Maandiko Matakatifu
1 Nefi 12


Mlango wa 12

Nefi anaona katika ono nchi ya ahadi; haki, uovu, na uangamizo wa wenyeji wake; kuja kwa Mwanakondoo wa Mungu miongoni mwao; jinsi wale Wanafunzi Kumi na Wawili pamoja na wale Mitume Kumi na Wawili watahukumu Israeli; na hali ya machukizo na uchafu ya wale ambao wanafifia katika kutoamini. Karibia mwaka 600–592 K.K.

1 Na ikawa kwamba malaika akaniambia: Angalia, na uone uzao wako, na pia uzao wa kaka zako. Na nikaangalia na kuona nchi ya ahadi; na nikaona vikundi vya watu, ndiyo, hata hesabu yao ilikuwa nyingi kama mchanga wa bahari.

2 Na ikawa kwamba niliona vikundi vimekusanyika pamoja kupigana, moja dhidi ya mwingine; na nikaona vita, na uvumi wa vita, na mauaji makuu kwa upanga miongoni mwa watu wangu.

3 Na ikawa kwamba niliona vizazi vingi vikipita, baada ya vita vya namna hii na mabishano katika nchi; na nikaona miji mingi, ndiyo, hata sikuihesabu.

4 Na ikawa kwamba niliona ukungu mweusi usoni mwa nchi ya ahadi; na nikaona umeme, na nikasikia radi, na mitetemeko ya ardhi, na aina zote za misukosuko na makelele; na nikaona ardhi, na miamba, kwamba ilipasuka; na nikaona milima ikivunjika vipande vipande; na nikaona tambarare za ardhi, kwamba zilipasuka; na nikaona miji mingi imezama; na nikaona mingi iliyochomwa kwa moto; na nikaona mingi iliyoanguka chini, kwa sababu ya ile mitetemeko.

5 Na ikawa baada ya kuona vitu hivi, nikaona ule ukungu wa giza, ukitoweka kutoka usoni mwa ulimwengu; na tazama, nikaona makundi ya wale ambao hawakuanguka kwa sababu ya hukumu kuu ya kuhofisha kwa Bwana.

6 Na nikaona mbingu zikifunguka, na Mwanakondoo wa Mungu akiteremka kutoka mbinguni; na akashuka chini na akajionyesha kwao.

7 Na pia niliona na ninashuhudia kwamba Roho Mtakatifu aliwashukia wengine kumi na wawili; na walichaguliwa na kuteuliwa, na Mungu.

8 Na malaika akanizungumzia, na kusema: Tazama wale wanafunzi kumi na wawili wa Mwanakondoo, ambao wameteuliwa kuhudumia uzao wako.

9 Na akaniambia: Je, unawakumbuka wale mitume kumi na wawili wa Mwanakondoo? Tazama ni wao watakaohukumu yale makabila kumi na mawili ya Israeli; kwa hivyo, wale wahudumu kumi na wawili wa uzao wako watahukumiwa na wao; kwani ninyi ni wa nyumba ya Israeli.

10 Na hawa wahudumu kumi na wawili uwaonao watahukumu uzao wako. Na, tazama, wao ni watakatifu milele; kwa sababu ya imani yao katika Mwanakondoo wa Mungu mavazi yao yanafanywa kuwa meupe kwa damu yake.

11 Na malaika akaniambia: Angalia! Na nikaangalia, na kuona vizazi vitatu vikiishi kwa haki; na mavazi yao yalikuwa meupe kama ya Mwanakondoo wa Mungu. Na malaika akaniambia: Hawa wamefanywa kuwa weupe kwa damu ya Mwanakondoo, kwa sababu ya imani yao kwake.

12 Na mimi, Nefi, pia nikaona wengi katika kizazi cha nne wakiishi katika haki.

13 Na ikawa kwamba niliona vikundi vya dunia vimekusanyika pamoja.

14 Na malaika akaniambia: Tazama uzao wako, na pia uzao wa kaka zako.

15 Na ikawa kwamba niliangalia na kuona watu wa uzao wangu wamekusanyika pamoja katika vikundi kupigana na uzao wa kaka zangu; na walikusanyika pamoja wapigane vita.

16 Na malaika akanizungumzia, akisema: Tazama chemchemi ya maji machafu ambayo baba yako aliiona; ndiyo, hata mto ambao aliuzungumzia; na kilindi chake ni kilindi cha jehanamu.

17 Na ukungu wa giza ni majaribio ya ibilisi, yanayopofusha macho, na ambayo yanashupaza mioyo ya watoto wa watu, na kuwaelekeza kwenye njia pana, ili waangamie na kupotea.

18 Na jengo kubwa na pana, ambalo baba yako aliliona, ni mawazo yasiyofaa na kiburi cha watoto wa watu. Na shimo kubwa la kuhofisha linawagawanya; ndiyo, hata neno la haki la Mungu wa Milele, na Masiya ambaye ni Mwanakondoo wa Mungu, ambaye anashuhudiwa na Roho Mtakatifu, tangu mwanzo wa ulimwengu hadi sasa, na tangu sasa hadi milele.

19 Na wakati malaika alipokuwa akisema maneno haya, nikatazama na kuona kwamba uzao wa kaka zangu walichokozana na uzao wangu, kulingana na maneno ya malaika; na kwa sababu ya kiburi cha uzao wangu, na majaribio ya ibilisi, nikaona kwamba uzao wa kaka zangu waliwashinda watu wa uzao wangu.

20 Na ikawa kwamba nilitazama, na kuona kwamba watu wa uzao wa kaka zangu waliwashinda uzao wangu; na wakendelea mbele katika vikundi kwenye uso wa nchi.

21 Na nikawaona wamekusanyika pamoja katika vikundi; na nikaona vita na uvumi wa vita miongoni mwao; na nikaona vizazi vingi vikiishi kwenye vita na uvumi wa vita.

22 Na malaika akaniambia: Tazama hawa watafifia katika kutoamini.

23 Na ikawa kwamba niliona, baada ya wao kufifia katika kutoamini wakawa watu wa giza, wenye makuruhu, wenye uchafu, waliojaa uzembe na namna zote za machukizo.