Maandiko Matakatifu
1 Nefi 1


Kitabu cha Kwanza cha Nefi

Utawala na Huduma Yake

Historia ya Lehi na mkewe Saria, na wanawe wanne, wanaoitwa, (kuanzia kifungua mimba) Lamani, Lemueli, Samu, na Nefi. Bwana anamwonya Lehi aondoke kutoka nchi ya Yerusalemu, kwa sababu alitoa unabii kuhusu maovu ya watu nao wanatafuta kutoa uhai wake. Anaelekea nyikani na kusafiri kwa siku tatu akiwa na jamii yake. Nefi anawachukua kaka zake na kurejea nchi ya Yerusalemu kuchukua maandishi ya Wayahudi. Historia ya mateso yao. Wanawaoa mabinti za Ishmaeli. Wanachukua jamaa zao na kuelekea nyikani. Mateso na masumbuko yao wakati wakiwa nyikani. Njia zao safarini. Wanafikia maji makubwa. Kaka za Nefi wanamuasi. Anawafadhaisha, na kujenga merikebu. Walipaita pahali pa Neema. Wanavuka bahari na kufika katika nchi ya ahadi, na hali kadhalika. Haya ni kulingana na historia ya Nefi; hii ina maana kwamba, mimi, Nefi, ndiye niliyeandika maandishi haya.

Mlango wa 1

Nefi anaanza maandishi ya watu wake—Lehi aona ono la nguzo ya moto na kusoma kutoka kitabu cha unabii—Anamsifu Mungu, anatabiri kuja kwa Masiya, na kutoa unabii kuhusu maangamizo ya Yerusalemu—Anateswa na Wayahudi. Karibia mwaka 600 K.K.

1 Mimi, Nefi, nikiwa nimezaliwa na wazazi wema, kwa hivyo nilikuwa nimefundishwa karibu yote ambayo baba yangu alijua; na baada ya kushuhudia masumbuko mengi maisha mwangu, haidhuru, nikiwa nimebarikiwa na Bwana maishani mwangu; ndiyo, nikiwa nimepokea ufahamu wa wema na siri za Mungu, kwa hivyo naandika maandishi juu ya mambo ya maisha yangu.

2 Ndiyo, naandika maandishi kwa lugha ya baba yangu, ambayo ni pamoja na elimu ya Wayahudi na lugha ya Wamisri.

3 Na ninajua kwamba maandishi ambayo ninaandika ni ya kweli; na ninayaandika kwa mkono wangu; na ninayaandika kadiri nijuavyo.

4 Kwani ikawa mwanzoni mwa mwaka wa kwanza wa utawala wa Zedekia, mfalme wa Yuda, (baba yangu, Lehi, akiwa ameishi katika Yerusalemu maisha yake yote); na katika mwaka huo walikuja manabii wengi, wakitoa unabii na kuwaambia watu kwamba lazima watubu, au sivyo mji mkuu wa Yerusalemu lazima uangamizwe.

5 Kwa hivyo ikawa baba yangu, Lehi, aliendelea mbele aliomba dua kwa Bwana, ndiyo, hata na moyo wake wote, kwa niaba ya watu wake.

6 Na ikawa alipokuwa akimwomba Bwana, palitokea moto mfano wa nguzo na ukatua juu ya mwamba uliokuwa mbele yake; na akaona na kusikia mengi; na kwa sababu ya vitu alivyoona na kusikia alitetemeka na kutapatapa kupita kiasi.

7 Na ikawa kwamba alirejea nyumbani kwake Yerusalemu; na akajitupa kitandani mwake, akiwa amelemewa na Roho na vitu alivyoviona.

8 Na ikiwa amelemewa na Roho, alichukuliwa kwa ono, hata kwamba aliona mbingu zikifunguka, na akadhani kuwa alimwona Mungu ameketi kwenye kiti chake cha enzi, akizingirwa na malaika wasio na idadi wakiwa katika hali ya kumwimbia na kumsifu Mungu wao.

9 Na ikawa kwamba alimwona Mmoja akishuka kutoka katikati ya mbingu, na akaona mngʼaro wake ulikuwa zaidi ya jua la adhuhuri.

10 Na pia akaona wengine kumi na wawili wakimfuata, na mngʼaro wao ulikuwa zaidi ya ule wa nyota angani.

11 Na wakaja chini na wakatembea usoni mwa dunia; na wa kwanza akaja na kusimama mbele ya baba yangu, na akampatia kitabu, na akamwamuru asome.

12 Na ikawa alipokuwa akisoma, alijazwa na Roho wa Bwana.

13 Na akasoma, akisema: Ole, ole kwa Yerusalemu, kwani nimeona machukizo yako! Ndiyo, na vitu vingi vilisomwa na baba yangu kuhusu Yerusalemu—kwamba itaangamizwa, na wenyeji wake pia; wengi wangekufa kwa upanga, na wengi wangetekwa nyara na kupelekwa Babilonia.

14 Na ikawa kwamba baada ya baba yangu kusoma na kuona vitu vingi vikubwa na vya ajabu, alipaza sauti kwa Bwana akisema vitu vingi; kama: Kazi zako ni kuu na za ajabu, Ewe Bwana Mungu Mwenyezi! Kiti chako cha enzi kiko juu mbinguni, na nguvu zako, na wema wako, na rehema zako ziko juu ya wakazi wote wa dunia; na, kwa sababu una huruma, hutakubali wale ambao watakuja kwako waangamie!

15 Na baba yangu alitumia maneno kama haya kwa kumsifu Mungu wake; kwani nafsi yake ilishangilia, na moyo wake wote ulijaa furaha, kwa sababu ya vitu vile alivyokuwa ameona, ndiyo, vile Bwana alivyokuwa amemwonyesha.

16 Na sasa mimi, Nefi, siandiki maandishi yote ambayo baba yangu aliandika, kwani ameandika vitu vingi ambavyo aliona kwa maono na kwa ndoto; na pia ameandika vitu vingi ambavyo alitoa unabii na kuwaambia watoto wake, ambayo mimi sitaandika yote.

17 Lakini nitaandika maandishi ya matendo yangu maishani mwangu. Tazama, ninafupisha maandishi ya baba yangu, na kuyaandika katika mabamba ambayo nilitengeneza kwa mikono yangu mwenyewe; kwa hivyo, baada ya kufupisha maandishi ya baba yangu ndipo nitaandika maandishi kuhusu maisha yangu.

18 Kwa hivyo, ningetaka mjue, kwamba baada ya Bwana kumwonyesha baba yangu, Lehi, vitu vingi vya ajabu, ndiyo, kuhusu kuangamizwa kwa Yerusalemu, tazama alienda miongoni mwa watu, na akaanza kutoa unabii na kuwatangazia vile vitu alivyokuwa ameviona na kusikia.

19 Na ikawa kwamba Wayahudi walimfanyia mzaha kwa sababu ya vitu vile alivyowashuhudia; kwa kweli aliwashuhudia kuhusu uovu wao na machukizo yao; na akawashuhudia kwamba vitu vile ambavyo alivyokuwa ameviona na kusikia, na pia vitu ambavyo alikuwa amesoma katika kitabu, vilidhihirisha wazi kuja kwa Masiya, na pia ukombozi wa ulimwengu.

20 Na wakati Wayahudi waliposikia vitu hivi, walimkasirikia; ndiyo, jinsi ilivyokuwa kwa manabii wa kale, ambao walikuwa wamewatupa nje, na kuwapiga kwa mawe, na kuwaua; na pia walimtafuta ili watoe uhai wake. Lakini tazama, mimi, Nefi, nitawaonyesha ninyi kuwa Bwana ana huruma nyororo juu ya wale ambao amewachagua, kwa sababu ya imani yao, kuwatia nguvu hata kwenye uwezo wa ukombozi.