2022
Agano la Milele
Oktoba 2022


“Agano la Milele,” Liahona, Okt. 2022.

Ujumbe wa Kila mwezi wa Liahona, Oktoba 2022

Agano la Milele

Wale wote ambao wamefanya agano na Mungu wana njia ya kupata aina maalumu ya upendo na rehema.

Picha
mchoro wa Yesu Kristo

Bwana Yesu Kristo, na Del Parson

Katika ulimwengu huu uliovurugwa na vita na uvumi wa vita, haja ya ukweli, nuru na upendo safi wa Yesu Kristo ni mkubwa kuliko hapo awali. Injili ya Kristo ni tukufu, na tumebarikiwa kujifunza na kuiishi kulingana na maagizo yake. Tunafurahia katika nafasi zetu za kuishiriki—kushuhudia juu ya kweli zake popote tulipo.

Nimezungumzia mara kwa mara kuhusu umuhimu wa agano la Ibrahimu na kukusanywa kwa Israeli. Tunapokumbatia injili na kubatizwa, tunajichukulia juu yetu wenyewe jina takatifu la Yesu Kristo. Ubatizo ni lango ambalo huelekeza kwenye kuwa warithi wa pamoja wa ahadi zote zilizotolewa na Bwana kwa Ibrahimu, Isaka, Yakobo na uzao wao.1

“Agano jipya na la milele”2 (Mafundisho na Maagano 132:6) na agano la Ibrahimu kiuhalisia ni agano lile lile—ni njia mbili za kuelezea agano ambalo Mungu alifanya na wanaume na wanawake katika nyakati tofauti.

Kivumishi la milele humaanisha kwamba agano lilikuwapo hata kabla ya kuwekwa kwa msingi wa dunia! Mpango ulioandaliwa katika Baraza Kuu Mbinguni ulijumuisha utambuzi wa dhahiri kwamba sisi tungekatiliwa mbali kutoka uwepo wa Mungu. Hata hivyo, Mungu aliahidi kwamba Yeye angemtoa Mwokozi ambaye angeshinda matokeo ya Anguko. Mungu alimwambia Adamu baada ya ubatizo wake:

“Na wewe ni kwa mfano wake yeye ambaye hana mwanzo wa siku au mwisho wa miaka, kutoka milele yote hadi milele yote.

“Tazama, wewe u mmoja ndani yangu, mwana wa Mungu; na hivyo wote wapate kuwa wana wangu” (Musa 6:67–68).

Adamu na Hawa walikubali ibada ya ubatizo na kuanza mchakato wa kuwa wamoja na Mungu. Waliingia katika njia ya agano.

Wakati mimi na wewe tunapoingia katika njia hiyo, tunakuwa na njia mpya ya maisha. Sisi kwa hiyo tunanzisha uhusiano na Mungu ambao unamwezesha Yeye kutubariki na kutubadilisha. Njia ya agano hutuongoza kurudi Kwake. Kama tunamruhusu Mungu ashinde katika maisha yetu, agano hilo litatusogeza karibu na karibu zaidi na Yeye. Maagano yote yanakusudiwa kufunga pamoja. Yanatengeneza uhusiano wenye viunganishi vya milele.

Upendo na Rehema Maalumu

Mara tunapofanya agano na Mungu, tunaondoka kwenye uwanda wa katikati kwa milele yote. Mungu hatatupilia mbali uhusiano Wake na wale ambao wameunda mfungamano kama huo na Yeye. Hakika, wale wote ambao wamefanya agano na Mungu wana njia ya kupata aina maalumu ya upendo na rehema. Katika lugha ya Kiebrania, huo upendo wa kimaagano unaitwa hesed (חֶסֶד).3

Hesed halina kisawe cha Kiingereza chenye kujitosheleza. Wafasiri wa Toleo la King James la Biblia lazima walisumbuka na jinsi ya kutafsiri hesed kwa Kiingereza. Mara nyingi walichagua “fadhili.” Hii inakaribia lakini sio maana yote ya hesed. Fasili zingine pia zilitafsiri, kama “rehema” na “wema.” Hesed ni neno la kipekee linaloelezea uhusiano wa agano ambapo pande zote zinafungwa ili ziwe tiifu na aminifu kila mmoja kwa mwingine.

Ndoa ya selestia ni uhusiano wa agano kama hilo. Mume na mke wanafanya agano pamoja na Mungu na kwa kila mmoja wao ili kuwa watiifu na waaminifu kwa kila mmoja.

Hesed ni aina maalumu ya upendo na rehema ambayo Mungu huhisi kwa ajili ya na hutoa kwa wale ambao wamefanya agano Naye. Na sisi hali kadhalika tunaonyesha Hesed Kwake.

Picha
wenzi waliofunga ndoa karibuni wakiwa nje ya hekalu

Mimi na wewe tukiwa tayari tumefanya agano na Mungu, uhusiano wetu na Yeye unakuwa wa karibu sana kuliko kabla ya agano letu. Sasa tumeunganishwa pamoja.

Picha na Jerry L. Garns

Kwa sababu Mungu ana hesed kwa wale ambao wamefanya agano Naye, Yeye atawapenda wao. Yeye ataendelea kufanya kazi pamoja nao na kuwapa nafasi za kubadilika. Yeye atawasamehe wao wanapotubu. Na kama watapotoka, Yeye atawasaidia kupata njia yao ya kurudi Kwake.

Wewe na mimi tunapokuwa tumefanya agano na Mungu, uhusiano wetu na Yeye unakuwa wa karibu sana kuliko kabla ya agano letu. Sasa tumeunganishwa pamoja. Kwa sababu ya agano letu na Mungu, Yeye kamwe hatachoka katika juhudi Zake za kutusaidia sisi, na kamwe sisi hatuwezi kumaliza subira Yake ya rehema kwetu. Kila mmoja wetu ana sehemu maalum katika moyo wa Mungu. Yeye ana matumaini makubwa kwa ajili yetu.

Wewe unajua tamko la kihistoria Bwana alilotoa kwa Nabii Joseph Smith. Lilikuja kwa ufunuo. Bwana alimwambia Joseph, “Ahadi hii ni yenu pia, kwa sababu ninyi ni wa Ibrahimu, na ahadi ilifanywa kwa Ibrahimu” (Mafundisho na Maagano 132:31).

Kwa hiyo, hili agano la milele lilirejeshwa kama sehemu ya Urejesho mkuu wa injili katika utimilifu wake. Fikiria hilo! Agano la ndoa lililofanywa ndani ya hekalu limefungwa moja kwa moja na lile agano la Ibrahimu. Ndani ya hekalu wenzi wanatambulishwa baraka zote zilizohifadhiwa kwa ajili ya uzao wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo.

Kama alivyofanya Adamu, wewe na mimi binafsi tunaingia katika njia ya agano wakati wa ubatizo. Kisha tunaliingia agano kikamilifu zaidi katika hekalu. Baraka za agano la Ibrahimu hutunukiwa katika mahekalu matakatifu. Baraka hizi zinaturuhusu sisi, baada ya kufufuliwa, “kurithi viti vya enzi, falme, uwezo, himaya za kifalme, na mamlaka, kwenye ‘kuinuliwa kwetu na utukufu katika vitu vyote’ [Mafundisho na Maagano 132:19].”4

Katika maandishi ya kuhitimisha ya Agano la Kale, tunasoma ahadi ya Malaki kwamba Eliya “ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao” (Malaki 4:6). Katika Israeli ya kale, marejeo hayo ya baba yangejumuisha akina baba Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Ahadi hii inafafanuliwa tunaposoma toleo tofauti la mstari huu ambalo Moroni alinukuu kwa Nabii Joseph Smith, “Yeye [Eliya] atapanda katika mioyo ya watoto ahadi zilizofanywa kwa baba, na mioyo ya watoto itawageukia baba zao” (Joseph Smith—Historia 1:39). Akina baba hao kwa kweli hujumuisha Ibrahimu, Isaka na Yakobo. (Ona Mafundisho na Maagano 27:9–10.)

Picha
picha ya Yesu Kristo

Wale ambao wanafanya maagano na kuyashika wanaahidiwa uzima wa milele na kuinuliwa. Yesu Kristo ni mdhamini wa maagano hayo.

Maelezo kutoka Kristo na Kijana Tajiri Mtawala, na Heinrich Hofman

Yesu Kristo: Kiini cha Agano

Dhabihu ya upatanisho ya Mwokozi ilimwezesha Baba kutimiza ahadi Zake alizozifanya kwa watoto Wake. Kwa sababu Yesu Kristo ndiye “njia, kweli, na uzima,” ndiyo maana “mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya [Yeye]” (Yohana 14:6). Utimizo wa agano la Ibrahimu unaonekana kuwezakana kwa sababu ya Upatanisho wa Mwokozi wetu, Bwana Yesu Kristo. Yesu Kristo ndiye kinii cha agano la Ibrahimu.

Agano la Kale sio tu kitabu cha maandiko; pia ni kitabu cha historia. Wewe unakumbuka kuhusu ndoa ya Sarai na Abramu. Kwa sababu walikuwa hawana mtoto, Sarai alimtoa kijakazi wake, Hajiri, kuwa pia mke wa Abramu, kulingana na maelekezo ya Bwana. Hajiri akimzaa Ishmaeli.5 Abramu alimpenda Ishmaeli, lakini hakuwa mtoto ambaye agano lingeweza kupitia kwake. (Ona Mwanzo 11:29–30; 16:1, 3, 11; Mafundisho na Maagano 132:34.)

Kama baraka kutoka kwa Mungu, na jibu kwa imani ya Sarai,6 yeye alipata ujauzito katika miaka yake ya uzeeni ili kwamba agano lingepitia katika mwana wake, Isaka (ona Mwanzo 17:19). Alizaliwa katika agano.

Mungu aliwapa Sarai na Abramu majina mapya—Sara and Ibrahimu (ona Mwanzo 17:5, 15). Kupeana kwa majina hayo mapya kulianzisha mwanzo wa maisha mapya na kudra mpya kwa familia hii.

Ibrahimu aliwapenda wote Ishmaeli na Isaka. Mungu alimwambia Ibrahimu kwamba angemzidisha na kuwa taifa kuu (ona Mwanzo 17:20). Vile vile, Mungu aliweka wazi kwamba agano la milele lingefanyika kupitia Isaka (ona Mwanzo 17:19

Wale wanaokubali injili watakuwa sehemu ya uzao wa Ibrahimu. Katika Wagalatia tunasoma:

“Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo.

“… Ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu.

“Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi” (Wagalatia 3:27–29).

Kwa hiyo, tunaweza kuwa warithi kupitia kuzaliwa au kuasiliwa.

Picha
watu wamekusanyika katika ibada ya ubatizo

Mara tunapofanya agano na Mungu, tunaondoka kwenye uwanda wa katikati milele. Mungu hatatupilia mbali uhusiano Wake na wale ambao wameunda mfungamano kama huo na Yeye.

Mwana wa Isaka na Rebeka, Yakobo alizaliwa katika agano. Zaidi ya hivyo, yeye alichagua kuingia kwa hiari yake mwenyewe. Kama unavyojua, jina la Yakobo lilibadilishwa kuwa Israeli (ona Mwanzo 32:28), kumaanisha “acha Mungu ashinde” au “mtu anayeshindana na Mungu.”7

Katika kitabu cha Kutoka tunasoma kwamba “Mungu akakumbuka agano lake alilolifanya na Ibrahimu na Isaka na Yakobo” (Kutoka 2:24). Mungu aliwaambia wana wa Israeli, “Ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu” (Kutoka 19:5).

Kirai “tunu” ilitafsiriwa kutoka kwa Kiebrania segullah, kumaanisha kitu cha thamani kuu— “tunu.”8

Kitabu cha Kumbukumbu la Torati husimulia umuhimu wa agano. Mitume wa Agano Jipya walijua kuhusu agano hili. Baada ya Petro kumponya mtu kilema kwenye ngazi za hekalu, aliwafunza watazamaji kuhusu Yesu. Petro alisema, “Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa baba zetu, amemtukuza Mwana wake Yesu” (Matendo ya Mitume 3:13).

Petro alifunga ujumbe wake kwa kuiambia hadhira yake, “Ninyi ni watoto wa manabii; na ninyi ni wa nyumba ya Israeli; na ni wa agano ambalo Baba alifanya na babu zenu akisema kwa Ibrahimu: Na kupitia uzao wako, makabila yote ya dunia yatabarikiwa” (Matendo ya Mitume 3:25). Petro aliwaambia wazi kwamba sehemu ya huduma ya Kristo ni kutimiza agano la Mungu.

Bwana alitoa mahubiri kama hayo kwa watu wa Amerika. Huko, Kristo aliyefufuka aliwaambia watu asili yao. Alisema:

“Na tazama, ninyi ni watoto wa manabii; na ninyi ni wa nyumba ya Israeli; na ni wa agano ambalo Baba alifanya na babu zenu akisema kwa Ibrahimu: Na kupitia uzao wako, makabila yote ya dunia yatabarikiwa.

“Baba alinitayarisha mimi kwanza, na kunituma niwabariki ninyi kwa kugeuza kila mmoja wenu kutoka kwa uovu wake; na hivyo ni kwa sababu ninyi ni watoto wa agano” (3 Nefi 20:25–26).

Je, unaona umuhimu wa hili? Wale ambao wanashika maagano yao watapokea nafsi kinzani dhidi ya dhambi! Wale ambao wanashika maagano yao watakuwa na nguvu za kukinza ushawishi wa ulimwengu wa kila mara.

Picha
mtu akipokea sakramenti

Wale ambao wanashika maagano yao watapokea nafsi kinzani dhidi ya dhambi! Wale ambao wanashika maagano yao watakuwa na nguvu za kukinza ushawishi wa ulimwengu wa kila mara.

Kazi ya Umisionari: Kushiriki Agano

Bwana ameamuru kwamba tueneze injili na kushiriki agano. Hiyo ndiyo sababu tuna wamisionari. Yeye anatumaini kila mmoja wa watoto Wake kuwa na fursa ya kuchagua injili ya Mwokozi na kuendelea kwenye njia ya agano. Mungu anataka kuwaunganisha watu wote kwenye agano ambalo Yeye alilifanya na Ibrahimu zamani za kale.

Kwa hiyo, kazi ya umisionari ni sehemu ya muhimu ya kusanyiko kuu la Israeli. Kusanyiko hilo ni kazi muhimu sana inayofanyika duniani hivi leo. Hakuna kitu kingine kinachoweza kulinganishwa kwa ukubwa na kazi hii. Hakuna kitu kingine kinachoweza kulinganishwa kwa umuhimu na kazi hii. Wamisionari wa Bwana—wafuasi Wake—wanashughulika katika changamoto hii kuu, kusudi kuu, kazi kuu duniani leo.

Lakini kuna hata zaidi—zaidi sana. Kuna haja kubwa ya kueneza injili kwa watu walio kwenye upande mwingine wa pazia. Mungu anamhitaji kila mtu, kwenye pande zote za pazia, kufurahia baraka za agano Lake. Njia ya agano iko wazi kwa wote. Tunamsihi kila moja kutembea hiyo njia pamoja nasi. Hakuna kazi nyingine inayojumuisha ulimwenguni kote kama hii. Kwani “Bwana ana huruma kwa wote ambao, kwa uaminifu wa mioyo yao, wanamlingana katika jina lake takatifu” (Helamani 3:27).

Kwa sababu Ukuhani wa Melkizedeki umerejeshwa, wanawake na wanaume washika maagano wana fursa za “baraka zote za kiroho” za injili (Mafundisho na Maagano 107:18; msisitizo umeongezwa).

Wakati wa kuwekwa wakfu kwa Hekalu la Kirtland mwaka 1836, chini ya maelekezo ya Bwana, Eliya alitokeza. Madhumuni yake? “Kuwageuza … watoto kwa baba” (Mafundisho na Maagano 110:15). Elia pia alitokeza. Madhumuni yake? Kuwakabidhi Joseph Smith na Oliver Cowdery “kipindi cha injili ya Ibrahimu, akisema kwamba kupitia sisi na uzao wetu vizazi vyote baada yetu vitabarikiwa” (Mafundisho na Maagano 110:12). Kwa hiyo, Bwana aliwatunuku Joseph Smith na Oliver Cowdery mamlaka ya ukuhani na haki ya kutoa baraka za kipekee za agano la Ibrahimu kwa wengine.9

Katika Kanisa, tunatembea katika njia ya agano binafsi na kwa pamoja. Kama vile ndoa na familia hushiriki muunganiko wa kipekee ulio sawa ambao hujenga upendo maalumu, vivyo hivyo na uhusiano mpya unaoundwa tunapojifunga wenyewe kwa agano na kuwa wima kwa Mungu wetu!

Hii inaweza kuwa kile Nefi alimaanisha wakati alisema kwamba Mungu “anawapenda wale ambao watataka yeye awe Mungu wao” (1 Nefi 17:40). Hiyo ndio hasa kwa nini, kama sehemu ya agano, rehema na upendo maalumu—au hesed—hupatikana kwa wote ambao wanaingia katika uhusiano huu wa undani na wa dhati pamoja na Mungu, hata “vizazi elfu” (Kumbukumbu la Torati 7:9).

Kufanya agano na Mungu hubadilisha uhusiano wetu na Yeye milele. Hutubariki kwa kiasi kikubwa cha upendo na rehema.10 Huathiri jinsi sisi tulivyo na jinsi Mungu atatusaidia kuwa kile tunachoweza kuwa. Tuliahidiwa kwamba sisi, pia, tunaweza kuwa “tunu ya kipekee” Kwake (Zaburi 135:4).

Ahadi na Fursa

Wale ambao wanafanya maagano matakatifu na kuyashika wanaahidiwa uzima wa milele na kuinuliwa, “kipawa kikuu kati ya vipawa vyote vya Mungu” (Mafundisho na Maagano 14:5). Yesu Kristo ni mdhamini wa maagano hayo (ona Waebrania 7:22; 8:6). Washika maagano ambao wanampenda Mungu na kumruhusu Yeye ashinde juu ya vitu vyote vingine katika maisha yao humfanya Yeye kuwa ushawishi wa nguvu sana katika maisha yao.

Katika siku yetu tuna fursa za kupokea baraka za patriaki na kujifunza muunganiko wetu na mapatriaki wa kale. Baraka hizo pia hutoa taswira ya kile kilicho mbele yetu.

Picha
Yesu akizungumza na Petro

Kwa sababu ya agano letu na Mungu, Yeye kamwe hatachoka katika juhudi Zake za kutusaidia sisi, na kamwe sisi hatuwezi kumaliza subira Yake ya rehema kwetu.

Je, Wanipenda Mimi Zaidi Ya Hawa? na David Lindsley

Wito wetu kama Israeli ya agano ni kuhakikisha kila muumini wa Kanisa anapata furaha na fursa zinazohusiana na kufanya maagano na Mungu. Ni wito wa kuhimiza kila mwanaume na mwanamke, mvulana na msichana mwenye kushika maagano, kushiriki injili na wale ambao wanakuja katika mazingira ya ushawishi wao. Pia ni wito wa kuwasaidia na kuwatia moyo wamisionari wetu, ambao wanatumwa na maelekezo ya kubatiza na kusaidia kukusanya Israeli, ili kwamba pamoja tuweze kuwa watoto wa Mungu na Yeye atakuwa Mungu wetu (ona Mafundisho na Maagano 42:9).

Kila mwanaume na mwanamke ambaye hushiriki katika ibada za ukuhani na hufanya na kushika maagano na Mungu moja kwa moja anaweza kupata nguvu za Mungu. Tunajichukulia juu yetu jina la Bwana kama watu binafsi. Pia tunajichukulia jina Lake juu yetu kama watu. Kuwa na shauku kuhusu kutumia jina sahihi la Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni njia muhimu ambayo sisi kama watu tunajichukulia jina Lake juu yetu. Kwa kweli, kila tendo la ukarimu la Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho na waumini wake ni onyesho la hesed ya Mungu.

Kwa nini Israeli ilitawanywa? Kwa sababu watu walivunja amri na kuwapiga mawe manabii. Baba mwenye upendo lakini mwenye huzuni alijibu kwa kuitawanya Israeli mbali sana.11

Hata hivyo, Yeye aliwatawanya na ahadi kwamba siku moja Israeli ingekusanywa tena katika zizi Lake.

Kabila ya Yuda ilipatiwa jukumu la kuuandaa ulimwengu kwa ajili ya ujio wa kwanza wa Bwana. Kutoka kabila hiyo, Mariamu aliitwa kuwa mama wa Mwana wa Mungu.

Kabila ya Yusufu, kupitia wanawe na wana wa Asenathi, Efraimu na Manase (ona Mwanzo 41:50–52; 46:20), ilipatiwa jukumu la kuongoza katika kukusanya Israeli, kuuandaa ulimwengu kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Bwana.

Katika uhusiano wa milele wa hesed kama huo, ni kawaida tu kwamba Mungu anataka kuikusanya Israeli. Yeye ni Baba yetu wa Mbinguni! Yeye anataka kila mmoja wa watoto Wake—pande zote za pazia—kusikia ujumbe wa injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo.

Njia ya Upendo

Njia ya agano ni njia ya upendo—ni hiyo hesed kuu, ni huko kujali kwa huruma kwa ajili ya na kufikiana kila mmoja kwa mwingine. Kuhisi upendo huo huleta uhuru na kuinua. Furaha kuu ambayo utaipata ni wakati unatumia upendo huo kwa ajili ya Mungu na kwa watoto wote wa Mungu.

Kumpenda Mungu zaidi kuliko mtu yeyote au kitu kingine chochote ni sharti ambalo huleta amani ya kweli, faraja, kujiamini na shangwe.

Njia ya agano ni kuhusu uhusiano wetu na Mungu—uhusiano wetu wa hesed pamoja Naye. Tunapofanya agano na Mungu, tunafanya agano na Yeye ambaye daima ataweka ahadi Yake. Yeye atafanya kila kitu anachoweza, bila kuhujumu haki yetu ya kujiamulia, ili kutusaidia kuweka ahadi zetu.

Kitabu cha Mormoni huanza na kutamatisha na rejeo la hili agano la milele. Kutoka ukurasa wa kichwa chake hadi shuhuda za kutamatisha za Mormoni na Moroni, Kitabu cha Mormoni hutoa marejeo ya agano hilo (ona Mormoni 5:20; 9:37). “Kutokea kwa Kitabu cha Mormoni ni ishara kwa ulimwengu mzima kwamba Bwana ameanza kukusanya Israeli na kutimiza maagano Aliyoyafanya kwa Ibrahimu, Isaka, na Yakobo.”12

Kaka na dada zangu wapendwa, tumeitwa katika wakati huu muhimu katika historia ya dunia kuufundisha ulimwengu kuhusu uzuri na nguvu za agano la milele. Baba yetu wa Mbinguni anatuamini kabisa kuifanya kazi hii kuu.

Ujumbe huu pia ulitolewa katika mkutano wa uongozi wa mkutano mkuu mnamo Machi 31, 2022

Mihtasari

  1. Ona Russell M. Nelson, “Children of the Covenant,” Ensign, May 1995, 34:

  2. Agano jipya na la milele ni utimilifu wa injili ya Yesu Kristo. Hujumuisha ibada zote na maagano yanayohitajika kwa ajili ya wokovu wetu (ona Mafundisho na Maagano 66:2). Ni “jipya” wakati wowote Bwana hulifanya upya au kulirejesha, na ni la “milele” kwa sababu halibadiliki.

  3. Mazungumzo kwa mapana kuhusu hesed na agano la milele yanapatikana katika Kerry Muhlestein, God Will Prevail: Ancient Covenants, Modern Blessings, and the Gathering of Israel (2021).

  4. Russell M. Nelson, katika “Special Witnesses of Christ,” Liahona, Apr. 2001, 7.

  5. Neno la Kiebrania Ishmael humaanisha “Mungu anasikia” (Kamusi ya Biblia, “Ishmaeli”).

  6. “Kwa imani hata Sara mwenyewe alipokea uwezo wa kuwa na mimba; alipokuwa amepita wakati wake; kwa kuwa alimhesabu yeye aliyeahidi kuwa mwaminifu.” (Waebrania 11:11).

  7. Kamusi ya Biblia, “Israeli.”

  8. Ona Kamusi ya Biblia, “Kipekee”; “Hebrew and Chaldee Dictionary,” Strong’s Exhaustive Concordance of the Bible (1984), 82, word 5459.

  9. Ona Russell M. Nelson, “Thanks for the Covenant” (Brigham Young University devotional, Nov. 22, 1988), 4, speeches.byu.edu.

  10. “Kila agano na Mungu ni fursa za kusogea karibu naye. Kwa mtu yeyote anayetafakari kwa dakika juu ya kile ambacho tayari wamehisi kuhusu upendo wa Mungu, kufanya muunganiko huo kuwa imara na uhusiano huo kuwa wa karibu ni zawadi isiyoweza kukataliwa” (Henry B. Eyring, “Making Covenants with God” [Brigham Young University fireside, Sept. 8, 1996], 3, speeches.byu.edu).

  11. “Bwana pia alitumia huu mtawanyiko kwa watu Wake waliochaguliwa miongoni mwa mataifa ya ulimwengu kubariki mataifa hayo” (Mwongozo wa Maandiko, “Israeli,” scriptures.ChurchofJesusChrist.org; ona pia Yakobo 5:1-8, 20).

  12. Russell M. Nelson, “Siku za Baadaye za Kanisa: Kuuandaa Ulimwengu kwa Ajili ya Ujio wa Pili wa Mwokozi,” Liahona, Apr. 2020, 9–17.