Maandiko Matakatifu
2 Nefi 10


Mlango wa 10

Yakobo anaeleza kwamba Wayahudi watamsulubisha Mungu wao—Watatawanywa mpaka waanze kumwamini Yeye—Marekani itakuwa nchi ya uhuru ambako hakuna mfalme yeyote atakayetawala—Jipatanisheni na Mungu na pokeeni wokovu kwa neema Yake. Karibia mwaka 559–545 K.K.

1 Na sasa mimi, Yakobo, nawazungumzia tena, ndugu zangu wapendwa, kuhusu tawi hili takatifu ambalo nimelitaja.

2 Kwani tazama, ahadi ambazo tumepokea ni ahadi kwetu kuhusu kimwili; kwa hivyo, kwa vile nimeonyeshwa kwamba watoto wetu wengi wataangamia kimwili kwa sababu ya kutoamini, walakini, Mungu atawarehemu wengi; na watoto wetu watarejeshwa, ili wapokee kile ambacho kitawapatia ufahamu wa kweli wa Mkombozi wao.

3 Kwa hivyo, kama vile nilivyowaambia, lazima inahitajika kwamba Kristo—kwani usiku uliopita malaika aliniambia kwamba hili litakuwa jina lake—atakuja miongoni mwa Wayahudi, miongoni mwa wale ambao ni waovu zaidi ulimwenguni; na watamsulubu—hivyo ndivyo ilimpasa Mungu wetu, na hakuna taifa lingine duniani ambalo lingemsulubu Mungu wao.

4 Kwani miujiza mikuu ingetendwa miongoni mwa mataifa mengine wangetubu, na wangejua kwamba yeye ni Mungu wao.

5 Lakini kwa sababu ya ukuhani wa uongo, walio Yerusalemu watamkazia shingo zao, hata mpaka asulubiwe.

6 Kwa hivyo, kwa sababu ya uovu wao, maangamizo, njaa, tauni, na umwagaji wa damu zitawapata; na wale ambao hawataangamizwa watatawanywa miongoni mwa mataifa yote.

7 Lakini tazama, hivyo ndivyo asemavyo Bwana Mungu: Siku itakapofika watakaponiamini, kwamba mimi ni Kristo, basi nimeagana na baba zao kwamba watarejeshwa kimwili, duniani, kwenye nchi za urithi wao.

8 Na itakuwa kwamba watakusanywa kutoka mtawanyiko wao wa muda mrefu, kutoka visiwa vya bahari, na kutoka sehemu nne za dunia; na mataifa ya Wayunani yatakuwa makuu machoni mwangu, asema Mungu, kwa kuwapeleka katika nchi zao za urithi.

9 Ndiyo, wafalme wa Wayunani watakuwa baba zao walezi, na malkia wao watakuwa mama walezi; kwa hivyo, ahadi za Bwana ni kuu kwa Wayunani, kwani ameizungumza, na nani anayeweza kubisha?

10 Lakini tazama, nchi hii, Mungu alisema, itakuwa nchi ya urithi wako, na Wayunani watabarikiwa katika nchi hii.

11 Na nchi hii itakuwa nchi ya uhuru kwa Wayunani, na hakutakuwa na wafalme katika nchi hii, ambao watainuka juu ya Wayunani.

12 Na nitaimarisha nchi hii dhidi ya nchi zingine zote.

13 Na yule anayepigana na Sayuni ataangamia, asema Mungu.

14 Kwani yule anayeniinulia mfalme ataangamia, kwani mimi, Bwana, mfalme wa mbingu, nitakuwa mfalme wao, na nitakuwa nuru kwao milele, kwa wale wanaosikia maneno yangu.

15 Kwa hivyo, kwa sababu hii, ili maagano yangu niliyoagana na watoto wa watu yaweze kutimizwa, yale nitakayowatendea kimwili, lazima niangamize kazi za siri za giza, na za mauaji, na za machukizo.

16 Kwa hivyo, yule anayepigana dhidi ya Sayuni, Myahudi na Myunani, mateka na walio huru, waume kwa wake, wataangamia; kwani wao ndiyo makahaba wa dunia yote; kwani wale wasio wangu wako dhidi yangu, asema Mungu.

17 Kwani nitatimiza ahadi zangu ambazo niliagana na wanadamu, kwamba nitawatendea kimwili—

18 Kwa hivyo, ndugu zangu wapendwa, hivyo ndivyo asemavyo Mungu wetu: Nitasumbua uzao wenu kwa mkono wa Wayunani; walakini, nitalainisha mioyo ya Wayunani, kwamba watakuwa kama baba kwao; kwa hivyo, Wayunani watabarikiwa na kuhesabiwa miongoni mwa nyumba ya Israeli.

19 Kwa hivyo, nitaiwekea wakfu uzao wako hii nchi, na wale watakao hesabiwa miongoni mwa uzao wako, milele, kuwa nchi yao ya urithi; kwani ni nchi bora, Mungu ananiambia, zaidi ya nchi zingine zote, kwa hivyo nitawataka wanadamu wote wanaoishi juu yake kwamba wataniabudu, asema Mungu.

20 Na sasa, ndugu zangu wapendwa, kwa vile Mungu wetu wa huruma ametupatia ufahamu mkuu hivyo kuhusu vitu hivi, hebu tumkumbuke, na kuacha dhambi zetu, na tusiinamishe vichwa vyetu, kwani hatujatupwa; walakini, tumefukuzwa kutoka nchi yetu ya urithi; lakini tumeongozwa hadi nchi ile iliyo bora zaidi, kwani Bwana amesababisha bahari kuwa njia yetu, na tuko kwenye kisiwa cha bahari.

21 Lakini kubwa ni ahadi za Bwana kwa wale walio kwenye visiwa vya bahari; kwa hivyo kama vile inavyosema visiwa, lazima pawe na zaidi ya haya, na pia wale wanaoishi humo ni ndugu zetu.

22 Kwani tazama, Bwana Mungu ametoa kutoka nyumba ya Israeli mara kwa mara, kulingana na nia na furaha yake. Na sasa tazama, Bwana hukumbuka wale wote waliotengwa, kwa hivyo anatukumbuka pia sisi.

23 Kwa hivyo, changamsheni mioyo yenu, na kumbukeni kwamba mko huru kujitendeakuchagua njia ya kifo kisicho na mwisho au njia ya uzima wa milele.

24 Kwa hivyo, ndugu zangu wapendwa, jipatanisheni na nia ya Mungu, na sio kwa nia ya ibilisi na mwili; na kumbukeni, baada ya kupatanishwa na Mungu, kwamba ni kwa kupitia neema ya Mungu pekee mnaokolewa.

25 Kwa hivyo, Mungu awafufue kutoka kwa wafu kwa nguvu za ufufuo, na pia kutoka kifo kisicho na mwisho kwa nguvu za upatanisho, kwamba mpokelewe katika ufalme wa milele wa Mungu, kwamba mmsifu kwa neema takatifu. Amina.