Maandiko Matakatifu
Etheri 12


Mlango wa 12

Nabii Etheri anawasihi watu waamini katika Mungu—Moroni anasimulia maajabu na miujiza inayofanywa kwa imani—Imani ilimwezesha kaka wa Yaredi kumwona Kristo—Bwana huwapa watu udhaifu ili wawe wanyenyekevu—Kaka wa Yaredi aliusogeza mlima Zerini kwa imani—Imani, tumaini, na hisani ni muhimu kwa wokovu—Moroni alimwona Yesu uso kwa uso.

1 Na ikawa kwamba siku za Etheri zilikuwa katika siku za utawala wa Koriantumuri; na Koriantumuri alikuwa mfalme wa nchi yote.

2 Na Etheri alikuwa nabii wa Bwana; kwa hivyo Etheri alijitokeza katika siku za Koriantumuri, na akaanza kutabiri kwa watu, kwani hangeweza kuzuiliwa kwa sababu ya Roho wa Bwana ambayo ilikuwa ndani yake.

3 Kwani alihubiri kutoka asubuhi, hata mpaka kwenda chini kwa jua, akihimiza watu kuamini katika Mungu kwenye toba wasije wakaharibiwa, na akiwaambia kwamba kwa imani vitu vyote hutimizwa—

4 Kwa hivyo, yeyote aaminiye katika Mungu angeweza kwa hakika kutumaini ulimwengu bora, ndiyo, hata mahali katika mkono wa kulia wa Mungu, tumaini ambalo huja kutokana na imani, hutengeneza nanga kwa roho za watu, ambayo ingewafanya kuwa imara na thabiti, wakizidi sana kutenda kazi njema, wakiongozwa kumtukuza Mungu.

5 Na ikawa kwamba Etheri alitabiri vitu vikubwa vya ajabu kwa watu, ambavyo hawakuamini, kwa sababu hawakuviona.

6 Na sasa, mimi, Moroni, nitazungumza machache kuhusu vitu hivi; ninataka kuonyesha ulimwengu kwamba imani ni vitu ambavyo vinatumainiwa na havionekani; kwa hivyo, msishindane kwa sababu hamwoni, kwani hamtapata ushahidi wowote mpaka baada ya majaribu ya imani yenu.

7 Kwani ilikuwa kwa imani kwamba Kristo alijionyesha kwa babu zetu, baada ya kuamka kutoka kwa wafu; na hakujionyesha kwao mpaka walipokuwa na imani ndani yake; kwa hivyo, lazima iwe kwamba wengine walikuwa na imani ndani yake, kwani hakujionyesha kwa ulimwengu.

8 Lakini kwa sababu ya imani ya watu amejionyesha kwa watu wa ulimwengu, na kulitukuza jina la Baba, na alitayarisha njia ambayo kwake wengine wangeshiriki kwa mwito wa zawadi ya mbinguni, kwamba wangetumainia vitu hivyo ambavyo hawajaviona.

9 Kwa hivyo, mnaweza kuwa pia na tumaini, na muwe washiriki wa zawadi, ikiwa mtakuwa tu na imani.

10 Tazama ilikuwa kwa imani kwamba wale wa kale waliitwa kwa mpango mtakatifu wa Mungu.

11 Kwa hivyo, kwa imani, sheria ya Musa ilitolewa. Lakini katika kipawa cha Mwana wake Mungu ametayarisha njia bora zaidi; na ni kwa imani kwamba imetimizwa.

12 Kwani kama hakuna imani miongoni mwa watoto wa watu, Mungu hawezi kufanya miujiza miongoni mwao; kwa hivyo, hakujionyesha mpaka baada ya imani yao.

13 Tazama, ilikuwa imani ya Alma na Amuleki ambayo ilisababisha gereza kuanguka chini.

14 Tazama, ilikuwa imani ya Nefi na Lehi ambayo ilileta mabadiliko juu ya Walamani, kwamba walibatizwa kwa moto na kwa Roho Mtakatifu.

15 Tazama, ilikuwa imani ya Amoni na ndugu zake ambayo ilileta muujiza mkuu miongoni mwa Walamani.

16 Ndiyo, na hata wote waliofanya miujiza waliifanya kwa sababu ya imani, hata wale walioishi kabla ya Kristo na pia wale waliokuwako baadaye.

17 Na ilikuwa kwa imani kwamba wale wanafunzi watatu walipata ahadi kwamba hawangeona kifo; na hawakupokea ahadi hiyo mpaka baada ya wao kuwa na imani.

18 Na wala kwa muda wowote hakujawa na yeyote ambaye amefanya miujiza mpaka awe na imani; kwa hivyo waliamini kwanza katika Mwana wa Mungu.

19 Na kulikuwa na wengi ambao imani yao ilikuwa na nguvu sana, hata kabla ya Kristo kuja, ambao hawangeweza kuwekwa nyuma ya pazia, lakini kwa ukweli waliona kwa macho yao vitu ambavyo walikuwa wameona kwa jicho la imani, na walifurahi.

20 Na tazama, tumeona katika maandishi haya kwamba mmoja wa hao alikuwa kaka wa Yaredi; kwani imani yake ilikuwa kubwa sana katika Mungu, kwamba Mungu alipoweka kidole chake mbele hakuweza kukificha kutoka kwa uwezo wa kuona wa kaka wa Yaredi, kwa sababu ya neno lake ambalo alikuwa amemzungumzia, neno ambalo alikuwa amepokea kwa imani.

21 Na baada ya kaka wa Yaredi kuona kidole cha Bwana, kwa sababu ya ahadi ambayo kaka wa Yaredi alikuwa amepata kwa imani, Bwana hangeweza kumzuia kuona chochote; kwa hivyo alimwonyesha vitu vyote, kwani hangeweza tena kuwekwa nje ya pazia.

22 Na ni kwa imani kwamba babu zangu wamepata ahadi kwamba vitu hivi vitakuja kwa ndugu zao kupitia kwa Wayunani; kwa hivyo Bwana ameniamuru, ndiyo, hata Yesu Kristo.

23 Na nikasema kwake: Bwana, Wayunani watachekelea vitu hivi, kwa sababu ya unyonge wetu katika maandishi; kwani Bwana umetufanya wakubwa katika neno kwa imani, lakini hujatufanya wakubwa kwenye maandishi; kwani umefanya watu hawa wote kwamba wanaweza kusema sana, kwa sababu ya Roho Mtakatifu ambaye umewapatia.

24 Na umetufanya kwamba tuweze kuandika tu machache, kwa sababu ya mikono yetu kutokuwa miepesi. Tazama, hujatufanya mabingwa kwa uandishi kama kaka wa Yaredi, kwani ulimfanya ili vitu ambavyo aliandika viwe vikubwa hata vile wewe ulivyo, kwa kushinda mtu kuvisoma.

25 Umefanya pia maneno yetu yawe yenye nguvu na makubwa, hata kwamba hatuwezi kuyaandika; kwa hivyo, tunapoandika tunaona udhaifu wetu, na kuanguka kwa sababu ya upangaji wa maneno yetu; na ninaogopa Wayunani wasije wakacheka maneno yetu.

26 Na nilipokuwa nimesema hivi, Bwana alinizungumzia, akisema: Wajinga hucheka, lakini wataomboleza; na neema yangu unatosha kwa walio wanyenyekevu, kwamba hawatafaidika na udhaifu wenu;

27 Na ikiwa watu watakuja kwangu nitawaonyesha udhaifu wao. Ninawapatia watu udhaifu ili katika udhaifu wao wawe wanyenyekevu; na neema yangu inatosha watu wote ambao hujinyenyekeza mbele yangu; kwani wakijinyenyekeza mbele yangu, na kuwa na imani ndani yangu, ndipo nitafanya vitu dhaifu kuwa vya nguvu kwao.

28 Tazama, nitawaonyesha Wayunani udhaifu wao, na nitawaonyesha kwamba imani, tumaini na hisani huwaleta kwangu—chimbuko la haki yote.

29 Na mimi, Moroni, baada ya kusikia maneno haya, nilifarijika, na kusema: Ee Bwana, haki yako itafanyika, kwani najua kwamba unafanya miujiza kwa watoto wa watu kufuatana na imani yao;

30 Kwani kaka wa Yaredi alisema kwa mlima Zerini, Nenda—na ulisonga. Na ikiwa hangekuwa na imani haungesonga; kwa hivyo unafanya miujiza baada ya watu kuwa na imani.

31 Kwa njia hii ulijionyesha kwa wanafunzi wako; kwani baada ya wao kuwa na imani, na kuzungumza katika jina lako, ulijidhihirisha kwao kwa uwezo mkuu.

32 Na ninakumbuka kwamba umesema kwamba umetayarisha nyumba kwa watu, ndiyo, hata miongoni mwa nyumba za Baba yako, ambamo kwake binadamu angekuwa na tumaini kamili; kwa hivyo lazima binadamu atumaini, au hatapokea urithi mahali ambapo umetayarisha.

33 Na tena, ninakumbuka kwamba umesema kwamba unawapenda watu wote duniani, hata kwenye kuweka maisha yako chini kwa ajili ya walimwengu, ili ungeyachukua tena kutayarisha mahali kwa watoto wa watu.

34 Na sasa najua kwamba huu upendo ambao umekuwa nao kwa watoto wa watu ni hisani; kwa hivyo, isipokuwa watu wawe na hisani hawawezi kurithi pale mahali ambapo umetayarisha nyumbani kwa Baba yako.

35 Kwa hivyo, ninajua kwa kitu hiki ambacho umesema, kwamba ikiwa Wayunani hawana hisani, kwa sababu ya unyonge wetu, kwamba utawahukumu, na kuchukua kutoka kwao talanta zao, ndiyo, hata ile ambayo wamepokea, na uwapatie wale ambao watakuwa na nyingi zaidi.

36 Na ikawa kwamba niliomba kwa Bwana kwamba awape neema Wayunani, ili wapate kuwa na hisani.

37 Na ikawa kwamba Bwana akasema nami: Kama hawana hisani haikuhusu wewe, umekuwa mwaminifu; kwa hivyo, nguo zako zitafanywa safi. Na kwa sababu umeuona udhaifu wako utafanywa kuwa mwenye nguvu, hata kwa kukaa mahali ambapo nimepatayarisha katika nyumba ya Baba yangu.

38 Na sasa mimi, Moroni, ninaaga kwa Wayunani, ndiyo, na pia kwa ndugu zangu ambao ninawapenda, mpaka tutakapokutana mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ambapo watu wote watajua kwamba mavazi yangu hayajawekwa mawaa na damu yenu.

39 Na ndipo mtakapojua kwamba nimemwona Yesu, na kwamba amenizungumzia uso kwa uso, na kwamba aliniambia katika unyenyekevu ulio wazi, hata vile mtu humwambia mwenzake kwa lugha yangu, kuhusu vitu hivi;

40 Na ni vichache tu ambavyo nimeandika, kwa sababu ya udhaifu wangu kwa kuandika.

41 Na sasa, nimekupendekeza kumtafuta huyu Yesu ambaye manabii na mitume wameandika kumhusu, kwamba neema ya Mungu Baba, na pia Bwana Yesu Kristo, na Roho Mtakatifu, ambaye anashuhudia kwao, iwe na kuishi ndani yenu milele. Amina.