwingine ila Percy Fetzer—babu aliyewapa ahadi. Sasa, katika cheo chake kama rais wa hekalu ya Bern Switzerland, aliwaalika katika nyumba ya Bwana, kwa utimizo wa ahadi ile, na kufunganisha mume na mke pamoja na watoto kwa wazazi wao.

Binti kijana hatimaye aliolewa katika nyumba ya Bwana. Kijana mdogo alipokea mwito wake na kutimiza misheni ya muda wote.

“Tutakuona hekaluni!”

Kwa wengine wetu, safari yetu kwenda hekaluni ni karibu. Kwa wengine, kuna bahari ya kuvuka na maili za kuenda kabla hawajaingia hekalu takatifu la Mungu.

Miaka michache iliopita, kabla ya kumalizika kwa hekalu la Afrika Kusini, nikihudhuria mkutano mkuu wa wilaya kwa kile kilichokuwa mbeleni Salisbury, Rhodesia, nilikutana na rais wa wilaya, Reginald J. Nield. Yeye pamoja na mabinti zake warembo walikutana nami nilipokuwa nikiingia kanisani. Waliniambia kwamba walikuwa wakihifadhi pesa zao na walikuwa wakijitayarisha kwa siku ambapo watasafiri kwenda kwa hekalu la Bwana. Lakini, aha, hekalu lilikuwa mbali sana.

Mwisho wa mkutano, mabinti wanne warembo waliniuliza maswali kuhusu hekalu: “Hekalu linafananaje? Yote ambayo tumeona ni picha.” “tutahisije tutakapoingia hekaluni?” “Ni nini tutakachokumbuka zaidi?” kwa kadri ya saa moja nilikuwa na fursa ya kuongea na mabinti wane kuhusu nyumba ya Bwana. Nilivyoondoka kuelekea uwanja wa ndege, walinipungia mikono, na binti mdogo alisema alisema, “Tutakuona hekaluni!”

Mwaka moja baadaye nilipata fursa ya kuwasalimia familia ya Nield katika Hekalu la Salt Lake. Katika chumba cha amani cha ufunganisho nilikuwa na fursa ya kuwaunganisha kwa milele, vile vile kwa muda. Ndugu na Dada Nield. Milango ilifunguliwa, na wale mabinti warembo, kila mmoja amevalia mavazi meupe yasiyo madoadoa, wakaingia chumbani. Wakamkumbatia mama, halafu baba. Machozi yalikuwa kwenye macho yao, na shukrani ikawa katika moyo wao. Tulikuwa karibu na mbinguni. Vyema kila mmoja angeweza kusema, “Sasa tu familia milele.”

Hii ni baraka ya ajabu inayowasubiri wale wanaokuja hekaluni. Acha kila mmoja wetu aishi maisha yanayostahili, kwa mikono misafi na mioyo safi, ili kwamba hekalu iweze kugusa maisha yetu na familia yetu.

Mbinguni ni mbali kiasi gani? Nashuhudia kwamba katika hekalu takatifu sio mbali kamwe—kwani ni katika sehemu hizi takatifu ambako mbinguni na ardhi zinakutana na Baba wetu wa Mbinguni anawapatia watoto Wake baraka zake kuu.