Maandiko Matakatifu
3 Nefi 18


Mlango wa 18

Yesu anaanzisha sakramenti miongoni mwa Wanefi—Wanaamriwa kuomba wakati wote katika jina Lake—Wale wanaokula mwili Wake na kunywa damu Yake bila kustahili wanalaaniwa—Wanafunzi wanapewa uwezo wa kutunukia Roho Mtakatifu. Karibia mwaka 34 B.K.

1 Na ikawa kwamba Yesu aliamuru wanafunzi kwamba walete mkate na divai kwake.

2 Na walipokuwa wameenda kuleta mkate na divai, aliamuru umati kwamba ukae ardhini.

3 Na baada ya wanafunzi kurejea na mkate na divai, alichukua mkate na kuumega kwa vipande na kuutakasa; na akawapatia wanafunzi na kuwaamuru kwamba wale.

4 Na baada ya kula na kushiba, aliwaamuru kwamba watoe kwa umati.

5 Na baada ya umati kula na kushiba, aliwaambia wanafunzi: Tazama kutakuwa na mmoja atakayetawazwa miongoni mwenu, na kwake nitatolea uwezo kwamba atamega mkate na kuubariki na kuwapatia watu wa kanisa langu, kwa wote ambao wataamini na kubatizwa katika jina langu.

6 Na hii mtakumbuka kufanya daima, hata vile nimefanya, hata vile nimemega mkate na kuubariki na kuwapatia.

7 Na hii mtafanya kwa ukumbusho wa mwili wangu, ambao nimewaonesha. Na itakuwa ushuhuda kwa Baba kwamba daima mnanikumbuka. Na ikiwa mtanikumbuka daima Roho yangu itakuwa na ninyi.

8 Na ikawa kwamba baada ya kusema maneno haya, aliwaamuru wanafunzi wake kwamba wachukue divai ndani ya kikombe na wainywe, na kwamba wawapatie umati ili wanywe.

9 Na ikawa kwamba walifanya hivyo, na wakainywa na kushiba; na kuupatia umati, na wakanywa, na wakashiba.

10 Na baada ya wanafunzi kufanya hivyo, Yesu aliwaambia: Mna heri kwa hiki kitu ambacho mmefanya, kwani hii ni kutimiza amri zangu, na hii inashuhudia kwa Baba kwamba mko tayari kufanya yale ambayo nimewaamuru.

11 Na daima mtafanya hivi kwa wale wanaotubu na kubatizwa katika jina langu; na mtafanya hivi kwa ukumbusho wa damu yangu, ambayo nilimwaga kwa ajili yenu, ili mshuhudie kwa Baba kwamba daima mnanikumbuka. Na ikiwa mnanikumbuka daima Roho yangu itukuwa na ninyi.

12 Na ninawapatia amri kwamba mtafanya hivi vitu. Na ikiwa mtafanya hivi vitu daima mna baraka, kwani mmejengwa juu ya mwamba wangu.

13 Lakini yeyote miongoni mwenu ambaye atafanya zaidi au ndogo kuliko haya hajajengwa juu ya mwamba wangu, lakini wamejengwa kwenye msingi wa mchanga; na wakati mvua inateremka, na mafuriko kuja, na pepo kuvuma, na kujipigisha juu yao, wataanguka, na milango ya jehanamu iko tayari kuwapokea.

14 Kwa hivyo mnabaraka ninyi kama mtatii amri zangu, ambazo Baba ameniamuru kwamba nitoe kwenu.

15 Kweli, kweli, ninawaambia, lazima mjihadhari na kuomba siku zote, msije mkajaribiwa na ibilisi, na mwongozwe mbali kama mateka wake.

16 Na kama vile nimeomba miongoni mwenu, basi nanyi muombe hivyo katika kanisa langu, miongoni mwa watu wangu wanaotubu na kubatizwa katika jina langu. Tazama, mimi ndimi nuru; nimewapatia mfano.

17 Na ikawa kwamba baada ya Yesu kuzungumza maneno haya kwa wanafunzi wake, aliugeukia tena umati na kuwaambia:

18 Tazama, kweli, kweli, nawaambia: lazima mjihadhari na kusali siku zote, msije mkaingia majaribuni; kwani Shetani amewataka ninyi, ili apate kuwapepeta kama vile ngano.

19 Kwa hivyo lazima msali siku zote kwa Baba katika jina langu;

20 Na chochote mtakachomwomba Baba katika jina langu, ambacho ni haki, mkiamini kwamba mtapata, tazama, kitapewa kwenu.

21 Ombeni katika ukoo wenu kwa Baba, daima katika jina langu, kwamba wake zenu na watoto wenu wabarikiwe.

22 Na tazama mtakutana pamoja mara kwa mara; na hamtamzuia mtu yeyote kuja kwenu wakati mnakutana pamoja, lakini wakubalie kwamba waje kwenu na msiwazuie;

23 Lakini mtawaombea, na hamtawatupa nje; na ikiwa kwamba watakuja kwenu mara kwa mara, mtawaombea kwa Baba, katika jina langu.

24 Kwa hivyo, inueni juu nuru yenu kwamba iangaze juu ya dunia. Tazama mimi ni mwangaza ambao mtainua—kwamba mfanye yale ambayo mmeniona nikifanya. Tazama mnaona kwamba nimeomba kwa Baba, na nyote mmeshuhudia.

25 Na mnaona kwamba nimeamuru kwamba yeyote miongoni mwenu asiende, lakini nimeamuru kwamba mje kwangu, kwamba mngenipapasa na kuniona; hata hivyo mtafanya kwa ulimwengu; na yeyote anayeasi hii amri anakubali mwenyewe kuongozwa majaribuni.

26 Na sasa ikawa kwamba baada ya Yesu kusema maneno haya, aligeuza macho yake tena kuwaelekea wanafunzi ambao alikuwa amewachagua, na kuwaambia:

27 Tazameni kweli, kweli, ninawaambia, ninawapa amri ingine, na ndipo niteanda kwa Baba yangu ili nitimize amri zingine ambazo amenipatia.

28 Na sasa tazama, hii ndiyo amri ninayowapatia, kwamba msikubali yeyote kuonja mwili wangu na damu bila kustahili, wakati mtahudumu;

29 Kwani yeyote alaye na anywaye mwili wangu na damu asipostahili hula na kunywa lawama kwa nafsi yake; kwa hivyo kama mnajua kwamba mtu hastahili kula na kunywa mwili wangu na damu, mtamzuia.

30 Walakini, hamtamtupa nje kutoka miongoni mwenu, lakini mtamhudumia na mtamwombea kwa Baba, katika jina langu; na ikiwa kwamba atatubu na kubatizwa katika jina langu, ndipo mtampokea, na mtamhudumia mwili wangu na damu yangu.

31 Lakini asipotubu hatahesabiwa miongoni mwa watu wangu, ili asiharibu watu wangu, kwani tazama najua kondoo wangu, na wamehesabiwa.

32 Walakini, hamtamtupa nje ya masinagogi yenu, au mahali penu pa kuabudu, kwani kwa hawa mtaendelea kuwahudumia; kwani hamjui kama watarudi na kutubu, na kuja kwangu kwa moyo wa lengo moja, na nitawaponya; na ndipo mtakuwa njia ya kuwaletea wokovu.

33 Kwa hivyo, tii maneno haya ambayo nimewaamuru kwamba msije mkawa chini ya hukumu; kwani ole kwa yule ambaye Baba anamhukumu.

34 Na ninawapatia amri hizi kwa sababu ya ugomvi ambao umekuwa miongoni mwenu. Na heri ninyi kama hamna ugomvi miongoni mwenu.

35 Na sasa nitaenda kwa Baba, kwa sababu ni muhimu kwamba niende kwa Baba kwa ajili yenu.

36 Na ikawa kwamba baada ya Yesu kumaliza maneno haya, aliwagusa wanafunzi ambao alikuwa amewachagua kwa mkono wake mmoja mmoja mpaka alipowagusa wote, na aliwazungumzia akiwagusa.

37 Na umati haukusikia maneno ambayo alisema, kwa hivyo hawakushuhudia; lakini wanafunzi wanashuhudia kwamba aliwapatia uwezo kutoa Roho Mtakatifu. Na nitawaonyesha baadaye kwamba huu ushahidi ni wa kweli.

38 Na ikawa kwamba baada ya Yesu kuwagusa wote, kulitokea wingu na likafunika umati kwamba haungemwona Yesu.

39 Na wakati walipokuwa wamefunikwa aliondoka kutoka kwao, na kupaa mbinguni. Na wanafunzi waliona na wanashudia kwamba alipaa tena mbinguni.