Maandiko Matakatifu
1 Nefi 15


Mlango wa 15

Uzao wa Lehi utapokea injili kutoka kwa Wayunani katika siku za mwisho—Kusanyiko la Israeli unafananishwa na mti wa mzeituni ambao matawi yake ya asili yatapandikizwa tena—Nefi anatafsiri ono la mti wa uzima na anazungumza kuhusu haki ya Mungu katika kuwatenga waovu kutoka kwa watakatifu. Karibia mwaka 600–592 K.K.

1 Na ikawa kwamba baada ya mimi, Nefi, kunyakuliwa katika Roho, na kuona mambo haya yote, nilirudi kwenye hema la baba yangu.

2 Na ikawa kwamba niliona kaka zangu, na walikuwa wakibishana kuhusu vile vitu ambavyo baba yangu aliwazungumzia.

3 Kwa kweli aliwazungumzia vitu vikubwa, vilivyokuwa vigumu kueleweka, isipokuwa mtu amuulize Bwana; na wao wakiwa wagumu mioyoni mwao, kwa hivyo hawakumtazama Bwana jinsi ilivyowapasa.

4 Na sasa mimi, Nefi, nilihuzunika kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao, na pia, kwa sababu ya vitu ambavyo niliviona, na nilijua lazima vitimizwe kwa sababu ya uovu mkuu wa wanadamu.

5 Na ikawa kwamba nililemewa na masumbuko yangu, kwa maana nilidhani kwamba masumbuko yangu yalizidi yote, kwa sababu ya kuangamia kwa watu wangu, kwani nilikuwa nimeona kuanguka kwao.

6 Na ikawa kwamba baada ya kupokea nguvu nikawazungumzia kaka zangu, nikitaka kujua chanzo cha ugomvi wao.

7 Na wakasema: Tazama, hatuwezi kuelewa maneno ambayo baba yetu amesema kuhusu matawi ya asili ya mti wa mzeituni, na pia kuhusu Wayunani.

8 Na nikawaambia: Je mmemuuliza Bwana?

9 Na wakasema: Hapana; kwani Bwana hatujulishi vitu hivi.

10 Tazama, nikawaambia: Kwa nini hamtii amri za Bwana? Kwa nini mwangamie, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu?

11 Kwani hamkumbuki vitu ambavyo Bwana amesema?—Kama hamtashupaza mioyo yenu, na mniulize kwa imani, mkiamini kwamba mtapokea, kwa bidii katika kutii amri zangu, kwa kweli vitu hivi vitafanywa vijulikane kwenu.

12 Tazama, nawaambia, kuwa nyumba ya Israeli ililinganishwa na mti wa mzeituni, na Roho wa Bwana aliyekuwa ndani ya baba yetu; na tazama si sisi tumetokana na nyumba ya Israeli, na si sisi ni tawi la nyumba ya Israeli?

13 Na sasa, kitu ambacho baba yetu anamaanisha kuhusu kupandikizwa kwa matawi ya asili kwa kupitia utimilifu wa Wayunani, ni, kwamba katika siku za baadaye, wakati uzao wetu utakuwa umefifia katika kutoamini, ndiyo, kwa muda wa miaka mingi, na vizazi vingi baada ya Masiya kudhihirishwa katika mwili kwa watoto wa watu, ndipo utimilifu wa injili ya Masiya utawafikia Wayunani, na kutoka kwa Wayunani hadi kwa baki la uzao wetu—

14 Na katika siku ile baki la uzao wetu litajua kwamba wao ni wa nyumba ya Israeli, na kwamba wao ni watu wa agano la Bwana; na kisha watajua na pia kupata ufahamu wa babu zao, na pia ufahamu wa injili ya Mkombozi wao, ambayo aliwahudumia babu zao; kwa hivyo, watamfahamu Mkombozi wao na mambo halisi ya mafundisho yake, ili waweze kujua jinsi ya kumkaribia na waokolewe.

15 Na basi katika siku ile, si watashangilia na kumsifu Mungu asiye na mwisho, mwamba wao na wokovu wao? Ndiyo, katika siku ile, si watapokea nguvu na malisho kutoka kwa ule mizabibu wa kweli? Ndiyo, si wataungana na zizi la kweli la Mungu?

16 Na tazama, nawaambia, Ndiyo; watakumbukwa tena miongoni mwa nyumba ya Israeli; watapandikizwa ndani, wakiwa tawi la asili la mti wa mzeituni, kwenye mti wa mzeituni wa kweli.

17 Na hii ndiyo baba yetu anamaanisha; na anamaanisha kwamba haitatimizwa hadi watawanywe na Wayunani; na anamaanisha itatimizwa na Wayunani, ili Bwana awaonyeshe Wayunani nguvu zake, na kwa sababu hii atakataliwa na Wayahudi, au na nyumba ya Israeli.

18 Kwa hivyo, baba yetu hajazungumza juu ya uzao wetu pekee, lakini pia nyumba yote ya Israeli, akilenga agano ambalo litatimizwa katika siku za baadaye; agano ambalo Bwana aliagana na baba yetu Ibrahimu, akisema: Kwa uzao wako makabila yote ya dunia yatabarikiwa.

19 Na ikawa kwamba mimi, Nefi, niliwaambia mengi kuhusu vitu hivi; ndiyo, niliwaambia kuhusu uamsho wa Wayahudi katika siku za baadaye.

20 Na nikawasimulia maneno ya Isaya, ambaye alizungumza kuhusu kurudi kwa Wayahudi, au nyumba ya Israeli; na baada ya wao kuamshwa hawatachanganyika tena, wala kutawanyika tena. Na ikawa kwamba niliwaelezea kaka zangu maneno mengi, hata kwamba waliridhika na wakajinyenyekeza mbele ya Bwana.

21 Na ikawa kwamba walinizungumzia tena, wakisema: Kitu hiki kinamaanisha nini ambacho Baba yetu alikiona ndotoni? Nini maana ya ule mti aliouona?

22 Na nikawaambia: Ni kielelezo cha mti wa uzima.

23 Na wakaniambia: Nini maana ya fimbo ya chuma ambayo baba aliona, ikielekeza kwenye ule mti?

24 Na nikawaambia kwamba ilikuwa neno la Mungu; na yeyote atakayesikiza hilo neno la Mungu, na alizingatie, hataangamia; wala majaribu na mishale ya moto ya adui kuwalemea na kuwapofusha, ili kuwaelekeza kwenye maangamio.

25 Kwa hivyo, mimi, Nefi, niliwasihi wasikize neno la Bwana; ndiyo, niliwasihi kwa nguvu zote za nafsi yangu, na kwa uwezo wote ambao nilikuwa nao, kwamba wasikilize neno la Mungu na wakumbuke kutii amri zake kila wakati katika vitu vyote.

26 Na wakaniuliza: Nini maana ya ule mto ambao baba yetu aliuona?

27 Na nikawaambia kwamba yale maji ambayo baba aliona ni uchafu; na mawazo yake yalikuwa yamemezwa katika vitu vingine kwamba hakuona uchafu wa yale maji.

28 Nikawaambia kwamba lilikuwa ni shimo la kuogopesha, ambalo liligawanya waovu kutokana na mti wa uzima, na pia kutoka kwa watakatifu wa Mungu.

29 Nikawaambia kwamba ilikuwa kielelezo cha ile jehanamu ya kuogopesha, ambayo yule malaika aliniambia imetayarishwa kwa waovu.

30 Na nikawaambia kwamba baba yetu pia aliona kwamba haki ya Mungu imewatenga waovu kutoka kwa watakatifu; na mngʼaro wake ulikuwa ni kama mngʼaro wa moto, ambao unapaa kwa Mungu milele na milele, bila mwisho.

31 Na wakaniambia: Je, hii inamaanisha mateso ya mwili wakati wa majaribio, au hali ya mwisho ya nafsi baada ya kifo cha mwili, au inazungumza kuhusu vitu ambavyo ni vya muda?

32 Na ikawa kwamba niliwaambia kuwa ilikuwa ni kielelezo cha vitu ambavyo ni vya muda na kiroho; kwa maana siku itafika watakapohukumiwa kulingana na matendo yao, ndiyo, hata matendo yaliyotendwa katika mwili wa muda katika siku zao za majaribio.

33 Kwa hivyo, wakifa katika uovu wao lazima watupwe pia, kulingana na vitu vya kiroho, ambavyo vinalingana na haki; kwa hivyo, lazima waletwe kusimama mbele ya Mungu, wahukumiwe kulingana na matendo yao; na kama matendo yao yalikuwa machafu lazima wao wawe wachafu; na kama wao ni wachafu lazima iwe kwamba hawawezi kuishi katika ufalme wa Mungu; au ikiwa hivyo, ufalme wa Mungu lazima uwe mchafu pia.

34 Lakini tazama, nawaambia, ufalme wa Mungu sio mchafu, na hakuna kitu chochote kichafu kiwezacho kuingia katika ufalme wa Mungu; kwa hivyo lazima pawe na mahali pa uchafu ambapo pametayarishiwa yale ambayo ni machafu.

35 Na kuna pahali pametayarishwa, ndiyo, hata ile jehanamu ya kuogofya ambayo nimeizungumzia, na ibilisi ndiye mtayarishaji; kwa hivyo hali ya mwisho ya nafsi za wanadamu ni kuishi katika ufalme wa Mungu, au kutupwa nje kwa sababu ya ile haki ambayo nimezungumzia.

36 Kwa hivyo, waovu wamekataliwa kutoka kwa watakatifu, na pia kutoka kwa mti wa uzima, ambao matunda yake ni yenye thamani na bora zaidi ya matunda mengine; ndiyo, na ni karama ya Mungu ambayo ni kuu zaidi ya karama zote. Na hivyo ndivyo nilivyowazungumzia kaka zangu. Amina.