Maandiko Matakatifu
Alma 15


Mlango wa 15

Alma na Amuleki wanaenda Sidomu na kuanzisha kanisa—Alma anamponya Zeezromu, ambaye anajiunga na Kanisa—Wengi wanabatizwa, na Kanisa linafanikiwa—Alma na Amuleki wanaenda Zarahemla. Karibia mwaka 81 K.K.

1 Na ikawa kwamba Alma na Amuleki waliamriwa waondoke kutoka ule mji; na wakaondoka, na kufika hata katika nchi ya Sidomu; na tazama, kule waliwapata watu wote ambao walikuwa wametoka nchi ya Amoniha, na ambao walikuwa wametupwa nje na kupigwa kwa mawe, kwa sababu walikuwa wameamini maneno ya Alma.

2 Na wakawaelezea yale yote ambayo yalikuwa yamefanyika kwa wake na watoto wao, na pia kuwahusu wao wenyewe, na nguvu za ukombozi.

3 Na pia Zeezromu aliugua huko Sidomu, kwa homa kali, ambayo ilisababishwa na masumbuko mengi akilini mwake kwa sababu ya uovu wake, kwani alidhani kwamba Alma na Amuleki walikuwa hawako tena; na alidhani kwamba walikuwa wameuliwa kwa sababu ya uovu wake. Na dhambi hii kubwa, na dhambi zake zingine nyingi, zilimsumbua katika mawazo yake hadi zikawa kama vidonda vikubwa, kwani hakuwa na ukombozi; kwa hivyo aliaanza kuchomwa kwa joto kali.

4 Sasa, aliposikia kwamba Alma na Amuleki walikuwa katika nchi ya Sidomu, moyo wake ulianza kupata ujasiri; na akawatumia ujumbe mara moja, akihitaji wamtembelee.

5 Na ikawa kwamba walikwenda mara moja, kwani walitii ule ujumbe ambao alikuwa amewatumia; na wakaenda ndani ya nyumba ya Zeezromu; na wakamkuta kitandani mwake, akiwa mgonjwa, akiwa mnyonge kwa homa kali; na alikuwa na maumivu mengi katika akili yake kwa sababu ya maovu yake; na alipowaona, aliunyosha mkono wake, na kuwasihi kwamba wamponye.

6 Na ikawa kwamba Alma alimwambia, akimchukua kwa mkono wake: Je, unaziamini nguvu za wokovu za Kristo?

7 Na akajibu kwa kusema: Ndiyo, ninaamini maneno yote ambayo mmefundisha.

8 Na Alma akasema: Kama unaamini katika ukombozi wa Kristo wewe unaweza kuponywa.

9 Na akasema: Ndiyo, ninaamini kulingana na maneno yako.

10 Na ndipo Alma akamlilia Bwana, na kusema: Ee Bwana Mungu wetu, mrehemu mtu huyu, na umponye kulingana na imani yake ambayo iko katika Kristo.

11 Na Alma aliposema maneno haya, Zeezromu aliinuka kwa miguu yake, na kuanza kutembea; na hii ilifanywa kwa mshangao wa watu wote; na kitendo hiki kilijulikana kote katika nchi ya Sidomu.

12 Na Alma akambatiza Zeezromu katika Bwana; na akaanza tangu wakati ule na kuendelea kuwahubiria watu.

13 Na Alma alianzisha kanisa katika nchi ya Sidomu, na akawaweka makuhani na walimu wakfu katika nchi, wabatize yeyote aliyetaka kubatizwa katika Bwana.

14 Na ikawa kwamba walikuwa wengi; kwani walikusanyika kutoka sehemu zote za Sidomu, na wakabatizwa.

15 Lakini kwa watu waliokuwa katika nchi ya Amoniha, bado walibaki na mioyo migumu na shingo ngumu; na hawakutubu dhambi zao, wakifikiria nguvu za Alma na Amuleki kuwa za ibilisi; kwani walikuwa wafuasi wa dini ya Nehori, na hawakuamini katika kutubu dhambi zao.

16 Na ikawa kwamba Alma na Amuleki, Amuleki akiwa ameiacha dhahabu yake yote, na fedha, na vitu vyake vya thamani, vilivyokuwa katika nchi ya Amoniha, kwa neno la Mungu, yeye akikataliwa na wale ambao walikuwa marafiki zake kitambo, na pia na baba yake na jamaa yake;

17 Kwa hivyo, baada ya Alma kuimarisha kanisa katika Sidomu, na kuona zuio kuu, ndiyo, akiona kwamba watu walizuiliwa kutokana na kiburi kilichokuwa katika mioyo yao, na wakaanza kunyenyekea mbele ya Mungu, na wakaanza kujikusanya pamoja katika makao yao matakatifu kumwabudu Mungu mbele ya madhabahu, wakiwa waangalifu na wakiomba daima, kwamba wakombolewe kutokana na Shetani, na kutoka kifo, na kutoka maangamizo—

18 Sasa kama nilivyosema, baada ya Alma kuona hivi vitu vyote, kwa hivyo alimchukua Amuleki na kuvuka katika nchi ya Zarahemla, na akampeleka katika nyumba yake mwenyewe, na kumhudumia katika mateso yake, na kumtia nguvu katika Bwana.

19 Na hivyo mwaka wa kumi wa utawala wa waamuzi juu ya watu wa Nefi uliisha.