Maandiko Matakatifu
2 Nefi 32


Mlango wa 32

Malaika wanazungumza kwa uwezo wa Roho Mtakatifu—Wanadamu lazima wasali na kupokea ufahamu kwa wao wenyewe kutoka kwa Roho Mtakatifu. Karibia mwaka 559–545 K.K.

1 Na sasa, tazama, ndugu zangu wapendwa, nadhani kwamba mnawaza machache mioyoni mwenu kuhusu yale mtakayotenda baada ya kuingia kwa njia hiyo. Lakini, tazama, kwa nini mnawaza vitu hivi mioyoni mwenu?

2 Je, hamkumbuki kwamba niliwaambia kwamba baada ya kupokea Roho Mtakatifu mngezungumza kwa lugha ya malaika? Na sasa, vipi mngezungumza kwa lugha ya malaika bila Roho Mtakatifu?

3 Malaika wanazungumza kwa uwezo wa Roho Mtakatifu; kwa hivyo, wanazungumza maneno ya Kristo. Kwa hivyo, niliwaambia, shiriki maneno ya Kristo; kwani tazama, maneno ya Kristo yatawaelezea vitu vyote mnavyostahili kutenda.

4 Kwa hivyo, na sasa baada ya kuzungumza maneno haya, kama hamwezi kuyafahamu, ni kwa sababu hamuombi, wala kubisha; kwa hivyo, hamjaletwa kwenye nuru, lakini lazima mwangamie gizani.

5 Kwani tazama, tena nawaambia kwamba kama mtaingia kwa njia hiyo, na kupokea Roho Mtakatifu, atawaonyesha vitu vyote ambavyo mnastahili kutenda.

6 Tazameni, haya ndiyo mafundisho ya Kristo, na hakutakuwa na mafundisho mengine yatakayotolewa hadi atakapojidhihirisha kwenu katika mwili. Na atakapojithirihisha kwenu katika mwili, mtachunguza na kufanya vile vitu atakavyowaambia.

7 Na sasa mimi, Nefi, siwezi kuzungumza zaidi; Roho anayokomesha mazungumzo yangu, na ninaachwa kuomboleza kwa sababu ya kutoamini, na uovu, na ujinga, na majivuno ya wanadamu; kwani hawatatafuta ufahamu, wala kuelewa ufahamu wa juu, wanapoelezewa wazi wazi, hata wazi vile neno linaweza kuwa.

8 Na sasa, ndugu zangu wapendwa, naona kwamba bado mnatafakari mioyoni mwenu; na inanihuzunisha kwamba lazima nizungumze kuhusu kitu hiki. Kwani ikiwa mtasikiliza Roho ambaye anawafundisha wanadamu kusali, mtajua kwamba lazima msali, kwani roho mchafu hawafundishi mwanadamu kusali, lakini humfundisha kwamba lazima asisali.

9 Lakini tazameni, nawaambia kwamba lazima msali kila wakati, na msife moyo; na kwamba msifanye lolote kwa Bwana bila kumuomba Baba kwa jina la Kristo, kwamba awatakasie matendo yenu, kwamba matendo yenu yawe ni kwa ajili ya ustawi wa nafsi yako.