2018
Ushiriki wa Akina Dada katika Kukusanya Israeli
Novemba 2018


Picha
ministering

Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Novemba 2018

Ushiriki wa Akina Dada katika Kukusanya Israeli

Ninatoa ombi la kinabii kwenu, wanawake wa Kanisa, kupanga wakati ujao kwa kusaidia kukusanya Israeli iliyotawanyika.

Ni jambo la kupendeza kuwa nanyi, dada zangu wapendwa na wenye thamani. Pengine tukio la hivi karibuni litawapa uzoefu wa jinsi ninavyohisi kuhusu ninyi na uwezo wa kiungu mliobarikiwa nao.

Siku moja wakati nikizungumza katika mkutano huko Amerika ya Kusini, nilipata hisia za kusisimua sana kuhusu mada yangu, na katika wakati muhimu, nilisema, “Kama mama wa watoto 10, ninaweza kuwaambia kwamba …” Na kisha nikaendelea kumalizia ujumbe wangu.

Sikuwa nimetambua nilisema neno mama. Mtafsiri wangu, akidhani nilikuwa nimekosea, alibadilisha neno mama kuwa baba, hivyo mkutano kamwe haukujua kwamba nilijitaja mimi kama mama. Lakini mke wangu Wendy alisikia, na alipendezwa sana na kuteleza ulimi kwangu.

Katika wasaa ule, shauku kubwa ya moyo wangu kuleta tofauti ulimwenguni—kama vile mama pekee anavyofanya—iliongezeka kutoka moyoni mwangu. Kwa miaka mingi, kila mara ninapoulizwa kwa nini nilichagua kuwa daktari, jibu langu daima limekuwa moja: “Kwa sababu nisingeweza kuchagua kuwa mama.”

Tafadhali kumbukeni kwamba kila wakati ninapotumia neno mama, sizungumzi tu kuhusu wanawake ambao wamezaa au wameasili watoto katika maisha haya. Ninazungumza kuhusu mabinti wote wakubwa wa Wazazi wetu wa Mbinguni. Kila mwanamke ni mama kwa wema wa asili yake takatifu ya milele.

Hivyo usiku huu, kama baba wa watoto 10—mabinti tisa na mwana mmoja—na kama Rais wa Kanisa, ninaomba kwamba mtahisi jinsi gani ninahisi kuhusu ninyi—kuhusu ninyi ni kina nani na yote mazuri mnayofanya. Hakuna anayeweza kufanya kile mke mwema anachoweza kufanya. Hakuna anayeweza kutoa nakala ya ushawishi wa mama.

Wanaume wanaweza na mara nyingi wanaonyesha upendo wa Baba wa Mbinguni na Mwokozi kwa wengine. Lakini wanawake wana kipawa maalumu kwa hilo—endaumenti takatifu. Ninyi mna uwezo wa kuhisi kile mtu fulani anahitaji—na wakati gani wanakihitaji. Mnaweza kumfikia, kumfariji, kumfundisha, na kumuimarisha mtu katika muda wake hasa wa uhitaji.

Wanawake wanaona mambo kitofauti kuliko wanaume, na ee, ni jinsi gani tunahitaji mtazamo wenu! Uhalisia wenu unawaongoza kuwafikiria wengine kwanza, kufikiria athari ambayo tendo lolote litaleta kwa wengine.

Kama vile Rais Eyring alivyosema, Ilikuwa ni Mama yetu mtukufu Hawa—na maono yake ya mbali ya mpango wa Baba yetu wa Mbinguni—ambaye alianzisha kile tunachoita “Anguko.” Uchaguzi wake wa hekima na ujasiri na uamuzi wa kuunga mkono wa Adamu vilisogeza mbele mpango wa Mungu wa furaha. Walifanya iwezekane kwa kila mmoja wetu kuja duniani, kupata mwili, na kuthibitisha kwamba tungechagua kusimama kwa ajili ya Yesu Kristo sasa, kama tulivyofanya kabla ya kuja duniani.

Dada zangu wapendwa, mna vipawa vya kiroho na hulka za kipekee. Usiku huu ninawasihi, kwa tumaini lote la moyo wangu, kuomba ili kuvielewa vipawa vyenu vya kiroho—kuviendeleza, kuvitumia, na kuvikuza, hata zaidi ya mlivyowahi kufanya. Mtabadilisha ulimwengu mnapofanya hivyo.

Kama wanawake, mnawapa msukumo wengine kuweka kiwango kinachofaa kuigwa. Acha niwape historia kidogo juu ya matangazo makubwa mawili yaliyotolewa katika mkutano wetu mkuu uliopita. Ninyi, dada zangu wapendwa, mlikuwa muhimu kwa kila moja.

Kwanza, kuhudumu. Kiwango cha juu cha kuhudumu ni kile cha Mwokozi wetu,Yesu Kristo. Kwa kawaida, wanawake ni, na daima wamekuwa, karibu na kiwango hicho kuliko wanaume. Mnapohudumu kwa dhati, mnafuata hisia zenu kumsaidia mtu mwingine kupata uzoefu zaidi wa upendo wa Mwokozi. Hamu ya kutoa huduma ni muhimu kwa wanawake wema. Ninawajua wanawake wanaosali kila siku, “Ni nani Ungependa nimsaidie leo?”

Kabla ya tangazo la Aprili 2018 kuhusu njia kuu na takatifu ya kuwatunza wengine, tabia ya baadhi ya wanaume ilikuwa ni kuwekea vema jukumu lao la mafundisho ya nyumbani kama “limefanyika” na kusonga mbele na kazi nyingine.

Lakini ninyi mlipohisi kwamba dada mliyekuwa mkimfanyia mafundisho ya kutembelea alihitaji msaada, mliitikia haraka na kisha kwa mwezi mzima. Hivyo, ilikuwa ni jinsi mlivyofundisha kwa kutembelea ambako kulishawishi kusogea kwetu juu kwenye kuhudumu.

Pili, katika mkutano mkuu uliopita, tulipanga pia upya akidi za Ukuhani wa Melkizedeki. Tulipopambana na jinsi ya kuwasaidia wanaume wa Kanisa kuwa wafanisi zaidi katika majukumu yao, kwa umakini tulizingatia mfano wa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama.

Katika Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama, wanawake katika umri na hatua tofauti za maisha hukutana pamoja. Kila muongo wa maisha huleta changamoto za kipekee, na bado, mlikuwepo wiki baada ya wiki, mkijumuika pamoja, mkikua na kufundisha injili pamoja, na kuleta tofauti halisi ulimwenguni.

Sasa, kufuatia mfano wenu, wenye ukuhani wa Melkizedeki ni washiriki wa akidi ya wazee. Wanaume hawa wanajumuisha umri kuanzia 18 mpaka 98 (au zaidi), na mjumuisho wa pamoja wa ukuhani na uzoefu wa Kanisa. Akina kaka hawa sasa wanatengeneza muunganiko imara wa kindugu, wanajifunza pamoja, na kubariki wengine kwa ufanisi zaidi.

Kama mnavyokumbuka Juni iliyopita, Dada Nelson nami tulizungumza na vijana wa Kanisa. Tuliwaalika wajiandikishe kwenye batalioni ya vijana ya Bwana kusaidia kukusanya Israeli pande zote za pazia. Ukusanyaji huu ni “changamoto kuu, kusudi kuu, na kazi kuu duniani leo!1

Ni kusudi ambalo linawahitaji sana wanawake, kwa sababu wanawake wanaupanga wakati ujao. Hivyo, usiku huu ninatoa ombi la kinabii kwenu, wanawake wa kanisa, kupanga wakati ujao kwa kusaidia kukusanya Israeli iliyotawanyika.

Wapi mnaweza kuanzia?

Ninatoa mialiko minne:

Kwanza, ninawaalika mshiriki katika mfungo wa siku‑10 kuepuka mitandao ya kijamii na chombo chochote cha habari ambacho huleta mawazo hasi na yasiyo safi kwenye akili yako. Sali kujua ni ushawishi gani uondoe wakati wa mfungo wako. Matokeo ya mfungo wako wa siku‑10 yanaweza kukushangaza. Ni nini unagundua baada ya kuchukua likizo kutoka kwenye mitazamo ya ulimwengu ambayo imekua ikijeruhi roho yako? Je, kuna badiliko katika wapi sasa unataka kutumia muda na nguvu zako? Je, kuna chochote kati ya vipaumbele vyako ambavyo vimebadilika—hata kidogo tu? Ninawasihi kuandika na kukamilisha jukumu kwa kila msukumo.

Pili, ninawaalika kusoma Kitabu cha Mormoni kati ya sasa na mwisho wa mwaka. Kama isivyowezekana jinsi hilo linavyoweza kuonekana pamoja na yote mnayojaribu kufanikisha katika maisha yenu, kama mtakubali mwaliko huu kwa lengo kamili la moyo, Bwana atawasaidia kupata njia ya kulifanikisha. Na, mnapojifunza kwa maombi, ninaahidi kwamba mbingu zitakufungukieni. Bwana atawabariki kwa ongezeko la msukumo na ufunuo.

Mnaposoma, ningewatia moyo kuwekea alama kila mstari ambao unamzungumzia au kumtaja Mwokozi. Kisha, kuwa na makusudi ya kuzungumza kuhusu Kristo, kufurahi katika Kristo, kuhubiri kuhusu Kristo pamoja na familia na rafiki zako.2 Wewe na wao mtavutwa karibu na Mwokozi kupitia mchakato huu. Na mabadiliko, hata miujiza, vitaanza kutokea.

Asubuhi hii tangazo lilitolewa kuhusu ratiba mpya ya Jumapili na mtaala unaolenga‑nyumbani, unaosaidiwa na‑Kanisa. Nyinyi, dada zangu wapendwa, ni wa muhimu kwenye mafanikio ya juhudi hii mpya, ya ufundishaji wa‑injili ‑iliyo na usawa. Tafadhali wafundisheni wale mnaowapenda kile mnachojifunza kutoka kwenye maandiko. Wafundisheni jinsi ya kumgeukia Mwokozi kwa nguvu Yake ya uponyaji na utakaso wakati wanapofanya dhambi. Na wafundisheni jinsi ya kuvuta nguvu Yake ya uimarisho kila siku ya maisha yao.

Tatu, jenga mpangilio wa kuhudhuria hekaluni mara kwa mara. Hili linaweza kuhitaji zaidi dhabihu katika maisha yenu. Muda wa kila mara hekaluni utamruhusu Bwana kukufundisha jinsi ya kuvuta nguvu Zake za ukuhani ambazo kwazo mmepewa endaumenti ndani ya hekalu Lake. Kwa wale ambao hawaishi karibu na hekalu, ninawaalika kujifunza kwa maombi kuhusu mahekalu katika maandiko na katika maneno ya manabii wanaoishi. Tafuta kujua zaidi, kuelewa zaidi, kuhisi zaidi kuhusu mahekalu kuliko ulivyowahi hapo awali.

Katika mkutano wetu wa vijana ulimwenguni kote Juni iliyopita, nilimzungumzia kijana mdogo ambaye maisha yake yalibadilika pale wazazi wake walipobadilishana simu janja yake kwa simu ndogo ya kufunua. Mama wa kijana huyu mdogo ni mwanamke jasiri wa imani. Alimuona mwanawe akivutwa kuelekea chaguzi ambazo zingemzuia kutumikia misheni. Alipeleka maombi yake hekaluni ili kujua njia nzuri ya kumsaidia mwanawe. Kisha alikamilisha jukumu kwa kila msukumo.

Alisema: “Nilihisi Roho akiniongoza kukagua simu ya mwanangu katika muda maalum kupata vitu maalum. Sijui jinsi ya kutumia hizi simu janja, lakini Roho aliniongoza kupitia mitandao yote ya kijamii ambayo hata siitumii! Ninajua Roho anawasaidia wazazi wanaotafuta mwongozo wa kuwalinda watoto wao. [Mwanzoni] mwanangu alikuwa na hasira na mimi. … Lakini baada ya siku tatu tu, alinishukuru! Aliweza kuhisi tofauti.”

Tabia na mtazamo wa mwanawe vilibadilika ghafla. Alikuwa msaada mkubwa nyumbani, alitabasamu zaidi, na alikuwa msikivu zaidi kanisani. Alifurahia kutumikia kwa muda katika ubatizo hekaluni na kujiandaa kwa ajili ya misheni yake.

Mwaliko wangu wa nne, kwenu ninyi ambao umri umefika, ni kushiriki kikamilifu katika Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama. Ninawasihi kujifunza kauli ya sasa yenye lengo la Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama. Inaleta msukumo. Inaweza kukuongoza katika kutengeneza kauli yako mwenyewe yenye lengo kwa ajili ya maisha yako mwenyewe. Ninawasihi pia kufurahia kweli katika tangazo la Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama lililochapishwa takriban miaka 20 iliyopita.3 Nakala yenye fremu ya tangazo hili inaning’inia ukutani ndani ya ofisi ya Urais wa Kwanza. Nasisimka kila mara ninapoisoma Inaelezea ninyi ni kina nani na ni nani Bwana anataka ninyi muwe katika wakati huu muafaka mnapofanya sehemu yenu kusaidia kukusanya Israeli iliyotawanyika.

Dada zangu wapendwa, tunawahitaji! “Tunahitaji nguvu yenu, uongofu wenu, kusadiki kwenu, uwezo wenu wa kuongoza, busara yenu, na sauti zenu.”4 Hatuwezi kiurahisi kukusanya Israeli bila ninyi.

Ninawapenda na kuwashukuru na sasa ninawabariki kwa uwezo wa kuacha ulimwengu nyuma mnaposaidia katika kazi hii muhimu na ya haraka. Kwa pamoja tunaweza kufanya yote ambayo Baba yetu wa Mbinguni anatutaka tufanye kuuandaa ulimwengu kwa Ujio wa Pili wa Mwana Wake Mpendwa.

Yesu ndiye Kristo. Hili ni kanisa Lake. Juu ya hili ninashuhudia katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Russell M. Nelson, “Hope of Israel” (worldwide youth devotional, June 3, 2018), HopeofIsrael.lds.org.

  2. Ona 2 Nefi 25:26.

  3. Kwa ajili ya tangazo la Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama, ona Mary Ellen Smoot, “Rejoice, Daughters of Zion,” Liahona, Jan. 2000, 111–14.

  4. Russell M. Nelson, “Ombi kwa Dada Zangu,” Liahona, Nov. 2015, 96; imetiliwa mkazo.