2011
Njoo Hekaluni na Udai Baraka Zako
Julai 2011


Ujumbe wa Mwalimu Mtembelezi, Julai 2011

Njoo Hekalu na Udai Baraka Zako

Soma kifaa hiki, na kama ifaavyo, ukijadili pamoja na kina dada unaowatembelea. Tumia maswali ili kukusaidia kuwaimarisha dada zako na kuufanya Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama kuwa sehemu hai ya maisha yako mwenyewe.

Imani • Familia • Usaidizi

Kina dada, tumebarikiwa sana. Mwokozi Anasimama kwenye kichwa cha Kanisa hili. Tunaongozwa na manabii wanaoishi. Tunayo maandiko matakatifu. Na tuna mahekalu mengi matakatifu ulimwenguni kote ambako tunaweza kupokea maagizo muhimu ili kutusaidia kurudi kwa Baba yetu wa Mbinguni.

Tunaenda hekaluni kwanza kwa ajili yetu wenyewe. “Dhamira ya msingi ya hekalu,” alifafanua Mzee Robert D. Hales wa Jamii ya wale Mitume Kumi na Wawili, “ni kupeana maagizo muhimu kwa ajili ya kuinuliwa kwetu katika ufalme wa selestia. Maagizo ya hekalu hutuelekeza kwa Mwokozi wetu na kutupatia baraka zinazotujia kupitia kwa Upatanisho wa Yesu Kristo. Mahekalu ni chuo kikuu cha kujifunza kinachofahamika na mwanadamu, kinachotupa ujuzi na hekima juu ya Uumbaji wa ulimwengu. Maagizo ya endaumenti yanapeana mwongozo jinsi tunavyopaswa kuishi maisha yetu hapa duniani. … Ibada hiyo inajumuisha mfuatano wa maagizo kuhusu jinsi tunavyopaswa kuishi na maagano tunayofanya ili kuishi kitakatifu kwa kumfuata Mwokozi wetu.1

Lakini huduma yetu ya hekalu haikomei hapo. Rais Boyd K. Packer, Rais wa Jamii ya Mitume wale Kumi na Wawili, alifundisha: “Kutumika kama wakala wa mtu ambaye amekufa, utakuwa umetekeleza maagano uliyoweka. Utakuwa umeimarisha akilini mwako baraka kuu za kiroho zinazohusiana na nyumba ya Bwana. … Katika maagano na maagizo kunayo baraka unazoweza kudai katika hekalu takatifu.”2

Njoo hekaluni halafu uje tena. Kufanya na kutimiza maagano ya hekalu kutatutayarisha kwa baraka kuu zaidi zote—uzima wa milele.

Barbara Thompson, Mshauri wa Pili katika urais mkuu wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama

Kutoka kwa Maandiko

Isaya 2:3; 1 Wakorintho 11:11; Ufunuo 7:13–15; Maandiko na Maagano 109

Kutoka kwa Historia Yetu

Nabii Joseph aliongea kila mara na kina dada wa Muungano wa Usaidizi wa kina mama katika mikutano yao. Hekalu la Nauvoo likiwa katika ujenzi, Nabii aliwafunza kina dada mafundisho, akiwatayarisha kupokea ujuzi mwingi kupitia kwa maagizo ya hekalu. Mnamo 1842 alimwambia Mercy Fielding Thompson kuwa endaumenti “itakuondoa gizani hadi kwa nuru ya ajabu.”3

Takribani Watakatifu wa Siku za Mwisho 6,000 walipokea maagizo ya hekalu kabla ya kutoka Nauvoo. Rais Brigham Young (1801–77) alisema, “Hivyo ndivyo imekuwa hamu uliodhihirishwa na watakatifu ili kupokea maagizo[ya hekalu], na ndivyo ilivyo hamu upande wetu wa kuwahudumia, kwa sababu hiyo nimejitolea mhanga kwa kazi ya Bwana katika Hekalu usiku na mchana, bila kulala zaidi ya masaa manne, kwa kadiri, kila siku, na kuenda nyumbani mara moja kwa wiki.4 Uwezo na nguvu za maagano za hekalu ziliwaimarisha Watakatifu walivyoacha mji wao na hekalu kwa safari pasipojulikana.

Muhtasari

  1. Robert D. Hales, “Blessings of the Temple,” Liahona, Oct. 2009, 14.

  2. Boyd K. Packer, The Holy Temple (1980), 170, 171.

  3. Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith (2007), 451.

  4. Teachings of Presidents of the Church: Brigham Young (1997), 299

Ninaweza Kufanya Nini?

  1. Ni uzoefu gani nitakayoshiriki ili kuimarisha wale ninaowatembelea katika kauli yao ili “waje hekaluni”?

  2. Nawezaje kibinafsi kudai baraka za hekalu?