Maandiko Matakatifu
Alma 4


Mlango wa 4

Alma anabatiza maelfu ya waumini—Uovu unaingia kanisani, na maendeleo ya Kanisa yanacheleweshwa—Nefiha anachaguliwa kuwa mwamuzi mkuu—Alma, kama kuhani mkuu, anajitolea kwa huduma. Karibia mwaka 86–83 K.K.

1 Sasa ikawa kwamba katika mwaka wa sita wa utawala wa waamuzi juu ya watu wa Nefi, hakukuwa na mabishano wala vita katika nchi ya Zarahemla;

2 Lakini watu walisumbuliwa, ndiyo, walisumbuliwa sana kwa kupoteza ndugu zao, na pia hasara ya mifugo yao na wanyama wao, na pia hasara ya mashamba yao ya nafaka, ambayo ilikanyagwa kwa miguu na kuangamizwa na Walamani.

3 Na masumbuko yao yalikuwa makuu sana hata kwamba kila nafsi ilisababishwa kuomboleza; na waliamini kwamba ilikuwa ni hukumu ya Mungu juu yao kwa sababu ya uovu wao na machukizo yao; kwa hivyo walikumbushwa jukumu lao.

4 Na wakaanza kuimarisha sana kanisa; ndiyo, na wengi walibatizwa katika maji ya Sidoni na wakaunganishwa kwa kanisa la Mungu; ndiyo, walibatizwa kwa mkono wa Alma, ambaye alikuwa ametengwa kuwa kuhani mkuu juu ya watu wa kanisa, kwa mkono wa baba yake Alma.

5 Na ikawa kwamba katika mwaka wa saba wa utawala wa waamuzi nafsi elfu tatu na mia tano zilijiunga na kanisa la Mungu na kubatizwa. Na hivyo mwaka wa saba wa utawala wa waamuzi juu ya watu wa Nefi uliisha; na kulikuwa na amani daima kwa wakati huo wote.

6 Na ikawa kwamba katika mwaka wa nane wa utawala wa waamuzi, kwamba watu wa kanisa walianza kupata kiburi, kwa sababu ya utajiri wao wa kupita kiasi, na hariri zao za kuvutia, na vitani vyao vilivyovutia, na kwa sababu ya mifugo yao na wanyama wao wengi, na dhahabu yao na fedha yao, na kila aina ya vitu vya thamani, ambavyo walikuwa wamepata kwa sababu ya bidii yao; na katika vitu hivi vyote walijivuna kwa macho yao, kwani walianza kuvaa mavazi ya bei ghali.

7 Sasa hii ilimsumbua Alma sana, ndiyo, na pia watu wengi ambao Alma alikuwa amewatenga wawe walimu, na makuhani, na wazee wa kanisa; ndiyo, wengi wao walianza kuhuzunishwa na uovu ambao waliona umeanza kuwa miongoni mwa watu wao.

8 Kwani waliona na wakahuzunika sana kwamba watu wa kanisa walianza kujiinua kwa kiburi machoni mwao, na kuweka mioyo yao katika utajiri na vitu vya ulimwengu visivyofaidisha, kwamba walianza kufanyiana madharau, wao kwa wao, na wakaanza kuwatesa wale ambao hawakuamini kulingana na nia yao na mapenzi yao.

9 Na hivyo, katika mwaka huu wa nane wa utawala wa waamuzi, kulianza kuwa na mabishano mengi miongoni mwa watu wa kanisa; ndiyo, kulikuwa na wivu, na mzozo, na chuki, na mateso, na kiburi, hata kuzidi kiburi cha wale ambao hawakuwa washiriki wa kanisa la Mungu.

10 Na hivyo mwaka wa nane wa utawala wa waamuzi ulikwisha; na uovu wa kanisa ulikuwa ni kikwazo kikuu kwa wale ambao hawakuwa washiriki wa kanisa; na hivyo kanisa likaanza kukosa kuendelea.

11 Na ikawa kwamba katika mwanzo wa mwaka wa tisa, Alma aliona uovu wa kanisa, na pia akaona kwamba mfano wa kanisa ulianza kuwaongoza wale wasioamini kutoka uovu mmoja hadi mwingine, hivyo kuwaletea watu maangamizo.

12 Ndiyo, aliona ukosefu wa usawa miongoni mwa watu, wengine wakijiinua juu kwa kiburi chao, wakidharau wengine, wakikataa kuwasaidia wale ambao walikuwa na shida na walio uchi na wale ambao walikuwa na njaa, na wale ambao walikuwa na kiu, na wale ambao walikuwa wagonjwa na waliosumbuka.

13 Sasa hii ilikuwa ni sababu kuu ya maombolezi miongoni mwa watu, wakati wengine walikuwa wanajinyenyekeza, wakiwasaidia wale ambao walihitaji msaada, kama vile kupeana mali yao kwa wale ambao walikuwa masikini na wenye shida, wakiwalisha wenye njaa, na kuteseka kwa kila aina ya masumbuko, kwa sababu ya Kristo, ambaye angekuja kulingana na roho ya unabii;

14 Wakitazamia mbele kwenye siku ile, na hivyo wakidumisha msamaha wa dhambi zao; wakijazwa na shangwe kuu kwa sababu ya ufufuo wa wafu, kulingana na nia na uwezo na ukombozi wa Yesu Kristo kutoka kamba za kifo.

15 Na sasa ikawa kwamba Alma, baada ya kuona masumbuko ya wafuasi wanyenyekevu wa Mungu, na mateso ambayo walibandikwa na watu wake waliobaki, na kuona ukosefu wa usawa wao wote, alianza kuhuzunika sana; walakini Roho wa Bwana hakumwacha.

16 Na akamchagua mtu mwenye hekima miongoni mwa wazee wa kanisa, na akampatia nguvu kulingana na kura ya watu, kwamba apate uwezo wa kuandika sheria kulingana na sheria ambazo zilikuwa zimetolewa, na kuzitekeleza kulingana na uovu na uhalifu wa watu.

17 Sasa jina la mtu huyu lilikuwa Nefiha, na alichaguliwa kuwa mwamuzi mkuu; na alikaa katika kiti cha hukumu na kuwahukumu na kuwatawala watu.

18 Sasa Alma hakumkabidhi ofisi ya kuhani mkuu wa kanisa, lakini alijihifadhia ofisi ya kuhani mkuu; lakini akamkabidhi Nefiha kiti cha hukumu.

19 Na hii alifanya ili yeye mwenyewe aende miongoni mwa watu wake, au watu wa Nefi, kwamba awahubirie neno la Mungu, kuwasisimua wakumbuke wajibu wao, na kwamba ashushe chini, kwa neno la Mungu, kiburi chao chote na ujanja na mabishano yaliyokuwa miongoni mwa watu wake, kwani hakuona njia nyingine ya kuwaokoa watu wake isipokuwa kwa kuwashawishi ushuhuda halisi.

20 Na hivyo katika mwanzo wa mwaka wa tisa wa utawala wa waamuzi juu ya watu wa Nefi, Alma alimkabidhi Nefiha kiti cha hukumu, na akajitolea mwenyewe kabisa kwa ule ukuhani mkuu ulio mpango mtakatifu wa Mungu, kwa ushuhuda wa neno, kulingana na roho ya ufunuo na unabii.