Maandiko Matakatifu
Mormoni 7


Mlango wa 7

Mormoni anawaalika Walamani wa siku za mwisho kuamini katika Kristo, waikubali injili Yake, na waokolewe—Wote wanaoiamini Biblia pia wataamini Kitabu cha Mormoni. Karibia mwaka 385 B.K.

1 Na sasa, tazama, nataka kuzungumza machache kwa baki la watu hawa ambao wameachiliwa, ikiwa Mungu atawapatia maneno yangu, ili wajue kuhusu vitu vya baba zao; ndiyo, ninawazungumzia, ninyi baki la nyumba ya Israeli; na haya ndiyo maneno ambayo ninasema:

2 Nataka mjue kwamba ninyi ni wa nyumba ya Israeli.

3 Nataka mjue kwamba lazima mtubu, au hamtaokolewa.

4 Nataka mjue kwamba lazima muweke chini silaha za vita, na msifurahie tena katika umwagaji wa damu, na msizichukue tena, isipokuwa kama Mungu atawaamuru.

5 Nataka mjue kwamba lazima muelimike kuhusu babu zenu, na mtubu dhambi zenu zote na maovu, na kuamini katika Yesu Kristo, kwamba yeye ni Mwana wa Mungu, na kwamba aliuawa na Wayahudi, na kwa uwezo wa Baba amefufuka tena, kwa kufanya hivyo amepata ushindi juu ya mauti; na pia kupitia kwake uchungu wa kifo umetolewa.

6 Na anatimiza ufufuo wa wafu, ambako binadamu lazima atainuliwa kusimama mbele ya kiti cha hukumu.

7 Na ameleta kutimizwa ukombozi wa ulimwengu, ambako yule ambaye atapatikana bila makosa mbele yake katika siku ya hukumu atakubaliwa kuishi kwenye uwepo wa Mungu katika ufalme wake, kuimba sifa zisizo na mwisho na jamii ya waimbaji wa juu, kwa Baba, na kwa Mwana, na kwa Roho Mtakatifu, ambao ni Mungu mmoja, katika hali ya furaha ambayo haina mwisho.

8 Kwa hivyo tubuni, na mbatizwe katika jina la Yesu, na mkubali injili ya Kristo, ambayo itawekwa mbele yenu, sio tu kwa maandishi haya lakini pia kwa maandishi ambayo yatawajia Wayunani kutoka kwa Wayahudi, maandishi ambayo yatatoka kwa Wayunani hadi kwenu.

9 Kwani tazama, haya yameandikwa kwa kusudi kwamba mngeamini hayo; na mkiyaamini hayo mtaamini haya pia; na ikiwa mtaamini haya mtajua kuhusu babu zenu, na pia kazi za ajabu ambazo zimesababishwa na uwezo wa Mungu miongoni mwao.

10 Na mtajua pia kwamba ninyi ni baki la uzao wa Yakobo; kwa hivyo mmehesabiwa miongoni mwa watu wa agano la kwanza; na ikiwa itakuwa hivyo kwamba mtaamini katika Kristo, na mnabatizwa, kwanza kwa maji, halafu kwa moto na Roho Mtakatifu, mkifuata mfano wa Mwokozi wetu, kulingana na alivyotuamuru, itakuwa vema nanyi katika ile siku ya hukumu. Amina.